Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Cuba ni tishio kwa usalama wa Marekani - Marco Rubio

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa Cuba ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani na kuwa hakuna uwezekano wa kuafikiwa kwa makubaliano ya amani kati ya nchi hizo mbili.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Rais Ruto wa Kenya apunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shillingi 10

    Rais wa Kenya William Ruto, ametangaza kupunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shillingi kumi zaidi, katika mabadiliko ya bei ya mafuta yatakayo tangazwa mwezi Juni na Julai.

    Iwapo pendekezo la Rais litatekelezwa, bei ya mafuta ya dizeli itashuka na kufikia shillingi 222.86 au dola 1.72 kutoka shillingi 242.92 (dola 1.87)

    Awali serikali ilikuwa imetangaza kupunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shillingi kumi, huku rais Ruto akilaumu vita eneo la Mashariki ya Kati, kuwa vimechochea kupanda kwa bei ya mafuta.

    Rais Ruto alitoa taarifa hiyo baada ya kukutana na viongozi wa vyama na miungano ya magari ya uchukuzi, ambao walifanya mgomo mapema wiki hii wakilalamikia kupanda kwa bei ya mafuta.

    Viongozi wa muungano wa wamiliki magari ya uchukuzi maarafu matatu, wametangaza kuwa wamesitisha mgomo wao kabisa, baada ya kuafikiana na serikali kufanya mageuzi katika bei ya mafuta na kubadilishwa kwa sera zinazoiendesha sekta hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Madini ya urani yatabaki Iran - Mojtaba Khamenei

    Kiongozi mkuu wa Iran, Mojtaba Ali Khamenei, ametoa agizo kuwa madini ya urani yaliyorutubishwa, hayafai kuruhusiwa kutoka nje ya Iran, shirika la habari la Reuters limeripoti.

    Iran imesisitiza kuwa hawako tayari kusalimisha madini hayo, licha ya Marekani kusisitiza kuwa wanafaa kusitisha mpango wao wa nyuklia.

    Agizo la Mojtaba Khamenei, huenda likalemaza juhudi za kupatikana kwa amani nchini humo kupitia mazungumzo ya amani yanayoendelea.

    Trump aidha amesema hapo jana kuwa, hawataruhusu Iran kumiliki madini hayo au kuendelea na mpango wao wa nyuklia

    Pia unaweza kusoma:

  3. Marekani yasema imepiga hatua katika mazungumzo na Iran

    Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio amesema kwamba anatumai ziara ya mkuu wa jeshi la Pakistan nchini Iran, itasaidia kuendeleza diplomasia ya kumaliza vita, na kusema kuwa wamepiga hatua katika mazungumzo ya kupatikana kwa amani.

    Rubio alielezea kuwa ana matumaini na safari ya maafisa wa Pakistan walioenda Tehran na kusema kuwa safari hiyo itasaidia kuendeleza mazungumzo ya kumaliza vita

    Waziri huyo aidha aliikosoa tena jumuiya ya kujihami ya NATO kwa kutoshirikiana na Marekani katika vita dhidi ya Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Marekani yamuwekea vikwazo Mafwele kwa ukiukaji wa haki za binadamu

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imemuwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Faustine Jackson Mafwele kuingia nchini Marekani.

    Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio imesema kwa kuzingatia taarifa zinazoaminika, Mafwele alihusika katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

    “Mwaka jana, jeshi la polisi liliwakamata, kuwatesa na kuwafanyia ukatili wa kingono raia wa Uganda Agather Atuhaire na raia wa Kenya Boniface Mwangi, waliokuwa jijini Dar es Salaam kufuatilia kesi mahakamani dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Rubio.

    Mwezi Februari mwaka huu kitengo cha uchunguzi cha BBC Africa Eye kilitoa filamu iliyoitwa ‘Hali ya hofu Tanzania’ na kuchunguza juu ya wimbi la matukio ya utekaji Tanzania. Katika filamu hiyo manusura wa matukio hayo wakiwemo Atuhaire na Mwangi walimtaja Mafwele kama mhusika mkuu wa kadhia zilizowafika.

    Jeshi la Polisi na Mafwele hawakuwapa ushirikiano BBC licha ya kutafutwa. Hata hivyo serikali ya Tanzania iliiambia BBC Africa Eye kuwa wawili hao waliingia Tanzania kwa madhumuni ya utalii lakini uchunguzi wa idara ya uhamiaji ukagundua kuwa walikusudia kuhudhuria kesi kinyume na tamko lao la kuingia nchini.

    “Kukamatwa kwao kulifanyika kisheria. Idara ya uhamiaji inakanusha madai yoyote ya makosa,” serikali ya Tanzania iliiambia BBC Africa Eye.

    Unaweza kusoma;

  5. Tutachukua na kuharibu madini ya Urani ya Iran - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza kuwa watachukua akiba ya madini ya urani yaliyorutubishwa kutoka Iran.

    “Tutachukua madini hayo. Hatuitaji, hatuitaki. Huenda hata tukaiteketeza baada ya kuichukua, lakini hatutawaruhusu waitumie au kumiliki madini hayo,” alisema Trump

    Rais huyo aliongezea kuwa Marekani inaendelea na mazungumzo na Iran, na kwamba lengo lake kuu ni kuhakikisha Iran haina silaha za nyuklia.

    “Hatuwezi kuruhusu Iran iwe na silaha za nyuklia. Hatuwezi kuruhusu hilo. Kutakuwa na vita vya nyuklia Mashariki ya Kati, na vita hivyo vitafika huku na hata Ulaya.Hatuwezi kuruhusu hilo litokee. Na halitatokea,” aliongezea Trump.

    Shirika la habari la Reuters liliripoti awali kuwa, Kiongozi Mkuu wa Iran alitoa agizo la kutoruhusu madini ya Urani yaliyorutubishwa kutolewa nje ya nchi hiyo.

    Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema vita vya Iran havitamalizika hadi Iran iondoe akiba yake ya urani iliyorutubishwa, ikome kuziunga mkono makundi yaliyojihami na isitishe mradi wake wa kutengeneza makombora.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Umati wenye ghadhabu wachoma moto hospitali ya Ebola eneo la Ituri, DRC

    Umati wenye hasira ulichoma moto sehemu ya hospitali inayowashughulikia wagonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya familia na marafiki wa kijana aliyefariki katika hospitali hiyo kuchukua mwili wake kwa nguvu kwa ajili ya mazishi.

    “Walianza kurusha mawe. Hata walichoma mahema yaliyokuwa yakitumika kama wodi za kuwahifadhi wagonjwa waliotengwa,” mwanasiasa wa eneo hilo, Luc Malembe, aliiambia BBC kuhusu tukio lililoshuhudiwa katika Hospitali Kuu ya Rwampara.

    Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji.

    Mwili wa mtu aliyefariki kutokana na Ebola huwa na uwezo mkubwa wa kueneza ugonjwa huo, hivyo mamlaka hulazimika kuhakikisha mazishi yanafanyika kwa njia salama ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

    Wahudumu wa afya katika hospitali ya Rwampara, iliyoko karibu na mji wa Bunia katika jimbo la Ituri, ambako karibu visa vyote vya Ebola vimeripotiwa, wapo chini ya ulinzi wa jeshi huku polisi wakijaribu kurejesha utulivu eneo hilo.

    Jean Claude Mukendi, anayesimamia uratibu wa usalama dhidi ya ugonjwa Ebola eneo la Ituri, amesema kuwa kijana huyo aliyefariki alikuwa maarufu katika jamii hiyo na watu waliokuwa wameghadhabishwa na kifo chake hawaelewi hatari wa ugonjwa huo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Cuba ni tishio kwa usalama wa Marekani - Marco Rubio

    Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio amesema kuwa taifa la Cuba ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani, na kuwa hakuna uwezekano wa kuafikiwa kwa makubaliano ya amani kati ya nchi hizo mbili.

    Kauli hiyo imejiri siku moja tu baada ya Marekani kumshtaki rais wa zamani wa Cuba, Raúl Castro, kwa kosa la mauaji kuhusiana na kuangushwa kwa ndege mbili mwaka wa 1996, tukio lililosababisha vifo vya raia wa Marekani.

    Aidha Rubio alisema kuwa, Washington bado inatumia njia ya diplomasia kutatua tofauti kati yao na Cuba ila akaonya kuwa “Rais Trump ana haki na wajibu wa kuilinda Marekani dhidi ya tishio lolote”

    Rubio pia aliishutumu Cuba kuwa miongoni mwa wafadhili wakuu wa ugaidi, madai ambayo Waziri wa Mambo ya kigeni wa Cuba Bruno Rodríguez ameyakanusha vikali kupitia mtandao wa X.

    Rodríguez alimshutumu Rubio kwa kusema uongo na kwa kujaribu kuchochea uvamizi wa kijeshi, huku akiilaumu serikali ya Marekani kwa kutaka kuishambulia Cuba kimakusudi.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Ijumaa ya leo