Rare Earth: Je, madini haya yataleta maajabu Tanzania?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Hayang'ai kama dhahabu. Hayana mvuto wa kipekee kama Tanzanite. Kwa wengi, hata jina lake linaweza kuonekana geni.
Lakini katika zama ambazo dunia inakimbilia magari ya umeme, nishati safi na akili mnemba (AI), madini haya yamekuwa miongoni mwa rasilimali zinazotafutwa zaidi duniani.
Yanajulikana kama Rare Earth Elements (REEs)- kundi la madini 17 yenye uwezo mkubwa wa kuendesha teknolojia nyingi za kisasa.
Kuanzia simu za mkononi hadi mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo, vifaa vya hospitalini hadi mifumo ya kisasa ya ulinzi wa kijeshi, madini haya yamekuwa sehemu ya msingi wa mapinduzi mapya ya teknolojia duniani. Na sasa Tanzania imeingia kwenye ramani ya madini hayo.
Katika kijiji cha Mkiu, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Tanzania inatajwa kuwa na hifadhi kubwa ya madini ya Rare Earth, hususan Neodymium (Nd) na Praseodymium (Pr), madini yanayotumika katika teknolojia zinazobadilisha uchumi wa dunia.
Ugunduzi huo umeifanya Tanzania kuwa sehemu ya ushindani mpya wa kimataifa unaoendelea chini ya ardhi, lakini ambao athari zake zinaonekana katika kila kona ya dunia.
Tanzania katika ramani ya Rare Earth duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Tanzania imeanza kujitokeza kama moja ya maeneo muhimu zaidi ya Rare Earth barani Afrika wakati dunia ikihangaika kutafuta vyanzo vipya vya madini hayo yanayotumika katika teknolojia za nishati safi na akili mnemba.
Kwa mujibu wa tathmini za kijiolojia za mwaka 2025, Tanzania inakadiriwa kuwa na takribani tani 887,000 za hifadhi ya Rare Earth Oxide (REO), huku rasilimali zake za madini hayo zikizidi tani milioni 3.3. Kiwango hicho kinaifanya nchi kuwa miongoni mwa maeneo muhimu zaidi ya Rare Earth barani Afrika.
Miongoni mwa miradi inayovutia zaidi macho ya wawekezaji ni Ngualla, uliopo mkoani Songwe. Taarifa za mradi zinaonyesha kuwa eneo hilo lina zaidi ya tani milioni 214 za rasilimali za Rare Earth, jambo linaloufanya kuwa miongoni mwa miradi mikubwa na yenye ubora wa juu zaidi duniani.
Umuhimu wa Ngualla unaonekana pia katika kiwango cha uzalishaji kinachotarajiwa. Mgodi huo unatarajiwa kuzalisha takribani tani 37,200 za makinikia ya Rare Earth kila mwaka kwa zaidi ya miaka 20. Kati ya uzalishaji huo, wastani wa tani 1,800 za oksidi za Neodymium na Praseodymium (NdPr) zinatarajiwa kupatikana kila mwaka.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, mradi wa Ngualla umewekwa miongoni mwa miradi ya kimkakati ya taifa na unatarajiwa kuchimbwa kwa kipindi cha miaka 30 kupitia Kampuni ya Mamba Minerals Corporation Limited (MMCL), ubia kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji binafsi.
Lakini wakati macho ya wengi yakiwa yameelekezwa Songwe, tafiti mpya zimefungua ukurasa mwingine katika Mkoa wa Njombe.
Katika kijiji cha Mkiu, Wilaya ya Ludewa, watafiti wamebaini uwepo wa Neodymium na Praseodymium, madini yenye mahitaji makubwa katika soko la dunia kutokana na matumizi yake katika teknolojia za nishati safi. Ugunduzi huo umeifanya Serikali kuitaja Njombe kama kitovu kipya cha uwekezaji wa Rare Earth nchini.
Kwa wataalamu wa sekta ya madini, uwepo wa Ngualla mkoani Songwe na ugunduzi mpya wa Mkiu mkoani Njombe unaonyesha kuwa Tanzania si mwenye mradi mmoja tu wa Rare Earth, bali inaweza kuwa miongoni mwa nchi muhimu zaidi za Afrika katika ugavi wa madini yanayohitajika kuendesha teknolojia za karne ya 21.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa nchi nyingi zinazozalisha Rare Earth, mtihani mkubwa haupo katika uchimbaji pekee. Upo katika uwezo wa kusafisha na kuongeza thamani ya madini hayo. Kwa sasa China ndiyo inayotawala sehemu kubwa ya usafishaji wa Neodymium na Praseodymium duniani, hali inayofanya ushindani wa kimataifa kuhusu madini hayo kuendelea kuongezeka.
Kwa nini dunia inayapigania?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kadri dunia inavyopunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuongeza matumizi ya nishati safi, mahitaji ya Rare Earth yanaongezeka kwa kasi.
Kinachoyafanya kuwa muhimu si wingi wake, bali uwezo wake wa kutengeneza sumaku maalumu na vifaa vinavyotumika katika teknolojia za hali ya juu.
John Mavrogenes, Profesa wa Jiolojia ya Kiuchumi katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia, anasema madini hayo yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya binadamu wa kisasa.
"Madini haya yanaweza kutoa nishati katika uzalishaji wa umeme wa upepo, gari lako la umeme, lifti ya ghorofa na friji," anasema.
Katika ulimwengu wa leo, magari ya umeme, mitambo ya upepo, simu za kisasa, kompyuta, vifaa vya hospitali, mifumo ya mawasiliano, rada na teknolojia za akili mnemba hutegemea madini hayo.
Kadri dunia inavyopunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuelekea kwenye nishati safi, mahitaji ya Rare Earth yanaendelea kuongezeka.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), matumizi ya Rare Earth katika utengenezaji wa sumaku maalumu za kudumu (permanent magnets) ndiyo eneo linalokua kwa kasi zaidi na kwa sasa linachangia takribani asilimia 95 ya thamani yote ya matumizi ya madini hayo duniani.
Sumaku hizo, zinazotengenezwa kwa kutumia neodymium na praseodymium, ndiyo moyo wa teknolojia nyingi za kisasa ikiwemo magari ya umeme, mitambo ya upepo, roboti za viwandani, vituo vya data vya akili mnemba, vifaa vya anga na mifumo ya ulinzi.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kutokana na umuhimu huo, IEA inaeleza kuwa mahitaji ya madini hayo yameongezeka mara mbili tangu mwaka 2015 na yanatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya theluthi moja ifikapo mwaka 2030 kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya magari ya umeme, nishati safi na teknolojia za kidijitali.
Mchumi Beatrice Kimaro anaamini Tanzania ina nafasi ya kunufaika na mabadiliko hayo ya dunia ikiwa itawekeza katika kuongeza thamani ya madini hayo.
"Tanzania inapaswa kuitumia vyema fursa ya uwepo wa madini haya. Yanaweza kubadilisha maisha ya wananchi wake kwa haraka," anasema.
Lakini pamoja na umuhimu wake huo, si kila nchi inaweza kuyachimba na kuyasafisha kwa urahisi.
Kwa sasa China ndiyo nguvu kubwa zaidi katika mnyororo wa thamani wa Rare Earth duniani.
Kwa mujibu wa IEA, mwaka 2024 China ilichangia asilimia 60 ya uzalishaji wa madini ya Rare Earth yanayotumika kutengeneza sumaku za kisasa duniani, huku ikihusika na asilimia 91 ya usafishaji wa madini hayo.
Katika utengenezaji wa sumaku maalumu zinazotokana na Rare Earth, China inakadiriwa kuzalisha zaidi ya asilimia 90 ya bidhaa hizo duniani.
Hali hiyo imeifanya Marekani, Ulaya na mataifa mengine kutafuta vyanzo vipya vya madini hayo ili kupunguza utegemezi wao kwa nchi moja.
Katika mbio hizo mpya, Afrika imeanza kuvutia zaidi. Na Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotajwa kuwa na nafasi muhimu katika ramani hiyo.
Je, Tanzania itanufaika?

Chanzo cha picha, Peak Resources/Japhet Fungo
Pamoja na matumaini makubwa yanayoambatana na Rare Earth, swali muhimu bado linasalia: Je, Tanzania itanufaika kwa kiwango kinacholingana na thamani ya rasilimali zake?
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali, Adam Anthony, anasema changamoto kubwa kwa nchi nyingi zenye madini ya kimkakati si kuyapata, bali kuyapa thamani.
"Kwenye mjadala wa sasa, jambo kubwa si kuchimba tu. Ni kuangalia nchi za Afrika zenye madini kama haya zinawezaje kuongeza thamani badala ya kusafirisha malighafi," anasema.
Kwa mujibu wa Adam, sehemu kubwa ya faida ya madini ya Rare Earth hupatikana katika hatua za usafishaji, uchakataji na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na madini hayo. Hapo ndipo mataifa mengi yenye rasilimali nyingi yamekuwa yakikosa sehemu kubwa ya thamani ya uchumi wa madini hayo.
Serikali ya Tanzania inaeleza kuwa imeanza kuweka msingi wa kuhakikisha hali hiyo haijirudii.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anasema Serikali imekamilisha Mkakati wa Uongezaji Thamani Madini unaolenga kuhamisha sekta kutoka kuuza madini ghafi kwenda kuuza madini yaliyoongezewa thamani ndani ya nchi.
"Serikali itahakikisha Watanzania wananufaika na madini mkakati na madini muhimu," anasema.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali pia inaendelea kujenga kituo cha jiolojia kitakachotoa mafunzo na huduma za kitaalamu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Rare Earth inaipa Tanzania nafasi mpya ya kuingia katika moja ya masoko muhimu zaidi ya karne hii, kuvutia uwekezaji, kujenga viwanda, kuhamisha teknolojia na kuandaa kizazi kipya cha wataalamu.
Lakini pia ni mtihani. Uwepo wake na faida yake itapimwa kwa ajira zitakazozalishwa, ujuzi utakaopatikana, viwanda vitakavyojengwa na maisha yatakayobadilika.
Ndipo itakapojulikana kama Rare Earth itafailikuwa hadithi nyingine ya utajiri uliokuwa chini ya ardhi, au mwanzo wa sura mpya ya maendeleo ya Tanzania katika karne ya 21.














