Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Iran inajihatarisha katika harakati za kuudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz
Baada ya kukabiliana kwa makombora na Marekani kwa siku 10 kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz, viongozi wa Iran huenda wana kama chaguzi tatu hivi. Hakuna hata moja inayotoa ishara ya wazi ya ushindi.
Jambo la kwanza ni kukubali matakwa ya Washington: kuhakikisha usafiri salama bila malipo katika Mlango-Bahari wa Hormuz kwa kukomesha mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara, kuacha au kupunguza hazina ya urani iliyorutubishwa, na kukubali ukaguzi wa shirika la kimataifa la uangalizi wa nyuklia.
Kwa upande wake, Tehran inashinikiza kuondolewa kwa vizuizi vya majini vya Marekani dhidi ya bandari za Iran, kuondolewa vikwazo vya kiuchumi, na ulinzi dhidi ya mashambulizi zaidi.
Hii labda ni chaguo la gharama nafuu zaidi, lakini pia ni ghali zaidi kisiasa.
Kufungua tena Hormuz bila ya Iran kuwa na jukumu linalotambulika la kusimamia njia hiyo muhimu ya majini kutamaanisha kusalimisha kile ambacho baadhi ya watu wa Tehran wanakiona kama zana itakayo wawezesha kufikia malengo yao badala ya kutumia makombora ya Iran, washirika wa kikanda, au hata mpango wake wa nyuklia.
Kwa mara ya kwanza Iran imedhihirisha uwezo wake wa kuvuruga uchumi wa dunia kwa kujibu mashambulizi kutoka kwa maadui zake.
Mpango wa nyuklia, kwa muda mrefu umewasilishwa kama haki ambayo Iran haiwezi kushurutishwa kuachana nayo.
Kukubali kusitisha shughuli zake za nyuklia baada ya miezi kadhaa ya mashambulio kutatoa fursa kwa watu wenye msimamo mkali kukiri kwamba kuwa shinikizo la jeshi la Marekani lilifanya kazi. Inaweza pia kufungua msururu wa madai kuhusu mpango wa silaha wa Iran na uhusiano wake na Hezbollah huko Lebanon, makundi ya Kishia nchini Iraqi na Wahouthi wa Yemen.
Chaguo la pili ni kusimama kidete. Iran inaweza kuongeza mashambulizi yake dhidi ya kambi za Marekani katika eneo hilo, meli, na miundombinu muhimu katika mataifa ya Ghuba, ikitumai kwamba gharama ya juu ya nishati na usumbufu mkubwa utailazimu Washington na washirika wake kuafikiana.
Hili lina hatari kubwa zaidi ya kijeshi. Shambulio linalosababisha vifo vya watu wengi au uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya mataifa ya Ghuba unaweza kuwavutia majirani wa Iran moja kwa moja kwenye mzozo huo na kuiacha ikikabiliwa na mzozo mpana zaidi.
Chaguo la tatu ni kuendeleaza mgogoro unaoendelea kwa sasa: shinikizo dhidi ya meli za biashara na nishati ili kudumisha ushawishi, lakini haitoshi kuirudisha tena katika vita na Marekani.
Hili linaonekana kuendana na mawazo yaliyoanzishwa na Jamhuri ya Kiislamu. Iran haihitaji kumshinda adui mwenye nguvu zaidi ikiwa inaweza kuishi kwa muda mrefu kuliko adui huyo alivyo tayari kupigana. Kuponea mashambulizi yenyewe kunaweza kutafsiriwa kama ushindi. Lakini vikwazo, uharibifu wa vita na mfumuko wa bei vinaongeza shinikizo nchini kwa kasi.
Na kadri muda unavyosonga, kitendawili kinaweza kuibuka: Kadiri Iran inavyotumia Mlango wa Hormuz kama silaha, ndivyo inavyoweza kupungua nguvu ikiwa nchi zitapata njia mpya za kusafirisha nishati na bidhaa zingine nje ya eneo hilo.
Spika wa Bunge Mohammad Bagher Ghalibaf amekiri utata huo, akisema kwamba thamani ya Hormuz iko katika kuongeza idadi ya meli zinazopitia humo badala ya kuipunguza. Njia ya maji isiyo salama kabisa inahimiza ulimwengu kutafuta njia za kuzunguka Iran.
inavyotumia Mlango wa Hormuz kama silaha, ndivyo inavyoweza kupungua nguvu ikiwa nchi zitapata njia mpya za kusafirisha nishati na bidhaa zingine nje ya eneo hilo.
Spika wa Bunge Mohammad Bagher Ghalibaf amekiri utata huo, akisema kwamba thamani ya Hormuz inachangiwa na ongezeko la idadi ya meli zinazopitia humo badala ya kuipunguza. Njia hiyo ya majini isiyo salama inahimiza ulimwengu kutathmini njia mbada ya kuepuka Iran.
Nani anayefanya maamuzi?
Kinachozidisha utata huo ni hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu mchakato wa kufanya maamuzi wa Iran.
Chini ya Ayatollah Ali Khamenei, ambaye aliuawa katika mashambulizi ya mwanzoni mwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari, mizozo kati ya wanasiasa waliochaguliwa, taasisi za makasisi na Walinzi wa Mapinduzi hatimaye ilitatuliwa na kiongozi mkuu. Baada ya miezi kadhaa ya vita na chini ya uongozi mpya wa mwana wa Khamenei, Mojtaba, usawa huo wa madaraka hauko wazi.
Rais Masoud Pezeshkian na wanadiplomasia wake wanaweza kupendelea suluhu ili kupunguza shinikizo la kiuchumi na kurejesha utulivu. Wakati huo huo, watu wenye msimamo mkali bungeni, taasisi zenye nguvu ambazo hazijachaguliwa, na vyombo vya habari vya kihafidhina, wanaweza kuogopa kwamba makubaliano makubwa yatadhoofisha misingi ya kiitikadi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuwatenga wafuasi wake wakuu.
Swali kubwa zaidi linahusu vikosi vya jeshi, haswa Walinzi wa Mapinduzi. Programu ya makombora ya Iran, ushirikiano wa kikanda na mkakati katika Mlango wa Hormuz ni muhimu kwa ushawishi wa Walinzi wa Mapinduzi, lakini bado haijulikani ni kiasi gani makamanda wana uzito katika maamuzi kuhusu kuongezeka kwa uchumi na mazungumzo.
Chaguzi tatu zinazokabili Tehran hazitoi gharama sawa kwa sehemu tofauti za mfumo. Wale wanaoamini mambo kwa vitendo wanaweza kupendelea makubaliano, wale wanaoshikilia msimamo mkali wanaweza kupendelea uvumilivu, huku baadhi ya makamanda wa kijeshi wakiona kuongezeka kwa uchumi kama kuimarisha msimamo wa Iran katika majadiliano.
Kwa hivyo, swali si tu ni njia gani Iran inachagua, bali ni nani aliye na mamlaka ya kufanya uamuzii huo.
Wanachosema Wairan
Mtazamo wa uongozi kuhusu ustahimilivu ni tofauti sana na ule wa wale wanaotakiwa kustahimili hali hiyo.
Iran na Marekani zilitia saini Hati ya Makubaliano (MoU) mwezi Juni ili kusitisha operesheni za kijeshi na kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz, pamoja na kufikia makubaliano ya kumaliza vita ndani ya siku 60 zilizofuata. Hata hivyo, wiki tatu baada ya kusainiwa kwa hati hiyo, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa usitishaji huo wa mapigano umefikia mwisho kufuatia mashambulizi ya Iran dhidi ya meli katika eneo la Hormuz na mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Marekani.
Mwanamke mmoja nchini Iran aliambia BBC Persian kuwa alihisi "huzuni kubwa sana" wakati mapigano yalipoanza tena.
Alikuwa na matumaini kwamba hati hiyo ya makubaliano ingelitoa fursa kwa pande zote mbili kutatua migogoro iliyosalia na kurejesha utulivu. Badala yake, ana hofu ya kuharibiwa kwa miundombinu na vifo vya raia pamoja na wanajeshi.
Aliwalaumu watu wenye msimamo mkali ndani ya mfumo wa Iran kwa kutekeleza sera zenye madhara, huku pia akiwakosoa wapinzani walio nje ya nchi ambao, kwa mtazamo wake, walichochea vita.
Mwanamke mwingine mjini Tehran alisema kampuni ya biashara ya kimataifa aliyokuwa akifanyia kazi ilifungwa, na kumwacha bila ajira kwa miezi minne licha ya kuwa na shahada ya uzamivu (PhD) na uzoefu wa miaka 17.
"Hakuna anayeajiri kwa sababu hakuna anayejua nini kitatokea," alisema. Alielezea hali ya kupanda kwa bei, kukatika kwa umeme na maji, kuongezeka kwa wizi, na milio ya risasi inayosikika mara kwa mara usiku. Kwa sasa, amepunguza safari zake za kuzunguka jiji.
Maelezo haya hayaonyeshi hitimisho moja la kisiasa. Mashambulizi kutoka nje yanaweza kuzua hasira dhidi ya Marekani na Israel hata miongoni mwa wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu. Lakini pia yanaonyesha mipaka ya kuwataka wananchi kustahimili mateso yasiyo na kikomo kwa jina la upinzani.
Trump anakabiliwa na chaguzi ngumu: kupanua wigo wa vita, kuendeleza shinikizo la kijeshi na kiuchumi, au kukubali makubaliano yanayoruhusu Iran kuwa na mpango wa nyuklia wa kiraia wenye vikwazo na chini ya uangalizi mkali zaidi. Hakuna chaguo lolote kati ya hayo linalotoa njia ya wazi ya kupata ushindi.
Mvutano huo unaweza kuendelea kwa miezi kadhaa kupitia mzunguko wa mashambulizi, juhudi za upatanishi, na usitishaji wa muda wa mapigano. Swali muhimu ni kwa muda gani viongozi wa Iran wanaweza kutumia eneo la Hormuz kama kete ya mazungumzo bila kuchochea vita kamili, machafuko mapya, au ujenzi wa njia mbadala ambazo zingepunguza umuhimu wa mlango-bahari huo.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi