Kwa nini meli zilizokwama Hormuz zinawatia wasiwasi wanasayansi?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kunasababisha kile ambacho wanasayansi wanakiita "mgogoro wa dharura wa kiikolojia" na "tishio kubwa kwa usalama wa viumbe duniani", kwa mujibu wa ripoti ya timu ya kimataifa ya wanabiolojia wa baharini iliyochapishwa katika jarida la Biological Invasions.

Wanasayansi wanasema meli ambazo zimekwama kwa miezi kadhaa zimezipa viumbe vamizi muda ambao haujawahi kushuhudiwa wa kujijenga na kuongezeka.

Meli hizo zitakapoanza tena safari kuelekea sehemu mbalimbali duniani, zinaweza kusababisha kile wanabiolojia wanachokiita "tukio kubwa la kusambaza viumbe vamizi baharini duniani."

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takribani meli 1,500 zimekwama katika Ghuba ya Uajemi (Arabian/Persian Gulf) tangu Februari, huku mamia ya nyingine zikiwa zimekwama katika Ghuba ya Oman.

"Hali mbaya zaidi inayoweza kutokea"

Viumbe wengi wa baharini kama bakteria, mwani na wanyama wadogo wasiokuwa na uti wa mgongo hujishikiza haraka kwenye meli zinapokaa bila kusonga kwa muda mrefu. Hali hii inajulikana kama biofouling.

Profesa Mario Tamburri, mwanaikolojia wa baharini kutoka Chuo Kikuu cha Maryland nchini Marekani na mwandishi mkuu wa utafiti huo, anaeleza kuwa kuna kundi la viumbe wanaoitwa viumbe waliotulia (sessile) kwa sababu huishi maisha yao yote wakiwa wamejishikiza kwenye uso fulani.

Anasema kila kitu kipya kama vile ujenzi fulani unapofanyika baharini huanza kufunikwa na bakteria na vijidudu vingine vinavyounda tabaka linaloitwa biofilm.

Baadaye biofilm hiyo huvamiwa na mbegu za mwani, mabuu ya viumbe kama barnacle, minyoo na viumbe wengine wanaohitaji sehemu ngumu za kujishikiza ili kuishi.

Profesa Tamburri anasema sakafu ya Ghuba kwa kiasi kikubwa imefunikwa na matope, mchanga na tope laini, hivyo sehemu ngumu ni chache sana. Ndiyo maana meli zilizosimama kwa muda mrefu zimekuwa makazi mazuri kwa viumbe hawa.

Kwa kuwa Ghuba ni moja ya njia muhimu zaidi za usafiri wa baharini duniani, meli huleta viumbe hawa kutoka maeneo mbalimbali na pia huzikusanya zinapokaa bila kutoka.

Kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kumesababisha idadi kubwa ya meli kubwa kubaki mahali pamoja kwa muda mrefu kuliko ilivyowahi kutokea katika historia ya hivi karibuni.

Kwa mfano, kuzibwa kwa Mfereji wa Suez mwaka 2021 kulidumu kwa siku sita tu, wakati ajali ya daraja katika bandari ya Baltimore nchini Marekani mwaka 2024 iliathiri meli chache kwa takribani wiki 11.

Kwa kawaida, meli katika eneo la Ghuba hukaa bandarini kwa siku moja hadi tatu kabla ya kuondoka. Lakini watafiti wanasema viumbe vamizi vinaweza kuanza kuongezeka kwa kasi ndani ya siku 10 tu za meli kusimama.

Mwaka 2023, Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) lilipendekeza meli ambazo zimekaa kwa muda mrefu bandarini zichukue hatua za kuondoa biofouling kabla ya kuanza safari.

Lakini sasa meli nyingi zimekaa kwa miezi kadhaa.

"Kama ungependa kubuni mazingira mabaya zaidi ya kuenea kwa viumbe vamizi kupitia meli, usingepata mfano bora kuliko huu," anasema Profesa Tamburri.

Msimu wa joto umeongeza hatari

Watafiti wanasema viumbe wengi wa baharini huzaliana zaidi maji yanapoanza kupashwa joto.

Mlango-Bahari wa Hormuz ulifungwa mwishoni mwa Februari wakati maji yalikuwa yanaanza kupanda joto kuelekea kiangazi.

"Hali hiyo huchochea viumbe kutaga mayai, kukua na kutafuta sehemu mpya za kuishi. Kama kufungwa kungetokea katikati ya majira ya baridi, hatari ingekuwa ndogo zaidi," anasema Tamburri.

Ripoti hiyo inatoa mfano wa barnacle aitwaye Amphibalanus improvisus, ambaye ameenea duniani kupitia usafiri wa baharini. Kiumbe huyu anaweza kutoa hadi mabuu 36 kwa siku kutoka kwa kila mzazi mmoja katika joto la nyuzi 30 za Selsiasi.

Kwa hiyo, baadhi ya meli huenda zilitoa mamilioni ya mabuu wakati zilipokuwa zimekwama.

"Kinachoshangaza ni ukubwa wa tatizo na ukweli kwamba meli hizi husafiri karibu kila kona ya dunia," anasema Tamburri.

Madhara yanaweza kuwa makubwa

Iwapo viumbe hawa watahamishwa hadi mazingira mapya, wanaweza kusababisha madhara makubwa ya kiuchumi na kimazingira.

Wanaweza kushindana na viumbe wa asili, kusababisha baadhi yao kutoweka, kuathiri uvuvi na ufugaji wa viumbe wa majini, na hata kuziba mifumo ya kupooza mitambo ya kuzalisha umeme.

Tamburri anasema mara viumbe vamizi wanapojiimarisha katika mazingira ya baharini huwa vigumu sana kuwaondoa.

Aidha, viumbe hawa wanaweza kubeba vimelea na magonjwa hatari. Watafiti wanaonya kuwa maji ya joto ya Ghuba yanaweza kusaidia kuzalisha aina za viumbe wenye uwezo mkubwa wa kustahimili joto, ambazo zinaweza kuwa tishio zaidi zitakaposafirishwa sehemu nyingine duniani.

Athari kwa meli na Bandari

Biofouling pia husababisha hasara kwa meli.

Kadiri viumbe wanavyozidi kujikusanya kwenye gamba la meli, ndivyo uzito na msuguano wake ndani ya maji unavyoongezeka, jambo linaloifanya kutumia mafuta mengi zaidi.

Profesa Tamburri anasema hata tabaka dogo la biofilm linaweza kuongeza matumizi ya mafuta kwa asilimia 2 hadi 5.

Ikiwa meli imefunikwa na barnacle na kome, matumizi ya mafuta yanaweza kuongezeka hadi asilimia 25.

Ingawa kuna rangi maalumu za kuzuia biofouling zinazotumia kemikali za kuua viumbe, zinafanya kazi vizuri zaidi meli zinapokuwa zinasafiri. Zikikaa muda mrefu bila kusonga, ufanisi wake hupungua.

Kwa kuzingatia njia za usafiri wa baharini, muda wa safari na mazingira ya bahari, watafiti wamebaini kuwa bandari kadhaa pia ziko katika hatari kubwa ya kupokea viumbe hawa.

Bandari hizo ni pamoja na Jeddah (Saudi Arabia), Mumbai (India), Colombo (Sri Lanka), Singapore, Alexandria (Misri), Piraeus (Ugiriki), Algeciras (Uhispania), Rotterdam (Uholanzi). Bandari zenye maji yenye joto na chumvi nyingi zinaonekana kuwa katika hatari kubwa zaidi.

Ushirikiano wa kimataifa unahitajika

Kwa mujibu wa wataalamu, suluhisho bora lingekuwa kusafisha meli zote kabla hazijaondoka Ghuba.

Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya meli na ukubwa wake, pamoja na changamoto za kiteknolojia na kiutendaji, hatua hiyo inaonekana kuwa ngumu kutekelezwa.

Ingawa teknolojia za roboti zinaweza kusafisha meli huku zikikusanya viumbe hao ili wasirudi baharini, huduma nyingi za usafishaji katika eneo la Ghuba bado hazina uwezo huo.

Kwa sababu hiyo, watafiti wanasema bandari zitakazopokea meli kutoka eneo hilo zinapaswa kujiandaa kuzisafisha mara tu zitakapowasili ili kupunguza hatari ya kuenea kwa viumbe vamizi.

"Karibu tuna uhakika kwamba kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kutasababisha kuingizwa kwa viumbe wasio wa asili katika maeneo mapya," anasema Tamburri.

Anasisitiza kuwa baadhi ya viumbe vamizi huweza kuwepo bila kuonekana kwa muda mrefu, lakini wengine husababisha madhara makubwa mara wanapojikita.

Watafiti wanahitimisha kuwa iwapo hali hii itageuka kuwa tukio kubwa la kuenea kwa viumbe vamizi duniani itategemea zaidi jinsi nchi mbalimbali zitakavyoshirikiana kukabiliana na tatizo hilo.