Benjamin Netanyahu: Je, Israel iko tayari kumpa muhula mwingine madarakani?

    • Author, Raffi Berg
    • Nafasi, Mhariri Mashariki ya Kati
    • Author, Lucy Williamson
    • Nafasi, Mwandishi Mashariki ya Kati
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Waziri Mkuu wa Israel aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi, Benjamin Netanyahu, anatarajia kupata muhula wake wa saba baada ya uchaguzi wa bunge utakaofanyika tarehe 27 Oktoba.

Kwa miongo kadhaa, Netanyahu mwenye umri wa miaka 77 amejiwasilisha kama kiongozi wa usalama wa Israel na kujijengea sifa ya kuwa "Bw. Usalama" wa taifa hilo.

Hata hivyo, azma yake ya kuendelea kuongoza nchi inakuja baada ya kile ambacho baadhi ya Waisrael wanakiona kama ni pigo kubwa zaidi la kiusalama katika historia ya Israel, ni mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya taifa hilo.

Tangu wakati huo, ameelekeza nguvu zake katika vita dhidi ya Hamas na washirika wake, Hezbollah na Iran. Netanyahu amefanya yote hayo huku akikabiliwa na kesi ya ufisadi, tuhuma ambazo amekuwa akizikanusha mara kwa mara.

Wakati huohuo, bado anakabiliwa na kesi ya ufisadi, tuhuma ambazo ameendelea kuzikanusha

Kura za maoni zinaonyesha ushindani mkali kati ya muungano wake wa mrengo wa kulia na kambi ya upinzani inayoshirikiana kumng'oa madarakani. Upinzani huo unajumuisha aliyekuwa Waziri Mkuu Naftali Bennett na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, Gadi Eisenkot.

Athari za mashambulizi ya 7 Oktoba zinatarajiwa kuwa miongoni mwa masuala makuu yatakayowaongoza wapigakura katika uchaguzi huo.

Mwanasiasa aliyenusurika

Licha ya misukosuko mingi ya kisiasa, Benjamin Netanyahu amejijengea sifa ya kuwa mwanasiasa mwenye uwezo wa kusalia madarakani.

Alichaguliwa tena mwaka 2022 kwa muhula wake wa sita kama waziri mkuu na anaongoza moja ya serikali za mrengo wa kulia zaidi katika historia ya Israel. Kurejea kwake madarakani baada ya kipindi kifupi akiwa upinzani kuliwapa wafuasi wake imani kwamba bado ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa.

Hata hivyo, safari yake ya kutafuta muhula mwingine imeathiriwa na kumbukumbu za mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba 2023, ambayo Waisraeli wengi wanayaona kama mojawapo ya mapungufu makubwa zaidi ya kiusalama kuwahi kutokea nchini humo.

Netanyahu amekiri kuwapo kwa mapungufu yaliyoruhusu mashambulizi hayo kutokea, lakini amesema lawama zinapaswa kubebwa pia na viongozi wa usalama.

Wakati huohuo, vita vya Israel huko Gaza vimeendelea kuzua ukosoaji mkubwa wa kimataifa. Aidha, Netanyahu amekanusha madai kwamba alipokea tahadhari za wazi kuhusu mashambulizi ya Hamas kabla hayajatokea.

Mwaka 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati ya kukamatwa dhidi yake kuhusiana na tuhuma zinazotokana na operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza, madai ambayo yeye anayakanusha.

Urithi wa kaka yake

Benjamin Netanyahu alizaliwa Tel Aviv mwaka 1949. Mwaka 1963, familia yake ilihamia Marekani baada ya baba yake, Benzion Netanyahu, mwanahistoria na mwanaharakati wa Kizayuni, kupata nafasi ya kazi ya kitaaluma.

Akiwa na umri wa miaka 18, Netanyahu alirejea Israel na kuhudumu jeshini kwa miaka mitano, akifikia cheo cha nahodha katika kikosi maalum cha Sayeret Matkal. Alijeruhiwa mwaka 1972 wakati wa operesheni ya kuwaokoa mateka kutoka katika ndege iliyotekwa nyara na wanamgambo wa Kipalestina, na pia alipigana katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1973.

Mwaka 1976, kaka yake Jonathan Netanyahu aliuawa alipokuwa akiongoza operesheni ya kuwaokoa mateka katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe nchini Uganda. Kifo chake kiliacha athari kubwa kwa familia hiyo, huku Jonathan akitukuzwa kama shujaa wa taifa nchini Israel.

Kwa kumbukumbu ya kaka yake, Netanyahu alianzisha taasisi ya kupambana na ugaidi. Mwaka 1982, aliteuliwa kuwa naibu mkuu wa ujumbe wa kidiplomasia wa Israel mjini Washington.

Hapo ndipo safari yake ya kuwa kiongozi wa umma ilipoanza kushika kasi. Uwezo wake wa kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha ulimfanya kuwa sauti maarufu ya kuitetea Israel katika vyombo vya habari vya Marekani.

Mwaka 1984, aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa mjini New York.

Kuingia madarakani

Netanyahu alijitosa katika siasa mwaka 1988 baada ya kurejea Israel, aliposhinda kiti cha ubunge kupitia chama cha Likud na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.

Baadaye alichaguliwa kuwa kiongozi wa Likud na mwaka 1996 akawa Waziri Mkuu wa Israel kufuatia uchaguzi wa mapema uliofanyika baada ya kuuawa kwa Yitzhak Rabin.

Alikuwa kiongozi mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuiongoza Israel na wa kwanza kuzaliwa baada ya kuanzishwa kwa taifa hilo mwaka 1948.

Ingawa alipinga vikali Mkataba wa Oslo wa mwaka 1993 kati ya Israel na Wapalestina, mwaka 1997 alisaini makubaliano yaliyoweka asilimia 80 ya mji wa Hebron chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Palestina. Pia alikubali kuondolewa kwa baadhi ya majeshi ya Israel kutoka maeneo ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, hatua iliyokosolewa na wanasiasa wa mrengo wa kulia.

Mwaka 1999, alipoteza uwaziri mkuu baada ya kushindwa katika uchaguzi na kiongozi wa Chama cha Labour, Ehud Barak, ambaye aliwahi kuwa kamanda wake jeshini.

Kurejea kwake kisiasa

Netanyahu alijiuzulu uongozi wa chama cha Likud na nafasi yake kuchukuliwa na Ariel Sharon.

Baada ya Sharon kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 2001, Netanyahu alirejea serikalini, kwanza akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na baadaye Waziri wa Fedha. Mwaka 2005 alijiuzulu kupinga uamuzi wa Israel kuondoa walowezi na wanajeshi wake kutoka Ukanda wa Gaza.

Fursa yake ya kurejea madarakani ilijitokeza mwaka huohuo, wakati Sharon alipojiondoa Likud na kuanzisha chama kipya cha Kadima. Netanyahu alirejea kuongoza Likud na mwaka 2009 akachaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili.

Akiwa madarakani, alikubali kusitishwa kwa muda kwa ujenzi wa baadhi ya makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi ili kufungua njia ya mazungumzo ya amani na Wapalestina. Hata hivyo, mazungumzo hayo yalivunjika mwaka 2010.

Ingawa mwaka 2009 alionyesha kuunga mkono kwa masharti kuundwa kwa taifa la Palestina sambamba na Israel, baadaye alibadili msimamo huo na kuwa mkosoaji mkubwa wa wazo hilo.

Katika kipindi chake cha uongozi, ujenzi wa makazi ya walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi uliongezeka kwa kasi, jambo ambalo wakosoaji wanasema limeathiri juhudi za kufanikisha suluhisho la mataifa mawili.

Masuala ya usalama pia yalitawala uongozi wake, huku migogoro kati ya Israel na makundi ya Wapalestina ikiendelea kujirudia Gaza na maeneo mengine.

Katika maisha yake ya kisiasa, Netanyahu amekuwa akiitaja Iran kuwa tishio kubwa zaidi kwa usalama wa Israel, akisisitiza kwa miaka mingi kuwa Tehran ilikuwa ikijaribu kupata silaha za nyuklia na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kali zaidi dhidi yake.

Kesi iliyovutia umma

Baada ya mwaka 2016, Netanyahu alianza kukabiliwa na uchunguzi wa tuhuma za ufisadi, ambao ulisababisha kufunguliwa mashtaka dhidi yake mwezi Novemba 2019. Anakabiliwa na tuhuma za rushwa, udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka katika kesi tatu tofauti.

Netanyahu amekanusha tuhuma zote, akisisitiza kuwa ni sehemu ya kampeni ya kisiasa inayolenga kumchafua. Mwezi Mei 2020, aliingia katika historia ya Israel kwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza kufikishwa mahakamani akiwa bado madarakani.

Pia amewahi kuomba msamaha wa rais, lakini Rais Isaac Herzog amesema juhudi za kufikia makubaliano ya kisheria zinapaswa kupewa nafasi kwanza. Zaidi ya miaka sita baadaye, kesi hiyo bado haijafikia hitimisho na usikilizwaji wake unaendelea.

Wakati huo huo, mpango wa serikali yake wa kufanya mageuzi makubwa katika mfumo wa mahakama ulizua maandamano makubwa nchini Israel, ukifichua mgawanyiko mkubwa wa kisiasa kuhusu mwelekeo wa demokrasia na utambulisho wa taifa hilo.

Ingawa mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba 2023 yalihamisha mjadala wa kitaifa kwenye masuala ya usalama na vita, tofauti hizo za kisiasa bado hazijatatuliwa huku Israel ikijiandaa kwa uchaguzi mwingine.

Trump ties

Kuingia kwa Donald Trump madarakani mwaka 2017 kuliimarisha zaidi uhusiano kati ya Marekani na Israel. Ndani ya mwaka mmoja, Trump alitambua rasmi Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, hatua iliyozua hasira katika nchi nyingi za Kiarabu lakini ikampa Netanyahu ushindi mkubwa wa kisiasa na kidiplomasia.

Mwaka 2020, Netanyahu aliusifu mpango wa amani wa Trump kati ya Israel na Wapalestina, akiuita "fursa ya karne". Hata hivyo, Wapalestina waliukataa wakidai ulikuwa na upendeleo mkubwa kwa Israel.

Netanyahu na Trump pia walishirikiana kwa karibu kuhusu suala la Iran. Kiongozi huyo wa Israel aliunga mkono uamuzi wa Trump wa kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran mwaka 2018 na kurejesha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Tehran.

Hata hivyo, uhusiano wao uliwahi kuyumba baada ya Netanyahu kumpongeza Joe Biden kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais wa Marekani mwaka 2020. Trump alijibu kwa kauli kali, akimshutumu kwa kutokuwa mwaminifu.

Baadaye, uhusiano kati ya viongozi hao ulirejea kuwa imara. Katika muhula wake wa pili, Trump ameendelea kumuunga mkono Netanyahu, ikiwemo katika mzozo wa Israel na Iran. Pia ametoa wito wa kusamehewa kwa Netanyahu katika kesi za ufisadi zinazomkabili na amemkaribisha mara kadhaa katika Ikulu ya White House.

Netanyahu amekutana na Trump mara nane tangu rais huyo arejee madarakani Januari 2025, zaidi ya kiongozi mwingine yeyote duniani.

Siku chache kabla ya uchaguzi, Trump alionyesha tena kumuunga mkono Netanyahu kupitia mtandao wake wa Truth Social, akimtaja kuwa "waziri mkuu shujaa" na kiongozi "mwenye nguvu, jasiri na mwenye akili" anayekabili upinzani mkubwa.

Kwa wengi, uchaguzi huu ni mtihani mkubwa kwa mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi na utata mkubwa zaidi katika historia ya Israel. Wafuasi wake wanaamini bado ndiye kiongozi bora wa kuhakikisha usalama wa taifa, huku wakosoaji wakisema juhudi zake za kuendelea kusalia madarakani zinaihatarisha Israel.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi