Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Korea Kusini yaitaka Iran kuonesha msimamo wake kuhusu shambulio dhidi ya meli ya mafuta katika Mlango bahari wa Hormuz

Afisa mmoja wa Korea Kusini hapo awali alisema kuwa kuna uwezekano mdogo sana kwamba shambulio hilo lilifanywa na nchi nyingine tofauti na Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Korea Kusini yaitaka Iran kuonesha msimamo wake kuhusu shambulio dhidi ya meli ya mafuta katika Mlango bahari wa Hormuz

    Korea Kusini imeitaka Iran kueleza msimamo wake kuhusu shambulio la hivi karibuni dhidi ya moja ya meli zake za mafuta karibu na Mlango Bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini, Waziri wa Mambo ya Nje Cho Hyun alizungumza kwa simu na mwenzake wa Iran, na Seoul pamoja na Tehran zitaendelea kuwasiliana na kushauriana ili kuhakikisha usalama wa Mlango wa Hormuz.

    Afisa mmoja wa Korea Kusini hapo awali alisema kuwa kuna uwezekano mdogo sana kwamba shambulio hilo lilifanywa na nchi nyingine tofauti na Iran.

    Kwa mujibu wa maafisa wa Seoul, meli ya mizigo HMM Namo ilipigwa na “makombora mawili yasiyotambulika” tarehe 4 Mei.

    Shambulio hilo liliharibu meli hiyo na kusababisha moto katika chumba cha injini.

    Meli hiyo ilikuwa ikisafiri chini ya bendera ya Panama na inaendeshwa na kampuni ya usafirishaji ya Korea Kusini, HMM.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini ilitangaza Ijumaa, Mei 15, kwamba imeirejesha meli hiyo iliyoharibiwa nchini humo.

    Unaweza kusoma;

  2. Mkenya apinga ongezeko la bei ya mafuta mahakamani

    Kufuatia tangazo la kuongezeka kwa bei ya mafuta ya Petroli nchini Kenya mnamo Mei 14, Mkenya mmoja kwa jina Francis Awino amewasilisha kesi katika mahakama kuu akiiomba mahakama hiyo kusimamisha utekelezwaji wa tangazo la mamlaka ya kudhibiti bei ya mafuta na kawi nchini EPRA.

    Awino ameishtaki mamlaka hiyo kwa pamoja na mawaziri kadhaa nchini humo, akisema kwamba ongezeko la bei ya lita moja mafuta ya Petroli kwa shilingi 16 za Kenya sawia na senti 13 za Dola moja ya Marekani na shilingi 46.3 za Kenya sawia na senti 23 za Dola moja ya Marekani kwa kila lita ya Dizeli ni kiwango cha juu zaidi na itakuw ana Athari kubwa katika kupanda kwa gharama ya maisha.

    Aidha katika kesi hiyo, mlalamishi amesema kwamba taasisi husika hazikufuata sheria na Katiba ya nchi, zimefanya uamuzi ambao unabana zaidi mifuko ya Wakenya ambao tayari wanakabiliana na hali ngumu kiuchumi na hakukuwepo uwazi wowote.

    Kuwasilishwa kwa kesi hiyo mahakamani kunaweka wazi kero la wengi nchini kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha.

    Aidha katika stakabadhi za mahakama, Awino anaiomba mahakama kuiamrisha serikali utaratibu wa jinsi EPRA iliafikia kutangaza ongezeko la bei ya mafuta ya Petroli Mei 14.

    Mapema mwezi Mei, wizara ya biashara na viwanda nchini Kenya ilitangaza kwamba mafuta ya Petroli ambayo viwango vyake vya Sulphur vipo juu itakubaliwa kuuzwa nchini imetajwa katika kesi hiyo, huku mlalamishi akisema kwamba hatua hiyo inatishia kuchafua mazingira, kuharibu magari na kuchangia maradhi mbali mbali mwilini mwa binadamu.

    Haya yanajiri wakati ambapo wahudumu wa uchukuzi wa umma, wametishia kufanya mgomo kuanzia Jumatatu Mei 18, na kuongeza bei ya nauli kwa asilimia 50.

    Unaweza kusoma;

  3. Serikali ya DRC yasema hakuna kesi za Ebola zilizothibitishwa katika mji mkuu

    Serikali kuu ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, katika taarifa iliyotoa Jijini Kinshasa inasema hakuna kesi zilizothibitishwa za ugonjwa wa Ebola ambazo zimerekodiwa katika mji mkuu hadi sasa.

    Wizara ya Afya ya Umma, Usafi na Ustawi wa Jamii ilisisitiza kuwa Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Umma (INSP), kupitia Kituo chake cha Operesheni ya Dharura ya Umma (PHEOC) inasalia kuwa chanzo pekee rasmi cha habari kuhusu dharura za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Ufafanuzi huo unafuatia matamshi ya mapema leo ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO, ambaye alitangaza aina ya Ebola ya Bundibugyo kuwa Dharura ya Afya ya Jamii ya Kimataifa (PHEIC) nchini DRC na Uganda.

    Katika taarifa yake, alibainisha kuwa kisa kilichothibitishwa na maabara kiliripotiwa mjini Kinshasa kinachomhusisha msafiri kutoka Ituri.

  4. Kenya yajiweka katika tahadhari dhidi ya maambukizi ya Ebola

    Wizara ya Afya ya Kenya imetoa taarifa kuhusu mpango wa serikali ya nchi hiyo kukabiliana na maambukizi ya Ebola.

    Katika taarifa hiyo, Katibu Mkuu wa Afya Daktari Patrick Amoth amesema ; ‘ Kenya haijathibitisha wala kurekodi maambukizi ya aina ya Ebola inayofahamika kama NON – ZAIRE, lakini serikali inaangazia kwa akina hali ilivyo katika eneo la Afrika Mashariki na inashirikiana na wizara husika za afya katika mataifa jirani.’

    Kenya imesema kwamba hali ya hatari kwa sasa ni ndogo kwa taifa hilo, ila inaweka mipango ya kuchunguza wasafiri katika vituo vyote vya usafiri, kama vile mipakani, kwenye bandari za Mombasa na Lamu na viwanja vya ndege.

    Shirika la afya duniani WHO limetengaza mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola na kusema kwamba ni hali ya dharura ya afya ya umma ambayo inatishia usalama wa afya duniani.

    Mamlaka nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo zimethibisha kwamba hadi sasa takriban watu 80 wamefariki kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo ambao unasambazwa kupitia maji maji ya mwili wa binadamu.

    Wakati wahudumu wa afya wakikabiliana na mlipuko huu wa 17 nchini DRC, serikali za mataifa jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki, zimeombwa kuchukua kila tahadhari kuchunguza hali afya ya wanaosafiri katika mipaka yao, kujipanga kutoa huduma za matibbau za watakaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo na kuhamasisha jamii kuhusu njia bora ya kujikinga na kutambua dalili za ugonjwa huo.

    Unaweza kusoma;

  5. Rais Ruto auza sera ya mpango wa makazi ya bei nafuu ya Kenya katika mkutano wa kimataifa, Baku

    Rais wa Kenya, William Ruto yupo mjini Baku, Azerbaijan kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa upanuzi wa miji {World Urban Forum} ambapo anatarajiwa kuonesha mpango wake wa ujenzi wa makazi ya bei nafuu kama mojawapo ya njia za kukabiliana na uhaba wa makazi duniani.

    Mpango huo wa ujenzi wa makazi ya bei nafuu aliuanzisha pindi tu alipochaguliwa 2022, ila ulipingwa mahakamani na baadhi ya Wakenya ambao walihisi kuwatoza wafanyakazi kodi ya asilimia 1.5 ya mshahara kufadhili mradi huo ilikuwa kinyume cha sheria.

    Mahakama ilisimamisha mpango huo kwa muda kabla ya bunge kupitisha muswada wa serikali na kuifanya kuwa faradhi kwa wafanyakazi kulipa kodi ya makazi almaarufu {Affordable Housing levy}.

    Kwa mujibu wa wizara ya ujenzi na nyumba, Idara inayosimamia mpango wa ujenzi wa makazi ya bei nafuu imerekodi kwamba nyumba 111,975 zimekamilishwa katika kaunti 47 nchini Kenya, huku wanunuzi wakijiandikisha katika mpango wa Boma Yangu na kulipa pole pole kwa kipindi cha miaka 30.

    Katika kikao cha makazi kinachoandaliwa nchini Azerbaijan kati ya May 17 na 22, Kenya inajiandaa kuonesha jinsi serikali za mataifa mengi duniani zinavyoweza kutumia ufadhili wa ndani kukabiliana na uhaba wa makazi, huku Rais Ruto akisema kwamna kupitia mpango kama wa nyumba za bei nafuu, anakabiliana na makazi duni yaliyopo katika miji kadhaa ikiwemo Nairobi ambapo ina mitaa kadhaa ya mabanda.

    Mkutano wa kwanza wa makazi wa kimataifa uliandaliwa Kenya mnamo 2002.

  6. Habari za hivi punde, Chelsea yamteua Xabi Alonso kuwa kocha Mkuu

    Klabu inayoshirki kwenye Ligi kuu ya England – Chelsea imemteuwa kiungo wa zamani wa klabu ya Liverpool – Xavi Alonzo kukiongoza kikosi chake.

    Alonzo mwenye umri wa miaka 44 na rai awa Uhispania, ametia saini kandarasi ya miaka mitatu na Klabu hiyo iliyopo Jijini London, miezi minane tu baada ya kuagana na Klabu ya Uhispania ya Real Madrid alikokuwa mkufunzi Mkuu.

    Chelsea ambayo imekuwa ikikumbwa na matokeo duni katika msimu wa 2025/26, imesema kwamba ina matumaini makubwa kwamba Alonzo atabadili mambo katika uga wa Stamford Bridge, hasa baada ya kuwa na wakufunzi wakuu wawili msimu huu ambao wote waliondoka baada ya kupata matokeo ya kutoridhisha.

    Chelsea iliwatema Enzo Maresca na Liam Rosenior mapema katika msimu huu, huku Calum McFarlane akihudumu kama Mkufunzi Mkuu wa muda kwa mara ya pili – akitarajiwa kushikilia usukani hadi mwisho wa msimu huu ambao umesalia mechi mbili kukamilika.

    Tangazo la uteuzi wa Alonzo limetolewa siku moja baada ya THE BLUES kushindwa katika fainali ya kombe la FA na Manchester City .

    "Chelsea ni mojawapo ya Vilabu vikubwa duniani na nimejawa na furaha moyoni kwamba nimepewa fursa ya kuwa meneja mkuu wa klabu hii kuu, " alisema Alonso akiongezea kwamba,

    "Katika mazungumzo baina yangu na wamiliki wa Klabu hii, na uongozi wake, ni wazi kwamba tuna maono sawa na azma moja. Sote tungependa kuganga yajao na kuangazia kutia bidi ili kujenga timu ambayo itakuwa na uwezo wa kushinda vikombe."

    Alonzo aliichezea klabu ya Liverpool kwa miaka mitano, na kuchangia ushindi wa kombe la klabu bingwa barani Ulaya UCL mnamo 2005. Aidha kiungo huyo wa kati aliwahi pia kuzichezea klabu za Real Madrid, Real Sociedad na Bayern Munich.

    Aliichezea timu ya taifa ya Hispania, mara 114, na kushinda kombe la dunia na timu hiyo 2010. Alikuwa katika vikosi vya Uhispania vilivyoshinda mashindano ya Ulaya mara mbili.

  7. Venezuela yamtimulia Marekani mshirika wa Maduro ili akayakabili mashtaka ya jinai

    Mamlaka za Venezuela zimemfukuza Alex Saab, mfanyabiashara mwenye uraia wa Colombia na Venezuela pamoja na mshirika wa rais wa zamani Nicolás Maduro, kwenda Marekani siku ya Jumamosi, kulingana na taarifa ya Shirika la Utambulisho, Uhamiaji na Wageni la Venezuela (Saime).

    “Serikali ya Venezuela inatangaza kufukuzwa kwa raia wa Colombia, Alex Naim Saab Morán, kulikofanyika Jumamosi hii, Mei 16, 2026,” Saime ilisema kupitia akaunti yake ya X.

    Katika ujumbe mfupi, shirika hilo lilisema hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu Saab “anahusika katika kutekeleza uhalifu mbalimbali nchini Marekani,” jambo ambalo limesemwa hadharani na kuripotiwa sana.

    Mfanyabiashara huyo wa Colombia, ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda chini ya Maduro, anatuhumiwa na Marekani kwa kusafisha hadi dola milioni 350 za Kimarekani kupitia mfumo wa udhibiti wa fedha za kigeni wa Venezuela.

    Saab alikamatwa mjini Caracas mwezi Februari katika operesheni ya pamoja kati ya mamlaka za Marekani na Venezuela, kwa mujibu wa afisa mmoja wa sheria wa Marekani, Reuters iliripoti.

    Alex Saab alikua mtu muhimu sana nchini Venezuela wakati wa serikali ya Nicolás Maduro. Mwanzoni, alihusika katika miradi ya ujenzi wa nyumba.

    Baadaye, alipewa jukumu la kusimamia usambazaji wa mifuko ya chakula ya “CLAP”, mfumo ulioundwa na serikali ili kudhibiti uingizaji wa bidhaa ambazo baadaye zilisambazwa kwa wananchi kupitia Kamati za Mitaa za Ugavi na Uzalishaji (CLAP).

    Uhusiano wake katika biashara hizo mbili umekuwa ukikosolewa kutokana na madai ya vitendo vya rushwa na ufisadi.

    Kufukuzwa kwa Saab kwenda Marekani ni ishara ya mabadiliko yaliyotokea Venezuela tangu operesheni ya kijeshi iliyofanywa na serikali ya Marekani tarehe 3 Januari, ambapo Maduro na mke wake, Cilia Flores, walikamatwa.

    Unaweza kusoma;

  8. Raia wa Canada kutoka kwenye meli ya kitalii apatikana na Hantavirus

    Raia mmoja wa Canada aliyesafiri kwa meli ya watalii MV Hondius ambayo ilikumbwa na mlipuko wa Hantavirus mwezi Aprili, amepatikana na ugonjwa huo, maafisa wa afya katika jimbo la British Columbia wamesema.

    Mtu huyo alikuwa mmoja wa watu wanne waliokuwa wakijitenga katika kisiwa vya Vancouver baada ya kushuka kutoka melini, na alikuwa ameonyesha dalili za kiwango cha chini.

    Afisa mkuu wa afya wa jimbo hilo alisema kuwa watu hao wanne hawakuwa wamechangamana na umma tangu walipowasili Canada.

    Kisa hicho kinafanya jumla ya maambukizi kufikia watu 11, wote wakiwa abiria wa meli hiyo ya watalii.

    Watu watatu waliokuwa wamesafiri kwenye meli hiyo wamefariki dunia, huku wawili wao wakithibitishwa kuwa walikuwa na virusi hivyo.

    Afisa wa afya wa British Columbia, Bonnie Henry, alisema matokeo ya vipimo vya mtu huyo yalionesha kuwa ana uwezekano mkubwa wa kuwa na maambukizi ya Hantavirus siku ya Ijumaa, ingawa bado yanahitaji kuthibitishwa na maabara ya kitaifa ya microbiolojia.

    “Hili si jambo tulilotarajia, lakini ni jambo tulilokuwa tumejiandaa nalo,” alisema, akikaririwa na shirika la utangazaji la taifa la CBC.

    Dkt. Henry aliongeza kuwa: “Ninataka kusisitiza kwamba hantavirus ni virusi tofauti sana na virusi vingine vya mfumo wa upumuaji ambavyo tumekuwa tukikabiliana navyo, na bado hatuoni kuwa vina uwezo wa kusababisha janga la kimataifa.”

    Unaweza kusoma;

  9. WHO yatangaza mlipuko wa Ebola nchini DR Congo kuwa dharura ya kiafya duniani

    Shirika la Afya Duniani, WHO limetangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika jimbo la mashariki la Ituri nchini DRC ni dharura ya afya ya umma kimataifa.

    Shirika hilo liliongeza kuwa mlipuko huo, ambao una takribani visa 246 vinavyoshukiwa na vifo 80 vilivyoripotiwa, haujafikia kiwango cha kutangazwa kuwa janga la kimataifa.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alionya kuwa kwa sasa kuna “kutokuwa na uhakika mkubwa kuhusu idadi halisi ya walioambukizwa na pia maeneo ambayo ugonjwa umeenea.”

    WHO ilisema aina ya sasa ya Ebola imesababishwa na virusi vya Bundibugyo, ambavyo bado havina dawa au chanjo zilizoidhinishwa.

    Shirika hilo lilieleza kuwa hadi sasa kuna visa vinane vilivyothibitishwa maabara, pamoja na visa vingine vinavyoshukiwa na vifo katika maeneo matatu, yakiwemo Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, pamoja na miji ya uchimbaji dhahabu ya Mongwalu na Rwampara.

    WHO pia iliongeza kuwa virusi hivyo vimeenea nje ya DR Congo, ambapo visa viwili vilivyothibitishwa vimeripotiwa katika nchi jirani ya Uganda.

    Maafisa wa Uganda walisema mwanaume mwenye umri wa miaka 59 aliyefariki Alhamisi alipatikana na virusi vya Ebola.

    Nchi zinazopakana na DR Congo zinaonekana kuwa katika hatari kubwa ya kuenea zaidi kwa ugonjwa huo kutokana na watu kusafiri mara kwa mara, biashara na usafiri kati ya nchi hizo.

    Unaweza kusoma;

  10. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo