Chadema yataka haki ya Oktoba 29 na katiba mpya sasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, sasa kinaunganisha madai ya uwajibikaji kwa mauaji ya Oktoba 29, 2025 na shinikizo jipya la kusukuma mchakato wa Katiba Mpya, kikisema haki na mageuzi ya kisiasa haviwezi kutenganishwa.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, ametaka viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wawajibishwe kufuatia mauaji ya raia wasiokuwa na hatia yaliyoripotiwa wakati wa vuguvugu la Oktoba 29, 2025.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mnyika amesema wote waliohusika kufadhili au kutekeleza mauaji dhidi ya raia wanapaswa kuwajibishwa bila kujali nyadhifa zao.
''Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wawajibishwe kwa kushindwa kuwalinda Wananchi na kutuhumiwa kuhusika katika mauaji hayo na kushindwa kuzuia mauaji ya raia wasiokuwa na hatia'', asema Mnyika.
Ameongeza kuwa Kamati Kuu ya CHADEMA inataka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi ili kuchunguza kwa kina matukio ya Oktoba 29, 2025.
Wakati huohuo, Mnyika amesema Kamati Kuu ya chama hicho imefikia uamuzi kwamba Watanzania hawawezi kusubiri tena mchakato wa Katiba Mpya, akisisitiza kuwa muda wa mabadiliko ni sasa.
“Kamati Kuu inaona kwamba Watanzania hawawezi kusubiri tena Katiba Mpya kwa kipindi kingine isipokuwa sasa, Kamati Kuu imeadhimia kuundwa kwa Kamati ndogo ya Kamati Kuu ili kuandaa mkakati wa kukwamua mchakato wa Katiba Mpya ikiwa na majukumu ya kuandaa muswada wa sheria kwa niaba ya Wananchi,” amesema Mnyika.
Amesema CHADEMA imeamua kuunda kamati ndogo ya Kamati Kuu itakayoratibu mkakati wa kukwamua mchakato wa Katiba Mpya, ikiwemo kuandaa mapendekezo ya muswada wa sheria kwa niaba ya wananchi.
Soma zaidi:















