'Mzozo unatokota': Mauaji ya polisi ni sehemu ya vurugu zinazoendelea Ukingo wa Magharibi

    • Author, Paul Adams
    • Nafasi, Mwandishi wa BBC wa masuala ya kidiplomasia
    • Akiripoti kutoka, Tubas, West Bank
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati gari nyeupe lilipokaribia ofisi ya Polisi wa Forodha wa Palestina huko Tubas, mji wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, Abdel Nasser Sarhan hakuwa na sababu ya kuwa na shaka.

Kulingana na wafanyakazi wenzake Abdel Nasser, dereva wa gari hilo alitoka nje na kumsalimia kwa Kiarabu.

Ilikuwa ni asubuhi na mapema. Polisi aliyevalia sare mwenye umri wa miaka 24 ndio mwanzo alikuwa amekalisha zamu.

Picha za CCTV zinamuonyesha akitoka nje na kupita kituo cha walinzi, bunduki yake ikining'inia upande mmoja.

Sekunde chache baadaye, mwanamume aliyevalia suruali ya jeans na fulana nyeusi anatokea upande wa lile gari jeupe, askari wa Israel waliovalia sare wakiwa nyuma yake.

Ananyanyua bastola na kumpiga risasi Abdel Nasser.

Muda mfupi baadaye, barabara imejaa askari wa Israel. Wanachukua bunduki ya Abdel Nasser na, huku wenzake wakijaribu kuuchukua mwili wake, wanaendelea kufyatua risasi - yite haya yamenaswa kwenye kamera ya CCTV.

Asubuhi iliyofuata tulipotembelea eneo hilo mwishoni mwa Julai, tulipata mawe na maua yaliyonyauka mahali ambapo Abdel Nasser alianguka.

kituo cha walinzi na kuta zilizo karibu zilikuwa zimejaa matundu ya risasi, kila moja ikiwa na alama ya njano. Madoa ya damu yaliyokauka yalitapakaa ardhini na mlangoni.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya tukio, jeshi la Israel lilisema ufyatuaji risasi huo ulitokea wakati wa operesheni ya kuwazuilia watu wawili waliokuwa wakisakwa.

Wenzake Abdel Nasser mjini Tubas walisema watu hao walikamatwa katika nyumba iliyo karibu.

Jeshi lilisema kuwa wanajeshi "walikutana na magaidi wenye silaha" na kwamba "afisa wa forodha wa Mamlaka ya Palestina aliuawa wakati wa kufyatulianaji wa risasi".

Kutokana na ushahidi wa video za CCTV, taarifa hii ya mwisho ni ya uwongo inayodhihirishwa.

Afisa wa usalama wa Israel aliyewasiliana na BBC wiki mbili baadaye alisema tukio hilo lilikuwa "moja ya mamia, ikiwa si maelfu ya shughuli maalum ambazo zimepangwa na kutekelezwa kwa usahihi".

Hii ilikuwa ikikaguliwa, alisema, "kwa sababu haikuenda kama ilivyopangwa".

Inaonekana wazi kuwa hii ilikuwa operesheni ambayo ilienda vibaya.

Hakuna aliyeashiria kuwa Abdel Nasser au ofisi ya forodha ndio walikuwa walengwa wa operesheni hiyo.

Mlinzi huyo mchanga alikuwa na bahati mbaya ya kujikuta katika operesheni ya siri ya Israel, ambapo alipigwa risasi na kuuawa.

Lakini kwa wafanyakazi wenza wa Abdel Nasser katika idara ya forodha, tukio hili la kusikitisha ni sehemu ya mwelekeo mpana wa mienendo ambayo inafanya kuwa vigumu zaidi kuliko hapo awali kwa Mamlaka ya Palestina - ambayo kinadharia inawajibikia usalama katika maeneo ambayo hayako chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa kijeshi wa Israel - kufanya kazi yake. .

"Hili ni onyo, haswa kwetu sisi tunatoa huduma za usalama," Lt Ibrahim Ayyash, msemaji wa Polisi wa Forodha wa Palestina, alituambia.

"Tunawezaje kutekeleza sheria na kutoa huduma kwa watu na kuwalinda wakati unavuruga kazi yangu na kuua maafisa wangu?"

Maafisa wa forodha, walisema, walikuwa wakizidi kusita kuyaegesha kando magari wanayotiliwa shaka, kwa hofu ya kuwatatiza wanajeshi wa Israel wanaofanya kazi kisiri.

"Sasa ni jukumu lako, kama afisa wa forodha, kuchukua uamuzi wa kusimamisha gari au la," alisema.

"Ukisimamisha gari na [ndani] kuna Vikosi Maalum wanaweza kukuua."

Kama mashabiki wa kipindi cha televisheni cha Israel Fauda watakavyojua, shughuli za siri tayari zilikuwa ni jambo la kawaida katika Ukingo wa Magharibi hata kabla ya vita vya Gaza kuanza Oktoba mwaka jana.

Ushahidi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba mara kwa mara operesheni kama hizo zimeongezeka, huku visa vingi vya picha za CCTV zikionyesha vitengo vya Israel, wakiwa wamevalia kama raia, na hata madaktari, wakiwakamata Wapalestina wanaotafutwa katika mitaa ya jiji na kwenye vitanda vya hospitali.

Lakini shughuli hizo za siri ni sehemu ya picha kubwa zaidi.

Macho yote yakiwa yameelekezwa Gaza, vita vingine vinaendelea katika Ukingo wa Magharibi, huku jeshi la Israel likikabiliana na makundi yenye silaha ambayo inasema yanafadhiliwa na Iran.

"Hali ya mashinani ni ngumu sana," afisa wa usalama wa Israel aliniambia, kwa sharti la kutotajwa jina.

"Unaweza kusema kwamba mzozo unatokota."

Kuibuka kwa kizazi kipya cha vikundi vyenye silaha vya ndani, haswa katika kambi za wakimbizi za kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, kulianza karibu 2021, na kundi la kwanza likitokea Jenin.

Lakini vita vya Gaza vimechochea moto wa uasi katika miji mingine, kutoka Tulkarem hadi Qalqilya na, hivi karibuni zaidi, Tubas.

Ukandamizaji wa usalama wa Israel, vitendo vya kijeuri vya makundi ya walowezi wa Kiyahudi na imani kwamba Mamlaka ya Palestina haina uwezo wa kuwalinda umeongeza hali ya mvuano.

"Wamekasirishwa sana na Israel, wamechoshwa sana na Mamlaka ya Palestina na wanatafuta njia ya kujinasua," afisa wa usalama wa Israel alisema.

Wizara ya afya ya Palestina inasema zaidi ya Wapalestina 600 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi tangu Oktoba iliyopita. Takriban 10,000 wamekamatwa, kulingana na Jumuiya ya Wafungwa wa Palestina.

Takriban Waisrael 17, wakiwemo maafisa 12 wa vikosi vya usalama, pia wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Baadhi ya waangalizi wa zamani wanahofia kwamba mapigano ya kutumia silaha yanaweza kuzuka na kuwa uasi kamili, au intifada.

"Ikiwa itaingia kwenye intifada, hili ni tatizo kubwa zaidi," Jenerali Israel Ziv, mkuu wa zamani wa Kitengo cha Uendeshaji cha IDF, aliniambia.

"Kijeshi, tunashughulikia mambo vizuri au mbaya zaidi. Lakini inapoingia kwenye intifada, ni hadithi tofauti kabisa. Na inaweza kuelekea huko."

Huku jeshi la Israel bado likiangazia vita huko Gaza na mzozo unaoendelea kati yake na Hezbollah kwenye mpaka wake wa kaskazini, Jenerali Ziv alisema wanasitasita kutambua hatari karibu na nyumbani.

"Ni tatizo kubwa ambalo linaweza kulipua usoni mwetu katika eneo nyeti zaidi, [karibu] na vituo vya wakazi nchini Israel," alisema.

Huku hayo yakijiri, katika kambi ya wakimbizi ya Balata, pembezoni mwa Nablus, familia ya Abdel Nasser bado ina majonzi.

Wametazama picha za CCTV kutoka Tubas na kujiridhisha kuhusu vitendo vya kikatili vya jeshi la Israel.

"Alikuja kuua, kuua tu," mjomba wake Abdel Nasser, Ismail Mohammed Sarhan, anasema.

Baba yake Abdel Nasser, Mohannad, ameshindwa kuhimili uchungu wa kumpoteza mwanawe.

Alikuwaje, nikamuuliza.

“Mwenye maono, mwenye fadhili, anayetabasamu kila wakati,” alisema, akishindwa kuzuia machozi.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi