Je, unaujua ugonjwa wa Hantavirus unaoenezwa na panya?

Picha ya meli.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya meli
Muda wa kusoma: Dakika 2

Watu watatu wamefariki baada kushukiwa kuambukizwa virusi vya hantavirus katika meli moja ya kubeba abiria iliyokuwa ikisafiri katika bahari ya Atlantiki, hii ni kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika la afya duniani WHO.

Kisa kimoja cha hantavirus kimethibitishwa, huku visa vingine vitano vikiendelea kufanyiwa uchunguzi, WHO imesema.

Mlipuko wa virusi hivyo vimeripotiwa katika meli moja ya kitalii ya MV Hondius ambayo ilikuwa ikisafiri kutoka Argentina kuelekea Cape Verde.

Hantavirus ni nini?

Hantavirus ni aina ya virusi vinavyopatikana kwenye wanyama wagugunaji kama panya, na mara nyingi binadamu huambukizwa virusi hivyo kwa kupumua hewa inayotokana na kinyesi cha panya kilichokauka.

Maambukizi hutokea wakati hewa anayopumua binadamu inachanganyika na hewa inayotokana na mkojo, kinyesi au mate ya panya, hii ni kulingana na kituo cha kudhibiti kuenea kwa magonjwa CDC.

Ingawa maambukizi haya huwa nadra, mtu pia huweza kuambukizwa kwa kungatwa au kugwaruzwa na panya.

Virusi hivi husababisha magonjwa mawili, kwanza ni Hantavirus Pulmonary Syndrome (HPS), ambayo mara nyingi dalili yake huanza na uchovu, homa, maumivu ya misuli, kichwa kuuma, kizunguzungu na maumivu ya tumbo.

Ugonjwa huu huleta pia changamoto ya kupumua na kusababisha vifo kwa asilimia 38 ya watu wanaougua ugonjwa huo.

Ugonjwa wa pili unaotokana na virusi hivi ni Haemorrhagic Fever with Renal syndrome (HFRS) ambayo huathiri figo. Dalili zake ni shinikizo la chini la damu, kuvuja damu ndani ya mwili na kufeli kwa figo.

Kesi ngapi za Hantavirus huripotiwa duniani?

Takriban visa 150,000 vya HFRS huripotiwa duniani kila mwaka hasa bara Ulaya na Asia, kulingana na ripoti ya taasisi za kitaifa za afya (NIH). Nusu ya visa hivyo hutokea nchini China.

Nchini Marekani tangu mwaka wa 1993 hadi 2023 kumekuwa na visa 890.

Hata hivyo virusi aina ya Seoul ambavyo ni kiungo kikuu cha virusi vya hantavirus ambavyo hubebwa na panya wenye rangi ya kahawia (Norway Rats) inapatikana kote duniani.

Matibabu

Hakuna matibabu maalum ya maambukizi ya hantavirus.

Shirika la kudhibiti kuenea kwa magonjwa CDC, inapendekeza mgonjwa kupewa matibabu ya kudhibiti dalili za virusi hivyo kama kuongezewa hewa ya oksijeni na kufanyiwa usafishaji wa damu kupitia mashine ya figo, iwapo utendakazi wa figo utaathirika.

Wagonjwa ambao wataonyesha kuwa na dalili kali hulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

CDC pia inapendekeza kuwaondoa panya wote majumbani na hata sehemu za kazi ili kupunguza hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.

Shirika hilo pia linashauri kuvaa magwanda ya kujikinga wakati wa kusafisha kinyesi cha panya, ili kuepuka kupumua hewa iliochafuliwa.

Visa vya hivi karibuni

Mwezi Februari mwaka wa 2015, Betsy Arakawa, mke wa mwigizaji na mshindi wa tuzo la Oscar Gene Hackman alifariki kutokana na matatizo ya kupumua yaliyohusishwa na hantavirus.