Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mbivu na mbichi za matukio ya Oktoba 29 kujulikana leo Tanzania

Ripoti ya Tume ya Matukio ya Oktoba 29 inachukuliwa kama nyenzo muhimu ya kuweka wazi ukweli na kutoa mwelekeo wa taifa baada ya kipindi hicho kigumu.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Mashambulizi ya Marekani na Israel kitovu cha ukosefu wa usalama Ghuba, Hormuz - Iran

    Serikali ya Iran katika mtandao wa X inaeleza kwamba Waziri wa masuala ya kigeni wa taifa hilo amekutana na mjumbe maalum wa Korea Kusini Chung Byung-ha mjini Tehran, ambapo Waziri huyo ameyataka mataifa hayo “kuwa na msimamo thabiti katika kulaani mashambulizi ya Marekani na Israel.”

    Inaripoti Araghchi akisema kwamba Iran imechukua hatua chini ya sheria za kimataifa kulinda usalama na maslahi yake, ikiongeza kuwa washambuliaji wanapaswa kuwajibishwa.

    Jeshi la wanamaji la Iran (IRGC) limedai kushambulia meli tatu katika lango la bahari - zikikamata mbili - baada ya kuapa kulipiza kisasi kufuatia Marekani kuizuia meli ya mizigo yenye bendera ya Iran.

    Unaweza kusoma pia:

  2. Lamine Yamal apata jeraha

    Lamine Yamal amepata majeraha wakati akipiga penalti iliyoipa Barcelona ushindi mwembamba dhidi ya Celta Viga na kuongeza kileleni mwa La Liga kwa pointi tisa.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 alifunga penalti dakika ya 40 kwenye Uwanja wa Nou Camp baada ya kuingia ndani ya eneo la hatari na kuangushwa na Yoel Lago.

    Lakini mara tu baada ya kuingiza mpira wavuni kipa Lamine Yamal alikwenda chini huku ameshika paja lake la kushoto.

    Alitoka uwanjani kwa msaada wa madaktari wa timu na kuelekea moja kwa moja kwenye handaki huku nafasi yake ikichukuliwa na Roony Bardghji.

    Ushindi huo unawafikisha mabingwa watetezi wa La Liga, Barcelona - ambao wamebakiwa na michezo sita - kuelekea kutetea ubingwa wao.

    Hansi Flick anatumai jeraha la Lamine Yamal halitamzuia kucheza mechi ya Clasico mwezi ujao dhidi ya Real Madrid iliyo katika nafasi ya pili, huku Uhispania ikiwa na wasiwasi kuhusu utimamu wa mwili wa kijana huyo kwa Kombe la Dunia mwezi Juni.

    Lamine Yamal, ambaye amefunga mabao 16 na kutoa pasi 11 za mabao katika La Liga msimu huu, alitajwa kuwa Mchezaji Bora Kijana Katika Mashindano ya Euro 2024 huku Uhispania ikitwaa kombe hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Lebanon yaishutumu Israel kwa kumshambulia mwandishi wa habari na kumuua

    Waziri mkuu wa Lebanon ameishutumu Israeli kwa uhalifu wa kivita baada ya mashambulizi ya anga ya Israeli kumuua mwandishi mmoja wa habari na kumjeruhi mwingine kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano.

    Maafisa nchini Lebanon wanasema Amal Khalil na Zeinab Faraj walishambuliwa kimakusudi walipokuwa wakitafuta hifadhi katika nyumba baada ya shambulio la awali la anga kupiga gari lililokuwa mbele yao, na kuwaua wanaume wawili.

    Maafisa hao pia wanalishutumu Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) kwa kushambulia ambulensi kwa makusudi ilipojaribu kuwafikia waandishi wa habari katika kijiji cha Tayri.

    Jeshi la IDF limekana kwamba limezuia timu za uokoaji kufika katika eneo hilo na kusema haliwalengi waandishi wa habari.

    Waandishi wa habari Khalil, 43, ambaye alifanya kazi katika gazeti la Lebanoni la Al-Akhbar, na Faraj, mpiga picha huru, walikuwa wakisafiri pamoja.

    Wanaume wawili waliofariki hawajatajwa majina.

    Mapema mwezi huu, waandishi wa habari wawili waliuawa katika mashambulizi tofauti ya Israel nchini Lebanon.

    Mwezi uliopita, waandishi wa habari watatu wa Lebanon waliuawa katika shambulio la Israel katika mji wa Jezzine, waajiri wao walisema.

    Kwa uchache watu 2,475 wameuawa katika mashambulizi ya Israeli nchini Lebanon tangu vita vya hivi karibuni vianze, na zaidi ya 7,500 wamejeruhiwa, kulingana na mamlaka ya Lebanon. Idadi hiyo inajumuisha wanawake 274 na watoto 177.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Afisa mwingine wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani aachia ngazi

    Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani John Phelan anaondoka katika utawala wa Trump, imetangaza Pentagon siku ya Jumatano.

    Kuondoka kwake "ni mara moja," msemaji wa Pentagon Sean Parnell alisema katika chapisho la mitandao ya kijamii.

    Parnell aliongeza kuwa, Naibu Katibu Mkuu wa Jeshi la Wanamaji Hung Cao atahudumu kama kaimu katibu.

    Phelan ndiye kiongozi wa hivi karibuni wa ngazi ya juu wa kijeshi kuondoka katika utawala huo katika miezi ya hivi karibuni.

    Kuondoka kwake kunakuja wakati wa vita kati ya Marekani, Israeli na Iran na kuendelea kwa vizuizi vya Marekani kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.

    "Kwa niaba ya Waziri wa Vita na Naibu Waziri wa Vita, tunamshukuru Katibu Phelan kwa utumishi wake katika Jeshi la Wanamaji la Marekani," Parnell aliandika. "Tunamtakia kila la kheri katika maisha yake ya baadaye."

    Jeshi la Wanamaji halijatoa sababu ya kuondoka kwa Phelan.

    Hii inakuja wiki chache tu baada ya Waziri wa Vita/Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth kumtaka Mkuu wa Majeshi Randy George ajiuzulu kutoka wadhifa wake.

    Maafisa wengine wawili wa Jeshi, Jenerali David Hodne na Meja Jenerali William Green, pia wameondolewa katika nyadhifa zao hivi karibuni.

    Tangu aingie Pentagon, Hegseth amewafukuza kazi dazeni ya maafisa wakuu wa jeshi, akiwemo mkuu wa operesheni za majini na naibu mkuu wa wafanyakazi wa Jeshi la Anga.

    Jukumu la Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa kiasi kikubwa ni la kiutawala na linajumuisha kuunda sera, kuajiri, kutoa mafunzo na kuwapa vifaa Jeshi la Wanamaji, pamoja na kusimamia bajeti na vifaa kama vile ujenzi, na ukarabati wa meli na vifaa vya majini.

    Phelan, ambaye hakuwahi kuhudumu jeshini hapo awali, aliapishwa kama Katibu wa Jeshi la Wanamaji Machi 2025 baada ya kuteuliwa na Rais Donald Trump 2024.

    Mfanyabiashara huyo alikuwa mfadhili mkubwa wa kampeni ya Trump.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mamlaka zisitumie haki kama chombo cha kutolea adhabu pekee - Papa Leo

    Papa Leo amewataka viongozi wa Equatorial Guinea kutoitumia haki kama chombo cha adhabu pekee, wakati wa ziara yake katika gereza maarufu katikamji mkuu wa uchumi, Bata.

    Papa alisema kuwa mfumo wa haki unapaswa kulinda jamii, akisisitiza kwamba “hakuna haki bila maridhiano.”

    "Haki ya kweli haitafuti kuadhibu bali kusaidia kujenga upya maisha ya waathiriwa, wahalifu na jamii zilizojeruhiwa na uovu," Papa Leo alisisitiza.

    Maoni hayo yalifuatia ukosoaji wake wa awali wa hali ya wafungwa katika magereza ya nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ambayo makundi ya haki za binadamu yanasema iko chini ya utawala wa kimabavu.

    Akizungumza na mamia ya wafungwa waliokusanyika kwenye uwanja wa gereza, papa aliwahimiza wasikate tamaa, akisema, "hamko peke yenu."

    "Familia zenu zinawapenda na zinawasubiri. Watu wengi nje ya kuta hizi wanawaombea," aliongeza.

    Papa alipoondoka, wafungwa waliokuwa wamelowa kwenye mvua walipiga kelele wakisema"uhuru."

    Makundi ya haki za binadamu yanasema gereza hilo linatumika kuwanyima wapinzani na wakosoaji wa kisiasa uhuru wao, huku Amnesty International ikifichua kwamba wafungwa wanaripotiwa kupigwa mara kwa mara.

    Unaweza kusoma pia:

  6. Hormuz haitafunguliwa kutokana na ukiukaji wa usitishaji mapigano - Iran

    Mpatanishi mkuu wa Iran katika mazungumzo na Marekani alisema "haiwezekani" kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kufunguliwa kutokana na "ukiukwaji wa wazi wa usitishaji mapigano" uliofanywa na Marekani na Israel.

    Kupitia chapisho kwenye mtandao X Jumatano, Mohammad Bagher Ghalibaf, alisema "ukiukwaji" huo unajumuisha kizuizi cha majini cha Marekani dhidi ya bandari za Iran - ambacho alisema ni sawa na Israel kuuteka uchumi wa dunia - na "kuchochea vita" kutoka "katika pande zote".

    Iran iko tayari wazi kwa mazungumzo, alisema Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, lakini aliongeza, "ukiukwaji wa ahadi, vizuizi na vitisho ni vikwazo vikuu kwa mazungumzo ya kweli".

    Ilitarajiwa Jumanne kwamba Marekani na Iran zingefanya mazungumzo mapya ya amani nchini Pakistan wiki hii - lakini hayakufanyika.

    Unaweza kusoma pia:

  7. Serikali ya Zambia yachukua mwili wa rais wa zamani baada ya mvutano na familia

    Serikali ya Zambia inasema imechukua mwili wa rais wa zamani Edgar Lungu ambaye alifariki dunia Afrika Kusini miezi 10 iliyopita, uamuzi unaoenda kinyume na matakwa ya familia yake.

    Hili ni tukio la hivi karibuni katika mvutano kuhusu nini kifanyike na mwili wa kiongozi huyo wa zamani, kufuatia mgogoro wa muda mrefu kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema.

    Serikali imesisitiza kuwa, kama aliyewahi kuwa mkuu wa nchi, anapaswa kupewa heshima ya kitaifa na kuzikwa pamoja na marais wengine waliomtangulia katika eneo maalum la mazishi ya marais lililopo mji mkuu, Lusaka.

    Hata hivyo, familia ya Lungu ilitaka mazishi ya faragha baada ya mazungumzo na serikali kuhusu mipango ya mazishi kuvunjika.

    Mwezi Agosti mwaka jana, mahakama ya Afrika Kusini iliamua kuwa serikali ya Zambia inaweza kuurudisha mwili huo nyumbani na kufanya mazishi ya kitaifa.

    Familia iliwasilisha rufaa kupinga uamuzi huo, lakini kuhamishwa kwa mwili huo kumefuatia “kutoweza kwao kuendelea na kesi” katika mahakama ya rufaa, kwa mujibu wa taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha.

    Akizungumza kwenye kituo cha habari cha YouTube nchini Zambia Jumatano jioni, msemaji wa familia ya Lungu, Makebi Zulu, alipinga madai kwamba mchakato wa rufaa ulikuwa umefikia mwisho, akisema taratibu sahihi zilifuatwa.

    Sasa mawakili wa familia wamewasilisha ombi la dharura katika mahakama kuu ya Afrika Kusini ili mwili wa rais huyo wa zamani urejeshwe katika chumba cha kuhifadhia maiti ambako ulikuwa umehifadhiwa awali.

    Soma zaidi:

  8. Ripoti ya Tume ya Matukio ya Oktoba 29 kukabidhiwa leo Tanzania

    Macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa kwenye ripoti ya Tume ya Uchunguzi inayotarajiwa kukabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan baadae hii leo.

    Hii ndiyo siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu, baada ya miezi ya maswali mazito kufuatia matukio yaliyohusiana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

    Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mohamed Chande, ripoti hiyo ni matokeo ya uchunguzi wa kina uliogusa pande mbalimbali za jamii.

    Kauli za awali kutoka kwa rais zilieleza madai kuwa baadhi ya vijana waliingia mitaani kwa kushawishiwa kifedha, huku wengine wakidaiwa kufuata mkumbo bila kuelewa undani wa walichokuwa wakikifanya.

    Ripoti hii inachukuliwa kama nyenzo muhimu ya kuweka wazi ukweli na kutoa mwelekeo wa taifa baada ya kipindi hicho kigumu.

    Kwa wengi, ni fursa ya kupata majibu sahihi na kujenga imani upya kwa taasisi za nchi, huku ikibeba matumaini ya kuimarisha uwazi, haki na mshikamano wa kitaifa. Endelea kutufuatilia

    Pia unaweza kusoma:

  9. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.