Mahakama yamzuia Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua dhidi ya CHADEMA

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Babati, Manyara, imetoa amri ya muda inayomzuia Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua yoyote dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ikiwemo kukifuta, kukisimamisha au kukitoza faini, hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kuamuliwa.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji I.C. Mugeta katika shauri la Miscellaneous Cause No. 12812 of 2026, lililofunguliwa Mei 2026 na Katibu Mkuu wa CHADEMA pamoja na wadhamini wa chama hicho dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika maombi yao, waombaji waliiomba Mahakama kutoa ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya kimahakama pamoja na amri ya muda ya kuzuia hatua zozote dhidi ya chama hicho wakati kesi ikiendelea.
Chanzo cha Mgogoro
Mgogoro huo umetokana na barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya tarehe 7 Mei 2026, iliyokitaka CHADEMA kueleza sababu za kwanini kisichukuliwe hatua kwa madai ya kukiuka masharti ya usajili wa vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, CHADEMA ilitakiwa kuwasilisha majibu yake kabla ya tarehe 20 Mei 2026 saa 9:30 alasiri. Hata hivyo, mawakili wa chama hicho walidai kuwa kulikuwa na viashiria kuwa uamuzi dhidi ya chama tayari ulikuwa umefikiwa kabla hata ya majibu yao kusikilizwa.

Chanzo cha picha, chadema
Mawakili hao walidai kuwa katika suala hilo Msajili ndiye mlalamikaji, shahidi na wakati huo huo ndiye anayetarajiwa kutoa uamuzi, hali ambayo, kwa mujibu wao, haiwezi kutoa haki ya msingi kwa upande unaolalamikiwa.
Katika uamuzi wake, Jaji Mugeta alisema Mahakama imezingatia uwezekano wa madhara ambayo yanaweza kutokea iwapo hatua dhidi ya CHADEMA zitaruhusiwa kuendelea kabla ya kesi kusikilizwa.
“Nakubali kutozwa faini kunaweza kulipwa kwa kurejesha fedha, kwa kuwa haiwezekani kutabiriwa adhabu itakayotolewa endapo Msajili hatoridhika na maelezo ya CHADEMA. Mizania ya haki kwa uzito ipo kwa waombaji wa amri,” alisema Jaji Mugeta.
Aidha, alieleza kuwa kusimamishwa kwa usajili wa chama kunaweza kusababisha madhara makubwa yasiyoweza kufidiwa.
“Kusimamishwa kunaweza kuwa chaguo pia. Hasara itakayopatikana kutokana na kusimamishwa itakuwa isiyoweza kupimika kiasi kwamba hakuna aina ya fidia inaweza kupunguza hasara,” alisema.
Jaji Mugeta aliongeza kuwa Mahakama imeona ni bora kutoa amri ya muda ili kulinda hali iliyopo hadi kesi itakaposikilizwa kikamilifu.
“Hivyo kwa usawa wa urahisi, usajili wa CHADEMA ukisitishwa, itapata tabu zaidi dhidi ya hasara kutokana na kuzuiwa kwa amri inayoomwa kuliko itakavyokuwa kwa wajibu maombi kutokana na muombaji kupewa amri,” alisema.


















