CHADEMA vs Msajili, vita vya panzi au mgogoro wa mfumo?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kwa takribani miaka kadhaa sasa, uhusiano kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umekuwa ukichukua sura ya mvutano wa mara kwa mara. Kila kipindi kipya cha kisiasa kinaonekana kuzaa barua mpya, onyo jipya au hatua ya kinidhamu inayolenga chama hicho kikuu cha upinzani.

Katika siku za karibuni, barua nyingine imeibuka tena, ya Mei 7, 2026, Msajili akikikitaka CHADEMA kujieleza kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kusimamishwa au kutozwa faini kwa madai ya ukiukaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Hii si mara ya kwanza kwa hatua kama hizi kuchukuliwa dhidi ya vyama vya siasa hasa CHADEMA, jambo linalozidi kuchochea mjadala mpana kuhusu nafasi ya Msajili katika mfumo wa vyama vingi.

Wakati baadhi wakiona hatua hizi ni utekelezaji wa sheria na nidhamu ya vyama vya siasa, wengine wanaziona kama mwendelezo wa "kuandamwa kwa upinzani", hasa CHADEMA. Ndani ya mjadala huu, hoja za pande zote zimegusa masuala nyeti ambayo yamekuwa yakizunguka midomoni kila uchwao: Mamlaka ya Msajili, uhuru wa vyama, na mipaka ya usimamizi wa demokrasia.

Lakini swali kubwa linaloulizwa na wengi ni hili: Je, haya ni matukio ya kawaida ya kisheria au ni dalili za mgogoro wa kimuundo kati ya mdhibiti na wale anaowadhibiti?

Uhusiano wa paka na panya

Kuna uhusiano wa kipekee baina ya Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa Tanzania na vyama vya siasa, hasa vya upinzani vikiongozwa na CHADEMA.

Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Msajili ana jukumu la kusimamia, kuelimisha na kuhakikisha vyama vinafuata sheria. Kimsingi, ni nafasi ya "mlezi" wa mfumo wa vyama vingi.

Hata hivyo, katika vitendo, msimamo huu umeonekana kuchukua sura ya udhibiti mkali zaidi, ikijumuisha kutoa onyo, kusitisha ruzuku, na sasa hata kuzungumzia uwezekano wa kusimamisha usajili wa chama.

Wapinzani na wanaharakati wamekuwa wakikosoa sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2024, inayompa Msajili nguvu kubwa ya kuingilia mambo ya ndani ya vyama.

Tangu ukiwa katika hatua za mswaada, asasi za kiraia pia ziliikosoa sheria hiyo. Kundi lililojumlisha Twaweza, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Baraza la habari Tanzania (MCT), Centre for Strategic Litigation, Chama cha Waandishi wa Habari wa Maendeleo Zanzibar na Tanganyika Law Society lilisema sheria hiyo itakwenda kubadili majukumu ya msingi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Madai yao yanajikita kusema Ofisi hiyo imetoka kuwa"msajili" mpaka kuwa "mdhibiti" na hapo ndipo mwanzo wa mahusian ya paka na panya yanapoanzia kati ya ofisi hiyo na vyama vya upinzani hasa CHADEMA.

Wachambuzi wanaotetea msimamo wa Msajili wanasema hii ni "nidhamu ya lazima" kwa vyama vinavyokiuka sheria. Kwa mtazamo huo, CHADEMA huonekana kama chama kinachorudia makosa ya kinidhamu na hivyo kuhitaji kusimamiwa kwa ukaribu zaidi.

Lakini upande wa pili unaona picha tofauti, unaona kwamba Msajili amegeuka kutoka mlezi kuwa "mdhibiti mkali", na kwamba mamlaka yake yanatumiwa kwa namna inayovuka mipaka ya usimamizi wa kawaida wa vyama.

Kwa nini CHADEMA kila siku na sio CCM?

Swali linalorudi mara kwa mara ni kwa nini hatua mara nyingi zinaelekezwa CHADEMA kuliko vyama vingine?

Ofisi hiyo imekuwa ikijibu hoja hiyo kwa kusisitiza kuwa sheria inatumika kwa wote bila upendeleo.

"CCM tunawaandikia barua sana na huwa wanajibu… wanakuja kuomba radhi na wanawakemea makada wao.", anasema Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Bwana Sisty Nyahoza, alipozungumza na moja ya chombo cha habari cha ndani Tanzania.

Hata hivyo, upinzani unaona tofauti. Kwao, ukali wa hatua dhidi ya CHADEMA, ikiwemo kusimamishwa kwa ruzuku hapo awali na sasa tishio la kusimamishwa usajili au kufutwa, unaashiria hali ya upendeleo au matumizi ya sheria kwa namna inayobeba uzito wa kisiasa.

Katika mjadala huu, chama cha ACT Wazalendo pia kimeingia kwa nguvu, ikitaka msajili asitishe kile ilichokiita "vitisho dhidi ya vyama vya upinzani".

"Msajili anajua, Watanzania wanajua na Dunia inajua kuwa Kuna ushahidi wa kutosha wa CCM kufanya makosa makubwa kuliko hata ambayo Msajili ameituhumu CHADEMA, hatukuwahi kuona hatua zozote zimechukuliwa na Ofisi hii ya Msajili, Ofisi ya Msajili ijue Watanzania sio mabwege tunachukulia tishio lolote dhidi ya CHADEMA ni tishio dhidi ya Demokrasia", anasema Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kupitia mtandao wa X.

"Msajili afanye anachokitaka" - CHADEMA

'Vita' hivi vitaisha lini? Ni swali linalotawala wanaofuatilia siasa za Tanzania.

Kwa mtazamo wa wachambuzi wa siasa, mvutano wa Ofisi ya Msajili na CHADEMA na sasa ACT- Wazalendo inataka kuingia, unaakisi tatizo la muda mrefu, muundo. Muundo wa ofisi hii na majukumu yake umezaa mgogoro wa kimfumo na mipaka kati ya usimamizi na udhibiti wa vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa sheria, Msajili ana mamlaka makubwa, ikiwemo kusitisha shughuli za chama au hata kufuta usajili katika mazingira fulani. Pia Msajili anateuliwa na Rais ambaye ni Mwneyekiti wa CCM, hivyo mgongano wa maslahi unachukua sura yake.

Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), kiliwahi kupendekeza " Ili kuepuka mgongano wa maslahi, Msajili anapaswa kuandaa miongozo kwa vyama vya siasa kusimaia shughuli zake za utendaji bila yeye (Msajili) kuingilia".

Baadhi ya wataalamu wanapendekeza mageuzi ya sheria ili Msajili awe zaidi "mlezi" kuliko "mdhibiti", na ili kuwe na mifumo huru zaidi ya kusimamia migogoro ya vyama.

Katika mjadala huu, kauli za mwanasiasa mkongwe Zitto Kabwe zimezua mjadala zaidi. Kupitia mtandao wa X, alisema: "Zama za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa mchezaji namba moja wa CCM zimeisha… Watanzania sio mabwege."

CHADEMA yenyewe inasema kinachoendelea dhidi yao ni kile wanachokiita, Ofisi ya Msajili kutaka chama hicho kiache kuzungumzia masuala ya mauaji, wizi, deni la taifa, ukosefu wa ajira, ili kuzungumziwa ofisi hiyo.

"Sisi tumekataa kumzungumzia Msajili, afanye anachokitaka", anasema John Heche, Makamu mwenyekiti wa CHADEMA.