Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Ninafanya kazi ya kuwabebea wengine ujauzito'
- Author, Agnes Penda
- Nafasi, BBC Swahili, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Lorna Fidelia hufanya kazi ya kuwabebea wengine uja uzito. Amewahi kubeba mimba ya pacha watatu miaka michache iliyopita na sasa anatafuta kubeba mtoto mwingine.
Lorna ni miongoni mwa wanawake waliokumbatia kazi hii ili kuzisaidia familia ambazo zimekosa kupata watoto .
Nilikaa chini nikawaza nimekuwa single mother miaka mingi. Nikakaa nikafikiria mimi niko na hawa watoto Ninafanya kazi hata pesa haitoshi lakini kuna mtu ambaye hana watoto ako na provision anaweza afford rent, food , shule na hana mtoto. Nikaona naweza kusaidia mtu hana watoto at the same time anisaidie mimi na Watoto wangu" Lorna Fidelia
Kabla ya kukubalika kubeba uja uzito, anayebeba mimba na wazazi wa toto huandikishana mkataba wa kisheria. Katika mkataba huo, wanakubaliana malipo na vipengee kama vile anayebeba mimba kutokuwa na haki ya kumchukua mtoto anayezaliwa.
Baada ya hapo , mchakato mzima huanza hospitalini ambapo mtaalamu wa mayai ya uzazi huwapima wazazi husika na kutoka mayai ya kiume na ya kike kabla ya kupima afya ya anayebeba mimba alafu kufanya upandikizaji
Daktari Susan Karanja ni mtaalamu wa upandikizaji mimba katika hospitali ya Nairobi West jijini Nairobi anasema nchini Kenya anayebebea wengine mimba anafaa kuwa kati ya umri wa miaka 25 hadi 45 na hufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kukubalika.
'Huyu surrogate anapitia mchakato wa uchunguzi wa kiafya. Anaangaliwa kama yuko sawa, je damu yake iko sawa tukishamaliza daktari anaangalia nyumba ya mtoto kama iko sawa. Tukishatoa yale mayai mume anatoa mbegu zake tunachukua zile mbegu na mayai ya mke tunakutanisha alafu tunamuwekea huyo surrogate anayebeba mimba kwenye nyumba ya uzazi.'
Baada ya upandikizaji, anayebeba mimba hupumzika bila kufanya kazi ngumu ili asihatarishe uja uzito.
Kubeba uja uzito kuna faida za kifedha ambapo wazazi humlipa mjamzito kwa kila mwezi na kushughulikia mahitaji yake ya kila siku. Lorna alifaidika alipobeba pacha watatu.
'Kama kuna wakati sikusumbuka kupata chakula , karo ya shule wala kodi ya nyumba ni huo wakati.'
Malipo yanayotolewa kwa wanaobeba mimba barani Afrika yakionekana chini mno ikilinganishwa na mataifa yaliyoendelea.
Kwa mfano nchini Marekani kubeba mimba kunaweza kumfaidisha mbebaji kupata hadi kati ya dola $120,000 na $220,000 kwa mimba moja.
Nchini Kenya sheria hairuhusu malipo ila wazazi hutoa shukrani ambayo ni kutoka kiwango cha chini cha dola elfu moja kwa mwezi na kukidhi mahitaji yote ya mja mzito hadi dola elfu nane kulingana na masikizano.
Jiji la Nairobi lina vituo 15 vya upandikizaji mimba. Upandikizaji mimba au IVF na kubebea wengine mimba kumeanza kuwa maarufu barani Afrika kufuatia kupungua kwa uwezo wa kupata watoto kwa asilimia 37.
Ingawaje hali ilikuwa sawa kwa Lorna, wengine wamejipata kunyanyaswa kufuatia kuwepo kwa ma agenti wanao waunganisha na wazazi wanaotaka kubebewa mimba.
Maagenti hao huishia kuchukua kiwango kikubwa zaidi cha fedha kutoka kwa wazazi wanaobebewa mtoto na kumuacha anayebeba mimba na pesa kidogo.
Kando na kutoelewana kwa wazazi na anayebeba mimba kwa mfano anayebeba mimba kukatalia mtoto.
Ayieta Lumbasyo ni wakili wa masuala uzazi, anaeleza kuwa ukosefu wa sheria za teknolojia za uzazi kama hizi katika mataifa mengi barani Afrika Kumesababisha tatizo hilo .
'Utakuta msichana haelewi mkataba unasema nini . Kukosekana sheria kunafanya mtu hajui anachofaa kutarajia wasichana wanadanganywa pesa.. mtu wanakubaliana 700, 000 akishajifungua mtu anasema ni 400,000.'Ayeta Lumbasyo
Mataifa kama Kenya , Uganda na Tanzania hayana sheria za teknolojia ya uzazi. Nchini Kenya, huwabidi wazazi kuasili wana wao punde wanapozaliwa hali inayochukua muda mrefu kwani mtoto huandikishwa kuwa wa anayejifungua.
Isipokuwa sasa Kenya iko katika harakati za kupitisha sheria inayolinda teknolojia ya uzazi. Sheria hiyo mpya inaondoa sharti la kuasiliwa kwa mtoto na wazazi wake baada ya kuzaliwa na badala yake mzazi anaweza kumchukua mtoto punde tu anapozaliwa.
Kwa sasa nchini Kenya wazazi hulazimika kuasili mtoto wao aliyezaliwa kwani majina yanaoandikwa hospitalini huwa ya anayebeba mimba.
Wakili ana maoni tofauti kwamba huenda ikafanya kuwa rahisi kwa watoto kuibiwa.
' Shida ya huo muswada ni kuwa unaweza kutoa nafasi za watu kuiba Watoto .. Tunataka tu waondoe ugumu wa mtu kuchukua mtoto wake.'
Licha ya unyanyapaa dhidi ya watu walio na uwezo wa kupata watoto, teknolojia za kupandikiza mimba zimeanza kuwa maarufu barani Africa ila bila sheria muhimu, sekta hiyo itazidi kukumbwa na utata.