Mashambulizi ya Marekani na Israel kitovu cha ukosefu wa usalama Ghuba, Hormuz - Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Iran katika mtandao wa X inaeleza kwamba Waziri
wa masuala ya kigeni wa taifa hilo amekutana na mjumbe maalum wa Korea Kusini Chung
Byung-ha mjini Tehran, ambapo Waziri huyo ameyataka mataifa hayo “kuwa na
msimamo thabiti katika kulaani mashambulizi ya Marekani na Israel.”
Inaripoti Araghchi akisema kwamba Iran imechukua hatua chini ya sheria
za kimataifa kulinda usalama na maslahi yake, ikiongeza kuwa washambuliaji
wanapaswa kuwajibishwa.
Jeshi la wanamaji la Iran (IRGC) limedai
kushambulia meli tatu katika lango la bahari - zikikamata mbili - baada ya
kuapa kulipiza kisasi kufuatia Marekani
kuizuia meli ya mizigo yenye bendera ya Iran.
Maelezo ya picha, Lamine Yamal alifunga bao lake la 16 la La Liga msimu huu kabla ya kuondoka uwanjani akiwa majeruhi
Lamine Yamal amepata majeraha wakati akipiga penalti
iliyoipa Barcelona ushindi mwembamba dhidi ya Celta Viga na kuongeza kileleni
mwa La Liga kwa pointi tisa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 alifunga penalti dakika ya 40
kwenye Uwanja wa Nou Camp baada ya kuingia ndani ya eneo la hatari na
kuangushwa na Yoel Lago.
Lakini mara tu baada ya kuingiza mpira wavuni kipa Lamine Yamal alikwenda
chini huku ameshika paja lake la kushoto.
Alitoka uwanjani kwa msaada wa madaktari wa timu na kuelekea moja kwa
moja kwenye handaki huku nafasi yake ikichukuliwa na Roony Bardghji.
Ushindi huo unawafikisha mabingwa watetezi wa La Liga, Barcelona - ambao
wamebakiwa na michezo sita - kuelekea kutetea ubingwa wao.
Hansi Flick anatumai jeraha la Lamine Yamal halitamzuia kucheza mechi ya
Clasico mwezi ujao dhidi ya Real Madrid iliyo katika nafasi ya pili, huku
Uhispania ikiwa na wasiwasi kuhusu utimamu wa mwili wa kijana huyo kwa Kombe la
Dunia mwezi Juni.
Lamine Yamal, ambaye amefunga mabao 16 na kutoa pasi 11 za mabao katika
La Liga msimu huu, alitajwa kuwa Mchezaji Bora Kijana Katika Mashindano ya Euro
2024 huku Uhispania ikitwaa kombe hilo.
Lebanon yaishutumu Israel kwa kumshambulia mwandishi wa habari na kumuua
Chanzo cha picha, AP
Maelezo ya picha, Amal Khalil alikuwa mwandishi wa habari wa gazeti la Lebanoni la Al-Akhbar
Waziri mkuu wa Lebanon ameishutumu Israeli kwa uhalifu wa kivita baada
ya mashambulizi ya anga ya Israeli kumuua mwandishi mmoja wa habari na
kumjeruhi mwingine kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano.
Maafisa nchini Lebanon wanasema Amal Khalil na Zeinab Faraj walishambuliwa
kimakusudi walipokuwa wakitafuta hifadhi katika nyumba baada ya shambulio la
awali la anga kupiga gari lililokuwa mbele yao, na kuwaua wanaume wawili.
Maafisa hao pia wanalishutumu Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) kwa kushambulia
ambulensi kwa makusudi ilipojaribu kuwafikia waandishi wa habari katika kijiji
cha Tayri.
Jeshi la IDF limekana kwamba limezuia timu za uokoaji kufika katika eneo
hilo na kusema haliwalengi waandishi wa habari.
Waandishi wa habari Khalil, 43, ambaye alifanya kazi katika gazeti la
Lebanoni la Al-Akhbar, na Faraj, mpiga picha huru, walikuwa wakisafiri pamoja.
Wanaume wawili waliofariki hawajatajwa majina.
Mapema mwezi huu, waandishi wa habari wawili waliuawa katika
mashambulizi tofauti ya Israel nchini Lebanon.
Mwezi uliopita, waandishi wa habari watatu wa Lebanon waliuawa
katika shambulio la Israel katika mji wa Jezzine, waajiri wao walisema.
Kwa uchache watu 2,475 wameuawa katika mashambulizi ya Israeli nchini
Lebanon tangu vita vya hivi karibuni vianze, na zaidi ya 7,500 wamejeruhiwa,
kulingana na mamlaka ya Lebanon. Idadi hiyo inajumuisha wanawake 274 na watoto 177.
Afisa mwingine wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani aachia ngazi
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, John Phelan akiwa na Donald Trump
Katibu wa Jeshi la Wanamaji la
Marekani John Phelan anaondoka katika utawala wa Trump, imetangaza Pentagon siku
ya Jumatano.
Kuondoka kwake "ni mara moja," msemaji wa Pentagon Sean
Parnell alisema katika chapisho la mitandao ya kijamii.
Parnell aliongeza kuwa, Naibu Katibu Mkuu wa Jeshi la Wanamaji Hung Cao
atahudumu kama kaimu katibu.
Phelan ndiye kiongozi wa hivi karibuni wa ngazi ya juu wa kijeshi
kuondoka katika utawala huo katika miezi ya hivi karibuni.
Kuondoka kwake
kunakuja wakati wa vita kati ya Marekani, Israeli na Iran na kuendelea kwa
vizuizi vya Marekani kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.
"Kwa niaba ya Waziri wa Vita na Naibu Waziri wa Vita, tunamshukuru
Katibu Phelan kwa utumishi wake katika Jeshi la Wanamaji la Marekani,"
Parnell aliandika. "Tunamtakia kila la kheri katika maisha yake ya
baadaye."
Jeshi la Wanamaji halijatoa sababu ya kuondoka kwa Phelan.
Hii inakuja wiki chache tu baada ya Waziri wa Vita/Ulinzi wa Marekani
Pete Hegseth kumtaka Mkuu wa Majeshi Randy George ajiuzulu kutoka
wadhifa wake.
Maafisa wengine wawili wa Jeshi, Jenerali David Hodne na Meja Jenerali
William Green, pia wameondolewa katika nyadhifa zao hivi karibuni.
Tangu aingie Pentagon, Hegseth amewafukuza kazi dazeni ya maafisa wakuu
wa jeshi, akiwemo mkuu wa operesheni za majini na naibu mkuu wa wafanyakazi wa
Jeshi la Anga.
Jukumu la Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa kiasi kikubwa ni
la kiutawala na linajumuisha kuunda sera, kuajiri, kutoa mafunzo na kuwapa
vifaa Jeshi la Wanamaji, pamoja na kusimamia bajeti na vifaa kama vile ujenzi,
na ukarabati wa meli na vifaa vya majini.
Phelan, ambaye hakuwahi kuhudumu jeshini hapo awali, aliapishwa kama
Katibu wa Jeshi la Wanamaji Machi 2025 baada ya kuteuliwa na Rais Donald Trump 2024.
Mfanyabiashara huyo alikuwa mfadhili mkubwa wa kampeni ya Trump.
Mamlaka zisitumie haki kama chombo cha kutolea adhabu pekee - Papa Leo
Chanzo cha picha, Getty Images
Papa Leo amewataka viongozi wa Equatorial Guinea kutoitumia haki kama
chombo cha adhabu pekee, wakati wa ziara yake katika gereza maarufu katikamji mkuu wa uchumi, Bata.
Papa alisema kuwa mfumo wa haki unapaswa kulinda jamii, akisisitiza
kwamba “hakuna haki bila maridhiano.”
"Haki ya kweli haitafuti kuadhibu bali kusaidia kujenga upya maisha
ya waathiriwa, wahalifu na jamii zilizojeruhiwa na uovu," Papa Leo
alisisitiza.
Maoni hayo yalifuatia ukosoaji wake wa awali wa hali ya wafungwa katika magereza
ya nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ambayo makundi ya haki za binadamu
yanasema iko chini ya utawala wa kimabavu.
Akizungumza na mamia ya wafungwa waliokusanyika kwenye uwanja wa gereza,
papa aliwahimiza wasikate tamaa, akisema, "hamko peke yenu."
"Familia zenu zinawapenda na zinawasubiri. Watu wengi nje ya kuta
hizi wanawaombea," aliongeza.
Papa alipoondoka, wafungwa waliokuwa wamelowa kwenye mvua walipiga
kelele wakisema"uhuru."
Makundi ya haki za binadamu yanasema gereza hilo linatumika kuwanyima
wapinzani na wakosoaji wa kisiasa uhuru
wao, huku Amnesty International ikifichua kwamba wafungwa wanaripotiwa kupigwa
mara kwa mara.
Hormuz haitafunguliwa kutokana na ukiukaji wa usitishaji mapigano - Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Mpatanishi mkuu wa Iran katika mazungumzo na Marekani alisema
"haiwezekani" kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kufunguliwa kutokana na
"ukiukwaji wa wazi wa usitishaji mapigano" uliofanywa na Marekani na
Israel.
Kupitia chapisho kwenye mtandao X Jumatano, Mohammad Bagher Ghalibaf,
alisema "ukiukwaji" huo unajumuisha kizuizi cha majini cha Marekani
dhidi ya bandari za Iran - ambacho alisema ni sawa na Israel kuuteka uchumi wa dunia - na "kuchochea
vita" kutoka "katika pande
zote".
Iran iko tayari wazi kwa mazungumzo, alisema Rais wa Iran Masoud
Pezeshkian, lakini aliongeza, "ukiukwaji wa ahadi, vizuizi na vitisho ni
vikwazo vikuu kwa mazungumzo ya kweli".
Ilitarajiwa Jumanne kwamba Marekani na Iran zingefanya
mazungumzo mapya ya amani nchini Pakistan wiki hii - lakini hayakufanyika.
Serikali ya Zambia yachukua mwili wa rais wa zamani baada ya mvutano na familia
Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Zambia inasema imechukua mwili wa rais wa zamani Edgar Lungu ambaye
alifariki dunia Afrika Kusini miezi 10 iliyopita, uamuzi unaoenda kinyume na
matakwa ya familia yake.
Hili ni tukio la hivi karibuni katika mvutano kuhusu nini kifanyike na
mwili wa kiongozi huyo wa zamani, kufuatia mgogoro wa muda mrefu kati ya Lungu
na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema.
Serikali imesisitiza kuwa, kama aliyewahi kuwa mkuu wa nchi, anapaswa
kupewa heshima ya kitaifa na kuzikwa pamoja na marais wengine waliomtangulia
katika eneo maalum la mazishi ya marais lililopo mji mkuu, Lusaka.
Hata hivyo, familia ya Lungu ilitaka mazishi ya faragha baada ya
mazungumzo na serikali kuhusu mipango ya mazishi kuvunjika.
Mwezi Agosti mwaka jana, mahakama ya Afrika Kusini iliamua kuwa serikali
ya Zambia inaweza kuurudisha mwili huo nyumbani na kufanya mazishi ya kitaifa.
Familia iliwasilisha rufaa kupinga uamuzi huo, lakini kuhamishwa kwa
mwili huo kumefuatia “kutoweza kwao kuendelea na kesi” katika mahakama ya
rufaa, kwa mujibu wa taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha.
Akizungumza kwenye kituo cha habari cha YouTube nchini Zambia Jumatano
jioni, msemaji wa familia ya Lungu, Makebi Zulu, alipinga madai kwamba mchakato
wa rufaa ulikuwa umefikia mwisho, akisema taratibu sahihi zilifuatwa.
Sasa mawakili wa familia wamewasilisha ombi la dharura katika mahakama
kuu ya Afrika Kusini ili mwili wa rais huyo wa zamani urejeshwe katika chumba
cha kuhifadhia maiti ambako ulikuwa umehifadhiwa awali.
Ripoti ya Tume ya Matukio ya Oktoba 29 kukabidhiwa leo Tanzania
Chanzo cha picha, TUME
Macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa kwenye ripoti ya Tume ya Uchunguzi inayotarajiwa kukabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan baadae hii leo.
Hii ndiyo siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu, baada ya miezi ya maswali mazito kufuatia matukio yaliyohusiana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mohamed Chande, ripoti hiyo ni matokeo ya uchunguzi wa kina uliogusa pande mbalimbali za jamii.
Kauli za awali kutoka kwa rais zilieleza madai kuwa baadhi ya vijana waliingia mitaani kwa kushawishiwa kifedha, huku wengine wakidaiwa kufuata mkumbo bila kuelewa undani wa walichokuwa wakikifanya.
Ripoti hii inachukuliwa kama nyenzo muhimu ya kuweka wazi ukweli na kutoa mwelekeo wa taifa baada ya kipindi hicho kigumu.
Kwa wengi, ni fursa ya kupata majibu sahihi na kujenga imani upya kwa taasisi za nchi, huku ikibeba matumaini ya kuimarisha uwazi, haki na mshikamano wa kitaifa.
Endelea kutufuatilia