Hafidh Ameir ni nani? Mume wa Rais Samia aliyekuwa nyuma ya pazia

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Hafidh Ameir Hassan, mume wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amefariki dunia Septemba 7, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, Hafidh alikuwa akitibiwa ugonjwa wa moyo na alifariki dunia majira ya saa mbili asubuhi.

Akitoa salamu za pole, Makamu wa Rais alisema:

"Ninatoa pole kwa Mheshimiwa Rais, familia, ndugu, jamaa na marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu, na mpango wa mazishi unaendelea kufanyika Kizimkazi."

Lakini licha ya kuwa mwenza wa Rais wa Tanzania, Hafidh Ameir Hassan hakuwa mtu aliyezoeleka kuonekana hadharani.

Kwa miaka mingi, aliishi maisha ya faragha, akiwa mbali na siasa na mwanga wa vyombo vya habari. Hata pale aliposhiriki katika baadhi ya shughuli pamoja na mkewe, hakujitokeza sana.

Rehema Mema, mchambuzi kutoka Zanzibar, anamwelezea Hafidh kama mtu mpole, mkarimu na asiye na tamaa ya kujulikana.

"Ni baba ambaye hapendi kujulikana, mwenye mambo mengi, mpole, mkarimu, asiyependa makuu. Kama angekuwa baba mwingine, tungekuwa tunamfahamu sana."

Kwa Mema, ukimya huo ndio uliomfanya Hafidh kubaki mtu ambaye Watanzania wengi hawakumfahamu kwa undani, licha ya kuwa mume wa mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini.

"Kati ya watu 10, labda mmoja anamfahamu. Hata picha zake mitandaoni huwezi kuzipata. Ameishi sana nyuma ya pazia."

Hafidh alikuwa mtaalamu wa masuala ya kilimo na mstaafu wa taaluma hiyo. Alifunga ndoa na Samia Suluhu Hassan mwaka 1978 na walipata watoto wanne.

Wakati Hafidh akiendelea na maisha yake ya faragha, Samia alijenga safari yake ya kisiasa hatua kwa hatua, kuanzia kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, baadaye kuwa Waziri, Makamu wa Rais, na na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Safari hiyo ya kisiasa ilimuweka Samia zaidi katika macho ya umma, wakati mwenza wake akiendelea kubaki nyuma ya pazia.

Mwaka 2021, Samia alipokuwa Rais wa Tanzania, Hafidh akawa 'First Gentleman' wa kwanza katika historia ya nchi hiyo. Hata hivyo, nafasi hiyo haikumfanya kuwa mtu wa kujitokeza mara kwa mara katika shughuli za Rais.

Kuonekana kwake pamoja na Rais Samia kulikuwa kwa nadra, huku taarifa kuhusu maisha yake binafsi zikiendelea kuwa chache.

Kwa namna hiyo, Hafidh aliishi kwa zaidi ya miongo minne akiwa karibu na mtu mkubwa aliyekuja kuwa Rais, lakini bila kuwa sehemu kubwa ya maisha ya kisiasa yaliyozunguka familia hiyo.

Miongoni mwa watoto wao ni Wanu Hafidh Ameir, mwanasiasa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Makunduchi na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mipango ya mazishi ya Hafidh Ameir inaendelea kufanyika Kizimkazi, Zanzibar.