Kombe la Dunia 2026: Wachezaji 10 wenye asili ya Afrika wanaopeperusha bendera za Ulaya

k

Chanzo cha picha, getty

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Siku zinazidi kuyoyoma kuelekea michuano ya kihistoria ya Kombe la Dunia 2026, ambalo litafanyika Amerika Kaskazini katika mataifa matatu ya Marekani, Canada na Mexico.

Mataifa 48 yatashindana katika mashindano hayo katika majiji 16. Kwenye viwanja vya mpira 16. Viwanja 11 viko Marekani, vitatu vipo Mexico na viwili vipo Canada.

Mchezo wa soka kwa sasa unashuhudia mabadiliko makubwa ya vizazi. Wakati miungu ya soka kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakielekea ukingoni mwa ushindani, uwanja umeachwa wazi kwa ajili ya mashujaa wapya.

Labda tukiite kizazi cha dhahabu. Hawa ndio wachezaji nyota 10 wanaotikisa Ulimwengu wa Soka ambao asili yao ni kutoka Afrika, lakini watacheza kwa niaba ya mataifa mengine mbali na mataifa ya Afrika.

Kylian Mbappé (Ufaransa & Real Madrid)

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Kylian Mbappé anahesabika kama mmoja wa wachezaji bora duniani kwa sasa. Alizaliwa Desemba 20, 1998, katika kitongoji cha Bondy mjini Paris, Ufaransa, akitokea kwenye familia ya Kiafrika, baba ana asili ya Cameroon na mama ana asili ya Algeria.

Mbappé alipata umaarufu mkubwa akiwa na klabu ya AS Monaco kabla ya kuhamia Paris Saint-Germain (PSG) kwa ada iliyoweka rekodi. Akiwa PSG, alifunga mabao mengi na kuwa mfungaji bora muda wote wa klabu hiyo.

Katika ngazi ya taifa, aliiongoza Ufaransa kutwaa Ubingwa wa Dunia mwaka 2018 akiwa kijana mdogo, na kufunga magoli matatu katika fainali ya Kombe la Dunia ya mwaka 2022.

Baada ya miaka mingi ya uvumi, Mbappé alihamia Real Madrid ya Uhispania, ambako anaendelea kuandika historia yake kwenye klabu kubwa barani Ulaya.

Lamine Yamal (Uhispania & Barcelona)

l

Chanzo cha picha, PAP/EPA

Kinda huyu alizaliwa Julai 13, 2007, huko Esplugues de Llobregat, Uhispania. Mama yake anatokea Guinea ya Ikweta na Baba yake anatokea Morocco. Yamal ni zao la akademia maarufu ya Barcelona, La Masia.

Akiwa na umri wa miaka 15 tu, alicheza mechi yake ya kwanza ya kikosi cha kwanza cha Barcelona, na kuvunja rekodi karibu zote, za kucheza akiwa na umri mdogo katika klabu hiyo na Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Lamine Yamal alishangaza ulimwengu katika michuano ya Euro 2024, ambapo aliongoza timu ya taifa ya Uhispania kutwaa ubingwa huku akitwaa tuzo ya mchezaji mdogo bora wa mashindano.

Uwezo wake wa kuchanja mbuga na chenga za maudhi, na ukomavu wa maamuzi unamfanya kuonekana kuwa mrithi wa Lionel Messi ndani ya Spotify Camp Nou.

Bukayo Saka (Uingereza & Arsenal)

p;

Chanzo cha picha, Arsenal

Bukayo Saka alizaliwa Septemba 5, 2001, jijini London, Uingereza, kutoka kwa wazazi wenye asili ya Nigeria. Saka ni zao la akademia ya Arsenal (Hale End), na amekuwa ishara ya kufufuka kwa klabu hiyo chini ya kocha Mikel Arteta.

Saka anajulikana kwa nidhamu yake ya hali ya juu, uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao akitokea winga ya kulia.

Licha ya kukumbana na ubaguzi wa rangi baada ya kukosa penati katika fainali ya Euro 2020, alionyesha ustahimilivu mkubwa na kurejea akiwa imara zaidi.

Kwa sasa ni mchezaji muhimu katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza (Three Lions) na nahodha msaidizi wa Arsenal.

Jamal Musiala (Ujerumani & Bayern Munich)

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Akitajwa mara nyingi kwa jina la utani "Bambi" kutokana na chenga zake, Jamal Musiala alizaliwa Februari 26, 2003, huko Stuttgart, Ujerumani.

Baba mwenye asili ya Nigeria, na Mama mwenye asili ya Ujerumani, Bambi alilelewa nchini Uingereza na alichezea timu za vijana za Uingereza kabla ya kufanya uamuzi mgumu wa kuiwakilisha Ujerumani katika ngazi ya timu ya taifa ya wakubwa.

Musiala aliondoka kwenye akademia ya Chelsea mwaka 2019 na kujiunga na Bayern Munich, ambapo alikua kwa kasi ya ajabu na kuwa kiungo mchezeshaji tegemeo wa miamba hiyo ya Bavaria.

Uwezo wake wa kupita katikati ya mabeki kwenye nafasi ndogo unamfanya kuwa mmoja wa viungo washambuliaji hatari duniani.

Alphonso Davies (Canada & Bayern Munich)

k

Chanzo cha picha, Darryl Dyck/Canadian Press

Historia ya Alphonso Davies ni moja ya hadithi za kugusa hisia zaidi kwenye soka. Alizaliwa Novemba 2, 2000, katika kambi ya wakimbizi ya Buduburam nchini Ghana, baada ya wazazi wake kutoroka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia. Familia yake ilihamia Canada akiwa na umri wa miaka mitano.

Davies alionyesha kipaji kikubwa katika klabu ya Vancouver Whitecaps kabla ya kusajiliwa na Bayern Munich mwaka 2019.

Akiwa Ujerumani, alibadilishwa nafasi kutoka winga na kuwa beki wa kushoto mwenye kasi ya umeme.

Davies ameisaidia Bayern kutwaa mataji mengi yakiwemo ya UEFA Champions League na ndiye nahodha na nembo ya soka la timu ya taifa ya Canada.

Michael Olise (Ufaransa & Bayern Munich)

l

Chanzo cha picha, Goal

Michael Olise alizaliwa Desemba 12, 2001, nchini Uingereza. Ana historia ya kipekee: baba yake ni Mnigeria, mama yake ni Mfaransa mwenye asili ya Algeria, na alizaliwa Uingereza. Hii ilimfanya kuwa na sifa za kuchezea mataifa manne tofauti.

Baada ya kung'ara sana katika klabu za Reading na Crystal Palace nchini Uingereza kwa uwezo wake mkubwa wa kupiga krosi na mashuti ya mbali, Olise alihamia Bayern Munich.

Katika ngazi ya kimataifa, amechagua kuiwakilisha Ufaransa, ambapo aling'ara sana kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris na kupandishwa hadi kikosi cha kwanza cha Les Bleus.

William Saliba (Ufaransa & Arsenal)

,

Chanzo cha picha, Arsenal

Alizaliwa Machi 24, 2001, huko Bondy, Ufaransa (mji uleule aliozaliwa Mbappé). Saliba alisajiliwa na Arsenal 2019 akitokea Saint-Étienne lakini alitolewa kwa mkopo mara kadhaa nchini Uingereza na Ufaransa ili kukomaa.

Aliporejea Arsenal, Saliba alijithibitisha mara moja kama mmoja wa mabeki wa kati bora duniani.

Mtindo wake wa uchezaji una sifa ya utulivu mkubwa, kasi, na uwezo wa kusoma mchezo bila kufanya madhambi ya kizembe.

Saliba ambaye mama yake ana asili ya Cemeroon na baba mwenye asili ya Lebanon, ni mhimili muhimu wa ulinzi wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa.

Jules Koundé (Ufaransa & Barcelona)

l

Chanzo cha picha, GettyImages

Jules Koundé alizaliwa Novemba 12, 1998, huko Paris, Ufaransa, na ana asili ya Benin. Alijizolea umaarufu mkubwa alipokuwa akichezea Sevilla ya Uhispania, ambapo alishinda taji la Europa League kabla ya kununuliwa na Barcelona mwaka 2022.

Koundé ni beki wa kisasa mwenye uwezo wa kipekee: anaweza kucheza kama beki wa kati au beki wa kulia.

Pamoja na uwezo wake mkubwa uwanjani akiwa na Barcelona na Timu ya Taifa ya Ufaransa, Koundé pia anafahamika duniani kote kwa mtindo wake wa kipekee wa mavazi nje ya uwanja, na kumfanya kuwa nembo katika mitindo na soka.

Romelu Lukaku (Ubelgiji & Napoli)

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Romelu Lukaku alizaliwa Mei 13, 1993, huko Antwerp, Ubelgiji, kutoka kwa wazazi wenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (baba yake alikuwa mchezaji wa soka pia).

Lukaku ana uzoefu mkubwa wa soka la Ulaya, akiwa amezichezea klabu kubwa kama Anderlecht, Chelsea, Everton, Manchester United, Inter Milan, na AS Roma.

Kwa sasa, Lukaku anakipiga katika klabu ya Napoli nchini Italia chini ya mifumo inayomsaidia kutumia nguvu zake za mwili na uwezo wa kumalizia nafasi za magoli.

Katika ngazi ya taifa, Lukaku ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Ubelgiji, akiwa nguzo imara ya kile kinachoitwa "Kizazi cha Dhahabu" cha Ubelgiji.

Ibrahima Konaté (Ufaransa & Liverpool)

pp

Chanzo cha picha, Anfield

Ibrahima Konaté alizaliwa Mei 25, 1999, huko Paris, Ufaransa, katika familia yenye asili ya Mali. Alilelewa katika vitongoji vya Paris kabla ya kujiunga na akademia ya Sochaux na baadaye kukulia kisoka huko RB Leipzig nchini Ujerumani.

Mnamo 2021, Konaté alihamia Liverpool ya Uingereza, ambako amekuwa ngome imara ya ulinzi akishirikiana na Virgil van Dijk.

Anajulikana kwa kimo chake kirefu, nguvu za mwili, na kasi ya ajabu inayomfanya kuwa ngumu kupitika na washambuliaji wa Ligi Kuu ya Uingereza. Konaté pia ni sehemu muhimu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa.