Maandamano Senegal dhidi ya gharama ya juu ya maisha
Mamia ya watu waliingia mitaani jijini Dakar siku ya Jumamosi kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Katika maandamano hayo, yaliyoandaliwa na kundi la "30 Jours pour le Juste Prix" (ikimaanisha "Siku 30 kwa Bei Sahihi"), waandamanaji walibeba vyombo tupu vya jikoni huku wakipiga kelele za "Stop à la cherté de la vie" (komesheni gharama ya juu ya maisha).
"Maandamano haya ni kwa ajili ya bei nafuu, na kupinga gharama kubwa za maisha zisizoelezeka nchini Senegal.Umeme, kodi za nyumba, mafuta, chakula, imekuwa vigumu kumudu maisha," alisema mmoja wa washiriki.
Wanatumai kuwa baada ya siku hizo 30, mamlaka zitachukua hatua madhubuti kushughulikia malalamiko yao.
Katika kikao cha baraza la mawaziri mapema wiki hii, Rais Bassirou Diomaye Faye alisisitiza umuhimu wa kudhibiti bei za kodi za nyumba.
Serikali ya Senegal pia iliondoa marufuku ya uingizaji wa vitunguu nchini humo katika jitihada za kushusha bei.
Hata hivyo, kwa waandamanaji, hatua hizo bado hazitoshi. Kwa upande chanya, serikali imefikia makubaliano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu mpango mpya wa mkopo wa dola bilioni 2.2 (euro bilioni 1.9).
Mpango huo wa miezi 36 unalenga kusaidia mageuzi ya kiuchumi na kifedha kati ya mwaka 2026 na 2029, lakini bado unahitaji kuidhinishwa na bodi ya utendaji ya IMF.