Refa wa Somalia ateuliwa kusimamia kombe la UEFA Super Cup 2026

Chanzo cha picha, Getty Images
Refa wa Somalia Omar Artan ameteuliwa kuchezesha UEFA Super Cup ya 2026, wiki chache tu baada ya kunyimwa fursa ya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA kwa sababu alizuiwa kuingia Marekani.
UEFA ilitangaza siku ya Alhamisi kuwa refa huyo mwenye umri wa miaka 34 atasimamia mechi ya ufunguzi wa msimu wa Ulaya kati ya washindi wa UEFA Champions League Paris Saint-Germain na mabingwa wa UEFA Europa League Aston Villa tarehe 12 Agosti mjini Salzburg.
Uteuzi huo unafuatia mashauriano kati ya UEFA na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na unakuja huku kukiwa na uungwaji mkono mkubwa kwa Artan baada ya kuondolewa kwenye Kombe la Dunia.
Artan, ambaye amekuwa kwenye orodha ya waamuzi wa kimataifa wa FIFA tangu 2018, anachukuliwa kuwa mmoja wa maafisa wakuu wa mechi barani Afrika.
Alichaguliwa kuwa mwamuzi bora wa CAF wa Wanaume wa Mwaka 2025 na alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 waliochaguliwa na FIFA kwa Kombe la Dunia la 2026.
Hata hivyo, ndoto yake ya Kombe la Dunia ilizima ghafla alipozuiwa kuingia katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Miami licha ya kusafiri na pasipoti ya kidiplomasia na visa halali ya kuingia Marekani.
Hatua ya Marekani imefanya refa huyo kuungwa mkono kote barani Afrika na kwingineko, huku Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akimtaja Artan kama "ishara ya msukumo kwa kizazi kipya cha Wasomali".
Licha ya kukatishwa tamaa, Artan ameendelea kung’aa.
"Kila kitu kimepangwa kabla," alisema baada ya kurejea Mogadishu. "FIFA iliniunga mkono vyema na walikuwa wakiwasiliana nami hadi nilipofika Mogadishu. Ninawaahidi kuwa nitasimamia Kombe lijalo la Dunia."
Rais wa UEFA Aleksander Čeferin amesema uamuzi wa kumteua Artan kwenye Super Cup ni utambuzi wa uwezo wake wa kipekee na mchango wake katika mchezo huo.
"Omar Artan ni mwamuzi bora kijana lakini tayari mwenye uzoefu, ambaye amejidhihirisha katika ngazi ya juu ya mashindano ya Shirikisho la Soka la Afrika," Čeferin alisema.
"Kandanda inachezwa ili kuwaunganisha watu, na UEFA inataka kuonyesha heshima kwa Omar na ustadi wake bora, jambo ambalo lilimwezesha kuteuliwa kwa heshima. Ninamshukuru rafiki yangu Rais wa CAF Patrice Motsepe kwa kuunga mkono mpango wetu kwa shauku."
Rais wa CAF Patrice Motsepe alielezea uteuzi huo kama wakati wa kujivunia kwa Somalia na bara la Afrika.
Soma zaidi:












