Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Putin aishutumu NATO wakati wa sherehe za gwaride la kijeshi
Rais wa Urusi Vladimir Putin alitumia sherehe za kila mwaka za Siku ya Ushindi nchini mwake kuhalalisha vita vyake dhidi ya Ukraine na kushutumu NATO, katika hotuba yake aliyoitoa kwenye bustani ya Red Square katikati mwa jiji la Moscow.
Akizungumza na mamia ya wanajeshi, Putin alisema alikuwa akiendesha vita vya "haki", akielezea Ukraine kama "kikosi ambacho kinapokea silaha na kuungwa mkono na muungano mzima wa NATO."
Hotuba ya rais wa Urusi mwaka huu ilikuja huku kukiwa na kupungua kwa kiwango cha sherehe za kuadhimisha sikukuu ya kitaifa ya Urusi - ambayo iliashiria ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya Ujerumani ya Nazi.
Kabla ya sherehe hizo, ambazo zilipunguzwa kwa sababu za kiusalama huku kukiwa na hofu ya shambulio la Ukraine, Urusi na Ukraine zilikubali kutii usitishaji vita wa siku tatu, uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Ijumaa.
Hata hivyo, punde tu gwaride la kijeshi lilipomalizika, Wizara ya Ulinzi ya Urusi iliharakisha kuishutumu Ukraine kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano, bila maelezo zaidi. Ukraine haikutoa maoni yake mara moja kuhusu shutuma hizo za Urusi.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka, gwaride la kijeshi la Siku ya Ushindi huko Moscow halikuwa na magari ya kivita na makombora ya balestiki.
Chini ya hatua kali za usalama, gwaride la kijeshi la askari lilianza katika Red Square.
Putin alianza hotuba yake mbele ya umati wa watu kwa kusifu kujitolea mhanga kwa wanajeshi wa Soviet wakati wa Vita vya Kidunia vya pili, akisema kwamba "mafanikio makubwa ya kizazi cha washindi yanastahili kuwatia moyo wanajeshi ambao sasa wanafikia malengo ya operesheni maalum ya kijeshi inayoendelea," akimaanisha vita vya Ukraine, ambavyo vimeendelea kwa zaidi ya miaka minne.
Putin aliongeza: "Tunakabiliwa na nguvu kali ambayo inapokea silaha na msaada kutoka kwa muungano mzima wa NATO, na bado mashujaa wetu wanasonga mbele."
Rais wa Urusi aliendelea kuwasifu raia wenzake wa Urusi, akibainisha michango ya vikundi mbalimbali katika vita - ikiwa ni pamoja na wanasayansi, wavumbuzi, waandishi wa vita, madaktari, na walimu.
Putin alisema: "Haijalishi ni mabadiliko gani yatatokea katika mbinu za kijeshi, mustakabali wa nchi unabaki mikononi mwa watu wake."
Mara tu Putin alipomaliza hotuba yake, mizinga ilivuma kwa risasi mfululizo kabla ya muziki wa kijeshi kuanza kupigwa.
Wageni waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko, Mfalme wa Malaysia Sultan Ibrahim Ismail na Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev.
Robert Fico, Waziri Mkuu wa Slovakia, alikuwa mwakilishi pekee wa Umoja wa Ulaya; Fico pia alipigwa picha, akiwa amehudhuria gwaride la kijeshi na mkutano na Putin huko Kremlin.
Sherehe za mwaka huu zilishuhudia idadi ndogo ya viongozi wa dunia wakijitokeza ikilinganishwa na sherehe za mwaka jana, ambazo ziliambatana na maadhimisho ya miaka 80 ya Siku ya Ushindi na kushuhudia mahudhurio ya viongozi 27 wa dunia - akiwemo Rais Xi Jinping wa China na Rais wa Brazil Inacio Lula da Silva.
Baada ya hotuba ya Putin, televisheni ya Urusi ilionyesha wanajeshi wakiwa mstari wa mbele.
Baada ya sherehe hiyo katika Red Square, Putin aliweka mashada ya maua kwenye Kaburi la Askari Asiyejulikana, kabla ya kuhudhuria mapokezi huko Kremlin.
Mbali na Red Square ya Moscow, maeneo mengine kote Urusi yana maonyesho ya kusherehekea Siku ya Ushindi, ingawa maonyesho ya mwaka huu yamekuwa machache ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Katika Mashariki ya Mbali ya Urusi, katika jiji la Vladivostok, gwaride lilifanyika likiwa na "Machi ya Kikosi cha Kutokufa" kuwakumbuka wapiganaji wa Vita vikuu vya Patriotic.
Urusi ilianza uvamizi kamili wa Ukraine mnamo 2022; na licha ya kupelekwa kwa wanajeshi na zana za kijeshi kwenye mstari wa mbele, Urusi imedumisha maonyesho ya zana zake za kijeshi, kama vile vifaru, makombora na silaha zingine, wakati wa sherehe zake za kila mwaka huko Moscow.
Lakini wiki iliyopita, maafisa wa Urusi walitangaza kuwa maonyesho ya sherehe ya mwaka huu yatakuwa machache, kutokana na kile walichokiita "hali ya sasa ya uendeshaji".
Kuhusiana na hilo, mbunge Yevgeny Popov aliiambia BBC mapema wiki hii: "Vifaru vyetu viko na shughuli nyingi sasa, vinahusika katika mapigano. Tunavihitaji kwenye uwanja wa vita zaidi kuliko Red Square."
Hatua za usalama zimeimarishwa, na vitisho kutoka kwa ndege zisizo na rubani za Ukraine zimetumika kama kisingizio cha kupunguza ukubwa wa sherehe mwaka huu.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Urusi na Ukraine yalionekana kutekelezwa huku sherehe zikifanyika mjini Moscow, lakini muda mfupi baada ya sherehe hizo, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilidai kuwa Ukraine ilikiuka makubaliano hayo, na kuongeza kuwa Urusi kwa upande wake itaendelea kutii makubaliano hayo.
Mapema wiki hii, Putin alitangaza kusitisha mapigano kwa siku mbili kwa Mei 8 na 9, huku Kyiv akitoa wito wa kusitishwa kwa muda usiojulikana kuanzia Mei 6.
Tangu matangazo hayo yatangazwe, kila upande umemtuhumu mwenzake kwa kufanya ukiukaji mkubwa wa mapatano kwenye medani ya vita.