Rais wa Marekani, Donald Trump, ameyakataa vikali majibu ya Iran kwa mapendekezo ya Marekani ya kumaliza vita, akiyataja kuwa “hayakubaliki kabisa”.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim la Iran, Tehran iliwasilisha mapendekezo yake kupitia Pakistan, ambayo imekuwa ikipatanisha pande hizo.
Pendekezo hilo lilitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika maeneo yote, kuondolewa kwa mzingiro wa majini uliowekwa na Marekani pamoja na dhamana kwamba hakutakuwa na mashambulizi mengine dhidi ya Iran.
Usitishaji mapigano uliolenga kufungua njia ya mazungumzo ya kumaliza vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel mwezi Februari umeendelea kuheshimiwa kwa kiasi kikubwa, licha ya mashambulizi ya hapa na pale yaliyoripotiwa.
Mapema wiki hii, Trump alisema tena kuwa vita nchini Iran “vitamalizika haraka”.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema akiba ya Iran ya urani iliyorutubishwa lazima iondolewe kabisa kabla ya vita kutangazwa kumalizika.
“Bado kuna vituo vya kurutubisha urani vinavyopaswa kusambaratishwa,” Netanyahu alisema katika mahojiano na kipindi cha 60 Minutes cha CBS.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, hakuzungumzia moja kwa moja pendekezo hilo, lakini alisema Jumapili: “Hatutainamisha vichwa vyetu mbele ya adui. Mazungumzo au diplomasia havimaanishi kujisalimisha au kurudi nyuma.”
Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump aliandika: “Nimesoma majibu kutoka kwa wanaojiita ‘wawakilishi’ wa Iran. Siyakubali kabisa.”
Chombo cha habari cha Marekani cha Axios kiliripoti kuwa waraka wa Marekani wenye vipengele 14 unajumuisha masharti ya kusitishwa kwa urutubishaji wa nyuklia wa Iran, kuondolewa kwa vikwazo pamoja na kurejeshwa kwa uhuru wa usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz.
Ripoti hiyo ilinukuu maafisa wawili wa Marekani pamoja na vyanzo vingine viwili visivyotajwa majina vikisema kuwa utekelezaji wa masharti mengi unategemea kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho.
Iran imeendelea kuzuia njia ya Hormuz, hatua iliyochangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Kwa upande wake, Marekani imeendelea kuweka mzingiro katika bandari za Iran ili kuishinikiza Tehran kukubali masharti yake, jambo ambalo limeongeza hasira nchini Iran.