Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Iran yaweka masharti kabla ya kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz

Marekani, kwa upande wake, inaendelea kusisitiza kuwa Mlango wa Hormuz uko wazi na kwamba mabomu ya baharini yameondolewa, huku ikisema hakuna mazungumzo yaliyopangwa kwa sasa na Iran.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Muhoozi awatishia shemeji zake, kisha 'awasamehe'

    Mzozo wa kifamilia watokea katika familia ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni na kuenea hadharani kiwango cha Mkuu wa Mejeshi ya nchi hilo kutishia kumkamata shimeji wake.

    Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mkuu wa majesty Uganda, na Mtoto wa Rais Museveni kupitia mtandao wa X Mapema siku ya Ijumaa alizungumza kwa ukali akimkashifu shemeji yake drek Rwabwogo ambaye ni mume wa Askofu Patience Museveni Rwabogo.

    amesema kwamba atazungumza na dada zake wawili Patience na Natasha kutatua mzozo uliopo.

    Rwabogo aidha ni mshauri mwandamizi wa Rais Museveni na mwenyekiti wa Kamati inayoshughulikia mauzo ya nje na maendelo ya kiviwanda nchini Uganda.(PACEID)

    Kwa mujibu wa vyanzo nchini Uganda Mvutano kati ya Muhoozi na Rwabwogo umekuwa ukidhirika wazi kwa mda mrefu.

    Lakini umeingia katika awamu nyingine baada ya Muhoozi kumtuhumu Rwabwogo kwa ‘ufisadi’ na kutishia kumkamata huku akitaja kamati ya PACEID kama ilio kinyume cha sheria.

    Katika machapisho yake kwenya mtandao wa X, Muhoozi pia aliandika na kumkana Shemeji huyo na alilazimishwa tu na wazazi wake kumkubali. Katika ujumbe huo alimtaja shimeji yake mwingine Edwin Karugire kuwa kipenzi chake na kwamba maoni ya Watoto wa kiume yanapswa kuheshimiwa na wazazi hasa kuhusu ndoa za mabinti wao.

    Rwabwogo amewahi kukosoa kile alichokiita kutokuwapo kwa uwajibikaji na vikwazo dhidi ya uhuru wa kiraia nchini Uganda.

    Wafuasi wao pia wamekuwa wakizozana hadharani-ila kwa sasa, majibizano kati ya hao wawili yanazidi kuakisi mvutano mpana zaidi kuhusu ushawishi wa kisiasa na suala la urithi wa uongozi ndani ya mfumo tawala wa Uganda.

  2. Mshukiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda ahukumiwa kifungo cha maisha

    Mahakama nchini Uholanzi imemhukumu kifungo cha maisha gerezani mwanamume mwenye uraia wa Uholanzi na Rwanda kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.

    Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 66, aliyetajwa mahakamani kama Eugene N, alipatikana na hatia ya makosa kadhaa, yakiwemo ya kurusha guruneti katika kundi la Watutsi waliokuwa wametafuta hifadhi kwenye uwanja wa michezo.

    Jaji alisema kuwa alitiwa hatiani kwa uhalifu wa kivita na uhalifu wa mauaji ya kimbari, baada ya kubainika kwamba alitekeleza vitendo hivyo akiwa na nia ya kuchangia mauaji ya kimbari.

    Rwanda ilikuwa imeomba akabidhiwe nchini humo mwaka 2014 ili akabiliwe na sheria, lakini mamlaka za Uholanzi ziliamua kuendesha uchunguzi wake wenyewe dhidi yake, kwa kuwa alikuwa tayari amepata uraia wa Uholanzi.

    Katika kipindi cha siku 100 kuanzia Aprili 1994, takriban watu 800,000, wengi wao wakiwa Watutsi pamoja na Wahutu wenye misimamo ya wastani, waliuawa na Wahutu wenye msimamo mkali.

    Mahakama ya The Hague ilielezwa kuwa Eugene N alikuwa na nafasi ya uongozi katika jamii wakati wa mauaji hayo, akisimamia takriban watu 1,000 katika eneo la Mbazi, kusini mwa Rwanda.

    "Mtuhumiwa alikuwa mtu mwenye heshima kubwa katika jamii na lazima alitambua vyema nafasi na ushawishi aliokuwa nao kama kiongozi wa eneo hilo," mahakama ilisema, ikiongeza kuwa alihusika katika "uhalifu mkubwa kwa kiwango kikubwa".

    Kwa mujibu wa mahakama, akiwa katika uwanja wa mpira wa miguu, aliwaelekeza Wahutu kuhakikisha hakuna hata Mtutsi mmoja anayefaulu kutoroka.

    Mahakama ilisema kuwa Watutsi waliokuwa wamekwama ndani ya eneo hilo walipigwa mawe, kupigwa risasi na kurushiwa maguruneti.

    Walionusurika katika mashambulizi hayo baadaye waliuawa kwa kupigwa marungu na kukatwa kwa mapanga, mahakama ilieleza.

  3. UN yaitaka Tanzania kusitisha uhamishaji wa Wamasai Ngorongoro na Loliondo

    Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi (CERD) imeitaka Tanzania kusitisha mara moja kile ilichokitaja kuwa uhamishaji wa nguvu wa jamii ya Wamasai kutoka makazi ya mababu zao katika Ngorongoro na Loliondo.

    Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Agosti 28, kamati hiyo ilieleza wasiwasi kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya jamii hiyo, ikiwemo kufukuzwa na kuhamishwa kwa nguvu, pamoja na vikwazo vya kupata ardhi za mababu, maeneo ya makazi na rasilimali za asili.

    CERD pia iliitaka serikali ya Tanzania kuchunguza na kushughulikia madai ya ukiukwaji wa sheria yaliyoripotiwa, yakiwemo kukamatwa holela kwa baadhi ya wakazi na matumizi ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya dola.

    Kamati hiyo ilisema Tanzania inapaswa kurejesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za msingi katika maeneo husika, zikiwemo elimu, huduma za afya, maji safi na huduma za usafi wa mazingira.

    Aidha, ilitoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuhakikisha mazingira salama kwa watetezi wa haki za binadamu, mashirika ya kiraia, wanaharakati, wanasheria na waandishi wa habari wanaoshughulikia masuala yanayohusu haki za jamii za wenyeji.

    Katika mapendekezo yake, CERD iliitaka Tanzania kutangaza haraka matokeo na mapendekezo ya tume mbili za rais zilizoundwa Februari 2025 kuchunguza sera za matumizi ya ardhi, uhamishaji wa wakazi na uhifadhi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

    Kamati hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa kuhakikisha jamii ya Wamasai inashirikishwa kikamilifu katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa maeneo wanayoishi na kuyategemea kwa maisha yao.

    Serikali ya Tanzania mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kuhusu matumizi ya maeneo hayo kwa manufaa ya umma, ikizingatia sheria na masuala ya haki za binadamu.

  4. Iran yashutumu vikwazo vya Marekani, yataka mataifa yavipuuze

    Iran imeilaumu Marekani kwa kile ilichokiita "ugaidi wa kiuchumi" na kuzitaka nchi zote kutotekeleza vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran, ikisema hatua hiyo ni kinyume cha sheria za kimataifa.

    Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, serikali ya Tehran ilisema kuwa kushiriki katika utekelezaji wa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni sawa na kusaidia kulazimisha matakwa ya taifa moja dhidi ya nchi nyingine huru.

    “Kushiriki katika utekelezaji wa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran ni sawa na kushiriki katika kulazimisha matakwa haramu ya taifa moja juu ya mataifa huru na kuvuruga mahusiano yao halali ya kiuchumi na kibiashara,” ilisema taarifa hiyo.

    Iran ilidai kuwa hatua kama hizo zinadhoofisha mojawapo ya misingi muhimu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambayo ni kuheshimu usawa wa mamlaka na uhuru wa mataifa.

    Wizara hiyo ilisisitiza kuwa vikwazo vya Marekani ni “haramu kabisa na visivyo na uhalali”, ikidai vinakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa za kibinadamu pamoja na haki za binadamu.

    Kwa mujibu wa Tehran, mataifa yote yanapaswa kujiepusha na kutekeleza au kuidhinisha vikwazo hivyo na athari zake.

    Taarifa hiyo pia ilikosoa juhudi za Marekani za kuitenga Iran kiuchumi, ikisema hatua hiyo anakiuka kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na kudhoofisha ushirikiano wa kawaida wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa.

    Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Iran kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo.

    Katika barua yake, Tehran iliutaka Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kuchukua hatua dhidi ya kile ilichokitaja kuwa vitisho na shinikizo la Marekani kwa nchi nyingine ili zipunguze au kuvunja mahusiano yao ya kiuchumi na Iran.

    Iran imesema hatua hiyo ya Marekani inawalenga sio tu maafisa wa Iran, bali pia nchi na kampuni zinazofanya biashara halali na taifa hilo.

  5. Maandamano Kenya: Wafanyabiashara Nairobi wapinga ongezeko la kodi

    Mamia ya wafanyabiashara katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, wamefunga maduka yao na kuandamana kupinga ongezeko la kodi na ada za forodha kwa bidhaa zinazoingizwa nchini.

    Maandamano hayo yalifanyika Ijumaa katika eneo la katikati mwa jiji, ambapo wafanyabiashara walikusanyika na kuelekea katika ofisi za Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) kueleza malalamiko yao kuhusu hatua mpya za ushuru.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters na vyombo vya habari vya ndani, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wakati maandamano yalipoendelea kushika kasi.

    Mzozo huo unafuatia uamuzi wa KRA kuongeza ada kwa kontena la futi 40 lenye bidhaa mchanganyiko kutoka shilingi milioni 2.5 za Kenya (takriban dola 19,300) hadi shilingi milioni 3.2 za Kenya ($ 24,700).

    Kiwango hicho kipya, kilichoanza kutumika Agosti 20, 2026, kinaongeza gharama kwa shilingi 700,000 za Kenya ($5,400) kwa kila kontena.

    Hatua hiyo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wafanyabiashara wadogo, ambao kwa kawaida huagiza bidhaa kwa pamoja katika makontena yanayoshirikiwa na wafanyabiashara wengine ili kupunguza gharama. Wengi wao huingiza bidhaa kutoka China.

    Wafanyabiashara hao wanasema ongezeko hilo litaongeza gharama za kuagiza na kutoa bidhaa bandarini, jambo ambalo linaweza kuathiri biashara zao na bei za bidhaa kwa watumiaji.

    Mmoja wa wafanyabiashara walioshiriki maandamano hayo, Muturi Kariuki, alisema hatua yao inalenga kutetea haki ya kufanya biashara.

    “Tunatetea uraia wetu, haki yetu ya kufanya biashara na haki yetu ya kujenga maisha yetu ya baadaye,” Kariuki aliiambia Reuters.

    Biashara nyingi katia eneo la katikati mwa jiji la Nairobi zilifungwa wakati wa maandamano hayo, huku wafanyabiashara wakionyesha mshikamano dhidi ya kile walichokitaja kuwa mzigo mkubwa wa ushuru.

    Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha makundi ya waandamanaji yakipita katika mitaa ya jiji huku yakipuliza filimbi na vuvuzela.

    Wafanyabiashara hao wameonya kuwa wataendelea kuandamana kila Ijumaa hadi mamlaka husika zitakapokubali kuanzisha mazungumzo kuhusu malalamiko yao.

  6. Araqchi: Nafasi ya kurejea katika mazungumzo ya kidiplomasia bado ipo

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema bado kuna uwezekano wa Tehran na Washington kurejea katika mazungumzo ya kidiplomasia, lakini anasisitiza kuwa Marekani inapaswa kutambua kuwa shinikizo na matumizi ya nguvu haviwezi kuleta suluhisho.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Araqchi alielezea mazungumzo yake na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, kuwa ya "tija".

    Alisema kuwa kurejea kwa diplomasia kunawezekana ikiwa kutakuwa na mazingira ya kuaminiana kati ya pande husika.

    "Shinikizo halifanyi kazi. Marekani lazima ijenge imani, izungumze kwa heshima, itambue haki za Iran, na itimize ahadi zake," Araqchi aliandika.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Waziri Mkuu wa Qatar kutembelea Tehran siku ya Alhamisi, akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu kwa mazungumzo na viongozi wa Iran.

    Wakati wa ziara hiyo, Sheikh Mohammed alikutana na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, pamoja na Spika wa Bunge la nchi hiyo, Mohammad Baqer Qalibaf, ambapo walijadili masuala ya kikanda na njia za kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia.

    Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, mazungumzo hayo yalijikita katika hali ya sasa ya usalama na siasa katika Mashariki ya Kati, pamoja na juhudi za kuandaa mazingira yanayoweza kuwezesha mazungumzo yatakayochangia amani na utulivu wa eneo hilo.

    Taarifa hiyo ilisema viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo na ushirikiano wa kikanda ili kupunguza mivutano na kuimarisha usalama katika Mashariki ya Kati.

    Maelezo zaidi:

  7. Saudi Arabia yawakamata makumi ya Waethiopia kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya

    Mamlaka za Saudi Arabia zimesema zimewakamata takriban raia 60 wa Ethiopia katika operesheni mbalimbali zilizofanyika mwezi Agosti kwa tuhuma za kuhusika na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.

    Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Saudi Arabia, watu 15 walikamatwa Jumatano, Agosti 27, wakidaiwa kubeba kilo 290 za mirungi. Kurugenzi Kuu ya Walinzi wa Mipaka ilisema washukiwa hao walinaswa katika operesheni zilizofanyika karibu na maeneo ya mpakani.

    Mamlaka hizo pia ziliripoti kukamatwa kwa Waethiopia wengine 12 katika operesheni tatu tofauti zilizofanyika katika majimbo ya Jazan na Asir. Aidha, gazeti la Al-Riyadh liliripoti kuwa watu watatu zaidi walikamatwa katika jimbo la Riyadh wakiwa na vidonge 29,430 vya dawa zilizodhibitiwa.

    Kwa ujumla, vyombo vya habari vya Saudi Arabia vimeripoti kuwa washukiwa waliokamatwa katika operesheni za hivi karibuni wanatuhumiwa kujaribu kuingiza kilo 290 za mirungi, kilo 33 za bangi na zaidi ya vidonge 72,000 vya dawa zilizodhibitiwa nchini humo.

    Mamlaka zilisema watuhumiwa wamekamilisha taratibu za awali za kisheria na baadhi yao wamekabidhiwa kwa mamlaka husika za uchunguzi huku wengine wakipelekwa katika ofisi ya mwendesha mashtaka kwa hatua zaidi.

    Kukamatwa huku kunafanyika wakati Saudi Arabia ikiendelea kutekeleza adhabu ya kifo kwa baadhi ya makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

    Shirika la Human Rights Watch lilisema mwezi Julai kuwa takriban raia 17 wa Ethiopia walikuwa wameuawa nchini Saudi Arabia tangu Januari baada ya kutiwa hatiani kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya. Vyanzo vilivyonukuliwa na BBC pia vilisema kuwa takriban Waethiopia 200 wanadaiwa kuwa kwenye foleni ya kusubiri utekelezaji wa adhabu ya kifo.

    Takwimu rasmi za Saudi Arabia zinaonyesha kuwa kati ya watu 365 walinyongwa nchini humo mwaka uliopita, zaidi ya theluthi mbili walihukumiwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu, yakiwemo Human Rights Watch na Amnesty International, yameendelea kuikosoa Saudi Arabia kwa matumizi ya adhabu ya kifo katika makosa yasiyohusisha mauaji, yakieleza wasiwasi kuhusu haki za watuhumiwa na mwenendo wa mchakato wa kisheria.

    Haijabainika washukiwa waliokamatwa katika operesheni hizo za hivi karibuni wanakabiliwa na mashtaka gani au watachukuliwa hatua gani.

    Soma:

  8. Mfalme wa Norway aaga dunia

    Mfalme wa Norway, Harald V, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 89, baada ya kulazwa hospitalini wiki iliyopita. Mfalme huyo alikuwa anaugua ugonjwa adimu wa damu.

    Ikulu ya mfalme mjini Oslo imesema alifariki kwa amani mwendo wa saa kumi na mbili na nusu za asubuhi hii leo, katika hospitali ya taifa mjini Oslo. Bendera ya kifalme ya ikulu imeshushwa hadi nusu mlingoti.

    Nafasi yake imechukuliwa na mwanawe Haakon mwenye umri wa miaka 53.

    Baada ya miaka 35 kwenye kiti cha ufalme, Harald atakumbukwa kama mfalme aliyependwa na aliyefanya mageuzi makubwa, kwa kufanya taasisi ya kifalme kuwa ya kisasa, akavunja mila za kifalme kwa kumuoa mtu wa kawaida, na kuwa mtu wa kuwaunganisha wananchi wakati wa nyakati ngumu nchini Norway.

    Soma pia:

  9. Sudan yaondoa amri ya kutotoka nje usiku na hali ya dharura Khartoum

    Mamlaka nchini Sudan, zimeondoa amri ya kutotoka nje usiku, iliyodumu kwa miaka miwili na kumaliza hali ya dharura katika mji mkuu wa Khartoum.

    Kamati ya Usalama ya Jimbo la Khartoum imesema wakazi wa mji huo sasa watakuwa huru kusafiri na kufanya kazi wakati wowote, ingawa polisi wataendelea kushika doria na vituo vya ukaguzi vitaendelea kuwepo.

    Amri hiyo ya kutotoka nje iliwekwa mwezi Mei mwaka wa 2024, ikizuia watu kusafiri kati ya saa kumi na moja jioni hadi saa kumi na moja alfajiri, huku pia ikiweka vikwazo kwa baadhi ya shughuli za biashara na shughuli nyingine.

    Mamlaka pia zimeweka vikwazo vipya kwa wageni wanaoingia katika Jimbo la Khartoum. Chini ya kanuni hizo mpya, wageni wanaosafiri kwa mabasi ya masafa marefu, magari ya umma au binafsi, au treni wataruhusiwa kuingia katika jimbo hilo ikiwa tu wana vibali halali vya kuingia au vibali vinavyohitajika.

    Mabadiliko hayo yanakuja wakati mamlaka za Sudan zinajaribu kurejesha maisha ya kawaida mjini Khartoum, mji ambao uliharibiwa vibaya wakati wa mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF).

    Serikali kuu ya Sudan imekuwa ikirejesha taasisi za serikali katika mji mkuu, baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa mji huo.

    Hata hivyo, mapigano kati ya jeshi na RSF bado yanaendelea katika maeneo kadhaa, ikiwemo majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kaskazini, hali ambayo imesababisha watu wengi kuyahama makazi yao.

    Soma pia:

  10. Spika wa bunge apokea jina la Makamu wa Rais mteule

    Sasa ni zamu ya Bunge la Tanzania kuamua kuhusu jina la Makamu wa Rais mteule, Deogratius John Ndejembi.

    Spika wa Bunge, Mussa Zungu, leo amepokea rasmi jina la Ndejembi lililopendekezwa na Chama cha Mapinduzi, CCM, kwa ajili ya kuwasilishwa kwa wabunge.

    Jina hilo limewasilishwa na Katibu wa Rais, Balozi Ali Jabir Mwadini, akiwa ameambatana na Mpambe wa Rais, ADC, Brigedia Jenerali Nyamburi Mashauri.

    Baada ya kupokelewa kwa jina hilo, hatua inayofuata ni kura ya wabunge, ambao wataamua iwapo Ndejembi anafaa kuidhinishwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

    Ndejembi alipokelewa kwa shangwe na wabunge alipowasili bungeni.

    Bunge linatarajiwa kumpigia kura leo, katika hatua muhimu kuelekea kujaza nafasi hiyo baada ya kujiuzulu kwa Emmanuel Nchimbi.

  11. Kiongozi wa upinzani Zambia, Brian Mundubile anazuiliwa na polisi

    Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, ambaye amekuwa mafichoni baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa urais, amekamatwa kwa tuhuma za uhaini.

    Katika uchaguzi uliofanyika tarehe 13 mwezi Agosti, Rais Hakainde Hichilema alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata asilimia 60 ya kura zilizopigwa dhidi ya asilimia 38 alizopata Mundubile.

    Siku moja baada ya uchaguzi huo, vikosi vya usalama vilivamia nyumba moja katika mji mkuu, Lusaka, inayohusishwa na Mundubile. Katika uvamizi huo, waziri mmoja wa zamani wa serikali aliuawa na wanasiasa wengine kadhaa walikamatwa.

    Mamlaka ziliishtumu upinzani kwa kupanga uasi na kutaka kuipindua serikali, madai ambayo upinzani umekanusha.

    Mundubile na naibu wake Zulu walikuwa wamejificha katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Lusaka.

    Wawili hao wamekamatwa baada ya Rais Hakainde Hichilema kuishinikiza Umoja wa Mataifa kuwakabidhi kwa mamlaka za Zambia.

    Hapo jana, shirika la habari la taifa la Zambia,ZNBC, liliripoti kuwa wawili hao walikuwa wakihojiwa na maafisa wa usalama wakiwa na mawakili wao, baada ya polisi kudai kuwa, walikuwa wanajishughulisha na shughuli zinazoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

    Soma pia:

  12. Congo yaanza kutoa chanjo dhidi ya Ebola

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza kutoa chanjo dhidi ya Ebola, katika juhudi za kudhibiti mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa huo kuwahi kurekodiwa nchini humo.

    Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi mjini Kisangani, makao makuu ya mkoa wa Tshopo, mashariki mwa nchi.

    Wahudumu wa afya na watu wengine walio mstari wa mbele katika kukabiliana na Ebola ni miongoni mwa watakaopewa chanjo kwanza.

    Waziri wa Afya, Roger Kamba, amesema chanjo ya Ervebo itatolewa kwanza kwa wahudumu wa afya pamoja na watu waliowasiliana na wagonjwa.

    Mlipuko huo umeenea katika mikoa sita, huku takwimu za serikali zikionyesha kuwa hadi Jumanne kulikuwa na visa 5,713 vilivyothibitishwa na vifo 2,744.

    Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema mlipuko huo bado haujadhibitiwa na huenda ukazidi ukubwa wa mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016, uliosababisha zaidi ya vifo 11,000.

    Hata hivyo, kuna changamoto kuhusu chanjo hiyo. Ebola inayosababisha mlipuko wa sasa ni aina ya Bundibugyo, wakati Ervebo imeidhinishwa dhidi ya aina nyingine, Zaire ebolavirus.

    Kwa sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa mahsusi dhidi ya Ebola ya Bundibugyo. Chanjo ya Ervebo inatumika chini ya mpango wa matumizi ya huruma, huku wataalamu wakikusanya data ili kubaini iwapo inaweza kutoa kinga dhidi ya aina hiyo ya virusi.

    Kampeni hiyo inatarajiwa kuwafikia watu katika maeneo 14 ya afya katika mikoa ya Tshopo, Bas Uele na Haut Uele.

    Soma Pia:

  13. Trump aagiza Ziwa Ontario kuitwa Ziwa Amerika

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo la kiutendaji linalolenga kubadili jina la Ziwa Ontario na kuliita Ziwa Amerika.

    Hatua hiyo inakuja baada ya mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na Canada kuvunjika wiki iliyopita, huku Marekani ikiweka ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa za Canada zenye thamani ya dola bilioni 20.

    Trump amekuwa akitishia mara kadhaa kubadili jina la ziwa hilo, ambalo ni miongoni mwa maziwa makuu matano yanayopatikana katika eneo la Marekani na Canada.

    Kwa mujibu wa agizo hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani imepewa siku 30 kusasisha jina hilo katika hifadhidata rasmi ya majina ya maeneo ya kijiografia nchini humo.

    Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, amepinga hatua hiyo, akisema jina Ziwa Ontario lina historia ya zaidi ya miaka 400.

    Carney amesema ziwa hilo linaitwa Ontario na litaendelea kuitwa hivyo.

    Hii si mara ya kwanza kwa Trump kujaribu kubadili jina la eneo linaloshirikisha nchi nyingine. Mwaka 2025, alisaini agizo la kubadili jina la Ghuba ya Mexico kuwa Ghuba ya America, hatua ambayo Mexico imeikataa.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Vyombo vya habari Marekani: Mkuu wa CIA aishinikiza Urusi kutoshirikisha Iran taarifa za kijasusi

    Vyanzo vilivyo na ufahamu kuhusu suala hilo vimeviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, John Ratcliffe, aliiomba idara za ujasusi za Urusi kutoshirikisha Tehran taarifa ambazo zinaweza kuisaidia Iran, wakati wa ziara yake ya siri mjini Moscow.

    Inadaiwa pia kuwa suala la msaada wa Urusi kwa Iran lilikuwa miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa katika mazungumzo yake na maafisa wa Urusi.

    Ziara hiyo ni ya kwanza kwa mkuu wa CIA kwenda Moscow ambayo imefahamika hadharani tangu mwaka 2021. Kremlin imethibitisha kuwa Ratcliffe alikutana na maafisa wa ujasusi wa Urusi, lakini si Rais Vladimir Putin.

    Mbali na suala la Iran, Ratcliffe anaripotiwa kujadili pia wasiwasi wa Marekani kuhusu usalama wa wanachama wa NATO katika mazungumzo hayo.

    Hata hivyo, Marekani na Urusi hazijatoa maelezo rasmi kuhusu yaliyomo katika mazungumzo hayo, huku CIA ikikataa kutoa maoni kuhusu ziara hiyo.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, aliielezea ziara hiyo kuwa ya "kawaida kwa kiasi" na kusema mawasiliano hayo yanaweza kusaidia kusukuma mbele baadhi ya masuala, likiwemo suala la kumaliza vita nchini Ukraine. Hakutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo hayo.

    Ripoti kuhusu msaada wa kijasusi kutoka China na Urusi kwa Iran wakati wa vita kati ya Marekani, Israel na Iran zimeibuliwa mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni.

    Moscow nayo imekuwa ikiishutumu Marekani na washirika wake wa Ulaya kwa kuipatia Ukraine taarifa za kijasusi na imekuwa ikiitaka Washington kusitisha msaada huo.

    Maelezo zaidi:

  15. Idadi ya watu waliofariki Nepal na Tibet yafikia 469 huku kukiwa na hofu ya mafuriko zaidi

    Takriban watu 469 wamefariki dunia nchini Nepal na mamia hawajulikani walipo baada ya mafuriko makubwa ya ghafla yaliyokumba eneo la milimani mpakani mwa Nepal na Tibet Jumatano.

    Nchini Tibet, watu watatu wamefariki na zaidi ya 550 hawajulikani walipo. Haijafahamika iwapo baadhi ya watu hao wamehesabiwa pia katika takwimu za Nepal.

    Waokoaji wanaendelea kuwasaka manusura, lakini wanakabiliwa na hofu ya kutokea kwa mafuriko mengine katika eneo lililoharibiwa.

    Shirika la Msalaba Mwekundu limeiambia BBC kuwa waokoaji wako katika hali ya tahadhari kutokana na ripoti kwamba wimbi jingine la mafuriko linaweza kulikumba eneo hilo.

    Ziwa lenye maji yanayoongezeka limejitokeza karibu na mpaka wa China na Nepal, hali inayozua hofu kwamba huenda kingo zake zikapasuka na kusababisha mafuriko mengine.

    Maafisa wa eneo hilo wameiambia BBC kuwa kuporomoka kwa barafu ya mlima kulisababisha wimbi kubwa la maji lililosomba nyumba na barabara, pamoja na kuharibu kituo muhimu cha mpakani kinachounganisha Nepal na Tibet.

    Eneo hilo hutembelewa na makumi ya maelfu ya watalii kila mwaka.

    BBC imezungumza na ndugu za baadhi ya watu ambao bado hawajulikani walipo.

    Dada wawili ambao wazazi wao hawajulikani walipo wameeleza matumaini yao ya kuwaona tena, wakisema: "Tunawapenda sana na tunataka warudi nyumbani."

    Soma Zaidi hapa:

  16. Iran yaweka masharti kabla ya kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz

    Mkuu wa usalama wa Iran, Mohsen Rezaei, amesema Tehran inaandaa orodha ya masharti ambayo Marekani inapaswa kutimiza kabla ya Iran kuruhusu tena usafirishaji kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia maombi kutoka kwa wapatanishi wanaojaribu kupunguza mvutano kati ya Iran na Marekani.

    Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema utawala wa Rais Donald Trump unafanya maamuzi yasiyo sahihi kwa kutegemea taarifa potofu.

    Ghalibaf amesema Washington lazima itekeleze ahadi zake chini ya MOU kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

    Waziri Mkuu wa Qatar yuko Tehran katika juhudi za upatanishi, huku akijadili pamoja na viongozi wa Iran masuala muhimu, likiwemo suala la Mlango wa Hormuz na uwezekano wa kuanza tena kwa mazungumzo kati ya Tehran na Washington.

    Marekani, hata hivyo, inaendelea kusisitiza kuwa Mlango wa Hormuz uko wazi na kwamba mabomu ya baharini yameondolewa, huku ikisema hakuna mazungumzo yaliyopangwa kwa sasa na Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  17. Hujambo, natumai umzima na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya leo Ijumaa.