Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mpango mpya wa Trump kuhusu Gaza haukubaliki- Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema jeshi la Israel halitaondoka Gaza hadi Hamas iwe imeondoa silaha kikamilifu, akiongeza kuwa vinginevyo kundi hilo litaendelea kuwa tishio kwa wanajeshi na raia wa Israel.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu yaendelea baada ya kusimama kwa miezi 5

    Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amefikishwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo, Agosti 10, 2026, kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili.

    Kesi hiyo imeanza tena baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano tangu Februari 24, 2026.

    Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalohusishwa na kauli alizotoa kuhusu kusudio la kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

    Kesi hiyo inasikilizwa kwa mfululizo kuanzia leo hadi Septemba 7, 2026, chini ya Jopo la Majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

    Vikao vya maandalizi ya uendeshaji wa kesi hiyo vilifanyika kuanzia Agosti 5, 2026, vikihusisha Mahakama, upande wa Jamhuri, mshitakiwa Tundu Lissu pamoja na mawakili wake.

    Kwa sasa, kesi hiyo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi.

    Baadhi ya mashahidi, wakiwemo askari polisi na mashahidi wasiokuwa askari ambao ni mashahidi wanaolindwa, tayari wametoa ushahidi wao.

    Lissu amekuwa akishikiliwa gerezani tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025, na kushtakiwa siku iliyofuata kwa makosa ya uhaini na uchochezi.

  2. Uganda yaanzisha msako dhidi ya magari aina ya Subaru yanayotoa kelele

    Polisi nchini Uganda wameanzisha msako dhidi ya madereva wa magari aina ya Subaru yaliyofanyiwa marekebisho ya mfumo wa kutolea moshi na kutoa milio mikubwa.

    Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia malalamiko ya wakazi wa Lugazi kuhusu kelele zinazotokana na magari hayo, hasa nyakati za usiku.

    Polisi katika Manispaa ya Lugazi, wilayani Buikwe, wamemkamata dereva mmoja anayekabiliwa na tuhuma za kusababisha uchafuzi wa mazingira kwa kelele.

    Dereva huyo alikamatwa Jumamosi akiwa anaendesha Subaru yenye mfumo wa kutolea moshi uliorekebishwa, na gari hilo limezuiliwa na polisi.

    Msako huo unalenga kukabiliana na magari yanayotoa kelele kupita kiasi na kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za usalama na utulivu wa jamii.

  3. Uganda na Tanzania zakubaliana kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati kikanda

    Uganda na Tanzania zimezindua ushirikiano mpya wa nishati unaolenga kuifanya bandari ya Tanga kuwa kitovu muhimu cha nishati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Mpango huo unatarajiwa kuvutia uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 20, huku ukiwa na mpango wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta pamoja na miundombinu mingine ya nishati.

    Makubaliano hayo yamesainiwa kati ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta Uganda, UNOC, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, TPDC, pamoja na kampuni ya Vitol Bahrain EC.

    Mpango huo utaweka msingi wa ushoroba jumuishi wa nishati itakayounganisha Uganda na Tanzania kupitia mabomba ya kusafirisha bidhaa mbalimbali za mafuta, pamoja na miundombinu ya mafuta na gesi na vituo vya kuhifadhi nishati.

    Uganda na Tanzania zinasema ushirikiano huo unaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya mafuta na nishati katika Afrika Mashariki, huku Bandari ya Tanga ikitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mnyororo huo wa nishati.

    Haya yanajiri baada ya tajiri mkubwa barani Afrika Aliko Dangote kuchagua bandari ya lamu kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta, badala ya Tanzania kama ilivyokuwa imependekezwa.

  4. Mahakama ya Afrika Mashariki yaipa Uganda siku 45 kujibu kesi ya mateso kwa washukiwa

    Mahakama ya Afrika Mashariki ya Haki, EACJ, imeipa serikali ya Uganda siku 45 kuwasilisha majibu yake katika kesi inayopinga uamuzi wa Mahakama ya Katiba kuhusu ulinzi wa washukiwa wa uhalifu dhidi ya mateso.

    Kesi hiyo imewasilishwa na Chama cha Wanasheria Uganda, ULS, kikidai kuwa uamuzi wa Mahakama ya Katiba unadhoofisha ulinzi wa kisheria dhidi ya mateso kwa watu wanaoshukiwa kutenda uhalifu.

    Mahakama hiyo yenye makao yake Arusha, Tanzania, imeagiza Mwanasheria Mkuu wa Uganda kuwasilisha majibu ya serikali ndani ya siku 45.

    Mahakama imeonya kuwa iwapo serikali ya Uganda haitawasilisha majibu ndani ya muda huo, kesi inaweza kuendelea kusikilizwa na kuamuliwa bila majibu yake.

    Hatua hiyo inafungua njia kwa Mahakama ya Afrika Mashariki kuchunguza iwapo uamuzi unaolalamikiwa unaendana na wajibu wa Uganda wa kulinda haki za binadamu na kuzuia vitendo vya mateso dhidi ya washukiwa wa uhalifu.

  5. Wanajeshi 50,000 wa Korea Kaskazini wanatarajiwa kupelekwa Urusi - Zelensky

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema hadi wanajeshi 50,000 wa Korea Kaskazini wanaweza kupelekwa nchini Urusi kusaidia katika vita dhidi ya Ukraine.

    Zelenskyy amesema idadi hiyo ni ongezeko kutoka makadirio ya awali ya wanajeshi 30,000, huku akionya kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Moscow na Pyongyang unaendelea kuimarika.

    Amesema Ukraine imegundua makombora ya Korea Kaskazini katika ardhi yake na kwamba Pyongyang inaendelea kupata uzoefu wa vita vya kisasa pamoja na teknolojia na zana za kijeshi kutoka Urusi.

    Kwa mujibu wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine, kikosi cha makombora cha Korea Kaskazini kimeanza kupeleka wanajeshi na vifaa magharibi mwa Urusi. Kikosi hicho kinaweza kuwa na makombora 120 ya balistiki na vifaa sita vya kurushia makombora.

    Korea Kaskazini tayari ilipeleka takriban wanajeshi 14,000 katika eneo la Kursk nchini Urusi mwaka 2024, kusaidia vikosi vya Urusi katika mapigano dhidi ya Ukraine.

    Kutokana na kuongezeka kwa ushirikiano huo, Zelenskyy ameiomba Korea Kusini kuisaidia Ukraine kwa mifumo ya ulinzi wa anga, ambako Kyiv inakabiliwa na upungufu mkubwa wa silaha za kuzuia mashambulizi ya makombora ya balistiki.

    Wakati huo huo, mashambulizi ya Urusi yameendelea kulenga miji na miundombinu ya Ukraine, huku ripoti za hivi karibuni zikieleza kuwa raia wameuawa na wengine kujeruhiwa katika maeneo mbalimbali.

    Zelenskyy pia amewataka washirika wa Ukraine kuongeza msaada wa ulinzi wa anga, akisema uwezo huo ni muhimu katika kukabiliana na kuongezeka kwa mashambulizi ya makombora ya Urusi.

    Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Wes Streeting amezitaka nchi washirika kuongeza msaada wa mifumo ya ulinzi wa anga kwa Ukraine kabla ya majira ya baridi, akisema Rais Vladimir Putin anaweza kutumia msimu huo kama silaha dhidi ya Kyiv.

    Naye Papa Leo ametoa wito wa kusitishwa kwa vita kati ya Urusi na Ukraine, akisema idadi ya raia wanaouawa na kujeruhiwa, wakiwemo watoto, inaongezeka.

    Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake ukisema zaidi ya raia 16,000 wameuawa tangu kuanza kwa vita, huku wengi wao wakiwa raia wa Ukraine.

  6. Iran yamteua kiongozi mpya wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa

    Iran imemteua kiongozi mpya wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, katika mabadiliko muhimu ya uongozi wakati nchi hiyo ikikabiliana na mzozo kati yake, Marekani na Israel.

    Mohsen Rezaei, kamanda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameteuliwa kushika wadhifa huo wenye jukumu muhimu katika kuamua namna Iran itakavyokabiliana na mzozo huo.

    Rezaei amewahi kusema Iran inapaswa kudumisha udhibiti wa Mlango wa Hormuz, akisema hilo ni muhimu zaidi kuliko kumiliki silaha za nyuklia.

    Kwa kuzingatia historia yake ndefu ya kushika nyadhifa za juu serikalini, uteuzi wake unaonekana kuashiria kuwa kizazi cha zamani cha wanasiasa wa Iran bado kinaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika uongozi wa nchi hiyo.

    Hata hivyo, kumekuwa na utabiri kwamba wanasiasa vijana wanaweza kuanza kupewa nyadhifa za juu katika uongozi wa Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  7. CENTCOM yafichua meli zilizozuiwa tangu kuanza kwa vikwazo vya Marekani

    Kamandi Kuu ya Marekani CENTCOM, inayosimamia operesheni za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati, imesema tangu kuanza kwa zuio la baharini dhidi ya Iran, imezuia meli 55 za kibiashara na kusimamisha meli mbili kwa kutumia mashambulizi ya risasi.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, CENTCOM imesema zaidi ya meli 20 za kivita za Marekani zinafanya shughuli katika Mashariki ya Kati kuunga mkono operesheni za kijeshi, ikiwemo utekelezaji na ufuatiliaji wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

    CENTCOM pia imesema vikosi vya Marekani viliingia na kukagua meli mbili wakati wa utekelezaji wa zuio hilo la baharini.

  8. Trump: Iran imekuwa na utovu wa nidhamu kwa miaka 51

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran imekuwa na utovu wa nidhamu kwa miaka 51.

    Trump amesema hayo katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, akidai Iran imeiongoza dunia katika kile alichokiita tabia mbaya kwa kipindi cha miaka 51.

    Trump pia alichapisha picha inayoonyesha kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya Iran, rial, tangu mwanzoni mwa mwaka 2025 hadi sasa.

    Akiambatanisha picha hiyo, Trump amesema, “Iran haina pesa,” na kuongeza, “fedha yao haina thamani.”

    Soma Pia:

  9. Trump akanusha Marekani kuishiwa silaha za kivita

    Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa kwamba Marekani imepungukiwa na silaha na risasi, akisema nchi hiyo ina akiba kubwa ya silaha na kwamba nyingine zinaendelea kutengenezwa.

    Trump pia ameonya kuwa watu wanaoshukiwa kuvujisha taarifa za siri za serikali wataadhibiwa vikali.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye X Alhamisi, Trump amesema Marekani ina “idadi kubwa ya silaha na risasi”, hasa za aina fulani, huku akisema uzalishaji wa silaha hizo unaendelea na zinatumwa pale zinapohitajika.

    Trump na Wizara ya Ulinzi ya Marekani wanakabiliwa na maswali kuhusu hali ya akiba ya silaha nchini humo, huku vita vikiingia mwezi wa sita na makubaliano ya amani yakitarajiwa kuchukua muda kufikiwa.

    Kwa upande mwingine, Iran imesema silaha zinazozalishwa nchini humo zinaiwezesha kukabiliana na “tishio lolote”.

    Waziri wa Ulinzi wa Iran, Majid Ibn Reza, amesema dalili za kupungua kwa uwezo wa adui zinaendelea kuonekana kila siku, huku akisisitiza kuwa majeshi ya Iran yako tayari kukabiliana na hatari yoyote.

    Amesema teknolojia inayozalishwa nchini Iran ni bora kuliko teknolojia nyingine yoyote ya kijeshi katika eneo hilo.

    Taarifa hiyo inafuatia mashambulizi makubwa ya makombora yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Iran katika operesheni iliyopewa jina Epic Fury, pamoja na mashambulizi mengine ya kijeshi.

    Kwa mujibu wa CBS News, mshirika wa BBC, Marekani imetumia sehemu kubwa ya akiba yake ya kimataifa ya makombora ya masafa marefu na makombora yanayoongozwa kwa usahihi. Taarifa hiyo ilinukuu vyanzo viwili vinavyofahamu hali hiyo, vilivyozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina.

    Soma zaidi:

  10. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 9/08/2026.