Rais wa Kenya William Ruto aalikwa mkutano wa viongozi wa G7
Rais William Ruto amealikwa kuhudhuria Mkutano ujao wa Viongozi wa Kundi la nchi Saba tajiri zaidi duniani (G7) utakaofanyika Évian, Ufaransa, hatua inayoashiria kuimarika kwa nafasi ya Kenya katika diplomasia ya kiuchumi duniani.
Uthibitisho wa mwaliko huo umetolewa katika kikao cha ngazi ya juu kilichofanyika Paris kati ya Balozi wa Kenya nchini Ufaransa Betty Cherwon na Katibu Mkuu wa Mipango ya Kiuchumi Boniface Makokha, wakati nchi hiyo ikikamilisha maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Maendeleo wa G7.
Kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi, kikao hicho kilichofanyika ofisini kwa balozi kilijikita katika kutathmini utayari wa Kenya na kuimarisha misimamo yake ya sera kabla ya mazungumzo ya mawaziri yaliyofanyika Aprili 29 hadi 30 Paris.
Cherwon amesema mazungumzo hayo yameipa Kenya fursa muhimu ya kuratibu vipaumbele vyake na kuhakikisha mchango wake katika ajenda ya maendeleo ya G7 unakuwa na uwazi na athari.
Makokha, ambaye anaongoza ujumbe wa Kenya katika mkutano wa mawaziri, amesema mwaliko wa Kenya katika mkutano wa viongozi wa G7 ni uthibitisho wa nafasi inayokua ya nchi hiyo katika mijadala ya uchumi wa kimataifa.
Kenya itahudhuria mkutano wa Juni pamoja na nchi nyingine zilizoalikwa zikiwemo Korea Kusini, Brazil na India, hatua inayoonyesha kuongezeka kwa nafasi yake miongoni mwa nchi zinazoibukia kiuchumi zinazoshiriki majadiliano ya ngazi ya juu na mataifa makubwa ya viwanda duniani.
Soma zaidi: