Je, nyaya za intaneti chini ya bahari silaha mpya ya Iran?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Vyombo vya habari na makundi yenye misimamo mikali ya kisiasa nchini Iran vinaendelea kuiwasilisha Mlango wa Bahari wa Hormuz si tu kama njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta, bali pia kama njia ya kimkakati ya mawasiliano ya intaneti.

Kulingana na vyombo hivyo vya bahari, uwezo wa Iran kutoa shinikizo, ipo chini ya bahari, kupitia nyaya za kimataifa za intaneti zinazopita chini ya bahari.

Mjadala wa kuharibu nyaya hizo za intaneti umeibuka wakati mzozo kati ya Iran na Marekani unazidi kutokota, baada ya Marekani kuweka kizuizi cha kijeshi katika mlango bahari wa Hormuz.

Kulingana na mtaamo wao, Iran inaweza kuweka udhibiti kwa nyaya hizo za baharini zinazopita eneo hilo.

Ingawa hatua kama hiyo inaweza kukabiliwa na vikwazo vingi vya kisheria na kiufundi, mjadala huu unaonyesha juhudi za Iran za kupanua mbinu zake za kujilinda kwa njia zisizo za kawaida hata kama itaharibu miundombinu nyeti za intaneti.

Je, huu ni mwanzo wa mzozo mpya kuhusu mlango bahari wa Hormuz?

Kwa miongo kadhaa, Mlango wa Hormuz umehusishwa zaidi na meli za mafuta au nishati, kwani takriban 20% ya mafuta yanayosafirishwa kwa njia ya bahari duniani hupitia katika njia hiyo nyembamba.

Shirika la habari la Fars News Agency, ambalo lina uhusiano wa karibu na jeshi la Iran la Islamic Revolutionary Guard Corps, katika ripoti iliyochapishwa mwezi Mei tarhe 8 kupitia ilitoa wazo la kutumia nyaya za intaneti zilizopo chini ya bahari kama silaha na chombo cha shinikizo katika kumaliza mzozo huo.

Nyaya hizo husafirisha mawasiliano ya kimataifa pamoja na data za kifedha kati ya bara la Ulaya, Mashariki ya Kati, na bara Asia.

Kulingana na shirika la Tata Communications, kampuni inayofuatilia miundombinu ya mawasiliano duniani, mifumo mikubwa ya nyaya za mawasiliano kama Falcon, GBI na TGN-Gulf hupitia katika mlango bahari wa Hormuz, na kuwezesha usafirishaji wa data kati ya Ghuba ya Uajemi, Ulaya na bara Asia.

Mfumo wa TGN-Gulf pekee unaunganisha Oman, Falme za Kiarabu, Qatar, Bahrain na Saudi Arabia kwenye mtandao mpana wa mawasiliano ya kimataifa.

Shirika la habari la Fars News Agency pia ilisisitiza kuwa kampuni kubwa za teknolojia kama Google, Meta, na Microsoft zinatumia nyaya hizo zaidi kuliko hapo awali. Kwa mujibu wa chombo hicho cha habari, mifumo ya kifedha kama SWIFT pia hutegemea nyaya hizo za bahari.

Ripoti hiyo ya Fars inasema, "Ikiwa mafuta yalikuwa yanaendesha dunia katika karne ya 20, basi data ndiyo mafuta ya karne ya 21," ikisisitiza kuwa sasa Iran ina ushawishi wa kijiografia kuliko mataifa yote mawili yanayozozana nayo.

Ashreq News, shirika nyingine ya habari yenye ukaribu na jeshi la IRGC, pia kimeeleza mtazamo kama huo kwa kutumia nyaya za chini ya bahari kama "silaha ya Iran" ambayo "inaweza kuiangusha Marekani na washirika wake."

Mjadala huu wan nyaya za bahari unajiri wakati ambao maafisa wa Iran wamekuwa wakitoa onyo mara kwa mara kwamba Iran inahariri upya sera yake ya usalama wa kikanda baada ya kuzishutumu nchi za Ghuba kwa kuunga mkono operesheni za kijeshi za Marekani.

Kwa nini nyaya za chini ya bahari ni muhimu?

Kulingana na taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la Reuters, iliyochapishwa mwishoni mwa mwezi Aprili, takriban asilimia 99 ya mawasiliano ya kimataifa ya intaneti duniani hupitishwa kupitia nyaya za fiber-optic zilizowekwa chini ya bahari.

Kampuni ya utafiti wa miundombinu ya mawasiliano TeleGeography imezitambua AEE-1, Falcon, na Gulf Bridge International kama baadhi ya nyaya zinazofanya kazi na kupita katika mlango bahari wa Hormuz.

Uharibifu wowote katika eneo hilo unaweza kuathiri huduma za intaneti za kikanda, shughuli za benki, pamoja na mitandao ya kibiashara.

Ni nini hasa kinapendekezwa?

Vyombo vya habari vyenye misimamo mikali nchini Iran pamoja na watu wa karibu na serikali havijatoa wito wa kukata au kudhibiti nyaya za chini ya bahari moja kwa moja.

Badala yake, wamesisitiza kuwa watakusanya ushuru na kudhibiti usimamizi wa kidijitali wa eneo hilo

Kulingana na viongozi wa Iran, mlango bahari wa Hormuz ipo ndani ya maji ya eneo la Iran huku sehemu nyingine ikiwa chini ya Oman, na kwa hiyo Tehran inaweza kutumia mamlaka ya kisheria na ya kiutawala juu ya miundombinu kudhibiti nyaya hizo.

Mbunge mmoja wa Iran, aliambia Fars News Agency kuwa wamependekeza hatua kadhaa, ikiwemo kuhitaji vibali kwa nyaya za chini ya bahari, kuweka ada za kupitisha nyaya hizo, na Iran kuhusishwa katika shughuli ya kutengeneza na kukarabati nyaya hizo kwa lengo la kujiongezea mapato.

Nyaya za chini ya bahari kwa kawaida hutengenezwa kwa nyuzi nyingi za fiber-optic ambazo zinapita ndani ya chuma ambayo haiwezi kupata kutu.

Iran ina mamlaka ya kisheria kudhibiti nyaya hizo?

Iran inahoji kuwa ingawa meli za kimataifa zina haki ya kupita katika njia hiyo, hali hiyo "haiondoi mamlaka ya nchi za pwani" juu ya maji hayo.

Hata hivyo, sheria za kimataifa za bahari zinaweza kupinga tafsiri hiyo ya mamlaka ya Iran juu ya miundombinu ya mawasiliano ya kimataifa.

Zaidi ya hayo, mataifa makubwa duniani, yakiwemo Marekani pamoja na nchi za Ulaya, hayatakubali jaribio lolote la Iran kuweka vikwazo au kutoza ushuru wa upande mmoja kwenye miundombinu ya kimataifa ya intaneti.

Pia kuna vikwazo vya kiutendaji. Tofauti na meli, nyaya za chini ya bahari ni vigumu kufuatiliwa muda wote, na zinasimamiwa kupitia makubaliano tata ya kimataifa kati ya serikali na kampuni binafsi.

Hatua yoyote ya makusudi ya kuingilia nyaya hizo inaweza kusababisha hatua kali za kimataifa dhidi ya Iran.

Kwa nini mjadala huu unaibuliwa sasa?

Wazo hili limeibuliwa wakati Iran, imetangaza kuja na mbinu mpya ya ushawishi kupitia mlango bahari wa Hormuz.

Iran pia imetoa onyo kwa majirani zake, kutoendelea kushirikiana na Marekani.

Wazo hili lina uhalisia kiasi gani?

Jaribio lolote la kudhibiti au kutoza ushuru makampuni ya mawasiliano ya kimataifa ya intaneti litakumbana na vikwazo vikubwa vya kiufundi na kisiasa, na linaweza kuizidishia Iran kutengwa kimataifa wakati ambapo uchumi wake tayari unakabiliwa na shinikizo kubwa.

Hatua kama hiyo pia inaweza kuiathiri Iran yenyewe. Uchumi wa nchi za Ghuba ya Uajemi umeunganishwa kwa kiwango kikubwa na intaneti, na usumbufu wowote mkubwa kwenye miundombinu ya nyaya za chini ya bahari unaweza kuathiri pia mawasiliano ya kikanda ya Iran pamoja na biashara yake.