Iran inajengaje upya uwezo wake wa kijeshi huku vita vikiendelea?

    • Author, رضا ثابتی
    • Nafasi, روزنامه‌نگار
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 12

Miezi minane baada ya kuanza kwa vita vya siku 40 kati ya Marekani, Israel na Iran, picha za satelaiti zinaonyesha kuwa Iran imeanza kujenga upya baadhi ya vituo vyake vya kijeshi.

Tathmini za kijasusi pia zinaashiria kuwa sehemu kubwa ya uwezo wake wa kutengeneza na kutumia makombora na ndege zisizo na rubani bado ipo, licha ya mashambulizi makubwa yaliyolenga miundombinu yake ya kijeshi.

Uchunguzi wa BBC Verify wa picha za satelaiti zilizopigwa mapema Novemba umebaini shughuli za uchimbaji na ujenzi katika vituo viwili vya makombora vya Iran. Pia, kuna dalili za ukarabati na ujenzi upya katika angalau vituo vingine 12 vya kijeshi.

Mnamo Novemba 10, vyombo vya habari vya Iran vilichapisha picha za uzinduzi wa kile kilichotajwa kuwa jiji jipya la makombora la kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Maendeleo hayo yanazua swali kuhusu kiwango ambacho Iran imeweza kurejesha nguvu zake za kijeshi baada ya vita hivyo.

Hata hivyo, miezi saba iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alikuwa ametangaza kuwa Iran haina tena uwezo wa kutengeneza makombora ya masafa marefu, virushia makombora na ndege zisizo na rubani zinazotumika kushambulia.

Lakini katika kipindi hicho, tathmini za mashirika ya kijasusi kuhusu kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi hayo zimekuwa tofauti na kauli za maafisa wa utawala wa Rais Donald Trump.

Katika ripoti yake ya Oktoba 20, Huduma ya Utafiti ya Bunge la Marekani ilinukuu tathmini ya Shirika la Ujasusi wa Kijeshi la Marekani (DIA) ya mwezi Aprili, iliyosema Iran bado ilikuwa na maelfu ya makombora na ndege zisizo na rubani za mashambulizi.

Ripoti hiyo pia ilirejelea taarifa kuhusu ujenzi upya wa vituo vya makombora na uwezekano wa Iran kurejesha uzalishaji kwa kutumia vipuri vilivyokuwa vimehifadhiwa.

Michael Eisenstadt, Mkurugenzi wa Mpango wa Mafunzo ya Kijeshi na Usalama katika Taasisi ya Washington, aliiambia BBC Persian kuwa jeshi la anga na jeshi la wanamaji la Iran viliharibiwa kwa kiasi kikubwa katika vita hivyo vya siku 40.

Hata hivyo, anasema uwezo muhimu zaidi wa kijeshi wa Iran ambao umeendelea kuwepo ni vikosi vyake vya makombora na ndege zisizo na rubani.

Makombora: Tofauti kuhusu kiwango cha uharibifu na uwezo wa uzalishaji

Kabla ya vita hivyo, makombora ya balistiki yalikuwa miongoni mwa silaha muhimu zaidi ambazo Iran ilitumia kushambulia malengo yaliyokuwa mbali.

Hifadhidata ya makombora ya Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa (CSIS) nchini Marekani inaeleza kuwa Iran ina hazina kubwa zaidi na yenye aina mbalimbali za makombora katika Mashariki ya Kati.

Wakati wa vita vya hivi karibuni, Marekani na Israel zililenga maghala ya kuhifadhi makombora, virushia makombora na viwanda vinavyotengeneza silaha hizo.

Mnamo Aprili 8, wakati usitishaji mapigano ulipotangazwa, Jenerali Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, alisema vikosi vya Marekani vilishambulia zaidi ya maeneo 450 ya kuhifadhi makombora ya balistiki ya Iran.

Alidai kuwa mashambulizi hayo yaliharibu zaidi ya asilimia 80 ya miundombinu ya makombora ya Iran pamoja na uwezo wake wa kutengeneza injini za makombora yanayotumia mafuta mango.

Hata hivyo, tathmini za kijasusi zilizotolewa mwezi Mei zilionyesha picha tofauti kuhusu silaha zilizokuwa zimesalia.

Gazeti la Washington Post liliripoti kuwa Iran ilikuwa imehifadhi takribani asilimia 70 ya makombora yake na asilimia 75 ya virushia makombora vinavyohamishika.

Gazeti la New York Times lilitoa makadirio yanayokaribiana na hayo, likisema karibu asilimia 70 ya makombora na virushia makombora ilikuwa imesalia. Pia liliripoti kuwa Iran ilikuwa imeweza kurejesha ufikiaji wa takribani asilimia 90 ya hazina yake ya silaha zilizohifadhiwa chini ya ardhi.

Kamanda wa CENTCOM, Admirali Brad Cooper, alipinga makadirio hayo wakati huo na kuyataja kuwa si sahihi, lakini hakutoa takwimu nyingine.

Wakati huohuo, mtu aliyetambulishwa kama mmoja wa makamanda wa uzinduzi wa makombora hivi karibuni aliiambia televisheni ya Iran kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi bado lina mamia ya makombora aina ya Khyber Shakan.

Khyber Shakan ni kombora la balistiki lenye uwezo unaotajwa kufikia kilomita 1,450. Lilionyeshwa kwa mara ya kwanza mwaka 2011.

Kwa mujibu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, kichwa cha kombora hilo kina uwezo wa kubadilisha mwelekeo linapokuwa angani, jambo linaloweza kulisaidia kukwepa mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora.

Eisenstadt anakadiria kuwa Iran huenda bado ina takribani makombora 1,000 au hata zaidi.

Kwa mujibu wake, huenda Iran ilitumia muda mwingi baada ya vita kutathmini uzoefu wa mashambulizi hayo, kusafisha milango ya vichuguu vilivyoharibiwa katika vituo vyake vya makombora na kuimarisha ulinzi wa miundombinu iliyojengwa chini ya ardhi.

Eisenstadt aliiambia BBC Persian kuwa huenda Iran imekuwa ikitoa mitambo muhimu iliyokuwa imefunikwa na vifusi vya viwanda vilivyoshambuliwa na kutumia vipuri vya vifaa vilivyonusurika ili kuanzisha tena uzalishaji.

Katika ripoti ya hivi karibuni, shirika la habari la Bloomberg lilinukuu afisa mmoja wa nchi za Magharibi na tathmini za kijasusi za kijeshi zikisema kuwa, licha ya uharibifu mkubwa katika viwanda vyake vya silaha, Iran bado ina uwezo wa kutengeneza takribani makombora 50 ya balistiki kwa mwezi.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa huenda Iran bado ina angalau makombora 1,700 katika hazina yake.

Gazeti la Wall Street Journal pia liliripoti mwezi Septemba, likinukuu maafisa wa Marekani na mataifa ya eneo hilo, kuwa Iran ilikuwa imeanza kwa kiwango kidogo kuunganisha makombora katika vituo vya chini ya ardhi kwa kutumia vipuri vilivyohifadhiwa kabla ya vita.

Hata hivyo, Taasisi ya Utafiti wa Sera za Kigeni ya Marekani, katika uchunguzi wake wa picha za satelaiti za miundombinu ya uzalishaji wa makombora nchini Iran mwezi Oktoba, ilisema juhudi za kujenga upya viwanda vilivyo juu ya ardhi katika maeneo ya Parchin, Khojir na Shahrood bado zilikuwa katika hatua za awali.

Watafiti walibaini kuwa kazi za uchimbaji ziliendelea katika eneo la Shahrood, lakini hakukuwa na dalili nyingi za uzalishaji katika mojawapo ya vituo vilivyotambuliwa kuwa eneo la kuunganisha makombora.

Eisenstadt anasema kurejesha na kutengeneza mitambo iliyoharibiwa ili kuanzisha tena uzalishaji wa makombora katika viwanda salama vya chini ya ardhi ni mchakato unaochukua muda mrefu.

Anakadiria kuwa huenda ikachukua miaka kadhaa kwa Iran kurejesha uwezo wake wa kutengeneza makombora na ndege zisizo na rubani katika kiwango kilichokuwepo kabla ya vita.

Anasema ili kufikia lengo hilo, Iran italazimika kutoa mitambo iliyoharibiwa kwenye vifusi, kuitengeneza au kujenga mingine kwa kutumia vipuri vilivyosalia, pamoja na kuhamishia shughuli zake za viwandani katika vituo salama zaidi vilivyo chini ya ardhi.

Ndege zisizo na rubani: Akiba iliyosalia na mitandao ya nje

Ndege zisizo na rubani zinazotumika kushambulia hazihitaji mitambo mikubwa ya viwandani wala gharama kubwa kama ilivyo kwa makombora ya balistiki.

Kabla ya vita, Iran ilikuwa na uzoefu mkubwa wa kutengeneza aina mbalimbali za ndege hizo na pia ilikuwa imehamishia teknolojia yake ya uzalishaji nchini Urusi.

Gazeti la New York Times liliripoti mwezi Aprili, likinukuu maafisa wa kijasusi wa Marekani, kuwa hata baada ya siku 40 za vita, Iran ilikuwa bado na takribani asilimia 40 ya hazina yake ya ndege zisizo na rubani za mashambulizi iliyokuwa nayo kabla ya vita.

Mwezi Mei, CNN iliripoti kwa kunukuu vyanzo vya kijasusi kuwa Iran ilikuwa imeanza tena kutengeneza baadhi ya aina za ndege hizo.

Ripoti hiyo ilisema sekta hiyo ilikuwa inajijenga upya kwa kasi kubwa kuliko ilivyotarajiwa na huenda uwezo wa uzalishaji ungerudi katika kiwango cha kabla ya vita ndani ya miezi sita.

Eisenstadt aliiambia BBC Persian kuwa huenda Iran bado ina maelfu ya ndege zisizo na rubani na imeanza tena kutengeneza baadhi ya aina zake, ingawa kwa kiwango kidogo zaidi.

Kuhusu nafasi ya Urusi, anarejelea taarifa zinazoashiria kuwa Moscow imeipa Iran vifaa vya aina hiyo ili kufidia ndege zisizo na rubani zilizotumika au kupotea vitani.

Suala hilo liliwahi kuibuka mwezi Machi, wakati shirika la habari la Reuters liliporipoti, likinukuu Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, kuwa Urusi ilikuwa imeitumia Iran ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa nchini humo.

Akizungumzia taarifa za Urusi kupeleka ndege hizo nchini Iran, Eisenstadt alisema hazina ya ndege zisizo na rubani ya Iran huenda bado iko katika hali nzuri.

Hata hivyo, aliongeza kuwa kurejesha uwezo wa uzalishaji katika kiwango cha kabla ya vita kunaweza kuchukua miaka kadhaa.

Sehemu nyingine ya uwezo huo inategemea upatikanaji wa vipuri vinavyotumika kuunganisha ndege zisizo na rubani.

Katika uchunguzi wake wa hivi karibuni, Reuters iliripoti kuwa imebaini kuwepo kwa mtandao wa zaidi ya taasisi 5,000 zinazohusishwa na Wizara ya Ulinzi ya Iran.

Uchunguzi huo ulitokana na mapitio ya nyaraka za benki, forodha na kampuni mbalimbali.

Kwa mujibu wa Reuters, mtandao huo umeingiza nchini Iran vifaa na bidhaa zinazohusiana na shughuli za kijeshi zenye thamani ya angalau dola bilioni mbili tangu Januari 2025.

Baadhi ya shehena hizo ziliweza kuingia nchini hata baada ya kuanza kwa vita na kuwekwa kwa zuio la shughuli za usafirishaji baharini.

Mnamo Novemba 7, Kamandi Kuu ya Marekani inayosimamia shughuli za kijeshi katika Mashariki ya Kati, CENTCOM, ilitangaza kuanzishwa kwa kikosi kazi kinachoitwa Iron Gate.

Kikosi hicho kitashirikiana na taasisi nyingine za serikali ya Marekani kuzuia usafirishaji wa silaha za kisasa, teknolojia zinazoweza kutumika kwa madhumuni ya kijeshi na kiraia, pamoja na bidhaa zilizowekewa vikwazo, kupitia mipaka ya nchi kavu ya Iran na Bahari ya Caspian.

Kamanda wa CENTCOM, Admirali Brad Cooper, alisema lengo ni kuzuia Iran kujenga upya viwanda vyake vya silaha na kuongeza tena akiba yake ya kijeshi.

Ulinzi wa anga: Uharibifu wa mifumo ya rada

Mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran ilikuwa tayari imeathiriwa na mashambulizi ya Israel hata kabla ya kuanza kwa vita vya hivi karibuni.

Watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Sera za Kigeni ya Marekani, walipochunguza picha za satelaiti zilizopigwa kabla ya vita, walibaini kuwa baadhi ya virushia makombora vya mfumo wa S-300 vilikuwa vimerejeshwa katika maeneo yake ya awali.

Hata hivyo, rada kuu zinazotumika kuongoza mifumo hiyo ya ulinzi, ambazo zilikuwa zimeharibiwa katika mashambulizi ya awali, hazikuonekana katika maeneo hayo.

Wakati wa vita vya siku 40, Marekani na Israel zilishambulia tena rada, mifumo ya ulinzi wa anga na vituo vya kijeshi vya jeshi la anga la Iran.

Mnamo Aprili 8, Jenerali Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, alidai kuwa vikosi vya Marekani vilikuwa vimeharibu takribani asilimia 80 ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran na kushambulia zaidi ya maeneo 1,500 yanayohusiana na mifumo hiyo.

Inaripotiwa kuwa Iran ilikuwa imeanza kutafuta msaada wa Urusi katika kujenga upya mifumo yake ya ulinzi wa anga hata kabla ya vita vya hivi karibuni.

Gazeti la Financial Times liliripoti wiki moja kabla ya mashambulizi ya Marekani na Israel kuwa Tehran na Moscow zilikuwa zimesaini mkataba wa euro milioni 495 mwezi Desemba 2025.

Mkataba huo ulihusu ununuzi wa virushia makombora 500 vya mfumo wa ulinzi wa anga wa Verba vinavyobebeka na askari pamoja na makombora 2,500.

Baada ya kusitishwa kwa mapigano, Reuters iliripoti Julai 29, kwa kunukuu vyanzo vyake, kuwa Iran ilikuwa imesaini mkataba wa thamani ya dola milioni 60 hadi 70 kununua mifumo 300 hadi 400 ya ulinzi wa anga inayotengenezwa China.

Mifumo hiyo inajumuisha makombora ya QW-12 na FN-16.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilikanusha taarifa hizo na kuzitaja kuwa hazina msingi wowote, ikisema haikuwa imepeleka silaha hizo nchini Iran.

Silaha hizo zimeundwa kukabiliana na ndege zisizo na rubani, helikopta na ndege zinazoruka katika mwinuko wa chini.

Hata hivyo, haziwezi kuchukua nafasi ya mifumo mikubwa ya ulinzi wa anga yenye uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya masafa marefu kama vile S-300.

Iran pia imeunda mfumo wake wa ulinzi wa anga unaojulikana kama Bavar-373.

Lakini hadi sasa hakuna ushahidi huru unaoonyesha ni kwa kiwango gani Iran imefanikiwa kujenga upya mitandao yake ya rada na ulinzi wa anga tangu vita vilipomalizika.

Jeshi la wanamaji: Kutoka kuangamizwa kwa meli hadi kuongezeka kwa mashambulizi

Jeshi la wanamaji la Iran lilikuwa miongoni mwa vikosi vilivyokabiliwa na mashambulizi makubwa ya Marekani tangu siku za mwanzo za vita.

Mnamo Machi 28, CENTCOM ilitangaza kuwa zaidi ya meli 150 za Iran zilikuwa zimeharibiwa au kuzamishwa.

Mnamo Aprili 8, Jenerali Dan Caine alidai kuwa zaidi ya asilimia 90 ya meli za kawaida za kivita za Iran zilikuwa zimezama.

Pia alisema takribani nusu ya boti za mwendo kasi za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi zilikuwa zimeharibiwa.

Miongoni mwa meli zilizoharibiwa ni meli ya kivita ya Dena, iliyoshambuliwa kwa torpedo na manowari ya Marekani katika Bahari ya Hindi mnamo Machi 4.

Shirika la habari la Associated Press liliripoti, likinukuu maafisa wa Sri Lanka, kuwa miili ya wanajeshi 87 waliokuwa ndani ya meli hiyo ilipatikana huku wengine 32 wakiokolewa.

Licha ya hasara kubwa iliyopata Iran katika jeshi lake la wanamaji, mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Mlango Bahari wa Hormuz yameendelea, huku mbinu zinazotumiwa zikibadilika.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini, IMO, kufikia Novemba 9, matukio 131 ya kiusalama baharini yalikuwa yamethibitishwa katika Mlango Bahari wa Hormuz na maeneo mengine ya bahari katika ukanda huo.

Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati iliripoti Novemba 4 kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi lilikuwa limeongeza kwa kiasi kikubwa matumizi ya ndege zisizo na rubani zinazojilipua dhidi ya meli.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa taasisi hiyo, asilimia ya mashambulizi yaliyothibitishwa au kutajwa kuwa huenda yalihusisha ndege hizo iliongezeka kutoka asilimia 15 kabla ya katikati ya Julai hadi asilimia 62 kati ya katikati ya Julai na Oktoba 4.

Eisenstadt anasema Iran imekuwa ikijitahidi kudumisha uwezo wake wa kufuatilia na kulenga meli katika Ghuba ya Uajemi, licha ya mashambulizi ya Marekani yaliyolenga vikosi vyake vya pwani pamoja na vifaa vya upelelezi na uelekezaji wa mashambulizi ya majini katika miezi ya hivi karibuni.

Anasema lengo la Tehran ni kuhakikisha inaweza tena kuzuia usafiri wa meli katika njia za bahari za Ghuba ya Uajemi endapo vita vitaanza upya.

Hata hivyo, ana mashaka kama Iran kwa sasa ina uwezo huo.

Wakati huohuo, Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati katika ripoti yake ya Oktoba 30 ilisema uwezo wa Iran wa kuzuia usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa umepungua kwa kiasi fulani kufikia katikati ya Septemba.

Hali hiyo ilitokana na kuongezeka kwa meli za mafuta zilizokuwa zikisafiri katika eneo hilo chini ya ulinzi wa Marekani.

Hata hivyo, mashambulizi dhidi ya meli katika mwezi Oktoba yalifikia kiwango cha juu zaidi kwa mwezi mmoja tangu vita vilipoanza.

Kwa mujibu wa ripoti ya Novemba 5 ya kampuni ya Uingereza ya Lloyd's List Intelligence, inayochambua taarifa za usafiri wa majini, mashambulizi hayo yalisababisha kupungua kwa kiasi fulani kwa idadi ya meli zilizokuwa zikipita katika eneo hilo, ingawa usafiri haukusimama kabisa.

Muundo wa uongozi wa kijeshi na mabadiliko ya mkakati wa vita

Ali Khamenei, aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na makamanda kadhaa waandamizi wa kijeshi, waliuawa mwanzoni mwa vita vya siku 40.

Licha ya vifo hivyo, mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran yaliendelea.

Mwanzoni kabisa mwa vita, Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati ilitafsiri mwitikio wa haraka wa vikosi vya Iran kuwa ishara kwamba mamlaka fulani ya kufanya maamuzi ya kijeshi yalikuwa tayari yamekabidhiwa kwa makamanda wa ngazi za chini.

Tathmini hiyo iliungwa mkono na kauli za maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu.

Wakati usitishaji mapigano ulipotangazwa Aprili 8, Jenerali Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, alisema vikosi vya Marekani vilikuwa vimeshambulia na kuharibu zaidi ya vituo 2,000 katika mtandao wa mawasiliano na uratibu wa shughuli za kijeshi za Iran.

Ripoti mbalimbali za vyombo vya habari na ushahidi kutoka maeneo yaliyoshambuliwa zinaonyesha kuwa muundo wa maamuzi ya kijeshi nchini Iran pia umebadilika tangu Mojtaba Khamenei achaguliwe kuwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo wakati wa vita.

Mabadiliko hayo yameongeza nafasi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi na taasisi za usalama katika kufanya maamuzi ya kijeshi.

Katika uchambuzi wao wa mwezi Septemba, Michael Eisenstadt na Farzin Nadimi wa Taasisi ya Washington walisema kuharibiwa kwa sehemu kubwa ya vikosi vya anga na wanamaji vya Iran kumedhoofisha nafasi ya jeshi la kawaida katika kugombea rasilimali za kijeshi.

Kwa upande mwingine, hali hiyo imeimarisha ushawishi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi katika maamuzi ya kijeshi.

Wataalamu hao wanakadiria kuwa serikali ya Iran huenda ikaelekeza sehemu kubwa zaidi ya rasilimali zake chache katika kuendeleza uwezo wa makombora na ndege zisizo na rubani.

Katika mahojiano yake na BBC Persian, Eisenstadt pia ameeleza kuwa mkakati wa Iran wa kupigana vita unaonekana kubadilika.

Kwa mujibu wa tathmini yake, Tehran inajaribu kuepuka mashambulizi ya moja kwa moja yanayoweza kuchochea Marekani, Israel na mataifa ya Kiarabu katika Ghuba kujibu kwa nguvu zaidi.

Badala yake, Iran inaonekana kupanua wigo wa kijiografia wa mzozo kwa kutumia makundi washirika nchini Yemen na Iraq.

Ripoti ya Oktoba 30 ya Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati pia imeeleza kuendelea kwa mkakati huo wa kutumia makundi washirika kuweka shinikizo la kijeshi, hasa katika maeneo ya Jordan na Saudi Arabia.

Eisenstadt anaamini kuwa Marekani na Israel zina uwezo mkubwa zaidi wa kuishambulia na kuidhuru Iran.

Hata hivyo, anasema Jamhuri ya Kiislamu bado ina uwezo wa kuendeleza mapambano.

"Hakuna upande unaotaka vita vya muda mrefu. Lakini Iran imeonyesha kuwa ina uwezo wa kustahimili mashambulizi na kuendeleza vita licha ya gharama kubwa inayolazimika kulipa," anasema.