Mzozo wa Iran: Kwanini Trump anatishia kuishambulia Oman?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani Donald Trump amekataa pendekezo lililoripotiwa ambapo Oman na Iran walikuwa wakijadili mpango wa kutoza ushuru meli zinazopita kwenye Mlango wa bahari wa Hormuz.

"Oman haina budi kufuta mkondo wa watu wengine, la sivyo tutawaangamiza. Wanafikiri kila kitu kitakuwa sawa," Trump aliwaambia waandishi wa habari wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri katika Ikulu ya White House siku ya Jumatano.

Bloomberg iliripoti kwa mara ya kwanza mnamo Mei 21 kwamba Iran ilikuwa katika mazungumzo na Oman kuhusu utozaji ushuru wa meli zinazopita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.

Gazeti la New York Times baadaye liliripoti, likinukuu vyanzo viwili vinavyofahamu mazungumzo hayo, kwamba majadiliano hayakuwa juu ya kutoza ushuru wa moja kwa moja kwenye njia ya kupita Hormuz, bali kuhusu kutoza meli kwa huduma.

Kauli ya Trump inasemekana kuwashangaza waangalizi wa eneo hilo kwa sababu Oman kwa muda mrefu imekuwa ikizingatiwa kuwa mmoja ya washirika wa karibu wa Marekani katika eneo la Ghuba.

Mataifa hayo mawili yana mikataba ya ushirikiano wa kiulinzi ya miongo kadhaa ambapo jeshi la Marekani linaweza kufikia bandari na kambi za ndege za Oman, ambazo zinachukuliwa kuwa muhimu kwa operesheni za kijeshi za Marekani katika eneo la Ghuba na Bahari ya Hindi.

Pia kuna makubaliano ya biashara huria kati ya Oman na Amerika.

Oman ni mshirika wa karibu wa Marekani

Oman kwa muda mrefu imekuwa na jukumu muhimu kama mpatanishi kati ya Marekani na Iran, na katika mazungumzo ya nyuma ya pazia kabla ya kufikiwa kwa makubaliano ya nyuklia ya 2015.

Hata kabla ya Marekani na Israel kuanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran mnamo Februari 28, Oman ilikuwa ikiandaa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.

Mapema mwezi Februari, mjumbe wa Trump katika eneo la Mashariki ya Kati Steve Witkoff na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi walikutana mjini Muscat kwa mazungumzo ya nyuklia, lakini mazungumzo hayo hatimaye yaligonga mwamba.

Muscat imedumisha uhusiano wake na Iran na imejaribu kujiimarisha kama mpatanishi katika mizozo ya kikanda.

Siku ya Jumatano, Trump aliashiria kwamba makubaliano yoyote ya baadaye na Iran yanaweza pia kuhusishwa na Saudi Arabia na nchi nyingine zenye Waislamu wengi kurejesha uhusiano na Israel.

"Ikiwa hawatatia saini, sidhani tunastahili kuwa na makubaliano haya," Trump alisema.

Ingawa wiki iliyopita Trump alisema kwamba mpango wa kumaliza vita vya Mashariki ya Kati ulikuwa unakaribia kufikiwa, kauli yake ya Jumatano ilionyesha kuwa hana haraka kukamilisha makubaliano yoyote.

Kwa nini Oman ni tofauti na nchi nyingine za Ghuba?

Oman imekuwa na jukumu la kuleta utulivu nyuma ya pazia kuliko nchi zingine za Ghuba kama vile Qatar, Saudi Arabia na UAE.

Lakini muda mfupi kabla ya shambulio dhidi ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad Al-Busaidi, alitoa hadharani wito wa muda wa mazungumzo kuongezwa alipokuwa akizungumza na kituo cha habari cha CBS.

Mwezi Machi, Al-Busaidi aliandika makala katika gazeti la The Economist akionya kwamba kuwa hatua ya Marekani kushirikiana na Israel kuendeleza vita ilikuwa inaharibu uaminifu wake katika eneo hilo.

Aliandika, "Marekani imepoteza udhibiti wa sera yake ya kigeni."

Katika chapisho la mtandao wa kijamii mnamo mwezi Machi, Al-Busaidi alipinga madai ya utawala wa Trump kwamba Iran ilikuwa tishio kwa Marekani na washirika wake.

Aliandika, "Haijalishi msimamo wako ni upi kuhusu Iran, vita hivi havikuanzishwa na wao."

Marekani haina kambi za kudumu za kijeshi nchini Oman, tofauti na Qatar, Bahrain, UAE na Saudi Arabia.

Masharti mapya ya Trump

Kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao ni njia muhimu kwa takriban asilimia 20 ya biashara ya mafuta duniani, imekuwa suala kuu katika mazungumzo ya kumaliza vita vya Marekani na Iran.

Iran ilifunga njia hiyo ya baharini muda mfupi baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel mwezi Februari.

Licha ya tangazo la Trump la kusitisha mapigano mwezi Aprili, ambalo lilieleza kufunguliwa tena kamili kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na Iran, njia hiyo inasalia imefungwa kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na hili, bei ya gesi duniani imeongezeka.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa lilionya wiki iliyopita kwamba kukaribia kusimamishwa kwa trafiki ya baharini kupitia Hormuz kunaweza kutishia shida ya chakula duniani.

Oman kwa muda mrefu imekuwa na uhusiano mzuri na Marekani, lakini sio mwanachama wa Mkataba wa Abraham wa Trump.

Oman imekuwa na jukumu muhimu nyuma ya pazia kama mpatanishi katika mpango wa nyuklia wa Iran na mazungumzo ya hivi karibuni ya kumaliza vita.

Lakini Trump alikariri siku ya Jumatano kwamba Iran haitapata udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz chini ya makubaliano yoyote ya amani.

Alisema, "Mlango wa bahari wa Hormuz unapaswa kubaki wazi kwa kila mtu. Ni njia ya kimataifa ya baharini. Hakuna atakayekuwa na udhibiti juu yake. Tutaufuatilia, lakini hakuna atakayekuwa na udhibiti. Hii ni sehemu ya mazungumzo yetu."

Baada ya mkutano wa baraza la mawaziri, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ilikariri matamshi makali ya Trump kupitia chapisho la mtandao wa kijamii.