Kuoga na maji ya barafu hadi kunywa maziwa ya lozi: Siri ya mafanikio ya Mohamed Salah Liverpool

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Neda Hisham
- Nafasi, BBC Arabic
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Wakati mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, alipotangaza kuwa angeondoka klabuni mwishoni mwa msimu, aliyekuwa kocha wake kwa misimu mitano ya kwanza Anfield, Jürgen Klopp, alimwelezea kama mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika mchezo wa soka.
Katika kipindi hicho chini ya Klopp, Salah alifunga mabao 156 na kusaidia Liverpool kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu ya England, Kombe la Dunia la Klabu, UEFA Super Cup na mataji mengine ya ndani.
Hata hivyo, mafanikio ya Salah hayaishii ndani ya uwanja pekee. Safari yake imekuwa chanzo cha hamasa kwa mamilioni ya watu duniani kote, hususan barani Afrika, ulimwengu wa Kiarabu na jamii za Kiislamu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Safari iliyojaa changamoto
Salah alikulia eneo la Nagrig, kijiji cha mbali nchini Misri, na alianza maisha yake ya soka katika klabu ya Kiarabu ya Al-Maqawloun. Kuanzia umri wa miaka 14, angesafiri saa tisa kwa siku kwa basi kwenda treni mjini Cairo.
Njia ya Salah kuelekea kileleni haikuwa rahisi.
Akiwa bado kijana, aliwahi kukaa kwa miezi miwili benchi bila kucheza, jambo lililomvunja moyo.
"Nilikuwa nalia. Nilimwambia baba yangu siwezi kuendelea kukaa benchi kila siku," Salah aliwahi kusema.
Baba yake alimhimiza kuendelea kupambana, akimweleza kuwa mafanikio makubwa huambatana na changamoto kubwa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Wakati huo bado umewekwa akilini mwangu. Nilicheza tena muda mfupi baadaye na kila kitu kilikuwa sawa."
Baada ya miaka kadhaa ya kucheza soka la Misri, hatimaye Salah alihamia Ulaya na kipaji chake na kusaini mkataba na FC Basel katika Ligi Kuu ya Uswisi.
"Tangu siku ya kwanza nilipoondoka Misri kwenda Basel na majaribio, nilijitolea kuwa mchezaji tofauti," Salah alikiambia kipindi cha "Kel Youm" cha TV ya Misri. "Nilitaka kufikia kitu kikubwa, kuvutia umakini, na kuwa mchezaji ambaye watu wangempenda na kumfuata."
Walakini, umaarufu wake huko Uropa haukuja mara moja. Salah hakupata muda mwingi wa kucheza Chelsea na alilazimika kuhamia Serie A, akiichezea Fiorentina na kisha Roma, ambako alijijenga upya kabla ya kurejea England kupitia Liverpool mwaka 2017.
"Ningependa kucheza katika Ligi kuu ya EPL," alisema aliporejea Uingereza na kujiunga na Liverpool. "Nina furaha kurejea na kusisimka. Nitatoa kila kitu kwa ajili ya klabu hii. Nina furaha kuwa hapa na ninataka sana kusaidia timu hii kushinda taji."
"Ukinilinganisha na miaka mitano iliyopita, kila kitu kimebadilika kiakili na kimwili," Salah aliambia BBC Sport katika msimu wake wa kwanza Anfield. "Kila siku najaribu kuwa bora zaidi. Siku zote napenda kujituma ili kuimarika. Soka ni maisha yangu yote na hilo ndilo ninalofikiria."
Miaka tisa baadaye, kama alivyoahidi, aliacha urithi wa nyara nyingi na heshima.
Lakini muhimu zaidi, ilikuwa ni kufikia ndoto aliyokuwa ameieleza alipoondoka Afrika: "Kuwa mchezaji ambaye watu wanampenda."

Chanzo cha picha, Getty Images
Uzuri wa Salah katika msimu wa 2017-18 uliwafanya mashabiki wa Kop huko Anfield kumtengenezea wimbo mpya: "Mo Salah, Mo Salah, Mo Salah, wakiitia kwa kando, Salah, la la, la la, mfalme wa Misri!"
Kauli mbiu iliyoimbwa kwa wimbo "Sit Down" na bendi "James," bendi kutoka Liverpool ambayo inachukuliwa kuwa mpinzani wa jadi wa Manchester katika soka na muziki.
Lakini huo haukuwa wimbo pekee, na bendi ya London ya Doji pia ilihamasisha kauli mbiu na wimbo wao wa "Good Enough," ambao Salah anauita "kitu maalum."
Mashabiki wanaimba, wakirejelea fahari ya Salah katika utambulisho wake wa Kiislamu:
"Kama anafaa kwako, basi anafaa kwangu pia.
Akifunga mabao machache zaidi, nitabadili dini.
Kama anafaa kwako, basi anafaa kwangu pia.
Yuko msikitini, mahali ninapotamani kuwa."

Chanzo cha picha, Getty Images
Siri ya mwili wenye nguvu
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Opta za mwaka 2021, Mohamed Salah ni miongoni mwa wachezaji wenye kasi zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England, akiwa amewahi kufikia mwendo wa kilomita 36.64 kwa saa.
Salah ni winga anayependelea kutumia mguu wa kushoto na mara nyingi huanzia upande wa kulia wa ushambuliaji kabla ya kukata kuelekea katikati, akiwapita mabeki kwa kasi yake kubwa na mabadiliko ya ghafla ya mwendo, kisha kupiga mashuti makali kwa mguu wake wa kushoto.
Hata hivyo, nyota huyo wa Misri hajaridhika na uwezo huo pekee. Kwa miaka kadhaa amekuwa akifanya mazoezi maalum ya kuimarisha matumizi ya mguu wake wa kulia ili kuwa mchezaji kamili zaidi.
"Ninafanyia kazi udhaifu wangu na daima ninajitahidi kuwa bora zaidi," amesema Salah.
Lakini kwa Salah, kazi kubwa huanza anaporejea nyumbani. Anafuata ratiba kali inayojumuisha lishe, mazoezi na programu za urejeshaji mwili.
Mshambuliaji huyo hutumia vifaa vya kisasa vya mazoezi na tiba ya mwili, ikiwemo chumba maalum cha oksijeni ya shinikizo la juu nyumbani kwake, ambacho humsaidia kuharakisha urejeshaji wa mwili na kupunguza uchovu.
"Nina kila kitu nyumbani. Nyumba yangu ni kama hospitali," amesema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbali na kufanya mazoezi ya viungo angalau mara mbili kwa siku na kutumia mabafu ya barafu kupunguza maumivu na uvimbe wa misuli, Salah pia hufanya mazoezi ya yoga na Pilates ili kuongeza unyumbufu wa mwili na kujikinga dhidi ya majeraha.
Kwa upande wa lishe, Salah hufuata mpango mkali wenye protini nyingi na mboga mboga. Kwa kawaida hula milo mitano au sita iliyosawazishwa kwa siku, ikijumuisha mayai, parachichi, brokoli, viazi vitamu, uji wa shayiri, maziwa ya mlozi na matunda.
Huepuka sukari na hutumia mkate wa kahawia usio na gluteni pekee. Hata hivyo, anaporejea Misri bado hupata nafasi ya kufurahia koshari, chakula maarufu cha taifa hilo kinachotengenezwa kwa mchele, dengu na vitunguu vya kukaanga.
Kwa mujibu wa Salah, misuli ya tumbo hujengwa zaidi jikoni, na kula kwa kufuata ratiba ni jambo muhimu kwa mwanamichezo.
Afya ya akili pia ni sehemu muhimu ya mafanikio yake. Salah hutumia dakika 15 hadi 20 kila siku kutafakari kabla ya kulala au mara tu baada ya kuamka ili kuimarisha umakini na kuweka wazi malengo yake.
Aidha, hucheza mchezo wa chess mara kwa mara, akisema humsaidia kuongeza umakini na kuboresha uwezo wa kufanya maamuzi ndani na nje ya uwanja.
Mfalme wa Misri
Mbali na mafanikio yake uwanjani, Salah amekuwa ishara ya matumaini kwa vijana wengi nchini Misri.
mashabiki wengi wakimtaja kuwa "tumaini la kila mtoto wa Misri," jukumu ambalo analichukulia kwa uzito mkubwa.
"Ninataka Wamisri wote wafuate njia niliyopita ili kuwa bora zaidi," aliambia BBC Sport. "Sisi ni taifa kubwa lenye watoto wengi. Ninataka kila mmoja awe na ndoto na aamini kwamba anaweza kufanikisha jambo fulani maishani."
Salah si mtu wa maneno pekee, bali pia wa vitendo. Taasisi yake ya misaada, huwasaidia yatima, wajane, wanawake waliotalikiwa, wagonjwa na familia zenye uhitaji katika kijiji chake cha Nagrig.
Katika Liverpool, amepongezwa kwa taaluma, nidhamu, unyenyekevu na mchango wake katika kuunganisha jamii tofauti za mashabiki.
Akizungumza katika podikasti moja na mashabiki wa Liverpool, aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Jürgen Klopp, alisema:
"Natumaini siku yake ya mwisho klabuni mtakuwa na tabasamu nyusoni mwenu, mkiwa na furaha na shukrani kwa kushuhudia moja ya enzi za kipekee zaidi katika historia ya Liverpool."
Kuhusu uwezo wa Salah wa kufunga mabao, Klopp aliongeza:
"Mo siku zote anawaza kufunga mabao. Hilo si jambo linalofundishwa. Limo ndani yake na litabaki ndani yake maisha yake yote

Chanzo cha picha, Getty Images
Tetesi za hatma ya Salah zinaendelea kujadiliwa
Huku safari yake Liverpool ikifikia tamati, maswali kuhusu hatua inayofuata katika maisha ya soka ya Mohamed Salah yanaendelea kuzua mjadala mkubwa.
Mwaka 2023, iliripotiwa kuwa Liverpool ilikataa ofa ya dola milioni 200 kutoka kwa Al-Ittihad ya Saudi Arabia kwa ajili ya kumsajili nyota huyo wa Misri.
Mbali na Al Ittihad, klabu nyingine kubwa za Ligi Kuu ya Saudi Arabia, zikiwemo Al Hilal, Al Ahli Saudi FC na Al Nassr, zimehusishwa na nia ya kumwania mshambuliaji huyo.
Chaguzi nyingine zinazotajwa ni kuhamia Ligi Kuu ya Marekani (MLS), kucheza katika Ligi Kuu ya Uturuki au hata kurejea Italia, ambako aliwahi kung'ara akiwa na Fiorentina na Roma.
Katika ngazi ya timu ya taifa, kutwaa taji la Africa Cup of Nations bado ni miongoni mwa ndoto kubwa ambazo Salah hajazitimiza. Pia anatarajiwa kuiongoza timu ya kitaifa ya Misri katika kampeni ya 2026 FIFA World Cup, akilenga kufika hatua za mtoano.
Iwapo atafanikiwa kufanya hivyo, atakuwa amebakiza wiki chache tu kutimiza miaka 34. Kwa kuzingatia mtindo wake wa uchezaji unaotegemea kasi, nguvu za mwili, mbio za ghafla na kupenya nyuma ya mabeki, wengi wanaamini itakuwa changamoto kuendelea kudumisha kiwango cha juu kilichomweka miongoni mwa wachezaji bora duniani kwa zaidi ya muongo mmoja.
Hata hivyo, kwa mamilioni ya mashabiki wake duniani kote, Salah ataendelea kubaki kuwa "Mfalme wa Misri" bila kujali atachezea klabu gani siku zijazo.
Shabiki mmoja kutoka kijiji cha Nagrig, alikozaliwa Salah, alieleza hisia za wengi kwa kusema:
"Daima tutampenda na kumuunga mkono Mohamed Salah, popote atakapokwenda na kwa klabu yoyote atakayochezea."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












