Ndani ya bomba la gesi ambako Ukraine inapigana vita

    • Author, Jonathan Beale
    • Nafasi, Defence correspondent, near Kupyansk
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Katika vita vya Ukraine na Urusi, uwanja mpya wa mapambano umeibuka chini ya ardhi, ndani ya bomba la zamani la gesi.

Kwa miezi saba sasa, wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakiishi na kupambana na wanajeshi wa Urusi ndani ya bomba hilo lililojengwa enzi za Umoja wa Kisovieti, katika eneo la Kharkiv, kaskazini mashariki mwa Ukraine.

Bomba hilo lina kipenyo cha zaidi ya mita moja tu, hivyo nafasi ni finyu kiasi cha kulazimisha wanajeshi kutambaa wanaposonga mbele. Hata hivyo, linawapa ulinzi kiasi dhidi ya droni ambazo zimejaa angani katika maeneo ya mstari wa mbele na zinazofanya iwe vigumu kwa pande zote mbili kusonga mbele.

Kwa Zanuda, ambaye amehusika katika kupanga operesheni hiyo ya chini ya ardhi, mbinu hii sasa ndiyo njia pekee ya kupambana. Anaielezea kama ulimwengu mpya wa mapambano, ingawa anakiri kuwa si rahisi.

"Ukiwa juu ya ardhi, huwa na nafasi ya kufanya ujanja, lakini hapa unaweza kukabiliana na adui ana kwa ana pekee."

Safari ya kufika katika eneo hilo la mapambano chini ya ardhi katika mkoa wa Kharkiv yenyewe ilidhihirisha hatari zilizopo. Tulisafiri kwa kasi kwa gari kupitia mashamba yaliyo wazi, kabla ya kuendelea kwa miguu katika ardhi yenye matope, tukisindikizwa na wanajeshi wa Ukraine waliokuwa na silaha zao tayari kwa matumizi, iwapo wangekutana na droni za Urusi.

Tulipofika kwenye lango la kuingia kwenye bomba, jambo la kwanza tulilokutana nalo ni harufu iliyosalia ya gesi pamoja na hewa chafu yenye uvundo.

Pande zote mbili hutumia sehemu zilizofunguliwa kwenye bomba hilo kufika juu ya ardhi, ambako mapigano mengi hufanyika. Zimechimba njia kutoka ardhini na kutumia vifaa vya kulehemu kutoboa chuma kigumu cha bomba hilo.

Urusi ndiyo iliyokuwa ya kwanza kutumia bomba hilo kuingia kwa siri katika mji wa Kupyansk, Septemba 2025.

Si mara ya kwanza kwa wanajeshi wa Urusi kutumia mabomba ya chini ya ardhi katika operesheni za kijeshi. Walitumia mbinu hiyo wakati wa kuuteka mji wa Avdiivka mwaka 2024, na mwaka uliopita walipojaribu kurejesha maeneo ya mkoa wa Kursk nchini Urusi yaliyokuwa yamepotea.

Hata hivyo, wanajeshi wa Ukraine wameanza kubadili mwelekeo wa mapambano hayo.

Gari maalumu la umeme hutumika kusafirisha wanajeshi na vifaa ndani ya bomba hilo.

Wanaliita metro ya Kupyansk. Gari hilo huenda likaharibika mara kwa mara. Tulipanda na kusafiri kwa dakika 40, tukiwa tumeinamisha vichwa na kukunja miguu. Kila linapovuka sehemu ambazo bomba limeunganishwa kwa kulehemu, hutikisika. Safari hiyo inafanana na mchezo wa kupandishwa na kushushwa katika uwanja wa burudani, lakini bila burudani yoyote.

Tulikuwa tukielekea kwenye sehemu ya bomba iliyofunguliwa, ambako wanajeshi wa Ukraine wamejenga maficho ya kuhifadhi risasi na vifaa. Nafasi ni finyu kiasi cha kutosha tu kusimama.

Hapo ndipo mwanajeshi anayejulikana kwa jina la Musician anaporatibu usafirishaji wa wanajeshi na vifaa. Amekuwa akiishi chini ya ardhi kwa muda mrefu, huku uso wake ukiwa umefunikwa na uchafu na udongo.

Musician ananiambia amekuwa akiishi hapo kwa miezi mitatu iliyopita, akitoka juu ya ardhi mara chache tu kwa muda mfupi ili kujisafisha au kwenda kujisaidia.

Mara kwa mara, tunasikia milio ya makombora ya mizinga kutoka juu. Anasema tuko karibu na eneo ambako pande mbili za mapambano zinakutana.

"Lakini chini ya ardhi ni salama."

Gari hilo linaendelea na safari yake kuelekea ndani zaidi ya bomba. Baada ya takribani nusu saa, linarudi likiwa na wanajeshi wengine, ambao miili na nyuso zao zimefunikwa na udongo. Wametoka kupambana katika maeneo yaliyo juu ya ardhi.

Gari hilo linaendelea na safari yake kuelekea ndani zaidi ya bomba. Baada ya takribani nusu saa, linarudi likiwa na wanajeshi wengine, ambao miili na nyuso zao zimefunikwa na udongo. Wametoka kupambana katika maeneo yaliyo juu ya ardhi.

Nyuso zao zilizofunikwa na vumbi zinaonyesha hali ya nafuu.

"Ni afadhali ndani ya bomba kwa sababu droni haziruki hapa, wala makombora ya mizinga au mabomu yanayoteleza angani," anasema Vovochka, ambaye amekuwa akipigana juu ya ardhi kwa wiki tatu zilizopita.

Lakini mapambano yamefanyika pia ndani ya bomba hilo. Operesheni ya Veles, iliyopewa jina la 'mungu wa ulimwengu wa chini ya ardhi 'katika mitholojia ya Waslav, ilianza mwezi Aprili. Tangu wakati huo, Ukraine inasema imesonga mbele kilomita 15 ndani ya bomba hilo.

Imekuwa kazi ya taratibu, ngumu na inayochosha mwili, huku hofu ya kukutana na adui ikitawala kila wakati.

Tuliporudi juu ya ardhi, tulikutana na baadhi ya wanajeshi kutoka Brigedi ya 13 ya Khartiia ya Kikosi cha Walinzi wa Taifa la Ukraine, ambao wameshiriki katika operesheni hiyo. Kazi yao ya kwanza ilikuwa kuondoa uchafu, maji na vizuizi vilivyowekwa na wanajeshi wa Urusi ndani ya bomba.

Wanajeshi wa Ukraine wanasema baadhi ya vizuizi hivyo vilikuwa na mitego ya vilipuzi au vilikuwa vimerundikwa pamoja na miili ya wanajeshi wa Urusi.

"Tulipokuwa tukiviondoa au kuvipanda ili kuvuka, hatukujua kabisa kilichokuwa chini yake," anasema Chyzh.

Anasema hatari nyingine ilikuwa risasi zilizokuwa zikigonga sehemu za bomba na kurudi kuelekea upande mwingine, wakati walipojaribu kusonga mbele.

"Huwezi kujua risasi itakwenda wapi au itaruka kuelekea upande gani baada ya kugonga."

Mwanajeshi mwenzake, Kort, anasema: "Tulikuwa wote tukifyatua risasi na kuwasukuma nyuma."

Ukraine inasema katika kipindi cha operesheni hiyo, iliwaua zaidi ya wanajeshi 100 wa Urusi na kuwateka wengine 30.

"Ndiyo, kulikuwa na miili," anasema Kort. "Nililazimika hata kulala karibu nayo."

Uzoefu wa kamanda wao wa zamani akiwa mchimbaji migodi uliwasaidia wanajeshi kukabiliana na changamoto za kimwili na kisaikolojia za mapambano chini ya ardhi.

Katika jengo lililo juu ya ardhi, Biashym anaendelea kuwasiliana na wanajeshi wake ambao bado wako ndani ya bomba. Nyuma yake kuna kabati lililojaa dawa.

Wanajeshi walioko ndani ya bomba hutumia muda mwingi wakiwa wamepiga magoti, hali inayowasababishia michubuko. Biashym anakiri kuwa baadhi yao wamekuwa wakipatwa na hofu kali kutokana na kuishi katika eneo lenye nafasi finyu kiasi hicho, huku wengine wakipata shida ya kupumua.

Mamia ya wapiganaji wa kujitolea kutoka Colombia pia wamehusika katika operesheni hiyo, wakiwa sehemu ya Kikosi cha 23 cha RUG.

Wapiganaji wa kigeni wamekuwa wakisaidia kuongeza idadi ya wanajeshi wa Ukraine, ambayo imepungua kutokana na vita. Mmoja wa wapiganaji hao kutoka Colombia, anayejulikana kwa jina la Gecko, ananiambia iliwachukua siku 30 kusafisha sehemu ya bomba yenye urefu wa mita 500 pekee.

"Il ilikuwa ngumu, kulikuwa na joto na nilikuwa na hofu ndani ya bomba," anasema. "Lakini wakati fulani nilijiambia, sawa, nikabiliane na hali hii na tuendelee kusonga mbele."

Mapambano ndani ya bomba hilo bado hayajaisha.

Wanajeshi wa Urusi, kama wale wa Ukraine, wamejenga ngome za kujihami ndani ya bomba. Bado wanajaribu kuingia kwa siri katika maeneo yanayodhibitiwa na Ukraine, wakitumia njia za chini ya ardhi kuingia na kutoka kwenye bomba.

Kutoka katika chumba cha kudhibiti operesheni kilicho juu ya ardhi, tulishuhudia droni za Ukraine zikishambulia jaribio jingine la wanajeshi wa Urusi la kupenya na kuzunguka upande wa vikosi vya Ukraine.

Ingawa baadhi ya mapambano yanafanyika chini ya ardhi, vita bado vinaendelea juu ya ardhi na angani. Operesheni hiyo imehusisha mbinu mbalimbali za kijeshi kwa pamoja.

Hata hivyo, Zanuda, ambaye ni mkuu wa kitengo cha mipango katika Brigedi ya 13 ya Khartiia, anaamini kuwa mapambano ya aina hii ndiyo yatakayokuwa njia bora zaidi ya kupigana katika siku zijazo.

"Mapambano ya ardhini sasa karibu hayawezekani," anasema, akiongeza kuwa "kila mtu anaelewa kuwa kwa sasa, njia pekee ya kupigana ni chini ya ardhi."

Anaamini kuwa operesheni kama hiyo zitakuwa nyingi zaidi siku zijazo.

"Mabomba yapo kila mahali," anasema. "Unapaswa kukumbuka kuwa enzi za Umoja wa Kisovieti, mafuta, gesi na amonia vilisafirishwa kwenda Ulaya, huku njia nzima ya usafirishaji ikipitia Ukraine."

Kwa uhalisia, operesheni hiyo imekuwa kazi ya kikatili, yenye kuchosha na hatari, katika mazingira magumu sana.

Ukraine imechukua miezi saba kusafisha na kudhibiti kilomita 15 za bomba hilo.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amepongeza operesheni hiyo akisema imefanikiwa.

Imeisaidia Ukraine kurejesha baadhi ya maeneo iliyopoteza na kuongeza morali ya wanajeshi, lakini yenyewe haijabadilisha mwelekeo wa vita kwa ujumla.