Kwa nini gari lako huenda linakusanya na kutoa taarifa zako binafsi?

Chanzo cha picha, Serenity Strul/ Getty Images
Magari ya kisasa kimsingi ni kompyuta zilizo na magurudumu.
Mashirika makubwa sasa yanatumia zana hizi kukusanya maelezo ya faragha kuhusu maisha yako na kupata fedha zaidi.
Ikiwa unafikiri kuendesha gari ni fursa ya kujiskia huru, huenda utahitajika kutathmini upya mtazamo wako kwa sababu mambo yatazidi kuwa mabaya zaidi.
Ukichunguza sera za faragha za kampuni za magari utaona kuwa hili limeangaziwa ni vile tu pengine hukuwa makini.
Maelezo wanayokusanya yanaweza kujumuisha data sahihi ya kila mahali unapoenda, uko na nani kwenye gari, kile unachosikiliza kwenye redio, ipia inaonyesha kama umefunga mkanda wa usalama, unaendesha gari kwa kasi sana, au ikiwa unafunga breki mara kwa mara.
Baadhi ya hifadhidata hizi zinaweza kukusanya maelezo ambayo hukutarajia, kama vile uzani wako, umri, rangi na sura ya uso.
Magari mengine hata yana kamera zilizoelekezwa kwenye kiti cha dereva. Magari mengi pia yana muunganisho wa intaneti ambao unaweza kutuma data hii unapoendesha gari lako.
Hili ni suala la faragha ambalo linaweza kukugharimu fesha. Kampuni za bima ni miongoni mwa wateja wakubwa wa data ya gari, na hutumia data hii kuongeza malipo ya bima kwa baadhi ya madereva.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini huna njia ya kujua taarifa zako zinaenda wapi.
Baadhi ya makampuni ya magari yanakubali kuuza data yako, lakini hawana wajibu wa kusema ni nani aliyeinunua.
Wataalamu wanasema idadi kubwa ya watumiaji wengi hata hawana habari kuwa taarifa zao zinakusanywa na kuuzwa.
"Watu wanaweza kushangazwa na idadi ya pointi za data ambazo magari yao hukusanya na kutuma kwa mtengenezaji au programu za watu wengine," anasema Darrell West, mtafiti mkuu katika Kituo cha Ubunifu wa Teknolojia cha Taasisi ya Brookings huko Washington, Marekani.
"Hii ina maana kwamba maisha yako yanaweza kuchezwa upya kama kanda ya filamu inayoonyesha kila sekunde ya kile unachofanya kwa siku," anasema kwa ufupi kuhusu suala hilo.
Bado unabisha?
Zaidi ya hayo, kuna sheria inayopangwa kutekelezwa nchini Marekani ambayo itaruhusu kiwango cha data ambacho kifaa chako cha kielekroniki kinaweza kukusanya kukuhusu.
Hivi karibuni, kampuni za magari za Marekani zitahitajika kusweka kamera za za infrared na mifumo mingine ili kuchanganua mwenendo wako, na kubaini ikiwa umelewa au umechoka sana kuendesha gari.
Lakini hii pia itafungua hazina mpya ya data kuhusu afya na mwenendo wako. Hakuna sheria inayodhibiti kile ambacho kampuni za magari zinaweza kufanya na taarifa hizi za faragha.
Licha ya maelezo haya ambayo huenda yakawaathiri baadhi ya wenye magari wataalamu wanasema teknolojia hii pia ina kuna faida pia. Magari yaliyounganishwa na mtandao wa intaneti yanaweza kuboresha. Sensa zilizowekwa zinaweza kuwafanya waendeshaji magari kuwa makini na hii itasaidia kuimarisha usalama barabarani. Kampuni za bima zinaweza kukutoza ada kidogo kwa kuwa dereva mzuri.
Hofu ya data kuvujishwa
Kampuni ya ushauri ya McKinsey iLItabiri kuwa 50% ya magari barabarani yatakuwa na muunganisho wa intaneti kufikia 2021, na kwamba idadi hii itapanda hadi 95% ifikapo 2030.
Ikiwa gari lako limeunganishwa na mtandao wa intaneti, maelezo ya kibinafsi na faragha bila shaka ni mambo unayohitaji kutilia maanani.
Kampuni za magari pia zinaweza kukufuatilia unapounganisha simu yako kwenye mfumo wa infotainment au kutumia programu fulani zilizoundwa kwa ajili ya kuendesha gari.
Baadhi ya wenye magari hutumia mifumo ya telemetry ya makampuni ya bima, ambayo inaruhusu ufuatiliaji, ili kupunguziwa ada.
Uchambuzi uliofanywa mwaka wa 2023 na Mozilla, mtengenezaji wa mtandao wa Firefox, ulichunguza sera za faragha za chapa 25 za magari. Hakuna hata moja wao aliyofikia viwango vya faragha na usalama ambayo Mozilla ilitumia kulinganisha chapa. Mozilla ilisema kuwa magari yalikuwa "aina ya bidhaa mbaya zaidi walizochunguza katika suala la faragha."
Kulingana na ripoti hiyo, kampuni za magari zinahifadhi haki ya kukusanya maelezo ikiwa ni pamoja na jina lako, umri, rangi ya ngozi, uzani, taarifa za kifedha, sura ya uso, mielekeo ya kisaikolojia na kadhalika.
Kwa mfano, sera ya faragha ya Kia inasema kwamba kampuni inaweza kukusanya taarifa hata kuhusu "maisha yako ya ngono" na afya kwa ujumla.
Msemaji wa Kia James Bell anashikilia kuwa kampuni hiyo haijawahi kukusanya data kuhusu maisha ya kimapenzi au afya zao.
Bell anabainisha kuwa sababu ya maelezo haya kujumuishwa pekee katika sera ya faragha ya Kia ni kwa sababu kampuni inayaorodhesha chini ya ufafanuzi wa hali ya California wa "data za siri."
Bell anasisitiza kuwa kanuni za faragha za Kia ni wazi na kwamba kampuni hushiriki data na makampuni ya bima kwa ridhaa ya wenye magari . Hata hivyo, kampuni haijabaini ni aina gani za "data nyeti" inazokusanya.

Chanzo cha picha, Serenity Strul/ Getty Images
Magari yamewekwa sensa katika sehemu ambazo huwezi kufikiria.
Iwe ni kwenye viti, kwenye dashibodi, kwenye injini, kwenye usukani, yaani karibu kila mahali. Kwa mfano, magari mengi yana kamera ndani na nje.
Ikiwa unafanya kitu kwenye toleo la kisasa la gari mpya, kuna uwezekano mkubwa wa makampuni kujua kulihusu.
Mozilla ilisema kuwa kampuni 19 za magari zimeonyesha kuwa ziko tayari kuuza data, na hilo hasa ndilolinalofanyika.
Nchini Marekani, kampuni ya General Motors (GM) imeshtakiwa kwa madai ya kuuza data ya eneo gari lilipo bila idhini.
Maseneta wa Marekani pia wameishutumu kampuni y aHonda na Hyundai kwa vitendo sawia na hivyo, na hii ni mifano michache tu inayojulikana hadharani.
Hali huenda ni mbaya zaidi
Hali hii inaashiria kwamba kampuni zina uwezo wa kuingilia maisha yako ya kibinafsi wakati mwingine bila hata wewe mwenyewe kujua.
Kwa mfano, General Motors iliuza data ya madereva kwa kampuni ya udalali ya data inayofahamika kama LexisNexis. Kampuni hii hununua na kuuza taarifa kuhusu kuhusu watumiaji magari.
Dereva aliyepata nakala ya data hiyo alidai kuwa LexisNexis ilikuwa na kurasa 130 za data zinazoeleza kila safari ambayo yeye na mke wake walikuwa wameenda ndani ya muda wa miezi sita.
Dereva huyo aliliambia gazeti la New York Times kwamba baada ya malipo yake ya bima kuongezeka kwa asilimia 21, wakala wa bima aliyozungumza naye alisema kwamba takwimu hizo ndizo zilizochangia ongezeko hilo.
LexisNexis haikujibu ombi la kutoa maoni kuhusuiana na ripoti hiyo.
Tume ya Kitaifa ya Biashara ya Marekani ilichukua hatua dhidi ya GM na kampuni hiyo ilipigwa marufuku kuuza data ya gari kwa miaka mitano.
Lakini wataweza kuendelea na zoezi hili baadaye, mradi tu watimize masharti fulani, kama vile kupata idhini kutoka kwa wenye magari.
Huku hayo yakijiri, kampuni kama vile LexisNexis zinaendelea kuuza data wanazokusanya kutoka kwa watengenezaji wa magari na programu ambazo watu hutumia wanapoendesha gari.
GM na LexisNexis hawakujibu ombi letu la kupata kauli yao kuhusiana na hilo.
Makubaliano kati ya makampuni ya bima, watengenezaji magari, na wakala wa data ni ya kawaida, na mradi tu mazoea yamebainishwa wazi katika sera za faragha unazokubali, kila kitu ni halali kabisa.
Michael DeLong, mtafiti wa bima ya magari katika Shirikisho la Wateja la Marekani, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu nchini Marekani, anasema, "Makampuni ya bima hukusanya kiasi kikubwa cha data ya watumiaji, hasa data ya kuendesha gari, na kuitumia kuwatoza watu malipo ya juu zaidi, kuwanyima huduma, au kuainisha wateja katika makundi mbalimbali."
Kampuni za magari zinasema zilipata idhini kabla ya kukufuatilia.
Kwa kawaida, hii inamaanisha kukubaliana na sera za faragha unaposanikisha mfumo wa infotainment au programu za gari lako. Katika baadhi ya magari, haya huonekana kila unapowasha injini. Lakini umezisoma? Bila shaka hujafanya hivyo.
Marekani haina sheria ya faragha ya kitaifa. Ulinzi dhidi ya ukiukaji wa faragha unatofautiana kutoka jimbo moja hadi lingine, kulingana na wataalam wengine, na hii haikidhi mahitaji.
Hali ni sahali barani Ulaya, haswa nchini Uingereza. Kuna ulinzi mahususi kwa aina za taarifa nyeti zinazochukuliwa, na watumiaji wana haki inayowawesha kufikia data zao na kuomba zifutwe kutoka kwa makampuni. Hata hivyo, suala hili bado halijatatuliwa hata huko Ulaya.
















