Mtangazaji wa televisheni wa Misri, Sarah Khalifa, na watu
wengine 11 wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya
makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa gazeti la serikali la al-Ahram, walikuwa sehemu ya
genge la uhalifu lililoingiza nchini humo malighafi zinazotumika kutengeneza
dawa za kulevya kwa nia ya kuziuza.
Pia walipatikana na silaha haramu na risasi. Khalifa, mwenye
umri wa miaka 39, anajulikana zaidi kwa kipindi chake cha televisheni kiitwacho
Mission Impossible, ambacho kiliangazia masuala ya uhalifu.
Amekanusha mashtaka hayo. Washitakiwa wengine tisa wamehukumiwa
kifungo cha maisha jela, huku saba wakiondolewa mashtaka na kuachiwa huru.
Wakili wa Khalifa alisema atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ya
kifo. Hukumu hiyo ilitangazwa kwa mara ya kwanza mwezi uliopita.
Hata hivyo, ilithibitishwa mwezi mmoja baadaye baada ya mahakama
kupata maoni ya kidini kutoka kwa Mufti Mkuu wa Misri,hatua ambayo ni sharti la
kisheria katika kesi zinazohusisha hukumu ya kifo.
Wakati wa kesi hiyo, mahakama ilielezwa kuwa mamlaka zilikuwa
zimekamata zaidi ya kilo 750 za dawa za kulevya pamoja na malighafi zilizokuwa
zimeingizwa nchini kwa ajili ya kuzitengeneza.
Mashahidi ishirini walitoa maelezo kwa waendesha mashtaka,
gazeti la *al-Ahram* liliripoti, sambamba na ushahidi wa kielektroniki uliotia
ndani mazungumzo na video.
Kwa mujibu wa gazeti la serikali la *Akhbar al-Youm*,
alipoulizwa na jaji kuhusu madai ya kuhusika kwake wakati wa kusikilizwa kwa
kesi hiyo mwezi Septemba mwaka jana, Khalifa alisema hakuwahi kuona dawa zozote
za kulevya hadi pale alipopigwa picha akiwa nazo ndani ya ofisi za mamlaka ya
kupambana na dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty International ya mwaka 2025,
kulikuwa na hukumu 492 za kifo katika mwaka huo, ambapo 23 kati yake
zilitekelezwa.
Washitakiwa walipatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya
na ubakaji, makosa ambayo "hayakufikia kiwango cha 'mauaji ya makusudi',
ambayo ndiyo kigezo pekee kinachoruhusu matumizi ya adhabu ya kifo kwa mujibu
wa sheria na viwango vya kimataifa," ripoti hiyo ilisema.