Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
CHADEMA: Hatutashiriki katika maridhiano ya kudanganyana
Chama hicho kimetoa mapendekezo kadhaa kabla ya kushiriki katika mazungumzo ya maridhiano ambayo yalikuwa yamependekezwa na serikali ya Tanzania.
Muhtasari
- CHADEMA: Hatutashiriki katika maridhiano ya kudanganyana
- Tumedungua ndege isiyo na rubani ya Marekani - Iran
- Maxence Melo atunukiwa tuzo ya kimataifa ya haki za binadamu
- Trump awasili Ufilipino kuanza ziara ya siku tatu bara Asia
- Ukraine yashambulia daraja la Crimea kwa makombora na droni
- Muhoozi atangaza kifungo cha miaka 10 kwa wanaomtukana Rais Museveni
- Papa Leo apinga pendekezo la kuruhusu mapadri waliooa kuhudumu
- Raia wanane wa Nigeria wakamatwa Canada kwa wizi wa magari ya kifahari
- Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji akabiliwa na kesi ya kuchochea maandamano baada ya uchaguzi
- Urusi imesema imefanya shambulio kubwa zaidi la droni dhidi ya Ukraine tangu kuanza kwa vita mwaka 2022
- Iran: Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa tu iwapo masharti saba ya Iran yatakubaliwa
- Ripoti: Ajali ya helikopta iliyomuua Chivayo isingeweza kuepukika
- Muhoozi aendelea kusisitiza azma ya kuwania Urais Uganda
- Tems, Burna Boy, Wizkid na Ayra Starr waongoza Waafrika kuwania tuzo za Grammy 2027
- Mtaalamu wa uchunguzi: Jeffrey Epstein aliuawa gerezani, hakujinyonga
- Imran Khan Aomba Huduma za Matibabu Kupitia Mahakama
- Makamu wa Rais wa Marekani: Hatutaruhusu vita vya Iran kudumu kwa miaka miwili
- Kocha wa Ureno Ajibu Shutuma za Mama yake Ronaldo
- Manchester United yamuwinda tena Lewis Hall- Tetesi za Jumanne
- Hitilafu ya kiufundi yaathiri huduma za benki kadhaa Marekani
- Trump kukutana na Xi Jinping na Vladimir Putin katika mkutano wa kihistoria
Moja kwa moja
Faidha Ngaga
CHADEMA: Hatutashiriki katika maridhiano ya kudanganyana
Aina yoyote ya mazungumzo hayawezi kufanyika katika mazingira tulio nayo kwa sasa, hii ni kauli ya naibu mwenyekiti wa chama cha CHADEMA John Heche.
Chama hicho kimetoa mapendekezo kadhaa kabla ya kushiriki katika mazungumzo ya maridhiano ambayo yalikuwa yamependekezwa na serikali ya Tanzania.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni:
- Lazima mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, aachiliwe huru.
- Watu ambao wametekwa, kupotezwa,na viongozi wa chama wanaoshikiliwa kwa sababu za kisiasa waachiliwe huru.
- Mpatanishi huru anayeweza kuleta pande zote mbili pamoja zinazozozana kuongoza maridhiano.
Kulingana na naibu mwenyekiti wa CHADEMA lazima pande zote mbili zikubali kuwa kuna matatizo na changamoto ambazo zinafaa kutatuliwa kabla ya kuanza mazungumzo ya maridhiano.
“Hakuna mazungumzo yoyote yenye tija yanaweza kufanyika bila CHADEMA, hatuwezi kushiriki katika mazungumzo yenye uwongo na kudanganyana”
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, hapo jana alipendekeza kuundwa kwa tume ya upatanishi na maridhiano ambayo pia itaratibu maandalizi ya mchakato wa marekebisho ya Katiba, alitoa tamko hilo baada ya kukutana na baraza la vyama vya siasa.
Mkutano wa jana ni mfufululizo wa jitihada za maridhiano ya kisiasa nchini humo
Tume hiyo mpya ya Maridhiano, itashirikisha pia vyama vitano vya kisiasa ikiwemo Chadema na ACT Wazalendo.
Serikali ya tanzania hata hivyo imekanusha kuhusika na masuala ya utekekaji. lakini pia wamesisitiza kwa maamuzi ya mahakama kuheshimiwa mara baada ya hukumu ya kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu.
Soma pia:
Tumedungua ndege isiyo na rubani ya Marekani - Iran
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imesema kuwa Iran imedungua ndege ya Marekani isiyo na rubani aina ya MQ-1, iliyokuwa ikifanya upelelezi na operesheni za kijeshi, kusini mwa Kisiwa cha Qeshm.
IRGC imesema ndege hiyo ililengwa kwa kutumia mfumo wake wa ulinzi wa anga, ikiwa ndengde ya 18 aina ya MQ-1 kudunguliwa na Iran.
Mapema leo, Jeshi la IRGC, lilitangaza kuwa lilikuwa limeteka ndege nyingine ya Marekani isiyo na rubani aina ya MQM-170.
Kituo kikuu kinachoendesha oparesheni za kijeshi za Marekani (CENTCOM) imekanusha taarifa kuwa, ndege zao zisizo na rubani zililengwa na Iran.
Soma pia:
Maxence Melo atunukiwa tuzo ya kimataifa ya haki za binadamu
Mwanzilishi wa mtandao maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki wa Jamii Forums Maxence Melo, ameshinda tuzo ya Haki za Binadamu ya Ubalozi wa Uholanzi ya mwaka 2026 (Netherlands Human Rights Embassy Tulip Award), kutokana na mchango wake kutetea uhuru wa kujieleza na haki za kidijitali nchini Tanzania.
Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvoets, amekaririwa na vyombo vya habari nchini humo kuwa Melo ametambuliwa kwa kazi yake kupitia JamiiForums katika kukuza mijadala ya umma na kulinda haki za watumiaji wa majukwaa ya kidijitali.
Melo ametambuliwa kwa mchango wake katika mageuzi ya sera, ikiwemo kuongoza muungano ulioshiriki kutetea kupitishwa kwa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi nchini Tanzania.
Kupitia ushindi huo Melo atapata kikombe cha shaba chenye umbo la ua la tulip, zawadi ya euro 5,000 pamoja na fursa za mafunzo, kujenga mtandao wa kimataifa na kutambuliwa kupitia vyombo vya habari.
Tuzo hiyo hutolewa na balozi za Uholanzi katika nchi mbalimbali duniani kwa kutambua watu binafsi na taasisi zinazochangia kukuza na kulinda haki za binadamu.
Melo ni miongoni mwa waasisi wa mtandao wa Jamii Forum, mtandao uliokuwa ukiibua masuala ya rushwa na kusaidia kushinikiza uwajibikaji wa viongozi wa kisiasa.
Trump awasili Ufilipino kuanza ziara ya siku tatu bara Asia
Rais wa Marekani Donald Trump amewasili nchini Ufilipino, ambapo amekutana na viongozi washirika wa Marekani ikiwemo Japan, India, Australia katika siku yake ya kwanza katika ziara ya bara Asia.
Trump hapo baadaye anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi, Vladimir Putin, na rais wa China, Xi Jinping.
Trump aliwasili katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila, mwishoni mwa mkutano wa kilele wa mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia, na kuanza ziara yake ya siku tatu katika eneo hilo kwa kuhudhuria mkutano wa kwanza baada ya miaka miwili wa kundi la Quad, linalojumuisha mataifa manne ya kidemokrasia ya eneo la Indo-Pasifiki.
"Nchi zetu zinaunda nguzo nne za eneo huru, lililo wazi, lenye utulivu na ustawi la Indo-Pasific," Trump alisema katika hotuba yake kabla ya mkutano huo.
Ziara ya Trump ya siku tatu bara Asia, inajumuisha kuhudhuria mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasific (APEC) mjini Shenzhen, China.
Ziara hiyo pia inafanyika wakati kukiwa na madai mapya ya ujasusi na hatua mpya za Marekani za kuzuia China kupata teknolojia ya hali ya juu za akili unde (AI).
Soma pia:
Ukraine yashambulia daraja la Crimea kwa makombora na droni
Ukraine imeshambulia daraja la Crimea, ambalo ni njia kuu inayounganisha Urusi na eneo la Crimea linalokaliwa na Urusi, kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora.
Ukraine inasema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Urusi yaliyolenga miundombinu ya Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema shambulio hilo lilikuwa hatua ya saba ya operesheni iliyochukua wiki kadhaa, iliyoandaliwa na kuratibiwa na idara ya usalama ya Ukraine (SBU) kwa ushirikiano na makao makuu ya jeshi.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin amejibu hatua za Ukraine kwa kusema kuwa kuwa daraja hilo litajengwa upya na kwa ubora zaidi kuliko lilivyokuwa awali.
Hapo jana, vikosi vya Urusi vilishambulia madaraja mawili yanayopita juu ya Mto Dnipro katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, pamoja na miundombinu mingine,kulingana na taarifa aliyotoa Meya wa mji huo Vitali Klitschko.
Soma pia:
Muhoozi atangaza kifungo cha miaka 10 kwa wanaomtukana Rais Museveni
Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametishia kuwafunga jela kwa miaka 10 watu watakaomtukana au kumdhalilisha Rais Yoweri Museveni, mwanafamilia wa Museveni ikiwemo yeye mwenyewe.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa X, Muhoozi, ambaye pia ni mwanaye Rais Museveni, alitoa onyo jingine kwa mashirika ya habari ya kimataifa yanayofanya kazi nchini Uganda, akidokeza kuwa serikali inapanga kuanzisha sera mpya itakayosimamia jinsi wanaendesha shughuli zao.
"Karibuni nitatangaza sera mpya kuhusu shughuli za vyombo vyote vya habari vya kigeni nchini Uganda. Siku zao za kuitukana nchi yetu zimefika mwisho," aliandika Muhoozi.
Hata hivyo, bado hajaeleza kwa kina sera hiyo inayopendekezwa wala kutaja hatua ambazo vyombo vya habari vya kigeni vinaweza kuchukuliwa.
Vitisho hivyo vinatolewa takriban siku kumi baada ya shirika la habari la AFP kuripoti, likinukuu vyanzo ndani ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), kuwa maafisa wakuu wa chama hicho walikuwa wamekataa pendekezo la Rais Museveni la kumtaka mwanawe kuwa mrithi wake.
Hata hivyo, NRM imekanusha taarifa hizo.
Licha ya katiba ya Uganda pamoja na kanuni za maadili za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) kuwataka maafisa wa kijeshi kutokuwa na misimamoya kisiasa na kuwazuia kushiriki katika shughuli za kisiasa za vyama, Muhoozi amekuwa akieleza mara kwa mara nia yake ya kuwania urais na kutoa vitisho dhidi ya viongozi wa upinzani.
Soma pia:
Papa Leo apinga pendekezo la kuruhusu mapadri waliooa kuhudumu
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo, amesema kwa sasa hana mpango wa kubadilisha mafundisho ya Kanisa hilo, ili kuruhusu mapadri waliooa kuhudumu, akisema suala hilo linaweza kuleta mgawanyiko miongoni mwa waumini wa Kanisa hilo, lenye takriban waumini bilioni 1.4.
Haya ni maoni yake ya kwanza hadharani,kuhusu pendekezo ambalo limekuwa likiungwa mkono kwa muda mrefu na baadhi ya Wakatoliki.
Ingawa Papa Leo hakufunga mlango wa uwezekano wa kuruhusu mapadri waliooa siku zijazo, aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa ndani ya ndege yake wakati akirejea Rome hii leo, baada ya ziara ya siku 12 Amerika Kusini, kuwa kipaumbele chake ni kuimarisha umoja ndani ya Kanisa Katoliki duniani.
"Huenda baadhi ya mambo yakabadilika siku zijazo. Hata hivyo, kwa sasa ninaamini kuwa sehemu muhimu ya huduma yangu ndani ya Kanisa ni kuponya majeraha na kuwaunganisha watu," alisema Papa Leo.
Kiapo cha kutooa
Mapadri wengi wa Kanisa Katoliki huapa kutooa na kuishi maisha ya useja.
Wanaounga mkono kuruhusiwa kwa mapadri waliooa wanasema hatua hiyo inaweza kuwavutia wanaume wengi zaidi kujiunga na huduma ya ukuhani, na hivyo kupunguza uhaba wa mapadri ambao umekuwa changamoto kubwa katika maeneo mengi ya mataifa ya Magharibi.
Papa Francis, aliyefariki Mwezi Aprili 2025 baada ya kuliongoza Kanisa Katoliki kwa miaka 12, pia alikataa kuidhinisha mabadiliko kuhusu suala hilo.
Soma pia:
Raia wanane wa Nigeria wakamatwa Canada kwa wizi wa magari ya kifahari
Polisi nchini Canada wamewakamata watu 12, wakiwemo raia wanane wa Nigeria, baada ya uchunguzi wa mtandao wa wizi wa magari.
Washukiwa hao wanatuhumiwa kuiba magari ya kifahari na kuyasafirisha kwa njia ya meli hadi Afrika Magharibi.
Polisi katika eneo la Peel, jimbo la Ontario, wamesema wamefanikiwa kurejesha magari 96 ya kifahari, yaliyokuwa yamefichwa ndani ya makontena kwa ajili ya kusafirishwa.
Magari hayo yenye thamani ya dola milioni 4.5 za Marekani, yalikuwa yakitarajiwa kusafirishwa kupitia bandari za Canada.
Kudhibiti usafirishaji haramu wa magari kutoka Amerika Kaskazini na Ulaya kwenda nchi za Afrika umekuwa suala linalotatiza idara za usalama haswa nchini Canada.
Washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 231, huku hati za kukamatwa kwa washukiwa wengine zikitolewa.
Polisi wamesema baadhi ya watuhumiwa wanaweza kufukuzwa nchini humo baada ya kukamilika kwa kesi zao za jinai.
Soma pia:
Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji akabiliwa na kesi ya kuchochea maandamano baada ya uchaguzi
Wasiwasi umeongezeka katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, huku idadi kubwa ya maafisa wa polisi wakitumwa mitaani kudumisha usalama, wakati kiongozi wa upinzani Venâncio Mondlane akifikishwa mahakamani, kuhusiana na maandamano yaliyosababisha vifo vya watu wengi baada ya uchaguzi wa mwaka 2024 uliokumbwa na utata.
Venâncio Mondlane anakabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwemo kuchochea ugaidi na uasi wa kiraia, baada ya maandamano yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu.
Hata hivyo, kiongozi huyo amekana kuhusika na makosa yoyote.
Ulinzi umeimarishwa katika eneo linalozunguka Mahakama ya Juu mjini Maputo, huku mamlaka zikihofia uwezekano wa kuzuka kwa wimbi jipya la maandamano kutoka kwa wafuasi wake.
Polisi wamewaomba wananchi kufuatilia kesi hiyo kwa utulivu na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Mondlane, ambaye alipinga matokeo ya uchaguzi wa urais baada ya ushindi wa Daniel Chapo wa chama tawala cha Frelimo, aliishutumu mamlaka kwa udanganyifu na kutoa wito wa raia kuandamana.
Maandamano hayo yaliendelea kwa miezi kadhaa, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakizishutumu vikosi vya usalama kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, likinukuu mashirika ya kiraia nchini humo, lilisema kuwa zaidi ya watu 300 waliuawa wakati wa machafuko hayo,hata hivyo, polisi wa Msumbiji walitaja idadi ya waliofariki kuwa 96, wakiwemo maafisa 17 wa polisi.
Soma pia:
Urusi yasema imeishambulia Ukraine kwa droni nyingi zaidi tangu 2022
Maafisa wa kijeshi wa Urusi wamesema kuwa vikosi vyao vilifanikiwa kudungua na kuharibu droni 2,049 pamoja na makombora manne ya masafa marefu ndani ya saa 24 zilizopita.
Kwa mujibu wa Meya wa Moscow, Sergei Sobyanin, takriban droni 600 zilielekezwa katika mji mkuu huo pekee. Wakati huo huo, Kyiv ilipokea rekodi ya tahadhari 17 za mashambulizi ya anga ndani ya siku moja.
Mashambulizi hayo yameripotiwa kusababisha vifo vya watu wasiopungua saba, huku zaidi ya watu 50,000 wakikosa umeme kutokana na mashambulizi yaliyolenga miundombinu ya nishati.
Mashambulizi hayo makali yamekuja siku chache baada ya wajumbe kutoka Marekani, Ukraine na Urusi kufanya mazungumzo yaliyolenga kutafuta njia ya kumaliza vita vinavyoendelea.
Vita vya Ukraine vilianza mwezi Februari 2022 baada ya Urusi kuanzisha uvamizi kamili dhidi ya nchi hiyo.
Licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoendelea kutafuta suluhu ya kumaliza vita hivyo, mashambulizi ya pande zote mbili yanaonyesha kuwa bado hakuna dalili za mapigano kupungua kwa sasa.
Kuongezeka kwa matumizi ya droni na mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu kumeendelea kuathiri maisha ya maelfu ya raia, huku hofu ya kuongezeka kwa mzozo huo ikizidi kutanda katika eneo lote la Ulaya Mashariki.
Unaweza pia kusoma:
Iran: Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa tu iwapo masharti saba ya Iran yatakubaliwa
Iran imeendelea kusisitiza msimamo wake kuhusu Mlango wa Hormuz, baada ya msemaji wa jeshi la nchi hiyo Amir Akraminia kusema kuwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta haitafunguliwa mpaka masharti saba ya Tehran yakubaliwe. Kauli hiyo imeambatana na onyo kwa meli dhidi ya kutumia njia ambazo hazijaidhinishwa na Iran, huku ikiongeza tahadhari kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi katika eneo hilo.
Akizungumza mjini Bandar Abbas, Akraminia amesema kuwa vikosi vya jeshi la Iran viko katika hali ya utayari wa hali ya juu na vinadhibiti kimkakati sehemu za mashariki na magharibi za Mlango wa Hormuz. Alisisitiza kuwa njia hiyo muhimu ya majini itafunguliwa tu ikiwa Marekani itakubali masharti ya Iran.
Kwa mujibu wa afisa huyo, meli zitakazotumia njia ambazo hazijaidhinishwa na Iran zinajiweka katika hatari ya kukumbana na mabomu ya majini, mashambulizi ya moto au milipuko. Aliongeza kuwa usalama wa meli unaweza kuhakikishwa tu kwa kufuata njia zilizoelekezwa na jeshi la Iran na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Msemaji huyo pia alionya kuhusu uwezekano wa kuzuka tena kwa mzozo wa kijeshi, akisema kuwa ikiwa kutatokea makosa mengine ya kimahesabu au baadhi ya nchi za eneo hilo zitatii kile alichokiita matakwa haramu ya Washington, basi kambi na maslahi ya adui vitakabiliwa na mashambulizi ya haraka na makali yatakayovuka mipaka ya kijiografia.
Unaweza pia kusoma:
Ajali ya helikopta iliyomuua Chivayo haingekuwa na manusura - Ripoti
Ripoti ya awali ya uchunguzi kuhusu ajali ya helikopta iliyomuua mfanyabiashara Wicknell Chivayo, mkewe Lucy Muteke na watu wengine watatu, imebaini kuwa hakuna aliyekuwa na uwezekano wa kunusurika katika ajali hiyo.
Helikopta hiyo ilianguka katika shamba la Kudenga tarehe 30 Septemba 2026.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nguvu kubwa iliyotokana na kusimama kwa kasi kwa helikopta wakati wa ajali, pamoja na ukubwa wa moto uliozuka baada ya kugonga ardhi, vilifanya ajali hiyo isiweze kunusurika.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa mwili wa helikopta ulisambaratika kutokana na athari za ajali, na kusababisha watu wote watano waliokuwa ndani kurushwa nje.
Hata hivyo, uchunguzi bado unaendelea, huku ripoti ya mwisho ikitarajiwa kutolewa baada ya kukamilika kwa uchambuzi zaidi wa ushahidi.
Soma Pia:
Muhoozi aendelea kusisitiza azma ya kuwania Urais Uganda
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema atagombea urais wa nchi hiyo baada ya baba yake, Rais Yoweri Museveni, kuondoka madarakani, akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayemzuia kutimiza azma hiyo.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X Jumanne, Muhoozi amesema matumaini yake yapo kwa Mwenyezi Mungu na wananchi wa Uganda.
"Nitagombea urais wa nchi hii baada ya Mzee. Hakuna mtu atakayenizuia. Ninaweka matumaini yangu kwa Mwenyezi Mungu na kwa wananchi wenzangu," ameandika.
Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) kukanusha taarifa kwamba kamati yake kuu ilikataa pendekezo la kumuunga mkono Muhoozi kuwa mrithi wa Museveni.
Katibu Mkuu wa NRM, Richard Todwong, alieleza kuwa taarifa hizo kuhusu kikao cha faragha cha kamati hiyo kilichofanyika Novemba 10 zilikuwa za uongo, akisema chama kitatoa maamuzi yake kupitia njia rasmi kwa wakati unaofaa.
Kauli ya Muhoozi pia inaongeza maswali kuhusu uwezekano wa mabadiliko ya uongozi ndani ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), huku kukiwa na mvutano kuhusu nafasi ya Muhoozi katika siasa za nchi hiyo.
Hata hivyo, bado haijabainika iwapo atapata uungwaji mkono wa kutosha ndani ya chama ili kutimiza azma yake ya kuwania urais.
Unaweza pia kusoma:
Tems, Burna Boy, Wizkid na Ayra Starr waongoza Waafrika kuwania tuzo za Grammy 2027
Wasanii wa Nigeria, akiwemo Tems, Burna Boy, Wizkid na Ayra Starr, ni miongoni mwa wasanii wa Afrika walioteuliwa kuwania tuzo za Grammy za mwaka 2027.
Tems amepata jumla ya uteuzi nne, ukiwemo wa Best R&B Solo Performance, ambako atachuana na Beyoncé, pamoja na vipengele vya Global Music Album na African Music Performance.
Burna Boy pia ameteuliwa kupitia ushirikiano wake na Shakira, huku Wizkid na Asake wakipata uteuzi katika vipengele mbalimbali. Ayra Starr naye ni miongoni mwa wasanii wa Nigeria waliotajwa.
Kwa upande mwingine, mwimbaji wa Uingereza Raye ameongoza kwa kupata uteuzi 11, huku Rosalía wa Uhispania akipata uteuzi tisa kupitia albamu yake Lux. Mwimbaji mkongwe wa Marekani Dolly Parton, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 80, pia ametambuliwa kwa uteuzi tatu.
Tuzo hizo za 69 za Grammy zinatarajiwa kufanyika Februari 7, 2027, jijini Los Angeles, Marekani.
Unaweza pia kusoma:
Mtaalamu wa uchunguzi: Jeffrey Epstein aliuawa gerezani, hakujinyonga
Mtaalamu wa uchunguzi wa maiti anaamini kuwa Jeffrey Epstein, aliyepatikana na hatia ya makosa ya kingono, aliuawa akiwa gerezani na kwamba kifo chake hakikutokana na kujiua.
Michael Freeman, profesa wa chuo kikuu na mtaalamu wa uchunguzi wa maiti baada ya kifo, ameiambia kipindi cha Newsnight cha BBC kuwa baada ya kupitia ripoti ya uchunguzi wa maiti ya Epstein iliyofanyika New York, alihitimisha kuwa Epstein alinyongwa hadi kufa na huenda muuaji wake alimshambulia kwa nyuma.
Hata hivyo, daktari aliyefanya uchunguzi wa maiti ya Epstein mwaka 2019 alihitimisha wakati huo kuwa majeraha yaliyobainika mwilini mwake yalilingana na hali ya mtu aliyejiua. Daktari huyo pia alisema hakukuwa na dalili za Epstein kujitetea dhidi ya shambulizi, jambo ambalo lingetarajiwa iwapo angeuawa.
Jeffrey Epstein alipatikana amefariki dunia katika gereza moja mjini New York, Agosti 10, 2019, wakati akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kusafirisha binadamu kwa madhumuni ya unyanyasaji wa kingono.
Nyaraka zilizopatikana katika kisiwa chake pamoja na madai kwamba Epstein aliwatumia wasichana wadogo kufanya ngono na watu mashuhuri vimekuwa chanzo cha utata mkubwa nchini Marekani kwa muda mrefu.
Kufichuliwa hadharani kwa taarifa zote zinazohusiana na kesi hiyo, hususan majina ya watu mashuhuri waliotembelea kisiwa cha Epstein au waliokuwa na uhusiano wa kijamii naye, bado ni miongoni mwa madai ya maelfu ya watu wanaoandamana kupinga suala hilo.
Unaweza pia kusoma:
Imran Khan aomba huduma za matibabu kupitia mahakama
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan, anayeshikiliwa katika gereza la Adiala mjini Rawalpindi, ametuma barua kwa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Kikatiba ya Shirikisho na Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Islamabad kupitia wakili wake, Salman Safdar.
Katika barua hiyo, Khan ameomba hatua za haraka zichukuliwe kushughulikia hali yake ya afya pamoja na ya mkewe, Bushra Bibi.
Khan amesema afya na maisha yake vinakabiliwa na vitisho vikubwa. Wakati huo huo, mkewe kupitia mawakili wake amewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Islamabad akitaka ahamishwe kutoka gerezani na kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Wiki iliyopita, Imran Khan alipelekwa katika Hospitali ya Pakistan Institute of Medical Research (PIMS) jijini Islamabad kwa uchunguzi wa afya na kuendelea na matibabu ya macho.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka hospitalini hapo, Khan alifanyiwa vipimo mbalimbali vya afya, ikiwemo uchunguzi wa macho kulingana na maelekezo ya daktari bingwa wa macho.
Hata hivyo, Waziri wa Masuala ya Bunge wa Pakistan, Tariq Fazal Chaudhry, amepinga madai ya Khan, akisema hayana msingi wa ukweli.
Chaudhry alisema afya ya Waziri Mkuu huyo wa zamani haiko hatarini na kwamba madaktari wamethibitisha hali yake ni nzuri.
Serikali ya Pakistan imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa Khan, ambaye anaugua tatizo la Central Retinal Vein Occlusion amakuziba kwa mshipa mkuu wa retinakatika jicho lake la kulia, amekuwa akipatiwa huduma bora za matibabu akiwa gerezani na hajawahi kucheleweshewa matibabu anayohitaji.
Unaweza pia kusoma:
Makamu wa Rais wa Marekani: Hatutaruhusu vita vya Iran kudumu kwa miaka miwili
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema utawala wa Rais Donald Trump hautaruhusu vita dhidi ya Iran kugeuka kuwa vita vya muda mrefu vinavyoweza kudumu kwa miaka miwili au zaidi.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Fox News, Vance alisema mpango wa nyuklia wa Iran bado ni tishio kwa Marekani, lakini akaahidi kuwa serikali haitajiingiza katika vita visivyo na mwisho.
"Tuliwaahidi Wamarekani kwamba hatutashiriki tena katika vita visivyoisha," alisema Vance.
Aliongeza kuwa Rais Trump anaamini mpango wa nyuklia wa Iran lazima uharibiwe kwa sababu unaleta tishio kwa Marekani, lakini akasisitiza kuwa hawataruhusu mzozo huo kuendelea kwa miaka 10, 15 au hata miwili.
Kauli hizo zinaonekana kurejelea miaka miwili iliyobaki katika muhula wa pili wa urais wa Trump.
Marekani na Israel zilianza vita dhidi ya Iran mwishoni mwa Februari. Katika kipindi hicho, Trump amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa Iran haiwezi kuruhusiwa kumiliki silaha za nyuklia.
Kwa upande wake, Iran imekuwa ikisisitiza kwa miaka mingi kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani na hauna lengo la kutengeneza bomu la nyuklia.
Kauli za Vance zimekuja siku chache baada ya Trump kusema amempa jukumu la kushughulikia madai ya ufisadi katika majimbo yanayoongozwa na chama cha Democratic, huku akimuondoa kwenye mazungumzo na usimamizi wa vita dhidi ya Iran.
Unaweza pia kusoma:
Kocha wa Ureno ajibu shutuma za mama yake Ronaldo
Kocha wa timu ya taifa ya Ureno, Jorge Jesus, amejibu kauli za mama wa Cristiano Ronaldo, Dolores Aveiro, aliyedai kuwa mwanawe alitendewa isivyo haki na benchi la ufundi la timu hiyo kabla ya kutangaza kustaafu soka la kimataifa.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, alitangaza kustaafu kuichezea Ureno tarehe 5 Novemba, akihitimisha safari ya miaka mingi iliyomshuhudia kucheza mechi 234 na kufunga mabao 146 akiwa na timu ya taifa.
Kabla ya kustaafu, Ronaldo alifungiwa kwa siku 30 na kutozwa faini baada ya kuondoka kambini mwezi Septemba alipofahamishwa kuwa hangeanza katika kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Ligi ya Mataifa dhidi ya Denmark.
Katika mechi ya kwanza ya Ureno tangu Ronaldo atangaze kustaafu, timu hiyo ilichapwa mabao 4-1 nyumbani na Denmark. Akizungumza kwenye hafla ya Sporting, Dolores Aveiro alisema mwanawe alihuzunishwa na jinsi alivyotendewa.
"Alidanganywa. Mimi pia nimehuzunika. Kushindwa kule kulistahili. Kwa kweli nilifurahia," alisema Aveiro.
Akizungumzia kauli hizo kabla ya mchezo wa Ligi ya Mataifa dhidi ya Wales, Jorge Jesus alisema anamheshimu sana mama wa Ronaldo.
"Sasa nahitaji kujibu kauli za mama wa Cristiano Ronaldo? Ni mwanamke ninayemheshimu sana. Alipitia mengi kuwalea watoto wake," alisema kocha huyo.
Alipoulizwa kama mjadala kuhusu kustaafu kwa Ronaldo utaisha hivi karibuni, Jesus alisema hawezi kujua.
"Sijui mjadala huu utaisha lini. Mkiendelea kuuliza maswali kuhusu Ronaldo, nitaendelea kujibu," alisema.
Unaweza pia kusoma:
Manchester United yamuwinda tena Lewis Hall- Tetesi za Jumanne
Manchester United imeambiwa haitakuwa rahisi kumsajili beki wa Newcastle, Lewis Hall, kwani klabu hiyo haitaki kuuza mchezaji huyo Januari.
Kiungo wa Arsenal, Martin Zubimendi, anafikiria mustakabali wake kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, huku Chelsea na Atletico Madrid zikivutiwa naye.
Chelsea inapanga kuwasajili nyota wawili wa Barcelona: kiungo Fermin Lopez na beki Jules Kounde kwa dau linaloripotiwa kufikia pauni milioni 150.
Winga wa Crystal Palace, Ismaila Sarr, anaweza kuondoka Januari baada ya mazungumzo ya mkataba mpya kusuasua.
Real Madrid inafuatilia kwa karibu vijana wa Brighton, Luka Vuskovic na Chema Andres.
Kipa chipukizi wa Bayern Munich, Leonard Prescott, anawinda njia ya kutoka klabuni huku Chelsea, Arsenal, Brighton na Aston Villa zikimtaka.
Leeds United imeulizia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Morocco, Bilal El Khannouss, kutoka Stuttgart.
Barcelona bado inamtamani beki wa Manchester City, Josko Gvardiol, ingawa inaona dili hilo ni gumu kutimia.
Newcastle na Liverpool zinashindania saini ya beki wa Lens, Ismaelo Ganiou.
Mshambuliaji wa Monaco, Folarin Balogun, anazungumza na AC Milan na Juventus kuhusu uhamisho wa Januari.
Tottenham iko tayari kumuuza Richarlison Januari kwa kati ya pauni milioni 10 hadi 15, huku Trabzonspor ikionyesha nia ya kumsajili.
Unaweza pia kusoma: