Kenya yatoa msamaha wa muda kwa raia wa Afrika Mashariki wasio na nyaraka
Serikali ya Kenya imetoa msamaha wa muda kwa raia wa Afrika Mashariki wasio na nyaraka halali, baada ya mamia ya Warundi kufurika katika Ubalozi wa Burundi jijini Nairobi Jumatatu wakitafuta hati za kusafiria, wakihofia kuondolewa nchini kufuatia hatua dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni.
Rais wa Kenya, William Ruto, wiki iliyopita aliagiza kufungwa kwa biashara zote ndogo ndogo zinazoendeshwa na raia wa kigeni kuanzia Jumatatu, baada ya kukutana na wafanyabiashara wa Kenya waliokuwa wakipinga marekebisho ya kodi.
Wizara ya Biashara ya Kenya baadaye ilifafanua kuwa agizo hilo linawahusu raia wa kigeni wanaofanya biashara bila vibali vya kufanya kazi.
Hatua hiyo ilisababisha sintofahamu nje ya Ubalozi wa Burundi Jumatatu, huku baadhi ya Waburundi wakisema walitishiwa na majirani tangu Rais Ruto alipotoa kauli hiyo.
Hata hivyo, hakukuwa na dalili za operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao jijini Nairobi Jumatatu.
Baadaye, msemaji wa serikali ya Rais Ruto alisema Kenya ina sera ya kutovumilia kabisa aina yoyote ya unyanyasaji, vitisho au ubaguzi dhidi ya wageni.
Serikali pia imewataka raia wa Afrika Mashariki wasio na nyaraka halali, hususan Warundi, kujisajili rasmi katika balozi zao.