Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini maambukizi ya kaswende na kisonono yamefikia viwango vya juu barani Ulaya?
Kisonono na kaswende, miongoni mwa maambukizi mengine ya zinaa (STIs), vinafikia viwango vya juu vya rekodi barani Ulaya.
Hili limegunduliwa katika utafiti wa Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (ECDC), ambao unaonyesha kwamba magonjwa yote mawili yalifikia viwango vya juu zaidi katika zaidi ya miaka 10 mwaka 2024.
Kulikuwa na visa 106,331 vya kisonono — ongezeko la 303% tangu 2015 — huku kaswende ikiongezeka zaidi ya mara mbili katika kipindi hicho hicho kufikia visa 45,557.
Shirika hilo la afya lilionyesha kwamba "mianya inayoongezeka katika upimaji na kinga" kwa kiasi fulani inaelezea ongezeko la maambukizi na kutoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.
"Maambukizi haya yanaweza kusababisha matatizo makubwa, kama vile maumivu ya muda mrefu na utasa, na kwa upande wa kaswende, matatizo ya moyo au mfumo wa neva," alisema Bruno Ciancio, mkurugenzi wa kitengo cha Magonjwa ya Maambukizi ya Moja kwa Moja na Yanayoweza Kuzuilika kwa Chanjo katika shirika hilo.
Aliongeza kuwa visa vya kaswende ya kuzaliwa — pale maambukizi "yanapopitia moja kwa moja kwa watoto wachanga, yakisababisha matatizo ya maisha yote" — karibu viliongezeka maradufu kati ya 2023 na 2024.
"Kulinda afya yako ya uzazi ni jambo kunasalia kuwa jambo la msingi. Tumia kondomu na wapenzi wapya au wengi na pia tafuta ushauri wa daktari ukijiona na dalili za maambukizi," aliongeza.
Takwimu zinasemaje
Uhispania ilirekodi idadi ya juu zaidi ya visa vilivyothibitishwa vya kisonono na kaswende miongoni mwa nchi za Ulaya zilizoshiriki utafiti huo mwaka 2024, ikiwa na visa 37,169 na 11,556 mtawalia.
ECDC ilibainisha kuwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao bado ndio kundi lililoathirika zaidi kwa kiwango kikubwa, likiwa na ongezeko kubwa la muda mrefu la kisonono na kaswende.
Pia iliripoti ongezeko kubwa la kaswende miongoni mwa wanawake wa jinsia tofauti walio katika umri wa kupata watoto.
Ingawa clamidia iliendelea kuwa maambukizi ya bakteria yaliyoripotiwa zaidi kwa jumla, visa vilipungua kwa 6% tangu 2015 hadi kufikia 213,443.
Uingereza haikushiriki katika utafiti huo tangu nchi hiyo ilipojiondoa katika Umoja wa Ulaya, ingawa serikali huchapisha takwimu zake kwa England kila mwaka.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Usalama wa Afya wa Uingereza iliyochapishwa Desemba, kulikuwa na visa 71,802 vya kisonono na visa 9,535 vya kaswende nchini England mwaka 2024.
Katika kipindi hicho hicho cha miezi 12, visa 168,889 vya klamidia viligunduliwa.
Uingereza ilianzisha chanjo ya kisonono mwaka 2025 baada ya visa kufikia rekodi ya 85,000 mwaka 2023.
Dalili ni zipi
Dalili za kisonono zinaweza kujumuisha maumivu, ute usio wa kawaida, na uvimbe wa sehemu za siri, ingawa katika baadhi ya matukio hakuna dalili zinazoonekana.
Ugonjwa huo unaweza kuzuiwa kwa kutumia kondomu ipasavyo na kupata chanjo ikiwa inapatikana, kulingana na mfumo wa afya ya umma wa Uingereza (NHS).
Dalili za kaswende ni pamoja na vidonda karibu na sehemu za siri na mdomoni, vipele mikononi, kupotea kwa nywele, na dalili zinazofanana na za mafua.
Mwanzoni huwa vigumu kugundua na zinaweza kuonekana na kutoweka kadri muda unavyopita.
Kama kisonono, unaweza kuzuiwa kwa kutumia kondomu na kutibiwa kwa kutumia antibiotiki.
Vyote viwili vinaweza kusababisha matatizo makubwa ikiwa havitatibiwa.
Kwa nini maambukizi ya zinaa yameongezeka barani Ulaya?
Katika ripoti yake, ECDC inaeleza ongezeko kubwa la visa vya kisonono na kaswende barani Ulaya kutokana na mambo kadhaa ya kijamii, kiafya na ya mabadiliko ya maambukizi.
Kwanza, inaelekeza kwenye mabadiliko katika tabia za kingono na mienendo ya maambukizi: ongezeko linalowezekana la idadi ya wapenzi, matumizi pungufu ya kondomu, na mabadiliko katika tabia za kijamii baada ya janga la COVID-19.
Pia inaangazia jukumu la programu za uchumba na kuongezeka kwa muunganiko wa kingono, ingawa inaepuka kuweka uhusiano wa moja kwa moja wa kisababishi.
Wakati huo huo, shirika hilo linakiri kwamba sehemu ya ongezeko inaweza kuelezwa na kuongezeka kwa ugunduzi wa visa.
Linaeleza kuwa katika nchi kadhaa vipimo vya utambuzi, programu za uchunguzi na upatikanaji wa vipimo vya jamii vimepanuliwa, hivyo kuwezesha kutambua maambukizi ambayo hapo awali yangeweza kutoonekana.
Hata hivyo, ECDC inasisitiza kuwa ongezeko linaloonekana — hasa katika kisonono na kaswende — ni kubwa sana na linaendelea kiasi kwamba haliwezi kuhusishwa tu na utambuzi bora.
Ripoti pia inaangazia matatizo ya kimuundo katika kinga na upatikanaji wa huduma za afya, ikisema kuwa nchi nyingi za Ulaya bado zina vikwazo vya kiuchumi na kisheria katika upatikanaji wa vipimo vya maambukizi ya zinaa.
Katika nchi 13, wagonjwa wanapaswa kulipia vipimo vya msingi, na nyingine zinahitaji idhini ya wazazi kwa watoto, jambo ambalo linaweza kukatisha tamaa uchunguzi wa mapema miongoni mwa vijana.
Kwa mujibu wa shirika hilo, hali hii inaambatana na mwitikio usio sawa wa nchi: si zote zilizo na mikakati mahsusi na ya kisasa ya kitaifa kuhusu maambukizi ya zinaa, na baadhi hazikusanyi data ya kutosha kuhusu kinga, chanjo au matumizi ya kondomu.
Jinsi ya kutatua tatizo
Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa kinaonya katika ripoti yake kwamba ongezeko linaloendelea la maambukizi ya magonjwa ya zinaa barani Ulaya linaweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya umma.
Moja ya masula yanayowaumiza vichwa wataalamu kwa kiasi kikubwa ni usugu wa dawa za kuua bakteria, hasa wa kisonono.
Ripoti inaeleza kuwa baadhi ya aina za ugonjwa huu zinaendeleza usugu wa antibiotiki, jambo ambalo linaweza kufanya matibabu yajayo kuwa magumu zaidi na kuongeza hatari ya maambukizi.
Kutokana na hali hii, inapendekeza kuimarisha mikakati ya kitaifa dhidi ya maambukizi ya zinaa na kusasisha mipango iliyopo.
Ripoti pia inapendekeza uratibu bora wa mifumo ya afya ya Ulaya, kupanua upatikanaji wa vipimo vya utambuzi, kuondoa vikwazo vya kiuchumi na kisheria kwa vipimo, na kuboresha ukusanyaji wa data.
Pia inaangazia kama kipaumbele kuimarisha kampeni za kinga kwa vijana na makundi yaliyo hatarini, kwa kusisitiza matumizi ya kondomu, elimu ya ngono na uchunguzi wa mapema.