Tikiti maji lina nguvu sawa na Viagra - Utafiti

Chanzo cha picha, Getty Images
Tikiti maji ni zuri kwa miili yetu, lina faida nyingi za kiafya, lakini watafiti nchini Marekani wamelinganisha tikiti maji na Viagra, dawa inayoongeza hamu ya tendo la ndoa.
Tikiti maji lina kemikali inayoitwa citrulline, ambayo ina sifa zinazofanana na Viagra.
Kulingana na Idara ya Afya ya Uingereza, vigra ni dawa inayotumika kutibu tatizo la kukosa nguvu za kiume kwa wanaume.
Viagra, ambayo pia inajulikana kama sildenafil, awali ilikusudiwa kusaidia moyo kwa sababu kazi yake kuu ni kuboresha mtiririko wa damu kwa kupanua mishipa ya damu.
Viagra husaidia mishipa ya damu mwilini kwa njia ile ile ambayo kemikali asilia ya citrulline inayopatikana kwenye tikiti maji husaidia mishipa ya damu mwilini.
Sitrulline iliyomo kwenye tikiti maji hulegeza mishipa ya damu mwilini ili kuboresha mzunguko wa damu. Mzunguko mzuri wa damu ndio ambao hufanya uume kusimama vizuri, damu ya kutosha inapofika katika mishipa.
Utafiti huu ulifanywa na Kituo cha Maendeleo ya Mboga cha Texas nchini Marekani.
Dkt. Bhimu Patel, aliyeongoza utafiti kuhusu tikiti maji, anasema, "Tunajua kwamba tikiti maji ni zuri kwa mwili. Uchunguzi bado unaendelea kuhusu faida zake zingine. Mambo mengi mazuri yanajitokeza kutokana na matumizi ya tikiti maji."
Faida zingine za tikiti maji

Chanzo cha picha, STEVE EVANS/ WIKIMEDIA COMMONS
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tikiti maji huongeza maji mwilini: Ni muhimu sana kwa mwili wa binadamu kuwa na maji ya kutosha.
Kwa sababu hata upungufu mdogo wa maji mwilini unaweza kusababisha uchovu, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, na shinikizo la damu.
Tikiti maji ni 92% ya maji, mwili unahitaji maji, kwa hivyo ni vizuri kula tikiti maji.
Linatumika kwa kudhibiti uzito: Tikiti maji lina kalori chache, kwa hivyo hata kama utakula tikiti maji jingi, hakuna hatari ya kupata uzito.
Maji mengi yaliyomo hufanya kushiba kwa haraka na kuzuia hisia za njaa au kula kupita kiasi.
Huboresha afya ya ngozi na macho: Rangi nyekundu ya tikiti maji ina virutubisho vingi vya carotenoids. Virutubisho hivi ni muhimu kwa ngozi.
Pia lina vitamini vya beta-carotene, ambavyo huboresha afya ya ngozi na pia huimarisha afya ya macho.
Hupunguza hatari ya saratani na kisukari: Tikiti maji pia lina lycopene, kemikali ambayo mwili huifyonza haraka.
Kuna tafiti kuhusu lycopene zinazoonyesha kuwa kemikali hii hupunguza hatari ya kupata saratani na kisukari.















