Tanzania inavyoufanya mtihani wa diplomasia ya dunia

Chanzo cha picha, URT
Tanzania imewahi kupitia nyakati ngumu katika historia yake. Vita ya Kagera mwaka 1978, baa la njaa la 1974, na mvutano wa kisiasa Zanzibar mwaka 2001 ni baadhi ya vipindi vilivyokuwa na majaribu makubwa kwa nchi hiyo.
Lakini matukio ya siku na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 yakafungua sura mpya kabisa, si ya mgogoro wa ndani pekee, bali mtihani katika diplomasia ya kimataifa.
Kwa mara ya kwanza, mjadala haukubaki ndani ya mipaka ya nchi. Ulikuwa wa dunia.
"Nchi hii mara hii imepitia mambo ambayo hatujawahi kupitia toka mwaka 1961," anasema Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Thabit Kombo.
Kwa mujibu wa Tume ya Jaji Othman Chande, watu 518 walipoteza maisha na 2,390 kujeruhiwa katika ghasia za baada ya uchaguzi.
Lakini nyuma ya takwimu hizo kulikuwa na hoja hii: Tanzania itauvuka mtihani huu kidiplomasia na kulinda uhusiano wake na dunia bila kudhoofisha maendeleo yake?
Ziara ya Rais Samia Hassan Suluhu nchini Urusi, na ile ya rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam alipotembelea Tanzania, zikajenga mzizi wa mjadala huu wa namna Tanzania inavyoufanya mtihani huu.
Dunia ilipoanza kuuliza maswali

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 uliompa ushindi wa asilimia 97% Rais Samia, Tanzania ilijikuta katikati ya mjadala wa kimataifa kuhusu demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kamati za Bunge la Ulaya zilipitisha azimio lililopendekeza kusitishwa kwa sehemu ya misaada ya maendeleo kwa Tanzania, likieleza wasiwasi kuhusu mazingira ya kisiasa nchini, japo Serikali ya Tanzani ilijitokeza kufafanua na kusema kwa kila kilichofanyika kilizingatia sheria na Katiba ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Ulaya, Tanzania ilikuwa inatarajiwa kupokea euro milioni 156 (takribani Shilingi bilioni 438) chini ya mpango wa NDICI–Global Europe.
Mchambuzi wa siasa na diplomasia Godwin Gonde anasema maamuzi hayo, ingawa si ya kisheria moja kwa moja, hubeba uzito wa kisiasa na kiuchumi.
"Kazi ya Bunge la Ulaya ni kutoa maoni yenye nguvu ya kidiplomasia, hata kama hayalazimishi kisheria," anasema.
Hata hivyo Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya mambo ya nje ikasema uamuzi huo sio wa mwisho na uhusiano kati ya Tanzania na nchi hiz, uko vizuri:
"Ni muhimu kufahamu kwamba uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi washirika wake, ikiwemo Tanzania, unaendeshwa kupitia Tume ya Ulaya, ambayo ndiyo chombo cha utendaji cha Umoja huo. Kama ilivyo katika mifumo mingi ya kibunge, mapendekezo yanayopitishwa na kamati za kibunge au na Bunge lenyewe huwasilishwa kwa taasisi husika za kiutendaji kwa ajili ya kuzingatiwa na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa,".
Barua 25 na diplomasia ya kurejesha imani

Chanzo cha picha, URT
Mtihani wa Oktoba 29 unaonekana kuzunguka masuala 6 muhimu ya kitaifa, ambayo ni kulinda amani ya ndani, kurejesha na kujenga upya imani ya wananchi na wadau wa ndani na nje, kuhakikisha mwendelezo wa miradi ya maendeleo, kuponya majeraha ya kijamii yaliyotokana na vurugu, kulinda uhuru wa taifa pamoja na kuimarisha diplomasia na uhusiano na mataifa ya nje.
Katika muktadha mpana wa nadharia ya diplomasia, utafiti wa Chuo Kikuu cha Al-Istiqlal, Jericho – Palestina, chini ya Saaida Mohammed, unaonyesha kuwa diplomasia kwa ujumla inajengwa juu ya nguzo kuu nne ambazo ni mawasiliano, mazungumzo, ujenzi wa mahusiano na kulinda maslahi ya taifa. Kwa pamoja, mitazamo hii miwili inaonyesha tofauti kati ya nadharia ya diplomasia na utekelezaji wake katika mazingira ya kisiasa na kijamii.
Katika muktadha huo, Tanzania inaonekana kulazimika kuingia katika diplomasia ya maelezo na mazungumzo kama njia ya kulinda nafasi yake ya maendeleo.
"Baada ya kuapishwa na baada ya kututeua, akanikabidhi barua 25 ambazo nilizipeleka duniani kueleza kilichotokea Tanzania," anasema Waziri Thabit Kombo.
Anasema katika baadhi ya nchi walikuta simulizi zilizosambaa kuhusu Tanzania hazikulingana na taarifa rasmi za serikali. "Taarifa tulizopewa si hizi alizoandika Rais kwa kalamu yake na amesaini. Kuanzia hapo mambo yamebadilika," anasema.
Katika kipindi kifupi, Tanzania inaonekana kuzidisha diplomasia ya uchumi bila kusahau diplomasia ya kinga, ikilenga kuvutia uwekezaji na kurejesha imani ya washirika wa maendeleo wakati huo huo kupunguza migogoro ya kisera na kisiasa.
Wiki hii, Rais wa Singapore Tharman Shanmugaratnam alifanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania, siku chache tu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara muhimu nchini Urusi, ikionyesha mwelekeo wa Tanzania kupanua wigo wa washirika wake wa maendeleo, nje ya mataifa ya Magharibi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mataifa mengine kama Korea Kusini yameidhinisha mikopo nafuu ya takribani dola bilioni 2.5 kwa miradi ya afya, bandari na elimu, na kuitambua Tanzania kama mshirika wa kipaumbele Afrika kwa kipindi cha 2026–2030.
China pia ilikubali msamaha wa deni la takribani RMB milioni 100 (sawa na takribani shilingi bilioni 34), hatua iliyopunguza mzigo wa kifedha kwa serikali na kuimarisha nafasi ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Kwa ujumla, mwelekeo huu unaonyesha Tanzania ikipanua wigo wake wa kidiplomasia, ikijenga mahusiano na washirika wapya wa maendeleo sambamba na kuimarisha yale ya jadi, wakati ambapo baadhi ya mataifa ya Magharibi yanaendelea kutoa mashinikizo kuhusu masuala ya kisiasa na haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, mwelekeo wa sasa ni kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuongeza uwekezaji, kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania na kukuza ushawishi wa nchi katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa mafanikio ya diplomasia hupimwa zaidi kwa matokeo yake ya muda mrefu kuliko idadi ya ziara, mikutano au makubaliano yanayofikiwa.
"Barua 25 ni hatua muhimu ya kidiplomasia kwa sababu zimeipa Tanzania nafasi ya kueleza mtazamo wake kwa dunia. Lakini katika diplomasia, maelezo huwa mwanzo wa safari, imani ya muda mrefu hujengwa na matokeo yanayoonekana. Hapo ndipo mtihani unaoendelea wa Tanzania ulipo," anasema mchambuzi wa masuala ya kimataifa na diplomasia, Salim Amin.
Rwanda, Kenya na somo la diplomasia Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Tanzania si ya kwanza kukutana na mtihani wa aina hii. Afrika imewahi kuona mataifa yakitumia diplomasia kama chombo cha kujenga upya imani ya ndani na kimataifa baada ya migogoro ya kisiasa.
Rwanda, baada ya mauaji ya kimbari ya 1994, ilitumia diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa kujijenga upya na sasa imekuwa mojawapo ya vituo muhimu vya mikutano ya kikanda. Mpaka leo imekuwa mstari wa mbele kujenga diplomasia yake ya uchumi.
Kenya, baada ya machafuko ya uchaguzi wa 2007- 2008, ilitumia maridhiano ya kisiasa na diplomasia ya kimataifa kurejesha utulivu na imani ya wawekezaji.
Kwa mchambuzi wa masuala ya diplomasia na siasa za kimataifa, Amin, Tanzania inaonekana kuingia katika mkondo unaofahamika katika historia ya Afrika.
"Rwanda ilipitia, Kenya ilipitia, hata Zanzibar mwaka 2001 ilionesha aina hiyo ya changamoto. Tanzania nayo inaingia katika njia hiyo, lakini muhimu ni jinsi dunia inavyoitazama na kiwango cha imani kinachojengwa baada ya hatua za mwanzo," anasema.
Utafiti wa Umoja wa Mataifa kuhusu kitu kinaitwa 'preventive diplomacy' unaeleza kuwa mataifa yanaposhindwa kudhibiti migogoro ya kisiasa mapema, athari zake huenea kutoka siasa hadi uchumi na jamii kwa muda mrefu, na hatimaye kuathiri uhusiano wa kimataifa.
Benki ya Dunia inakadiria kuwa gharama ya migogoro ya ndani inaweza kufikia zaidi ya miaka 30 ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) kwa nchi za kipato cha kati, na kuwa kubwa zaidi kwa nchi zilizo katika hatua za chini za maendeleo.
Kwa mtazamo huo, diplomasia haionekani tena kama chombo cha siasa za nje pekee, bali kama kinga ya uchumi wa taifa na maendeleo.














