Kwa nini nchi za Ulaya zinahamisha dhahabu yao kutoka Amerika Kaskazini?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati benki kuu ya Uholanzi ilipothibitisha wiki hii kwamba ilikuwa imehamisha tani kadhaa za dhahabu kutoka Amerika Kaskazini, ilieleza kwamba hatua hiyo itaifanya iwe "imejiandaa vizuri zaidi kukabiliana na migogoro mikubwa".

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, takribani tani 86 kati ya karibu tani 313 za dhahabu zilizokuwa zimehifadhiwa nchini Marekani na Canada zilihamishwa kwenda London, "kutokana na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na utulivu wa kisiasa duniani", ili dhahabu hiyo ya thamani iweze kuwa "inapatikana kwa urahisi na kutumika katika hali ya mgogoro."

Ilikuwa jambo lisiloepukika kwamba maswali yangeibuka. Kwa nini Waholanzi walifanya hivi? Je, walikuwa wanatarajia mshtuko mkubwa wa kiuchumi unaokuja?

Ingawa huenda isionekane hivyo, hatua hiyo ilikuwa wazi kuwa jibu kwa hali ya kutokuwa na utulivu na kutokuwa na uhakika duniani, ambapo vita vya kibiashara na kijeshi vimesababisha nchi kuchukua tahadhari na kuweka akiba yao ya dhahabu karibu zaidi na nyumbani.

Nyakati za kutokuwa na utulivu

Mwanzoni mwa mwaka huu, Ufaransa ilitangaza kwamba ilikuwa imehamisha akiba yake ya dhahabu kutoka Marekani na kuipeleka katika eneo la Ufaransa.

Wakati huohuo, Benki Kuu ya Ujerumani (Bundesbank) ilihamisha zaidi ya tani 216 za dhahabu kutoka kwenye akiba zake zilizo nje ya nchi kwa kipindi cha miaka kadhaa, hadi mwaka 2016. Kati ya hizo, tani 111 zilitoka New York na tani 105 zilitoka Paris.

Ni mkakati ambao umewahi kutumika hapo awali wakati wa vipindi vya kutokuwa na utulivu duniani. "Baadhi ya benki kuu za Ulaya zilihamisha sehemu ya akiba zao za dhahabu kwenda New York wakati wa Vita Baridi," walisema wachambuzi Lina Thomas na Daan Struyven wa Goldman Sachs.

Joseph Cavatoni, mtaalamu mkuu wa mikakati ya soko katika World Gold Council, aliiambia BBC kwamba ingawa vita na mvutano wa kibiashara "ulikuwa na ushawishi katika baadhi ya maamuzi haya," haukuwa "miongoni mwa sababu zilizopewa kipaumbele zaidi" katika kuamua hatua hizo.

Mfumuko wa bei, viwango vya riba, na pia kuwa na dhahabu katika sehemu ambako inaweza kuuzwa au kununuliwa kwa haraka vilikuwa na mchango katika maamuzi hayo.

"Sina hisia kwamba janga linakuja," alisema Cavatoni, "lakini ninachoamini ni kwamba watu sasa wana taarifa bora zaidi kuhusu jinsi ya kusimamia mali zao za akiba, kuziongeza, na kupata manufaa makubwa zaidi kutokana nazo."

Benki Kuu ya Uholanzi imetangaza kwamba dhahabu iliyotolewa kutoka Marekani na Canada kati ya Machi na Agosti mwaka huu sasa imehifadhiwa katika maghala salama ya Benki ya Uingereza.

"Tunatumaini kwamba hatutawahi kulazimika kuitumia, lakini tunahitaji kuimarisha uwezo wetu wa kukabiliana na hali mbalimbali na maandalizi yetu," alisema gavana wa benki kuu ya Uholanzi, Olaf Sleijpen.

London ilionekana kuwa chaguo bora zaidi kutokana na nafasi yake kama kituo kikuu cha biashara duniani. Ikiwa utahitaji kununua au kuuza dhahabu haraka wakati wa mgogoro, London ni mahali pazuri sana kufanya hivyo. Hivyo, Benki ya Uingereza imekuwa eneo maarufu sana la kuhifadhi dhahabu.

Hifadhi na biashara ya dhahabu

Benki ya Uingereza ni mojawapo ya taasisi kubwa zaidi duniani zinazohifadhi dhahabu kwa niaba ya wengine. Taasisi hii yenye historia ya zaidi ya miaka 300, iliyoko katikati ya London, huhifadhi takriban vipande 400,000 vya dhahabu vyenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 270.

Kwa mujibu wa tafiti za sekta zilizofanywa na World Gold Council, Benki ya Uingereza bado ndiyo sehemu maarufu zaidi kwa ajili ya uhifadhi salama wa metali za thamani, lakini benki kuu zinazidi kutawanya maeneo ambako zinahifadhi dhahabu zao.

Kwa mujibu wa Thomas na Struyven wa Goldman Sachs, mahali ambapo dhahabu ya nchi inahifadhiwa ni "jambo linalozidi kuwa la muhimu kwa wasimamizi wa akiba za taifa."

Katika ulimwengu wa kisasa, kuna njia nyingi za kuhamisha au kusafirisha mali yako ya thamani. Waholanzi waliuza takribani tani 59 za dhahabu huko New York na kisha wakainunua tena London. Hii ilimaanisha kwamba kiasi hicho hakikuhitaji kusafirishwa kuvuka Bahari ya Atlantiki.

Hata hivyo, zaidi ya tani 27 zilisafirishwa kutoka Marekani na Canada hadi mji wa Zeist nchini Uholanzi. Kiasi kinachokaribiana na hicho pia kilisafirishwa kutoka Zeist hadi London.

Kampuni zinazotoa huduma za aina hii huwa hazitoi maelezo mengi kuhusu jinsi shughuli hizo zinavyofanyika. Hata hivyo, ni muhimu kusema kwamba hatua za usalama na mipango inayowekwa ni ya kina sana ili kuzuia hatari ya kutokea kwa tukio kama lile la filamu The Italian Job, ambapo kundi la wahalifu huiba mzigo wa dhahabu wenye thamani kubwa.

Cavatoni kutoka World Gold Council alieleza kwamba mkakati wa kawaida wa kuhamisha umiliki wa dhahabu unahusisha kuuza dhahabu katika eneo moja na kuinunua katika eneo jingine.

"Kwa mfano, tuseme ninataka dhahabu yangu iwe New York lakini iko London. Ninaweza kuiuza London na kuinunua New York siku hiyohiyo na wakati huo huo. Kwa njia hiyo, uhamishaji wa umiliki unarekodiwa bila kuhitaji mabadiliko mengine ya usafirishaji."

Kuna kampuni chache tu zilizochaguliwa zinazoshughulikia usafirishaji wa dhahabu kuvuka mipaka ya nchi. Mojawapo ni Brink's Global Services, ambayo ilIiambia BBC kwamba katika nyakati za hivi karibuni imeona "ongezeko la mahitaji" kutoka kwa taasisi kama vile benki kuu.

"Kutokuwa na uhakika kunakoongezeka katika masuala ya kisiasa duniani na kiuchumi, pamoja na nafasi inayozidi kuwa muhimu ya dhahabu kama mali ya kimkakati ya akiba, inaonekana kuchangia mwenendo huu," alisema Nader Antar, makamu wa rais mtendaji wa Brink's.

Hifadhi ya gharama kubwa

Sababu ya uhifadhi wa dhahabu kuwa suala kubwa sana kwa benki kuu ni kwamba zimekuwa zikiongeza ununuzi wa metali hii ya thamani. Hata hivyo, kuihifadhi ndani ya nchi kuna gharama, kulingana na Thomas na Struyven wa Goldman Sachs.

"Uhifadhi wa ndani unahitaji uwekezaji katika usalama wa kimwili, mifumo ya ukaguzi na bima; gharama ambazo zinaweza kuwa kubwa kupita kiasi kwa benki kuu ndogo," walisema.

Kwa mujibu wa World Gold Council, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, benki kuu zimekusanya wastani wa tani 1,000 za dhahabu kwa mwaka, ongezeko kubwa kutoka wastani wa tani 500 kwa mwaka katika muongo uliotangulia.

Mwenendo huu ulianza wakati wa mgogoro wa kifedha duniani na unatarajiwa kuendelea kuongezeka mwaka ujao.

Dhahabu imekuwa ikipata umaarufu mkubwa katika miaka ya hivi karibuni. Bei yake imepanda na kufikia viwango vipya vya juu zaidi kuwahi kurekodiwa, ikivuka dola za Marekani 5,000 kwa wakia moja mwezi Januari.

Kuna sababu kadhaa zinazoeleza ongezeko hili kubwa la thamani yake, lakini sababu muhimu ni nafasi ambayo metali hii ya thamani inayo katika mtazamo wa binadamu kama mali salama ya kuhifadhi au kuwekeza, hasa wakati wa misukosuko ya kifedha na kisiasa duniani inayosababishwa na vita vya kibiashara na kijeshi.

Mfumuko wa bei na viwango vya riba pia vinaathiri umaarufu wa dhahabu. Kwa sababu dhahabu ni adimu na imepewa thamani kwa maelfu ya miaka, kwa kiasi fulani hustahimili athari za kupanda kwa bei, jambo linaloifanya kuwa uwekezaji mzuri.

Kwa mujibu wa benki ya uwekezaji Charles Schwab, "katika kipindi cha nusu karne iliyopita, bei ya dhahabu imeongezeka kwa kasi kubwa zaidi kuliko Consumer Price Index (CPI), kiashiria kinachofuatiliwa kwa karibu zaidi cha mfumuko wa bei."

Ingawa bei ya dhahabu imeshuka kutoka kiwango cha juu kabisa kilichofikiwa mwanzoni mwa mwaka huu, bado iko katika kiwango cha juu kihistoria.

Kwa mujibu wa watafiti wa Goldman Sachs, bei hiyo inatarajiwa kupanda hadi dola za Marekani 4,900 kwa wakia ya troy kufikia mwisho wa mwaka 2026, ikiwa ni dola 300 zaidi ya bei ya mwezi Agosti.

Kwa mujibu wa Thomas na Struyven, mahitaji ya dhahabu kutoka kwa benki kuu ni mojawapo ya sababu kuu zinazofanya bei ya dhahabu kupanda kwa kasi sana.