Wakenya wameingiwa na wasiwasi baada ya serikali kuongeza bei ya rejareja ya dizeli kwa Shilingi 46.29 za Kenya kwa lita na petroli kwa Shilingi 16.65 za kenya katika tangazo lililotolea na Mamlaka ya kudhibiti kawi na nishati ya (EPRA).
Jijini Nairobi, Petroli itauzwa kwa shilingi 214.25 za Kenya, wanaotumia dizeli ikiwalazimu kuinunua kwa shilingi 242.92 za Kenya huku watumiaji wa mafuta ya taa kuipata bidhaa hiyo na shilingi 152.78 za Kenya kwa kila lita kuanzia Alhamisi kwa siku 30 zijazo.
Kwa mujibu wa wachangunizi wa kiuchumi, ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza gharama za utengenezaji na usafirishaji, hali inayoweza kusababisha wawekezaji na wafanyabiashara kuongeza bei za bidhaa kwa wanunuzi.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, EPRA imesema bei ya mafuta ya taa haitabadilika katika kipindi cha bei kitakachoanza leo Mei 15 hadi Juni 14, 2026.
Hatua hiyo inafuta nafuu iliyoshuhudiwa mwezi uliopita baada ya serikali kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 13 hadi asilimia 8 kupitia Tangazo la Kisheria Na. 70 la Aprili 15, 2026.
“Katika kipindi hiki cha tathmini, bei ya juu inayoruhusiwa ya petroli imeongezeka kwa Shilingi 16.65 za Kenya kwa lita na dizeli kwa Shilingi 46.29 za Kenya kwa lita, huku mafuta ya taa yakibaki bila mabadiliko,” EPRA imesema.
Mamlaka hiyo ilieleza kuwa ongezeko hilo limetokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa pamoja na gharama kubwa za kuagiza mafuta kutoka nje.
Kwa mujibu wa EPRA, wastani wa gharama ya kuagiza petroli uliongezeka kwa asilimia 10 kutoka dola 823.27 za Marekani kwa mita ya ujazo mwezi Machi 2026 hadi dola 906.23 mwezi Aprili.
Dizeli ilirekodi ongezeko kubwa zaidi la asilimia 20.32, kutoka dola 1,073.82 hadi dola 1,291.98 kwa mita ya ujazo katika kipindi hicho.
EPRA ilibainisha kuwa bidhaa za mafuta katika soko la kimataifa huuzwa kwa dola za Marekani, hivyo huathiriwa na mabadiliko ya bei ya mafuta duniani pamoja na viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni.
Bei hizo pia zinajumuisha VAT kwa mujibu wa Sheria ya ushuru wa thamani VAT, Sheria ya Fedha na viwango vipya vya ushuru wa bidhaa.
Mamlaka hiyo imeongeza kuwa serikali itatumia takriban Shilingi bilioni 5 za Kenya kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Petroli kusaidia kupunguza makali ya ongezeko la bei ya dizeli na mafuta ya taa kwa watumiaji.
Katika kipindi kilichopita, petroli ilikuwa ikiuzwa kwa Shilingi 197.60 kwa lita pesa za Kenya huku dizeli ikiuzwa kwa Shilingi 196.63 za Kenya baada ya kupunguzwa kwa Shilingi 9.37 na Shilingi 10.21 mtawalia za Kenya.
Tangazo hili jipya linajiri wakati soko la mafuta duniani likiendelea kubadilika na huku gharama ya maisha ikiendelea kuongezeka.