Kwa nini Mossad ilitoa video ya operesheni yake ya siri Iran?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Muda mfupi baada ya Israel kuanzisha mashambulizi yake ya kwanza dhidi ya Iran asubuhi ya tarehe 13 Juni 2025, video yenye nembo rasmi ya shirika la ujasusi la Israel, Mossad, ilianza kusambazwa. Video hiyo ilionekana kuwaonyesha watu wanaodaiwa kuwa mawakala wa Mossad wakijiandaa na kuweka vifaa vya kijeshi ndani ya Iran.

Wakati video hiyo ikitolewa, mamlaka za Israel zilidai kuwa operesheni hiyo ilitekelezwa na mawakala wa Mossad waliokuwa ndani ya Iran, kwa lengo la kulenga na kudhoofisha mifumo ya ulinzi wa anga ya taifa hilo.

Hata hivyo, hatua ya kuchapisha video inayoonyesha shughuli za siri za shirika la ujasusi katika saa za mwanzo za vita ilionekana kuwa jambo lisilo la kawaida, na kuzua maswali kuhusu ujumbe uliokusudiwa kutumwa kupitia video hiyo.

Sasa, karibu miezi 16 baada ya kumalizika kwa vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran, aliyekuwa mkuu wa Mossad, David Barnea, amedai kuwa shirika hilo lilisambaza kwa makusudi video na picha za operesheni hiyo ili kuzipotosha mamlaka za usalama za Iran.

Kwa mujibu wa Barnea, hatua hiyo ilikusudiwa kufanya vyombo vya usalama vya Iran vikamate watu wengi waliowashuku kuwa mawakala wa Israel, jambo ambalo lingefanya iwe vigumu zaidi kubaini mawakala halisi wa Mossad waliokuwa wakifanya operesheni zao wakati wa vita.

Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa Barnea alitoa madai hayo katika hafla moja, akisema kuwa mkakati huo ulichangia kukamatwa kwa watu 21,000 nchini Iran katika siku ya pili ya vita hivyo.

Pia alidai kuwa asilimia 99.9 ya mawakala wa Mossad hawajawahi kutambuliwa, huku baadhi ya waliokuwa wakihusika katika operesheni hiyo wakidaiwa kuendelea kuwepo Tehran.

Kwa kawaida, mafanikio ya operesheni za siri na vita vya taarifa hutegemea usiri mkubwa na uwezo wa kuficha utambulisho wa mawakala wake. Hali hiyo imezua maswali kuhusu sababu zilizofanya Mossad kuweka hadharani sehemu ya shughuli zake za siri kupitia video na picha hizo.

Ova Gutman, mtafiti wa historia ya mashirika ya ujasusi katika Chuo Kikuu cha Aberystwyth nchini Uingereza, aliiambia BBC Persian kuwa kutolewa kwa video na picha hizo kulikuwa sehemu ya mkakati wa kuonyesha nguvu na kuathiri simulizi la vita.

Kwa mujibu wa Gutman, hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kama jaribio la Mossad kuonyesha uwezo wake wa kufanya operesheni ndani ya Iran, huku ikijenga taswira ya ubora wa kiintelijensia wa Israel katika kipindi cha mzozo huo.

Kwa mujibu wa Gutman, mkakati huo unaweza kuwa na athari mbili. Kwa upande mmoja, unaweza kuongeza imani na ari miongoni mwa Waisraeli. Kwa upande mwingine, unaweza kuibua hisia za shaka na kutokuaminiana ndani ya vyombo vya usalama vya Iran.

Gutman anaeleza hatua hiyo katika muktadha wa kile kinachoitwa "vita vya simulizi mtandaoni" (timeline warfare), ambapo pande zinazohusika katika mzozo hutumia majukwaa ya kidijitali kuathiri mtazamo wa umma kuhusu matukio yanayoendelea.

Alisema kuwa mashirika ya ujasusi sasa yanaelekea kutangaza mafanikio yao kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa zamani, kwa lengo la kudhibiti simulizi na kuathiri namna operesheni zao zinavyoeleweka na umma.

"Mossad inataka kudhibiti simulizi ya vita hivyo na kuhakikisha operesheni yake inaonekana kuwa mafanikio, ndani na nje ya Israel," alisema.

"Hakuna anayeweza kuaminiwa"

Wakati wa vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel mwezi Juni 2025, vyombo vya usalama vya Iran vilitangaza kukamatwa kwa watu kadhaa waliotuhumiwa kushirikiana na Israel na kuwataka raia kutoa taarifa kuhusu shughuli zozote zilizokuwa zikionekana za kutia shaka.

Katika kipindi hicho, vituo vya ukaguzi viliongezwa katika miji mbalimbali, huku mamlaka za mahakama zikisisitiza kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya watuhumiwa wa ujasusi.

Mnamo Agosti 11, 2025, msemaji wa Kamandi ya Usalama ya Iran, Saeed Montazer al-Mahdi, alisema kuwa takriban watu 21,000 walikamatwa wakati wa vita hivyo. Idadi hiyo sasa imehusishwa na madai yaliyotolewa na aliyekuwa mkuu wa Mossad, David Barnea, kuhusu operesheni za shirika hilo nchini Iran.

Barnea alidai kuwa ukamataji huo ulianza kwa kiwango kikubwa katika siku ya pili ya vita, huku mamlaka za Iran zikiripoti idadi hiyo kama jumla ya waliokamatwa katika kipindi chote cha vita vya siku 12. Alidai pia kuwa watu wengi waliokamatwa waliachiliwa baadaye.

Aidha, Barnea alisema kuwa baadhi ya watu waliokamatwa au hata kuhukumiwa kifo nchini Iran kwa tuhuma za kushirikiana na Israel hawakuwa na uhusiano wowote na Mossad.

Wakati huo huo, mnamo Juni 20, 2025, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilieleza wasiwasi kuhusu kile lilichokitaja kuwa ukamataji holela, mateso na hatari ya hukumu za kifo kwa watu waliotuhumiwa kushirikiana na Israel. Shirika hilo lilitaka Iran kuhakikisha haki za wote waliokuwa wakizuiliwa zinalindwa.

Kwa mujibu wa Ova Gutman, mtafiti wa historia ya vyombo vya ujasusi katika Chuo Kikuu cha Aberystwyth nchini Uingereza, Mossad ilitaka kuunda taswira kwamba mawakala wake walikuwa kila mahali ndani ya Iran.

Anasema mkakati huo ulilenga kupandikiza mashaka na mkanganyiko ndani ya mfumo wa usalama wa Iran, pamoja na kudhoofisha imani kati ya taasisi mbalimbali za serikali.

"Wakati kila mtu anapokuwa mshukiwa, mazingira ya kutoaminiana hutawala na kufanya iwe vigumu kuwatambua wahusika halisi," alisema.

Kwa mtazamo wa Gutman, Barnea sasa anawasilisha matukio hayo kama operesheni iliyofanikiwa ambayo, kwa mujibu wa madai yake, iliwasaidia mawakala wa Israel kujificha miongoni mwa idadi kubwa ya washukiwa.

Anasema idadi kubwa ya watu waliokuwa wakichunguzwa iliwakosesha vyombo vya usalama vya Iran uwezo wa kuwatambua kwa urahisi mawakala halisi wa Mossad, na hivyo kuwapa nafasi ya kuendelea na shughuli zao bila kugunduliwa.

Mossad Ilikuwa inajaribu kutuma ujumbe gani?

Kwa mujibu wa Oyva Gutman, kuchapisha picha au video za operesheni za kiintelijensia si jambo linalofanywa na Mossad pekee. Anataja mifano ya video za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine dhidi ya vituo vya kijeshi vya Urusi, pamoja na picha zilizotolewa na Marekani kuhusu baadhi ya mashambulizi yake dhidi ya kundi la ISIS.

Kwa mtazamo wake, hatua kama hizo huwa na malengo mawili makuu. Kwa upande mmoja, hulenga kuimarisha morali ya jeshi na umma wa nchi husika. Kwa upande mwingine, hulenga kudhoofisha morali ya upande pinzani.

Kulingana na Gutman, kudumisha usiri katika zama hizi za teknolojia ya kisasa hali si rahisi kama ilivyokuwa awali. Kamera za simu, mifumo ya ufuatiliaji na teknolojia za utambuzi wa sura kwa kutumia akili undeau mnemba zimeongeza uwezo wa kufuatilia watu, na kufanya iwe vigumu zaidi kwa mawakala na taasisi za ujasusi kuficha utambulisho wao.

Ameongeza kwamba wakati mwingine mashirika ya ujasusi hutumia taarifa zilizovuja kwa manufaa yao wenyewe. Badala ya kuzipinga au kuzificha, huweka hadharani baadhi ya taarifa za operesheni zao ili kudhibiti simulizi la matukio na kuelekeza mtazamo wa umma katika mwelekeo wanaoutaka.

Akijibu swali la BBC Persian kuhusu hatari ambazo Mossad inaweza kukabiliana nazo kwa kufichua taarifa za operesheni zake za siri, Gutman alisema:

"Athari ya hatua kama hiyo ni ndogo. Kwa kawaida, Mossad hutoa taarifa za operesheni zake pale tu inapojiridhisha kuwa mawakala wake hawawezi kufichuliwa na kwamba taarifa hizo haziwezi kutumiwa kuhujumu operesheni nyingine za siri," alisema.

Historia ya Mossad ya kutumia taarifa za kupotosha

Mossad imekuwa ikitumia taarifa kwa muda mrefu kama moja ya mbinu za kushawishi mitazamo na maamuzi ya walengwa wake.

Katika utafiti uliochapishwa mwaka 2024, mtafiti Ova Gutman alibaini kuwa shirika hilo limewahi kutumia taarifa kama sehemu ya mkakati wake wa operesheni za siri.

Utafiti huo uliangazia Operesheni Wrath of God, kampeni iliyoanzishwa na Israel baada ya kuuawa kwa wanamichezo 11 wa Israel katika Olimpiki ya Munich mwaka 1972. Kwa mujibu wa nyaraka alizochambua Gutman, Mossad iliwahi kuzipa taasisi za usalama za Ulaya taarifa za kiusalama ambazo, baadaye, zilisaidia kupunguza tuhuma dhidi ya Israel kuhusu baadhi ya operesheni zake.

Gutman anasema Mossad mara nyingi huchanganya taarifa za kupotosha na taarifa sahihi ili kuongeza uaminifu wa ujumbe wake. Mbinu hiyo ilisaidia kuathiri namna operesheni zake zilivyotafsiriwa na vyombo vya usalama vya nchi nyingine.

Kwa mtazamo wake, kuna ulinganifu kati ya mkakati huo wa zamani na hatua ya Mossad kusambaza video na picha wakati wa vita vya 2025 dhidi ya Iran. Ingawa mazingira na mbinu zilitofautiana, lengo lilibaki lilelile: kutumia taarifa kuathiri mtazamo, maamuzi na mwenendo wa walengwa.