Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Wanafunzi 16 wafariki katika moto wa bweni la shule ya Utumishi Girls, Kenya

Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema limefika kwa tukio la moto ulioteketeza bweni katika Chuo cha Wasichana Utumishi kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru, ambapo kuna hofu kuwa wanafunzi 16 wamepoteza maisha.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Kiongozi Mkuu wa Iran amesema kuwa Marekani na Israel wanajaribu “kuidhibiti” nchi yake

    Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Mojtaba Khamenei, amesema siku ya Alhamisi katika ujumbe wa maandishi uliosomwa kwenye televisheni ya serikali kuwa Marekani na Israel wanajaribu kuiyumbisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Ayatollah Mojtaba Khamenei, ambaye hajaonekana hadharani tangu alipoingia madarakani Machi mwaka jana, aliongeza kusema: “Mpango huo wa adui, baada ya vita vilivyolazimishwa, shinikizo la kiuchumi na kizuizi cha kisiasa na vyombo vya habari, ni kuleta migawanyiko na kusambaratika ili kufidia kushindwa kijeshi na kuinyong'onyeza Iran.”

    Haya yanajiri baada ya Jeshi la Mapinduzi la Iran kutangaza kuwa walilenga kituo cha kijeshi cha Marekani kujibu mashambulizi ya Marekani kusini mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Iran.

    Taarifa ya jeshi, iliyoripotiwa na televisheni ya Iran, ilisema: “Kufuatia shambulio lililofanywa asubuhi hii na jeshi la Marekani dhidi ya eneo karibu na uwanja wa ndege wa Bandar Abbas kwa kutumia mabomu ya angani, saa 4:50 asubuhi (01:20 GMT) kituo cha kitengo cha anga cha Marekani kilichokuwa chanzo cha shambulio hilo kililengwa.”

    Hakukuwa na maelezo ya wazi kuhusu eneo la kambi hiyo, lakini Kuwait, mshirika wa Marekani, ilitangaza asubuhi ya Alhamisi kuwa ilifanikiwa kudhibiti mashambulizi ya makombora na droni.

    Kuwait imekemea kile ilichokiita “mashambulizi ya kikatili ya Iran” yaliyolenga eneo lake, ikisema ni “ongezeko hatari la mivutano na ukiukaji wa wazi wa mamlaka yake, usalama na uadilifu wa eneo lake, pamoja na tishio la moja kwa moja kwa maisha ya raia na miundombinu muhimu,” kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait.

    Wizara hiyo ilisema katika taarifa yake kwamba “ongezeko hilo la mivutano linakuja wakati juhudi kubwa zinaendelea kufanywa… kupunguza mvutano na kutuliza hali na kuzuia eneo hilo kuingia katika mzunguko mpya wa migogoro, jambo linaloongeza uzito wa mashambulizi haya na kudhoofisha juhudi za kidiplomasia za kulinda usalama na utulivu wa kikanda,” na ikaishinikiza Iran “ikomeshe mara moja na bila masharti mashambulizi haya ya kikatili na kubeba jukumu kwa matendo hayo.”

    Unaweza kusoma;

  2. Mahakama Tanzania yafuta kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa mali ya Chadema

    Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam imeifuta kesi ya madai ya mgawanyo wa mali usio sawa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya bara na Zanzibar. Mwananchi imeripoti

    Kesi hiyo ya madai ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu ambaye ni marehemu.

    Wakili wa upande wa wadaiwa aliieleza mahakama kuwa kuna pingamizi la awali linalodai kesi hiyo ni batili kwa kushindwa kubainisha kwa uwazi muda wa kuanza kwa madai ya ubaguzi na mgawanyo wa mali kati ya CHADEMA Tanzania Bara na CHADEMA Zanzibar.

    Hii leo Alhamisi, Jaji wa Mahakama Kuu, David Ngunyale ameifuta kesi hiyo baada ya kuridhika kuwa hati ya madai ina kasoro kwani haielezi mgogoro huo, yaani madai ya ukiukaji wa sheria katika mgawanyo wa rasilimali uliodaiwa na walalamikaji ulianza lini.

    Unaweza kusoma;

  3. Mwanamke aliyepora benki baada ya kuwa mafichoni kwa miaka 30 ahukumiwa

    Aliyekuwa mfuasi wa kundi la Red Army Faction (RAF) la Ujerumani amehukumiwa kifungo cha miaka 13 gerezani kwa kutekeleza vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha kati ya mwaka 1999 na 2016.

    Daniela Klette, mwenye umri wa miaka 67, alikamatwa hatimaye katika nyumba moja mjini Berlin mwaka 2024 baada ya zaidi ya miaka 30 akiwa mafichoni.Kesi yake ilianza kusikilizwa mwaka uliopita.

    Wakili wake wa utetezi aliomba aachiliwe huru, lakini mahakama ya Verden, Lower Saxony, ilimkuta na hatia siku ya Jumatano kwa makosa ya ujambazi uliokithiri, kukiuka sheria za silaha, na makosa mengine yaliyotendeka katika kipindi cha miaka 17.

    Kundi la RAF, ambalo pia lilijulikana kama “Baader-Meinhof Gang,” hatimaye lilivunjika baada ya kampeni ya mauaji, utekaji nyara na mashambulizi ya mabomu kuanzia miaka ya 1970 hadi mapema miaka ya 1990.

    Mahakama ilielezwa kuwa Daniela Klette alihusika katika uporaji wa maduka makubwa na magari ya kubeba fedha pamoja na wafuasi wengine wawili wa zamani wa RAF, Burkhard Garweg na Ernst-Volker Staub, ambao bado hawajakamatwa.

    Kesi hiyo ililenga matukio manane yawizi yaliyotokea kaskazini na magharibi mwa Ujerumani, yaliyoanza katika mji wa Duisburg mwezi Julai 1999, ambapo washambuliaji waliovaa barakoa walifika kwenye ATM kwa gari na kuwatishia walinzi kwa silaha na mabomu ya mkono, kisha wakatoroka na kiasi kikubwa cha fedha.

    Shambulio la mwisho zaidi lilitokea Juni 2016, likihusisha gari la kubeba fedha lililokuwa karibu na mji wa Braunschweig. Wahalifu hao walitoroka na takriban euro milioni 1.4 (paundi milioni 1.2).

    Daniela Klette alikamatwa Februari 2024, akiwa amejificha kwa kutumia jina la bandia na pasipoti ya nchi ya kigeni, na akiishi katika mtaa tulivu eneo la Kreuzberg.

  4. Serikali ya Bangladesh yaingilia kati uchinjaji wa ng'ombe 'anayefanana na Trump'

    Kuchinjwa kwa fahali aliyekuwa akisemekana kufanana na kupewa jina la utani “Donald Trump” kutokana na nywele zake kusimama.

    Fahali huyo, ambaye alikuwa anatarajiwa kuchinjwa wakati wa Eid, amechukuliwa na serikali ya Bangladesh ambayo imesema imechukua jukumu la kumtunza.

    Siku moja kabla ya Eid al-Adha, ilitangazwa kuwa serikali imeamua kumlinda ng’ombe huyo dhidi ya kuchinjwa wakati wa sikukuu hiyo. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bangladesh, Salahuddin Ahmed, alichukua jukumu maalum katika suala hilo.

    Kwa mujibu wa polisi, fahali huyo alichukuliwa kutoka nyumbani kwa mmiliki wake siku ya Jumatano kufuatia amri kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bangladesh, Salahuddin Ahmed, aliiambia BBC Bangla kuwa alinunua fahali huyo aliyeitwa “Donald Trump.” Alisema serikali inapanga kulinda aina hiyo adimu ya ng’ombe.

    Siku chache kabla ya Eid al-Adha, fahali huyo mwenye ualbino alipata umaarufu mkubwa nchini Bangladesh.

    Mmiliki wa fahali huyo, Ziauddin, mwenye umri wa miaka 37, alisema kaka yake alimpa fahali huyo mwenye uzito wa kilo 700 jina la Rais wa Marekani Donald Trump kutokana na nywele zake.

    Ziauddin aliongeza kuwa watu walikuwa wakimiminika kila mara kuja kumuona fahali huyo katika mwezi mzima wa Mei.

  5. DRC yataka kurejeshewa fedha za tiketi zilizonunuliwa kwa ajili ya Kombe la Dunia

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeiomba FIFA kurejesha gharama za tiketi za Kombe la Dunia 2026 zilizonunuliwa na mashabiki ambao sasa hawawezi kuingia Marekani kutokana na vikwazo vya usafiri vinavyohusiana na Ebola.

    Leopards wamerejea kwenye jukwaa kubwa la soka duniani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974, lakini hali ya dharura ya afya ya umma iliyotangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) tarehe 16 Mei inatishia kuwazuia mashabiki kusafiri kwenda Marekani.

    Maafisa wanasema kuna zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola Afrika ya Kati na Mashariki, pamoja na vifo 223 vinavyodhaniwa kutokea tangu mlipuko huo kutangazwa.

    Idadi kubwa ya visa na vifo hivyo imeripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu Kinshasa umesitisha huduma za utoaji wa visa.

    Ingawa WHO haijashauri kuwekwa kwa vikwazo vya usafiri, Marekani imepiga marufuku kuingia kwa watu wasiokuwa Wamarekani ambao wamekuwa nchini DR Congo, Uganda au Sudan Kusini ndani ya siku 21 zilizopita.

    “Tuliiomba FIFA kuona kama itawezekana kuzingatia hali hii, kwa sababu tiketi hizo ni ghali kiasi,” alisema rais wa shirikisho la soka la DR Congo (Fecofa), Veron Mosengo-Omba, akizungumza na BBC Sport Africa.

    “Wanapata adhabu kwa sababu hawawezi kuingia [Marekani] kuhudhuria Kombe la Dunia ili kuiunga mkono timu yao.

    “Hatupendi mashabiki wetu, wanaopenda soka na Kombe la Dunia, kupoteza kila kitu.”

    Marekani inaandaa Kombe la Dunia pamoja na Canada na Mexico, huku bei za tiketi zikiwa hadi mara saba zaidi kuliko zile za mashindano ya mwaka 2022 nchini Qatar kutokana na mfumo wa FIFA wa upangaji bei unaobadilika kulingana na mahitaji ya soko.

    Unaweza kusoma;

  6. Mashambulizi Israel yalenga kusini mwa Lebanon baada ya amri ya watu kuhama

    Mawimbi ya mashambulizi ya anga ya Israel yamekumba kusini mwa Lebanon, yakilenga miundombinu ya Hezbollah, kwa mujibu wa jeshi la Israel.

    Video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kutoka mji wa Tyre, ambao ni mmoja wa miji mikubwa nchini Lebanon, zinaonesha umati wa watu waliokuwa wamefunikwa na vumbi wakikusanyika karibu na majengo yaliyoporomoka.

    Siku ya Jumatano, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilitoa onyo kwa wakazi kuhamia upande wa kaskazini wa Mto Zahrani, takriban kilomita 40 (maili 25) kutoka mpaka wa Israel, likisema litachukua hatua “kali sana”.

    Israel na Hezbollah, kundi lenye nguvu la Kishia linaloungwa mkono na Iran, wamekuwa wakituhumiana kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa tarehe 17 Aprili.

    Mashambulizi mawili ya Israel yalilipiga eneo la Tyre na sehemu ya mashariki mwa mji huo alfajiri ya Alhamisi, shirika la habari la serikali ya Lebanon (NNA) liliripoti.

    Picha za video kutoka Tyre zilionesha milipuko na moto uliokuwa ukiendelea kuwaka usiku kucha hadi asubuhi ya Alhamisi.

    Video hizo zilionesha mitaa ikiwa imeangazwa kwa rangi ya machungwa kutokana na moto, barabara zilizojaa moshi, na gari moja likiwa limeteketea kwa moto.

    Kulipopambazuka, mpira mkubwa wa moto ulirekodiwa ukilipuka karibu na majengo marefu ya makazi, ukipeleka wingu kubwa la moshi lililofanana na uyoga kupaa juu ya anga la mji huo.

    Unaweza kusoma;

  7. Rais wa Kenya Ruto aomboleza wanafunzi waliofariki katika moto wa bweni Gilgil

    Rais wa Kenya, William Ruto, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wanafunzi waliopoteza maisha kufuatia moto uliotokea katika bweni la shule ya Wasichana ya Utumishi Academy mjini Gilgil Alhamisi asubuhi.

    Katika ujumbe wake wa pole, Rais Ruto ameeleza tukio hilo kuwa janga kubwa lililoinyang’anya taifa maisha ya vijana waliokuwa na matumaini na ndoto.

    “Mioyo na sala zetu ziko pamoja na familia zilizopoteza mabinti zao wapendwa katika moto wa kusikitisha uliotokea Utumishi Girls Academy, Gilgil,” aliandika Rais Ruto kupitia mtandao wa X.

    “Hakuna maneno yanayoweza kweli kupunguza maumivu ya kupoteza maisha ya vijana waliokuwa na matumaini na ndoto za baadaye. Kama taifa, tunaomboleza pamoja na wazazi, walezi, walimu na wanafunzi wenzetu wanaopitia janga hili kubwa,” aliongeza.

    Rais amesema kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuwaokoa walioathirika, kuhakikisha majeruhi wanapata matibabu pamoja na kuzisaidia familia zilizoathirika huku uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo ukiendelea.

    “Kwa sasa nguvu zetu zimeelekezwa katika kuwaokoa walioathirika, kuwapatia matibabu majeruhi na kusaidia familia zao wakati uchunguzi kuhusu chanzo cha moto ukiendelea,” ameandika.

  8. Tunawaunganisha wanafunzi na wazazi wao – Maafisa wa huduma za watoto

    Wizara ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Watoto imesema maafisa wa huduma za watoto pamoja na wahudumu wa ulinzi wa mtoto wametumwa eneo la tukio kuratibu hatua za haraka za dharura, zikiwemo kuhakikisha usalama wa wanafunzi walioathirika, kusaidia kuwatafuta na kuwaunganisha watoto na familia zao, pamoja na kuhakikisha huduma muhimu za ulinzi wa mtoto zinapatikana.

    Imeongeza kuwa huduma za usaidizi wa kisaikolojia na ushauri nasaha zinaendelea kuratibiwa kwa manusura, familia zilizopoteza wapendwa wao, walimu na wahudumu wa kwanza wa uokoaji ili kusaidia uponaji wa kihisia na kuimarisha afya ya akili.

    Wizara hiyo pia imesema dawati maalumu za kutoa taarifa na kusaidia familia zinaanzishwa ili kuwasaidia wazazi na walezi pamoja na kurahisisha uratibu wa usimamizi wa kesi mbalimbali zinazohusiana na tukio hilo.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Idara ya Huduma za Watoto itashirikiana na taasisi nyingine za serikali, zikiwemo Wizara ya Elimu, serikali za kaunti, vikosi vya dharura, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya na wadau wengine katika uchunguzi pamoja na tathmini ya usalama wa watoto.

    Wizara imesisitiza haja ya kuimarisha viwango vya usalama mashuleni, mifumo ya maandalizi ya dharura na hatua za ulinzi wa watoto katika taasisi za elimu, kwa mujibu wa Sheria ya Watoto ya mwaka 2022.

    Aidha, imeutaka umma pamoja na vyombo vya habari kuheshimu utu na faragha ya wanafunzi na familia zilizoathirika kwa kuepuka kusambaza picha za kutisha, taarifa za watoto au habari ambazo hazijathibitishwa kuhusiana na tukio hilo.

  9. Katika Picha: Hali ilivyo katika shule ya wasichana ya Utumishi Academy iliyochomeka usiku

    Sehemu ya jengo la Chuo cha Utumishi Academy iliyoteketea kwa moto.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, Mkuu wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Mohamed Amin, Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi (DIG) Elius Lagat pamoja na maafisa wengine wamewasili katika eneo la mkasa.

    Watu wamekusanyika nje ya shule huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu moto huo na watoto wao.

  10. Wanafunzi 16 wateketea kwa moto nchini Kenya: Tunachojua kufikia sasa

    Takriban wanafunzi 16 wamethibitishwa kufariki dunia kufuatia moto ulioteketeza bweni katika Chuo cha Wasichana Utumishi kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru, katika saa za mapema za Alhamisi.

    Polisi wamesema wanafunzi wengine 74 wanapatiwa matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo.

    Moto huo ulianza majira ya saa saba usiku (1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki) na kuteketeza bweni la Meline Waithera lililokuwa na takriban wanafunzi 220, wakiwemo wa Kidato cha Pili, Kidato cha Tatu na Kidato cha Nne.

    Ripoti ya polisi inaeleza kuwa mkuu wa shule aliarifu mamlaka majira ya saa kumi na nusu alfajiri (4:30 asubuhi), hatua iliyosababisha operesheni ya dharura kuanzishwa. Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema tukio hilo liliripotiwa mapema zaidi, takriban saa 3:30 usiku.

    Timu za uokoaji zikiwemo wazima moto wa kaunti, maafisa wa polisi na wahudumu wa dharura zilifika eneo la tukio huku mamlaka zikianza oparesheni ya uokoaji, utafutaji na uhakiki wa idadi ya wanafunzi.

    Naibu Mkuu wa Pili wa Jeshi la Polisi, Masoud Mwinyi, amesema uchunguzi bado unaendelea kubaini chanzo cha moto huo pamoja na ukubwa wa madhara yake, akionya dhidi ya uvumi wakati wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi wakiendelea na kazi yao.

    Ameeleza kuwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) pamoja na wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi wamefika eneo la tukio.

    “Timu za DCI na wataalamu wa forensiki tayari wapo eneo la tukio, na eneo limezingirwa.”

    Ameongeza kuwa baadhi ya wanafunzi walikimbia kuelekea maeneo ya jirani wakati wa taharuki na bado wanatafutwa.

    “Kwa sasa, maafisa wetu wanachunguza eneo kwa sababu baadhi ya wanafunzi walikimbia kwa hofu na mshtuko usiku.”

    Mamlaka zinaendelea na zoezi la uhakiki wa majina ili kubaini idadi kamili ya wanafunzi wote waliokuwepo.

    “Tunafanya kazi ya kuwatafuta wanafunzi wote na kufanya uhakiki kamili kuhakikisha kila mmoja anahesabiwa,” alisema Mwinyi.

    Wazazi walijitokeza kwa wingi nje ya shule tangu asubuhi, wakiwa na wasiwasi mkubwa wakitafuta taarifa za watoto wao huku mlango wa shule ukibaki umefungwa kwa idadi kubwa ya watu.

    Uongozi wa shule ulisema kuwa ni wazazi pekee ndio wataruhusiwa kuingia ndani kusaidia mchakato wa utambuzi na uhakiki wa wanafunzi.

    Mashuhuda wamesema kulikuwa na hali ya taharuki kubwa wakati wanafunzi wakijaribu kutoroka kutoka katika jengo lililokuwa likiwaka moto.

    Wambui Nderitu, ambaye mpwa wake ni mwanafunzi shuleni hapo, amesema alipokea simu muda mfupi baada ya moto kuanza.

    “Niliambiwa saa nane usiku kuwa kuna moto, nikaitwa niende kuangalia mtoto wake,” amesema.

    Nderitu amesema wazazi waliowasili shuleni walikuta hali ya taharuki na hofu kutokana na taarifa za vifo na majeruhi.

    “Tulianza kufika mapema na tulipofika tulielekezwa kupanga foleni. Wengi tulikuwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu tulikuwa tumesikia kuna waliokufa na wengine wamejeruhiwa na wako hospitalini.”

    Amesema baadhi ya wanafunzi walijeruhiwa baada ya kuruka kutoka ghorofa ya juu wakijaribu kujiokoa.

    “Baadhi waliokuwa ghorofa ya juu walilazimika kuruka, ndiyo maana wameumia.”

    Nderitu ameeleza kuwa mpwa wake amenusurika moto huo lakini amevunjika mguu.

    “Nilimkuta mpwa wangu… yuko salama… lakini amevunjika mguu,” alisema.

    Kwa mujibu wa maelezo ya mpwa wake, moto huo huenda ulianza karibu na saa sita usiku.

    Chanzo cha moto huo bado hakijabainika.

    Mamlaka zimesema taarifa zaidi zitatolewa baada ya wanafunzi wote kuthibitishwa na uchunguzi kukamilika.

  11. Marekani yaanzisha kituo cha afya Kenya kuwahifadhi Wamarekani waliokumbwa na Ebola

    Japokuwa wizara ya afya ya Kenya ilikanusha kuwa imekubali kuweka karantini ya wamarekani walioambukizwa ebola, Ikulu ya Marekani imethibitisha Jumatano kuwa Marekani inaanzisha kituo cha afya nchini Kenya kitakachopokea Wamarekani waliokumbana na virusi vya Ebola katika maeneo yaliyoathirika na mlipuko unaoendelea.

    Kwa mujibu wa afisa wa utawala, Marekani itaanzisha kile alichokiita “kituo cha kisasa kabisa” nchini Kenya kupitia juhudi za pamoja kati ya Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu, na Wizara ya Vita.

    Taarifa hiyo iliripotiwa kwanza na gazeti la The Wall Street Journal.

    Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio amesema katika kikao cha Baraza la Mawaziri Jumatano kuwa serikali “haitaruhusu mtu yeyote aliyeambukizwa Ebola kuingia Marekani.”

    Afisa huyo amesema lengo na muundo wa kituo hicho ni “kutoa huduma bora kwa Wamarekani wanaohitaji kuondolewa haraka” kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kuwekwa karantini, akisema hatua hiyo itapunguza “hatari za safari ndefu ya kurejeshwa Marekani.”

    “Wagonjwa wa Ebola wanahitaji huduma kwa haraka, na kituo hiki kitawawezesha Wamarekani walioko eneo hilo wanaoambukizwa Ebola kupata huduma za kuokoa maisha haraka iwezekanavyo bila safari ya zaidi ya saa 12 ya ndege ya uokoaji wa kimatibabu,” amesema afisa huyo.

    Ameongeza kuwa uwezo wa matibabu katika kituo hicho cha Kenya unatarajiwa kushughulikia “aina zote za ugonjwa wa Ebola, ikiwemo huduma za wagonjwa mahututi,” lakini akaeleza kuwa wagonjwa watatathminiwa mmoja mmoja ili kuamua kama wanahitaji kuhamishwa kwenda vituo vingine vyenye huduma za juu zaidi.

    Rubio pia amesisitiza dhamira ya serikali yake ya kudhibiti Ebola, akisema kuwa “kipaumbele cha kwanza cha sera yetu ya mambo ya nje ni kulinda raia wa Marekani.”

    “Haturuhusu na hatutaruhusu mtu yoyote aliyeambukizwa Ebola kuingia Marekani,” amesema Rubio, akiongeza kuwa “mashirika mbalimbali ya serikali” yanahusika na “kufuatilia watu ili kuhakikisha hakuna anayeingia nchini akiwa na Ebola na kusababisha tatizo,” akisema hatua hizo zinaendelea vizuri.

    Serikali ya Marekani hapo awali ilitumia mamlaka yake chini ya kifungu cha Title 42 kuzuia safari za kuingia Marekani kwa wasio raia, isipokuwa baadhi, waliotembelea DRC, Uganda au Sudan Kusini ndani ya siku 21 zilizopita. Amri hiyo ilipanuliwa wiki iliyopita kujumuisha pia wenye kadi za ukaazi wa kudumu (green card).

    Raia wa Marekani waliotembelea nchi hizo wanaelekezwa kupitia viwanja maalum vya ndege kwa uchunguzi wa ziada wa afya, vikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles, John F. Kennedy New York, Hartsfield Jackson Atlanta, na George Bush Intercontinental Houston.

  12. Kenya: Mwongozo wa usalama wa shule mwaka wa 2008

    Serikali ya Kenya ilitoa mwongozo mpya mwaka wa 2008 kuhusu usalama shuleni, kufuatia ghasia zilizotokea nchini humo karibu na uchaguzi wa 2007.

    Ilijumuisha itifaki za usalama wa mabweni, ikiwa ni pamoja na sheria zinazosema kwamba kila bweni linapaswa kuwa na mlango kila eneo la mwisho na njia ya dharura ya ziada katikati.

    Sheria hiyo ni pamoja na kwamba madirisha ya mabweni yanapaswa kuwa bila vyuma na "lazima iwe rahisi kufungua nje". Pia inasema kuwa vifaa vya kuzima moto "vinapaswa kufanya kazi na kuwekwa katika kila njia ya kutoka na ving'ora vya moto vilivyowekwa kwenye sehemu zinazofikika kwa urahisi".

  13. Takriban wanafunzi 16 wamefariki katika moto wa bweni la shule ya Utumishi Girls, Gilgil

    Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema limefika kwa tukio la moto ulioteketeza bweni katika Chuo cha Wasichana Utumishi kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru, ambapo kuna hofu kuwa wanafunzi 16 wamepoteza maisha.

    Taarifa zinasema moto huo ulianza majira ya saa saba usiku na kuripotiwa takriban saa tisa na nusu usiku Alhamisi, kwa mujibu wa shirika la Msalaba Mwekundu Kenya.

    Katika taarifa yake, shirika hilo limesema:

    “Baada ya tukio la moto lililoripotiwa saa 9:30 usiku katika Shule ya Wasichana Utumishi, Kaunti ya Nakuru, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limefika katika eneo la tukio na kusaidia katika operesheni ya dharura inayoendelea.”

    Limeongeza kuwa:

    “Wahudumu wetu wa kwanza, kikosi cha ambulensi cha EMS Kenya pamoja na wataalamu wetu wa usaidizi wa kisaikolojia wako eneo la tukio kuwasaidia wanafunzi walioathirika pamoja na wahudumu wengine na mamlaka husika.”

    Shughuli za uokoaji na tathmini ya tukio hilo bado zinaendelea huku mamlaka zikichunguza chanzo cha moto huo.

    Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Samuel Ndanyi, amesema kuna wanafunzi wasiopungua kumi ambao bado hawajulikani walipo.

    “Timu zetu zipo eneo la tukio kukusanya taarifa zaidi na kuwabaini wanafunzi wote kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hili. Tuna vifo na ni muhimu familia ziarifiwe kwanza,” alisema.

    Wazazi wamejaa katika lango la shule baada ya taarifa za tukio hilo kusambaa Gilgil na maeneo jirani, huku polisi wakizuia idadi kubwa kuingia ndani ya shule na kuruhusu wazazi pekee wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.

    Wanafunzi waliojeruhiwa wamekimbizwa katika Hospitali ya St. Joseph’s Gilgil kwa matibabu na uchunguzi zaidi.

  14. Marekani yaishambulia Iran mara ya pili ndani ya siku tatu

    Jeshi la Marekani limetekeleza mashambulizi mapya dhidi ya Iran, likilenga eneo la kijeshi katika mji wa kimkakati wa bandarini wa Bandar Abbas.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika Mashariki ya Kati (Centcom) imesema vikosi vyake pia vilidungua droni nne za mashambulizi za Iran ambazo “zilikuwa tishio katika eneo la Mlango wa Hormuz”.

    Kwa mujibu wa Centcom, eneo lililoko Bandar Abbas lilishambuliwa wakati likiwa linajiandaa kurusha droni ya tano. Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa milipuko ilisikiwa mashariki mwa mji huo.

    Mashambulizi hayo yanakuja wakati wa usitishaji mapigano wenye hali tete kati ya Marekani na Iran, pamoja na mazungumzo yanayoendelea ya kumaliza vita vya miezi mitatu vilivyosababisha usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz kuvurugika na bei za nishati duniani kupanda kwa kasi.

    Hii ni mara ya pili ndani ya siku tatu kwa Marekani kushambulia maeneo nchini Iran, huku ikisema mashambulizi hayo yalifanywa kwa kujilinda.

    Mashambulizi hayo mapya yanaongeza hofu ya kuvunjika kwa usitishaji mapigano uliopo.

    Centcom ilieleza hatua zake kuwa “za tahadhari, za kujihami pekee, na zinazolenga kudumisha usitishaji mapigano.”

    Mapema wiki hii, jeshi hilo lilithibitisha kutekeleza mashambulizi mengine ya “kujilinda” kusini mwa Iran Jumatatu, ambapo lilisema lililenga maeneo ya makombora ya Iran pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kutega mabomu katika Mlango wa Hormuz.

    Kutokana na mzozo huo, maelfu ya meli za biashara na mafuta zimekwama katika eneo hilo.

    Centcom imesema mashambulizi hayo yalilenga “kulinda wanajeshi wa Marekani dhidi ya vitisho vya vikosi vya Iran.”

    Iran imeyalaani mashambulizi hayo na kuyataja kuwa “ukiukaji mkubwa wa usitishaji mapigano”, huku ikionya kuwa haitaliacha “tendo lolote la uhasama bila majibu.”

    Rais wa Marekani, Donald Trump, pia ametishia kurejesha mashambulizi makubwa ya mabomu iwapo Iran haitakubali masharti ya Washington.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Uganda yakubali mpango wa Marekani wa kuwaweka Wamarekani karantini kufuatia mlipuko wa Ebola

    Uganda imethibitisha kuwa Marekani imeiomba nchi hiyo kuanzisha kituo maalumu cha kuwaweka karantini na kuwahudumia Wamarekani waliokumbana na virusi vya Ebola, huku hofu ikiongezeka kuhusu kuenea kwa mlipuko huo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Akizungumza katika mahojiano na BBC, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Uganda, Diana Atwine, amesema Kampala iko tayari kushirikiana katika mpango huo kutokana na uzoefu mkubwa wa nchi hiyo katika kukabiliana na milipuko ya Ebola.

    “Ndiyo, walitufikia kuhusu kuanzisha kituo cha Ebola hapa. Tuko wazi kwa hilo. Tuna utaalamu mkubwa nchini,” alisema Dkt Atwine.

    Kauli yake imekuja wakati Uganda ikiimarisha udhibiti mipakani baada ya watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola kujaribu kuingia nchini humo kutoka maeneo yaliyoathirika zaidi mashariki mwa DRC.

    “Siku tatu zilizopita tuliona wagonjwa wakijaribu kuvuka na kuingia nchini mwetu. Wana ndugu hapa ambao wamekuwa wakiwaambia kuwa wakifika Uganda watapata matibabu na kupona,” amesema.

    Kwa mujibu wa Dkt Atwine, baadhi ya watu hao tayari walikuwa na dalili kali za Ebola na walikiri kupoteza ndugu zao kutokana na ugonjwa huo.

    “Walikuwa wanatoka katika maeneo yaliyo kitovu cha mlipuko, walikuwa na dalili kubwa za Ebola na pia walikuwa wakikiri kuwa wamepoteza baadhi ya ndugu zao.”

    Uganda ina hofu kuwa kuacha mipaka ikiwa wazi kutafanya iwe vigumu kudhibiti maambukizi hayo.

    “Tuligundua kuwa tukiendelea kuweka mipaka wazi hatutaweza kuudhibiti mlipuko huu,” aliongeza.

    Serikali ya Uganda pia imesema inashirikiana na DRC kuanzisha vituo vya upimaji na matibabu karibu na maeneo ya mpakani ili kupunguza watu kuvuka mipaka wakitafuta huduma za afya.

    “Tunafanya kazi pia na DRC kuanzisha vituo vya upimaji na matibabu upande wa mpakani kwa watu wanaotafuta huduma za afya na wanaojaribu kuvuka mpaka.”

    Hatua hizo zinakuja wakati Shirika la Afya Duniani likiendelea kuhimiza juhudi za haraka kudhibiti mlipuko huo wa Ebola ambao umeibua wasiwasi mkubwa wa kiafya katika eneo la Afrika ya Kati na Mashariki.

    Soma zaidi:

  16. Crystal Palace ndio mabingwa wa Kombe la Europa Conference

    Crystal Palace F.C. imeendelea kuandika historia baada ya kutwaa taji lake la tatu ndani ya miezi 12, kufuatia ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Rayo Vallecano katika fainali ya Conference League iliyochezwa mjini Leipzig.

    Mshambuliaji wa Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, ndiye aliyefunga bao la ushindi lililowapa Eagles taji lao la kwanza Ulaya na taji la pili kubwa katika historia ya klabu hiyo, baada ya kutwaa kombe la FA msimu uliopita.

    Bao hilo lilipatikana dakika sita baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, baada ya kipa wa Rayo Vallecano, Augusto Batalla, kuokoa shuti la Adam Wharton lakini mpira ukamkuta Mateta aliyefunga kwa karibu.

    Mateta sasa amefikisha mabao 16 msimu huu akiwa Palace, licha ya kuwa karibu kuondoka Januari kuelekea AC Milan kabla ya majeraha ya goti kuzuia uhamisho huo.

    Kocha anayeondoka Palace, Oliver Glasner, ameihitimisha safari yake ya miaka miwili na nusu Selhurst Park kwa mafanikio makubwa baada ya kuiongoza timu hiyo kutwaa FA Cup, Community Shield na sasa Conference League.

    Timu zote mbili zilikuwa zikicheza fainali yao ya kwanza kabisa ya mashindano ya Ulaya, jambo lililosababisha mchezo kuanza kwa tahadhari kubwa katika dimba la Red Bull Arena.

    Rayo Vallecano walipata nafasi chache kupitia Alemao na Unai Lopez, lakini Palace walionekana kuwa hatari zaidi kuelekea mapumziko, huku Tyrick Mitchell akikosa nafasi nzuri baada ya pasi safi ya Adam Wharton.

    Katika kipindi cha pili, Yeremy Pino aliipatia Rayo nafasi kadhaa za kusawazisha, ikiwemo mpira wa adhabu uliogonga nyavu za pembeni mara mbili, lakini Palace walibaki imara hadi mwisho na kutwaa ushindi huo wa kihistoria.

  17. Trump asema mazungumzo ya Marekani na Iran bado hayajafikia matokeo yanayoridhisha

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema mazungumzo kati ya Marekani na Iran bado hayajafikia matokeo yanayoridhisha, akionya kuwa huenda Washington ikalazimika “kumalizia kazi” ikiwa makubaliano hayatapatikana.

    Akizungumza Jumatano katika kikao muhimu na wajumbe wa baraza lake la mawaziri, Trump amesema mazungumzo hayo “hayajazaa matunda hadi sasa” na kwamba Marekani “bado haijafurahishwa nayo, lakini itafurahishwa.”

    “Ama iwe kwa njia hii, au tutalazimika kumalizia kazi,” amesema Trump.

    Akirejelea viongozi wa Iran, Trump amesema wanajadili kutoka katika nafasi ya udhaifu.

    “Wanajadili wakiwa katika hali ya udhaifu. Lakini tutaona kitakachotokea. Huenda tukalazimika kurejea na kumalizia kazi, au huenda isiwe hivyo.”

    Trump pia alisisitiza kuwa anaamini viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wako tayari kufikia makubaliano.

    Katika kauli nyingine, bila kutoa takwimu rasmi, rais huyo alisema uchumi wa Iran unaendelea kudorora kwa kasi.

    “Uchumi wao unaanguka. Wana mfumuko wa bei wa asilimia 250. Fedha yao haina thamani na mfumo wao mzima wa uchumi unasambaratika,” alisema.

    Katika miezi ya karibuni, Iran imeshuhudia viwango vya juu vya mfumuko wa bei, huku baadhi ya tathmini zikieleza kuwa hali hiyo ni miongoni mwa mibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha karibu karne moja.

    Trump pia amekanusha uwezekano wa Marekani kulegeza vikwazo dhidi ya Iran ili kuruhusu mafuta ghafi ya Iran kuuzwa katika soko la kimataifa.

    “Hapana, hatuzungumzii kulegeza vikwazo wala kutoa fedha. Hakuna vikwazo vitakavyoondolewa, hakuna fedha zitakazotolewa, hakuna chochote,” amesema.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya taarifa zinazochipuka za tarehe 28 Mei 2026.