Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, unawafahamu wanasoka 10 wakongwe zaidi kushiriki katika kombe la dunia
Wanasema ngoma ya vijana haikeshi na utu uzima dawa!
Katika historia ya kombe la dunia, kandanda hujulikana kama ngoma ya vijana.
Hata hivyo kuna baadhi ya wachezaji wamedhihirishia ulimwengu kuwa tajriba ni kipengee muhimu sana katika jukwaa hilo kubwa zaidi la soka la kimataifa.
Wachezaji hawa walishuka ugani na kutoa mchango mkubwa sana kwa timu zao za taifa katika michuano ya kombe la dunia licha ya umri wao.
Hii hapa mifano hai inayodhihirisha kuwa uzoefu na kujituma ni zaidi ya umri.
1. Essam El Hadary
Kileleni ni aliyekuwa mlinda lango wa timu ya Misri, 'mafarao' Essam El Hadary.
Kipa huyu wa zamani wa Misri anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza katika kombe la dunia.
Akiwa ni umri wa miaka 45 na siku 161, kipa huyu alishiriki katika mIichuano yake ya kwanza ya kombe la dunia akivunja rekodi iliyowekwa na kipa wa Colombia Faryd Mondragon aliyekuwa miaka 45.
Alijumuishwa kwenye kikosi cha Misrii dhidi ya Saudi Arabia Juni 25 mwaka 2018.
El Hadary katika mechi hiyo alikuwa nahodha wa misri na pia aliokoa penalti kutoka kwa mchezaji wa Saudia Arabia Fahad Al Muwallad akiwa kipa wa kwanza wa Afrika kuokoa penalti katika michuano ya kombe la dunia.
Ijapokuwa Misri haikufuzu katika raundi ya muondowano, rekodi zake zilimfanya kuwa mmoja ya wachezaji wanaoheshimika zaidi kutoka Afrika.
2. Faryd Mondragon
Mwengine ni kipa wa Colombia Faryd Mondragon, aliingiziwa kwenye timu wakati wa kombe la dunia mwaka 2014 akiwa na miaka 43 na siku 3.
3. Roger Milla
Ukidhani bara la Afrika huwakilishwa na chipukizi pekee la hasha, kuna Roger Milla, mmoja wa washambuliaji bora zaidi kuwahi kutokea katika bara la Afrika.
Yeye ndiye mchezaji bora zaidi kutokea Cameroon.
Katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1990, sogora huyu akiwa na miaka 38 alirejeshwa katika timu ya taifa baada ya kustaafu, alifunga mabao manne katika michuano hiyo, mabao mawili dhidi ya Romania katika hatua za makundi na mawili dhidi ya Colombia katika raundi ya 16.
Ulimwengu wa soka haukuamini miujiza yake akapata umaarufu duniani kote.
Mabao yake yaliisadia Cameroon kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufuzu kwa mara ya kwanza katika hatua za robo fainali ya michuano ya kombe la dunia.
Mnamo mwaka 1994, akiwa na miaka 42 na siku 39, alicheza tena kwenye michuano hiyo na kufunga bao dhidi ya Urusi akivunja rekodi yake mwenyewe kama mfungaji mkongwe zaidi wa michuano hiyo.
Roger Milla pia alijizoela umaarufu mkubwa kwa mtindo wake wa kusherehekea mabao, jinsi alivyokuwa akikimbilia kibendera cha kupiga kona na kupiga densi la kukata mauno.
Alipoulizwa kuhusu mtindo huo alijibu 'sikupanga nilitaka kuchezea tu mashabiki na kuonyesha furaha yangu.
4. Pat Jennings
Kwa wasiomjua huyu pia alikuwa kipa wa Ireland Kaskazini.
Alicheza mechi yake ya mwisho ya kombe la dunia mwaka 1990 dhidi ya Italia akiwa na miaka 40 na siku 292.
5. Peter Shilton
Peter Shilton ni mmoja wa makipa muhimu sana katika historia ya michuano ya kombe la dunia.
Alishiriki katika awamu tatu za mashindano hayo,1982 Kombe la Dunia nchini Uhispania, 1986 Kombe la Dunia nchini Mexico na walifika robo fainali na pia 1990 michuano ya Kombe la Dunia nchini Italia ambapo England ilifika hatua za nusu fainali.
Kwa jumla alicheza mechi 17 za michuano hiyo, rekodi kwa makipa wa England.
Aliweka 'clean sheets 10' yaani alizuiya timu yake kutofungwa bao katika mechi 10, rekodi alioiweka mpaka leo.
Pia atakumbukwa kwa ile mechi dhidi ya Argentina, nusu fainali ya kombe la mwaka 1986 ambapo Diego Maradona alifunga bao kwa mkono lililojulikana kama 'hand of God'.
Bado anasilia na rekodi ya mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi za taifa la England (mechi 125).
6. Dino Zoff
Huyu si mchezaji wa kawaida tu bali ni mshindi wa kombe la dunia.
Ni mmoja wa wachezaji wanaojivunia rekodi za kipekee katika kombe la dunia.
Alishiriki awamu nne za michuano hiyo, kwanza 1970 nchini Mexico, pili 1974 nchini Ujerumani, tatu 1978 nchini Argentina, awamu ya nne ni 1982 nchini Uhispania wakati huu alikuwa nahodha na alishinda michuano hiyo.
Mwaka 1982 kama nahodha wa Italia kushinda kombe hilo akiwa na miaka 40 na siku 133 hivyo kuorodheshwa rasmi kama mmoja ya wachezaji wakongwe zaidi kulishinda kombe hilo.
Ni mmoja wa wachezaji wanaothaminiwa pakubwa katika historia ya kombe la dunia kwa uzoezu wake na uongozi ngangari kwenye timu.
7. Ali Boumnijel
Aliichezea timu ya taifa ya Tunisia dhidi ya Ukraine mwaka 2006 akiwa na miaka 40.
8. Jim Leighton
Alikuwa mchezaji wa Uskwochi na alishiriki kombe la dunia mwaka 1998 akiwa na miaka 39 na siku 334 wakati huo bado akitamba sana mwisho wa soka lake.
9. David James
Wengi wa kizazi cha Millenia wanamtambua huyu mwamba,alikuwa kipa tajika wa timu ya England.
Alicheza katika michuano ya mwaka 2010 nchini Afrika Kusini akiwa na miaka 39 na siku 330 akionyesha utawala wake katikati ya milingoti kwa kushiriki michuano kadhaa ya kombe la dunia.
Kwa Bahati mbaya hakushinda taji ilo
10. Atiba Hutcinso
Alikuwa kiungo wa timu ya Canada na alicheza dhidi ya Morocco mwaka 2022 akiwa na miaka 39 na siku 296, alitajwa kuwa mmoja wa viungo bora kabisa katika historia ya kombe la dunia.
Mwaka huu katika kombe la dunia wapo wachezaji kadhaa wakongwe watakaoshiriki.
Hao ni pamoja na Lionell Mess iwa Argetina miaka 38, Luka Modric wa Croatia miaka 40, Gullermo Ochoa wa Mexico miaka 40, Manuel Neuer wa Ujerumani miaka 40, edin Dzeko wa Bosnia and Herzegovina miaka 40. Neymar wa Brazil miaka 34.
Hata hivyo macho yote yatakuwa na hamu ya kumtazama nguli wa soka Cristiano Ronaldo atakayekuwa mchezaji mkongwe zaidi michuano hii akiwakilisha timu ya Ureno.
Ronalo atakuwa anasaka taji pekee ambalo hajalishinda dunini, Kombe la dunia akiwa na miaka 41.