Moja kwa moja, Marekani yaitaka Iran kusitisha mashambulizi katika mlango bahari wa Hormuz

Marekani inataka Iran itangaze wazi kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz uko wazi kwa usafiri wa majini na iache kushambulia meli za kibiashara.

Muhtasari

Marekani yaitaka Iran kusitisha mashambulizi katika mlango bahari wa Hormuz

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Iran na Oman kujadili kuhusu usalama wa Mlango bahari wa Hormuz

    .

    Chanzo cha picha, ISNA

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amewasili mjini Muscat, Oman, kwa mazungumzo na maafisa wa serikali ya Oman.

    Kulingana na vymbo vya habari vya eneo hilo, Waziri huyo anatarajiwa kuongoza mazungumzo kati ya Iran na Oman kuhusu mlango bahari wa Hormuz

    Pande hizo mbili zinatarajiwa kuja na utaratibu utakaohakikisha meli zinapita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, kwa kuzingatia Kifungu cha 5 cha Hati ya Makubaliano ya Islamabad.

    Ziara hiyo inafanyika wakati mvutano kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz umeongezeka katika siku za hivi karibuni kufuatia mashambulizi kati ya Marekani na Iran.

    Hayo yakijiri, ujumbe wa wapatanishi kutoka Qatar umesafiri kwenda Iran kwa lengo la kuweka mazingira ya kuanza tena mazungumzo kati ya Iran na Marekani pamoja na kupunguza mvutano kati ya pande hizo mbili.

    Soma pia:

  2. Zaidi ya wanafunzi 25 waliotekwa nyara waokolewa Nigeria

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Ikulu ya Nigeria imetoa taarifa kuwa vikosi vya usalama vimewaokoa zaidi ya wanafunzi 25 pamoja na walimu kadhaa waliokuwa wametekwa nyara na watu waliojihami katika jimbo la Oyo mwezi Mei.

    Msemaji wa Rais wa Nigeria, Bayo Onanuga, amechapisha picha za baadhi ya wanafunzi waliotekwa nyara kutoka shule tatu zilizoko eneo la Oriyere.

    Ikulu ya Nigeria imesema hakuna fedha za fidia zilizolipwa ili kuwaachia mateka hao, na kwamba watu wanane wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi lililohusika na utekaji huo wamekamatwa.

    Visa vya utekaji nyara wa wanafunzi umekuwa ukishuhudiwa mara kwa mara kaskazini mwa Nigeria huku vyama vya walimu na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yakitaka serikali kuimarisha ulinzi shuleni.

    Soma pia:

  3. Trump atishia kuiangamiza Iran, iwapo watajaribu kumuua

    Picha ya Donald Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ameionya serikali ya Iran kwamba Marekani itafanya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya Iran ikiwa itachukua hatua yoyote ya kuhatarisha maisha yake au kujaribu kumuua.

    Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump aliandika, "Makombora elfu moja yako tayari na yameelekezwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ikiwa tishio la serikali ya Iran la kumuua Rais wa Marekani litatekelezwa, makombora zaidi ya elfu moja yatafyatuliwa mara moja."

    Trump pia alisema kuwa ametoa maagizo yanayohitajika na kwamba jeshi la Marekani liko tayari "kuangamiza kabisa maeneo yote ya Iran" kwa kipindi cha mwaka mmoja.

    Kauli ya Trump inajiri kufuatia ripoti za ujasusi kutoka Israel zinazodai kuwepo kwa njama mpya ya Iran ya kutaka kumuua Trump, pamoja na picha na mabango zilizoonekana wakati wa mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei.

    Maafisa wa Iran wamekanusha kuwepo kwa mpango wowote wa kumuua Trump.

    Soma pia:

  4. Hatujaomba kufanya mazungumzo na Marekani - Iran

    Picha ya Esmail Baghaei

    Chanzo cha picha, isna

    Maelezo ya picha, Picha ya Esmail Baghaei

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Iran, Esmail Baghaei, amesema kuwa Tehran haijaomba kufanya mazungumzo na Marekani, lakini imekubali ombi la mpatanishi mmoja wa kikanda kutembelea Iran na kujadili matukio yaliyojiri hivi karibuni.

    Akizungumza katika mahojiano ya televisheni, Baghaei alisema kuwa "Hatukuomba kufanya mazungumzo na Marekani, lakini kwa kuzingatia msimamo wetu wa kuwajibika, hatukukataa ombi la mmoja wa wapatanishi wa kikanda kuja Iran na kujadili hali ya sasa. Ziara hiyo tayari ilifanyika mjini Mashhad, na tuliwasilisha maoni na misimamo yetu kwa upande wa Qatar."

    Msemaji huyo aliongezea kuwa "Marekani imekuwa ikikiuka mara kwa mara vipengele mbalimbali vya makubaliano hayo katika kipindi hiki."

    Baghei alifafanua kuwa matukio ya Jumatano na Alhamisi yalikuwa ukiukaji wa kifungu cha kwanza na cha pili cha makubaliano ya kusitisha mapigano walioafikia na Marekani, huku uamuzi wa kufuta kibali cha kuuza mafuta ya Iran pia ukiwa ukiukaji mkubwa wa kifungu kingine cha makubaliano hayo.

    Kulingana na Baghaei, kuwekewa kwa Iran vikwazo vipya na Marekani ni kinyume na Kifungu cha 9 cha hati hiyo ya makubaliano.

    Hapo jana Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa Iran imewaomba wafanye mazungumzo ya kupata amani na kutangaza kuwa amefutilia mbali usitishaji mapigano.

    Soma pia:

  5. Marekani yaitaka Iran kusitisha mashambulizi katika mlango bahari wa Hormuz

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani inaitaka Iran itangaze wazi kuwa Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi kwa usafiri wa majini na iache kushambulia meli za kibiashara, kama sehemu ya mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika nchini Omanhii leo.

    Vyombo vya habari vya Marekani vimewanukuu maafisa ambao hawakutajwa majina wakisema kwamba Tehran ilikubali kuwa mashambulizi ya meli yalikuwa makosa, huku maafisa hao wa Iran wakidai mashambulizi hayo yalitekelezwa na kundi la waasi nchini humo.

    Trump amesema pande zote mbili zimekubaliana kuendelea na mazungumzo licha ya mapigano ya wiki hii kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz, ambayo Ikulu ya Marekani iliona kuwa yalikiuka makubaliano ya usitishaji mapigano.

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amesema nchi yake "imetimiza ahadi yake" kuhusu usitishaji mapigano, akidai kupitia mtandao wa X kwamba Marekani ndiyo iliyokiuka makubaliano hayo.

    Mwezi Juni, Marekani na Iran zilitia saini makubaliano ya usitishaji mapigano ambapo, miongoni mwa masharti yake, Iran ilikubali kuhakikisha meli za kibiashara zinapata njia salama ya kupita kutumia Mlango bahari wa Hormuz.

    Soma pia:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumamosi ya leo