Moja kwa moja, Trump asema majibu ya Iran kuhusu kumaliza vita 'hayakubaliki kabisa'

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, hakuzungumzia moja kwa moja pendekezo hilo, lakini alisema Jumapili: “Hatutanyenyekea mbele ya adui. Mazungumzo au diplomasia havimaanishi kujisalimisha au kurudi nyuma.”

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Bei ya mafuta yapaa kufuatia mvutano wa Marekani na Iran

    t

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kauli kali za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Iran pamoja na majibu ya nchi hiyo zimeathiri kwa haraka masoko ya mafuta barani Asia Jumatatu asubuhi, na kusababisha kupanda kwa bei kwa takriban asilimia 3.

    Mafuta ghafi ya Brent ya Bahari ya Kaskazini yalifikia dola 104.09 kwa pipa katika biashara za mapema Jumatatu asubuhi.

    Soma pia:

  2. Abiria wa MV Hondius waendelea kurejeshwa makwao baada ya mlipuko wa hantavirus

    F

    Chanzo cha picha, AP

    Makundi ya abiria na wafanyakazi wa meli ya kitalii iliyokumbwa na mlipuko hatari wa hantavirus yaliondoka melini Jumapili ili kusafirishwa kurejea katika mataifa yao, ambako watawekwa karantini kwa mujibu wa taratibu za afya za kila nchi ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

    Ndege za serikali zilizowabeba raia wa Hispania na Ufaransa zilitua Madrid na Paris Jumapili alasiri, huku abiria hao wakipelekwa hospitalini kwa mujibu wa serikali za mataifa hayo mawili.

    Mmoja kati ya abiria watano wa Ufaransa alionyesha dalili za ugonjwa huo akiwa ndani ya ndege ya kurejeshwa nyumbani, Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sebastien Lecornu, alisema kupitia mtandao wa X.

    Ndege kuelekea Canada, Uholanzi, Uturuki, Uingereza, Ireland na Marekani zilitarajiwa kuondoka kufikia saa 2:30 usiku kwa saa za eneo hilo Jumapili, huku safari za mwisho zikitarajiwa kuondoka Jumatatu kufikia saa moja usiku.

    Abiria hao watafanyiwa vipimo mara watakapowasili katika nchi zao, kabla ya kupelekwa hospitali za eneo husika, vituo vya karantini au kurejeshwa majumbani kwa ajili ya kujitenga.

    Shirika la Afya duniani - WHO - imependekeza karantini ya siku 42 kwa abiria wote waliokuwa ndani ya meli hiyo kuanzia Jumapili, kulingana na kauli ya mkurugenzi wa usimamizi wa magonjwa ya mlipuko na janga duniani, Maria Van Kerkhove, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

    Pia unaweza kusoma:

  3. El- Classico: Barcelona yailaza Real Madrid

    Ronald Araujo akinyanyua kombe baada ya kushinda taji la Barcelona

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ronald Araujo akinyanyua kombe baada ya kushinda taji la Barcelona

    Marcus Rashford alifunga mkwaju wa fauli na kuwasaidia Barcelona kuwalaza wapinzani wao Real Madrid na kufanikiwa kunyakua taji lao la 29 la La Liga huku zikiwa zimesalia mechi tatu kumalizika kwa msimu.

    Mshambuliaji huyo wa Uingereza aliwaweka wenyeji mbele kabla ya Ferran Torres kufunga bao la pili kwa umaliziaji mzuri wakati kikosi cha Hansi Flick kikishinda mechi ya El Clasico kwenye Uwanja wa Nou Camp.

    Wachezaji wote wawili walimkimbilia kocha wao mkuu walipofunga baada ya babake kuaga dunia wikendi.

    Barcelona sasa wako nyuma ya Real madrid kwa mataji baada ya kunyakua ligi kuu ya Uhispania kwa misimu miwili mfululizo.

    Wameshinda mechi 11 kwenye La Liga hadi kutwaa ubingwa na kuwaongoza wapinzani wao kwa pointi 14 zisizoweza kuepukika.

    Kiwango kizuri cha Barcelona nyumbani kimewasaidia kutwaa ubingwa, kwani huo ulikuwa ushindi wao wa 18 kati ya michezo 18 waliyocheza mbele ya mashabiki wao.

    Mshambuliaji wa Manchester United anayecheza kwa mkopo Rashford alianza vyema wakati alipopiga mpira wa adhabu wa mapema hadi kwenye kona ya juu na kumpita kipa wa Real Thibaut Courtois, ambaye mguso wake hafifu haukuweza kuuzuia mpira nje.

    Na baadaye kunako dakika ya 18 mchezo mzuri wa Dani Olmo aliyemtengenezea Torres pasi nzuri na kufunga goli la pili.

    Aurelien Tchouameni alianzishwa katika mechi hiyo kwa upande wa Real Madrid siku chache baada ya kugombana na mchezaji mwenzake Federico Valverde, ambaye alichanganyikiwa wakati wa mabishano na kukosa mchezo.

    Meneja wa Real aliye na shinikizo la chini, Alvaro Arbeloa hakuweza kuitia moyo timu yake, huku Gonzalo Garcia akishindwa kufunga moja ya nafasi chache walizopata kwenye kipindi cha kwanza.

    Sauti za "Mabingwa" zilisikika karibu na Nou Camp iliyoboreshwa huku saa zikiyoyoma kuthibitisha kwamba wenyeji walikuwa wamehifadhi taji lao la La Liga, huku Robert Lewandowski akikaribia kufanya matokeo kuwa 3-0.

    Soma zaidi:

  4. Trump asema majibu ya Iran kuhusu kumaliza vita 'hayakubaliki kabisa'

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameyakataa vikali majibu ya Iran kwa mapendekezo ya Marekani ya kumaliza vita, akiyataja kuwa “hayakubaliki kabisa”.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim la Iran, Tehran iliwasilisha mapendekezo yake kupitia Pakistan, ambayo imekuwa ikipatanisha pande hizo.

    Pendekezo hilo lilitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika maeneo yote, kuondolewa kwa mzingiro wa majini uliowekwa na Marekani pamoja na dhamana kwamba hakutakuwa na mashambulizi mengine dhidi ya Iran.

    Usitishaji mapigano uliolenga kufungua njia ya mazungumzo ya kumaliza vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel mwezi Februari umeendelea kuheshimiwa kwa kiasi kikubwa, licha ya mashambulizi ya hapa na pale yaliyoripotiwa.

    Mapema wiki hii, Trump alisema tena kuwa vita nchini Iran “vitamalizika haraka”.

    Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema akiba ya Iran ya urani iliyorutubishwa lazima iondolewe kabisa kabla ya vita kutangazwa kumalizika.

    “Bado kuna vituo vya kurutubisha urani vinavyopaswa kusambaratishwa,” Netanyahu alisema katika mahojiano na kipindi cha 60 Minutes cha CBS.

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, hakuzungumzia moja kwa moja pendekezo hilo, lakini alisema Jumapili: “Hatutainamisha vichwa vyetu mbele ya adui. Mazungumzo au diplomasia havimaanishi kujisalimisha au kurudi nyuma.”

    Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump aliandika: “Nimesoma majibu kutoka kwa wanaojiita ‘wawakilishi’ wa Iran. Siyakubali kabisa.”

    Chombo cha habari cha Marekani cha Axios kiliripoti kuwa waraka wa Marekani wenye vipengele 14 unajumuisha masharti ya kusitishwa kwa urutubishaji wa nyuklia wa Iran, kuondolewa kwa vikwazo pamoja na kurejeshwa kwa uhuru wa usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz.

    Ripoti hiyo ilinukuu maafisa wawili wa Marekani pamoja na vyanzo vingine viwili visivyotajwa majina vikisema kuwa utekelezaji wa masharti mengi unategemea kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho.

    Iran imeendelea kuzuia njia ya Hormuz, hatua iliyochangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

    Kwa upande wake, Marekani imeendelea kuweka mzingiro katika bandari za Iran ili kuishinikiza Tehran kukubali masharti yake, jambo ambalo limeongeza hasira nchini Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 11 Mei 2026.