Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ubalozi wa Iran watumia vipi mtandao wa X kama silaha wakati wa vita?
Wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipoweka makataa ya mwisho kwa Iran kukubali makubaliano kabla ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya kile alichokiita "madaraja na vituo vya umeme" vya nchi hiyo, akaunti ya ubalozi wa Iran nchini Zimbabwe kwenye mtandao wa X iliandika kwa kejeli: "Saa mbili usiku si rahisi sana. Mnaweza kuisogeza hadi saa saba au nane mchana? Au ikiwezekana, saa saba au nane usiku?"
Katika kipindi cha vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na hata baada ya usitishaji mapigano, akaunti za kidiplomasia za Iran kwenye mtandao wa X zilikuwa sehemu muhimu ya mkakati wa Tehran wa mawasiliano ya mtandaoni na ushawishi wa kisiasa.
Badala ya kutumia lugha ya kawaida ya kidiplomasia, akaunti hizo zilichukua mkondo usio wa kawaida kwa kutumia vichekesho, kejeli, meme na majibu yaliyoratibiwa kwa lengo la kuunda simulizi, kupinga ukosoaji na kuwajibu maafisa wa Marekani.
Tarehe 10 Aprili, Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social akirejelea kwa njia isiyo ya moja kwa moja kampeni hiyo ya Iran mtandaoni: "Wairani wanafanya vizuri zaidi kushughulikia vyombo vya habari vya upotoshaji na mahusiano ya umma kuliko wanavyofanya vitani."
Baada ya vita kuanza, akaunti za mabalozi wa Iran zilijiondoa katika lugha ya jadi ya kidiplomasia na badala yake kutumia ucheshi na kejeli kujibu lawama, kuimarisha ujumbe wa kupinga vita na kupambana na simulizi zilizotawala.
Mkakati huu unaonekana pia kuwa sehemu ya juhudi za Iran kujenga upya taswira yake kimataifa wakati wa vita, vilivyotokea chini ya miezi miwili baada ya ukandamizaji mbaya zaidi wa maandamano kuwahi kushuhudiwa katika Jamhuri ya Kiislamu.
Ni balozi zipi zilikuwa mstari wa mbele?
Balozi za Iran katika maeneo mbalimbali zilikuwa na mchango mkubwa, huku akaunti za Iran nchini Afrika Kusini, Zimbabwe, India na Japan zikiwa miongoni mwa zilizokuwa hai zaidi kwa ushiriki wa mtandaoni.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ina uhusiano na takriban akaunti 130 za balozi na ofisi za ubalozi, nyingi zikiwa sehemu ya kampeni iliyoratibiwa kwa karibu.
Ujumbe uliokuwa ukichapishwa mara nyingi ulionekana kuwa na uratibu wa sauti, muda na mwelekeo.
Miongoni mwa akaunti zilizovutia zaidi ni ujumbe wa Iran nchini Afrika Kusini, ambao ulijizolea wafuasi wengi kwa kuchapisha meme na video zilizosambaa haraka mtandaoni zikikosoa na kubeza sera za Marekani.
Ujumbe huo ulikuwa miongoni mwa taasisi za kwanza kutumia mbinu hiyo.
Walikuwa wanawalenga nani?
Ujumbe huu unaonekana kulenga zaidi hadhira ya kimataifa kuliko wananchi wa ndani ya Iran.
Mtandao wa X bado umezuiwa nchini Iran, na tangu vita vilipoanza Februari 28, wananchi wengi wa Iran wamekuwa na ufikiaji mdogo sana wa intaneti ya kimataifa kutokana na kuzimwa kwa mtandao kwa kiwango kikubwa ambako bado kunaendelea.
Machapisho mengi yaliandikwa kwa Kiingereza na yalilenga kuvutia makundi yanayokosoa sera za kigeni za Marekani, yakiwemo sauti za kupinga vita, sehemu ya umma wa Marekani, na hadhira katika kile kinachoitwa Kusini ya Dunia.
Mtindo wa maudhui haya, ambao mara nyingi ulikuwa wa mzaha, kejeli au uchokozi wa kimtandao, uliundwa mahsusi kuwavuta vijana na jamii za mtandaoni zenye mashaka na hatua za Marekani.
End of Pia unaweza kusoma:
Walikuwa wakichapisha maudhui ya aina gani?
Akaunti za balozi za Iran zilitumia aina mbalimbali za maudhui, kuanzia vichekesho na kejeli hadi video za hisia na maudhui yaliyotengenezwa kwa akili unde.
Moja ya mada kuu ilikuwa kubeza matamshi ya maafisa wa Marekani, hasa Donald Trump, ambaye mara nyingi aliwasilishwa kama kiongozi asiye na msimamo au mwenye kauli zinazojikanganya.
Mada nyingine iliyojitokeza sana ilikuwa tishio la Marekani kuhusu Mlango wa Hormuz. Akaunti za Iran zilijibu kwa ucheshi ulioratibiwa, zikiwemo kejeli zilizosambaa kuhusu "funguo zilizopotea" za njia hiyo ya bahari.
Baadhi ya maudhui yalikuwa ya uzito zaidi. Machapisho kadhaa yalitumia akili unde kuwaonyesha waathiriwa wa mashambulizi ya Marekani na Israel, yakisimulia kwa hisia madhara ya kibinadamu ya vita.
Katika mojawapo ya mashambulizi ya kimtandao dhidi ya viongozi wa Marekani, akaunti za Iran zilijibu kwa ukali baada ya Trump kutishia "kuirudisha Iran katika Enzi ya Mawe," zikisisitiza ustaarabu wa kale wa Iran kwa rejea za kihistoria.
Baada ya usitishaji mapigano, ujumbe uligeukia zaidi mada za ushindi na ustahimilivu, huku machapisho yakisisitiza nafasi ya Iran kama taifa lenye nguvu duniani.
Mojawapo ya machapisho maarufu zaidi kutoka ubalozi wa Iran nchini India lilikuwa picha iliyotengenezwa kwa akili unde ikiwa na ujumbe: "Pigeni magoti mbele ya ustaarabu wa Iran."
Mada nyingine iliyojirudia katika maudhui ya akili unde ilikuwa madai ya uhusiano wa Donald Trump na Jeffrey Epstein pamoja na sakata pana la Epstein.
Katika tukio jingine, akaunti za kidiplomasia za Iran zilijibu haraka baada ya Trump kukosolewa kwa kuchapisha picha ya akili unde iliyomuonyesha akiwa kama Yesu Kristo akimponya mgonjwa hospitalini.
Video iliyochapishwa na ubalozi wa Iran nchini Tajikistan ilihuisha picha hiyo, ikimuonyesha Yesu akitokea nyuma ya Trump na kumpiga ngumi. Chapisho hilo lilitazamwa zaidi ya mara milioni 24.
Masuala ya uchumi wa Marekani pia yalikuwa sehemu ya kampeni hiyo, huku baadhi ya machapisho yakilenga hadhira ya Marekani kwa kuonyesha gharama za vita, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta.
Nani mwingine alihusika zaidi ya akaunti za mabalozi?
Mbali na njia rasmi za kidiplomasia, baadhi ya viongozi wa Iran na watayarishaji wa maudhui wasio rasmi pia walihusika.
Mohammad Baqer Qalibaf, spika wa bunge la Iran, ambaye alikuwa miongoni mwa watoa maamuzi wakuu wakati wa vita na baadaye akawa msuluhishi mkuu wa Iran katika mazungumzo ya amani na Marekani, alikuwa miongoni mwa maafisa mashuhuri waliokuwa wakichapisha kwa Kiingereza.
Mwanzoni akaunti yake ilitumia lugha kali na meme, lakini wakati na baada ya mazungumzo ilibadili mwelekeo na kutumia sauti rasmi zaidi.
Video za uhuishaji wa mtindo wa Lego pia zilikuwa na nafasi kubwa katika kampeni hiyo. Video hizo, zilizosambazwa sana kwenye X na Instagram, zilibeba ujumbe wa kupinga vita na kuikosoa Marekani kwa muziki mwepesi na simulizi rahisi.
Watayarishaji wa video hizo, wanaojiita Explosive Media, hujitambulisha kama wa kujitegemea, lakini maudhui yao yalikuwa sambamba kwa karibu na simulizi za serikali ya Iran.
Video hizo zinaonekana kulenga hadhira ya Marekani, zikitumia muziki wa hip hop uliotengenezwa kwa akili unde na ujumbe mfupi lakini wenye uchokozi.
Katika simulizi hizo, Trump huwasilishwa kwa taswira hasi, akilaumiwa kwa vurugu, huku serikali ya Marekani ikituhumiwa kwa ufisadi na kushawishiwa na Israel.
Si rahisi kupima athari halisi ya kampeni ya Iran mtandaoni kwa hadhira ya Marekani. Hata hivyo, ni wazi kuwa kwa nyakati fulani iliweza kushindana kwa umakini wa hadhira na mmoja wa watu wenye sauti kubwa zaidi mtandaoni, Donald Trump.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid