Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ajali 7 mbaya zaidi za treni zilizotikisa dunia
Unapopanda treni, unatarajia kufika unakoenda salama. Huenda ukaketi, ukatazama mandhari kupitia dirishani au ukaendelea na shughuli zako, bila kufikiria kuwa safari hiyo inaweza kubadilika na kuwa janga ndani ya sekunde chache.
Lakini ajali iliyotokea Hispania Jumatano, Oktoba 28, 2026, imewakumbusha wengi jinsi ajali za treni zinavyoweza kuwa na madhara makubwa. Takriban watu 68 wamefariki dunia baada ya treni mbili za mwendo kasi kugongana karibu na Urda, kusini mwa Madrid, huku wengine wakijeruhiwa. Nchi hiyo imeanza siku tatu za maombolezo huku uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali ukiendelea.
Hii si mara ya kwanza kwa ajali ya treni kusababisha vifo vya watu wengi. Katika historia, ajali kama hizi zimeacha familia zikiwa na majonzi na jamii zikijiuliza nini kingefanywa kuzuia majanga kama hayo.
Kuanzia Kenya na Tanzania hadi India, Urusi na Ufaransa, hizi ni baadhi ya ajali mbaya zaidi za treni zilizowahi kushuhudiwa.
India: Ajali ya Bihar, 1981
Mwaka 1981, mvua kubwa za pepo za msimu katika Bahari ya Hindi zilikuwa zimesababisha mito kujaa nchini India. Treni iliyokuwa na karibu abiria 1,000 ilipokuwa ikivuka daraja katika jimbo la Bihar, mabehewa saba kati ya tisa yalitumbukia katika Mto Baghmati.
Hadi leo, maelezo kuhusu chanzo cha ajali hiyo yanatofautiana. Baadhi ya taarifa zinasema dereva alifunga breki ghafla ili kuepuka kumgonga ng'ombe aliyekuwa kwenye reli. Nyingine zinataja upepo mkali na hali mbaya ya hewa.
Makadirio yanaonyesha kuwa watu kati ya 500 na 800 walifariki. Eneo la ajali lilikuwa mbali na huduma za dharura, hivyo msaada ulichelewa kufika.
Urusi: Ajali ya Ufa, 1989
Mnamo Juni 1989, treni mbili za abiria zilipokuwa zikipishana katika eneo la Milima ya Ural nchini Urusi, gesi iliyokuwa imevuja kutoka kwenye bomba la karibu ililipuka.
Treni hizo zilikuwa na zaidi ya abiria 1,300, wakiwemo mamia ya watoto waliokuwa wakielekea au kurejea kutoka likizoni.
Cheche kutoka kwenye mojawapo ya treni ziliwasha gesi iliyokuwa imejikusanya katika bonde hilo na kusababisha mlipuko mkubwa.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa watu 575 walifariki, wakiwemo watoto 181, na zaidi ya 800 walijeruhiwa. Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vinakadiria kuwa idadi ya waliofariki huenda ilikuwa kubwa zaidi.
Mexico: Ajali ya Guadalajara, 1915
Wakati wa mapinduzi ya Mexico mwaka 1915, treni iliyokuwa imebeba zaidi ya abiria 900, wakiwemo familia za wanajeshi, iliondoka Colima kuelekea Guadalajara.
Treni hiyo ilikuwa imejaa kupita uwezo wake. Baadhi ya abiria waliripotiwa kusafiri juu ya paa na chini ya mabehewa.
Ilipokuwa ikishuka kwenye bonde, treni iliongeza kasi na kushindwa kupita kwenye kona kwa usalama. Breki zilishindwa kufanya kazi, na treni ikatoka kwenye reli na kutumbukia kwenye korongo.
Zaidi ya watu 600 wanakisiwa kufariki katika ajali hiyo.
Kenya: Ajali ya treni ya 1993
Nchini Kenya, mojawapo ya ajali mbaya zaidi za treni ilitokea mwaka 1993, wakati treni ilipokutana na daraja la reli lililokuwa limeharibika na kutumbukia katika mto uliokuwa umefurika.
Ajali hiyo, iliyotokea katika Mto Ngai Ndethya karibu na Mtito Andei, kwenye reli inayounganisha Nairobi na Mombasa, ilisababisha vifo vya watu 140 na kujeruhi mamia ya wengine, kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kuhusu tukio hilo.
Wengi wa waliofariki walikuwa katika mabehewa ya kwanza na ya pili. Abiria waliokuwa katika mabehewa ya daraja la tatu waliokolewa baada ya kondakta kuchukua hatua za haraka.
Miaka sita baadaye, ajali nyingine ya treni ilitokea kwenye reli ya Mombasa. Watu 32 walifariki na mamia kujeruhiwa baada ya treni kuacha njia.
Tanzania: Ajali ya Igandu, 2002
Tanzania pia ina kumbukumbu chungu ya ajali ya treni ya Igandu, iliyotokea Juni 24, 2002, karibu na Dodoma.
Takriban abiria 1,200 walikuwa ndani ya treni hiyo wakati injini iliposhindwa kufanya kazi na treni kuanza kurudi nyuma kwenye mteremko. Treni iliongeza kasi hadi takriban kilomita 200 kwa saa kabla ya kugongana na treni ya mizigo.
Mabehewa 19 kati ya 20 yalitoka kwenye reli na kupinduka. Baadhi ya watu walionusurika walikuwa wamenaswa ndani ya mabaki ya treni, wakiomba msaada hata saa kadhaa baada ya ajali.
Takriban watu 281 walifariki, na serikali ikatangaza siku mbili za maombolezo ya kitaifa. Ajali hiyo inasalia kuwa mbaya zaidi ya treni kuwahi kutokea Tanzania.
Misri: Ajali ya El Ayyat, 2002
Mwaka 2002, treni ya abiria iliyokuwa ikisafiri kutoka Cairo kuelekea Luxor nchini Misri ilishika moto baada ya mtungi wa gesi ya kupikia kulipuka ndani yake.
Treni ilikuwa imejaa kupita kiasi, na mabehewa saba ya nyuma yaliteketea kwa zaidi ya saa mbili kabla ya kondakta kugundua moto huo.
Kutokana na ukubwa wa moto, baadhi ya miili iliteketea kiasi cha kushindwa kutambuliwa. Idadi rasmi ya waliofariki ilitajwa kuwa 383, lakini kutokuwepo kwa orodha kamili ya abiria kumeibua maswali kuhusu iwapo idadi halisi ilikuwa kubwa zaidi.
Kwa nini ajali za treni zinaweza kuwa na madhara makubwa?
Treni hubeba idadi kubwa ya watu kwa wakati mmoja.
Treni huwa na uzito mkubwa na husafiri kwa kasi, kwahivyo ajali inapotokea, hugongana au kutoka kwenye reli na husababisha mabehewa kupinduka au kutumbukia bondeni.
Madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi pale breki zinaposhindwa kufanya kazi, mifumo ya usalama inapopata hitilafu, reli au madaraja yanapoharibika, au huduma za uokoaji zinapochelewa kufika.
Kwa mjubi wa wataalam wa masuala ya usafiri, ajali ya Hispania inadhihirisha kuwa hata nchi zilizo na mifumo ya kisasa ya reli zinahitaji kuendelea kuchunguza usalama wa miundombinu na taratibu za uendeshaji.
Chanzo cha ajali ya treni ya Hispania bado kinachunguzwa.