Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yaahirishwa huku Vance akijiondoa katika safari ya Uswizi

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Marekani kuondoa mzingiro wake wa kijeshi wa majini dhidi ya Iran.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid , Asha Juma, Lizzy Masinga

  1. “Fanyeni hivyo nyumbani pia” – Wanawake wawakosoa mashabiki wa Japan wanaosafisha viwanja vya Kombe la Dunia

    Kwa miaka mingi, mashabiki wa soka wa Japan wamekuwa wakisifiwa duniani kwa tabia yao ya kusafisha viwanja baada ya mechi za Kombe la Dunia.

    Hata hivyo, safari hii wanakabiliwa na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya watu nchini mwao.

    Picha zilipoonekana wiki hii zikionesha mashabiki wa Japan wakikusanya taka kwenye majukwaa ya watazamaji baada ya mechi, baadhi ya watu waliona hali hiyo kama kielelezo cha viwango viwili tofauti vya maadili: wanaume wanaosafisha maeneo ya umma lakini wanaacha majukumu ya nyumbani kwa wake zao.

    Picha moja iliyosambaa sana mtandaoni ilionesha mwanaume akikusanya taka uwanjani, huku picha nyingine ikimuonesha akiwa amelala kwenye sofa nyumbani akitumia simu yake karibu na kikapu cha nguo chafu, wakati mke wake akiosha vyombo jikoni.

    Maandishi yaliyoambatana na picha hiyo yalisema:

    "Wanaume nchini Japan wanapaswa kushiriki zaidi kazi za nyumbani," yakiongeza kuwa muda wanaotumia kufanya kazi za nyumbani ni mfupi zaidi duniani.

    Chapisho hilo limepata zaidi ya alama 60,000 za kupendwa kwenye mtandao wa X.

    Mmoja wa watumiaji wa X alinukuu kauli maarufu ya mwandishi wa Marekani P. J. O'Rourke akisema:

    "Kila mtu anataka kuokoa dunia, lakini hakuna anayependa kumsaidia mama kuosha vyombo."

    Mtumiaji mwingine aliandika:

    "Huenda miongoni mwa watu hawa wanaookota taka kuna mtu aliyeacha mke wake nyumbani akimhudumia mtoto mdogo ili aje kutazama Kombe la Dunia."

    Usafi na tabia ya kusafisha baada ya kutumia maeneo ya umma ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Japan, na mara nyingi huonekana kama mfano wa nidhamu na uwajibikaji wa kijamii.

    Hata hivyo, mjadala huu umeibua maswali kuhusu mgawanyo wa majukumu ya nyumbani na usawa wa kijinsia katika jamii ya Japan.

    Unaweza kusoma;

  2. Nahodha wa Morocco Hakimi kujibu mashtaka ya ubakaji

    Nahodha wa Morocco Achraf Hakimi atakabiliwa na kesi ya ubakaji, waendesha mashtaka wa Ufaransa wamethibitisha.

    Mwanamke mmoja alimshutumu mlinzi huyo wa Paris St-Germain kwa kumbaka nyumbani kwake katika mji mkuu wa Ufaransa mwaka 2023, alipokuwa na umri wa miaka 24.

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma huko Nanterre, kitongoji cha magharibi mwa Paris, ilianza uchunguzi wa awali mnamo Machi 2023.

    Jaji mchunguzi aliamuru kesi isikilizwe Februari 2026 na vyombo vya habari vya Ufaransa viliripoti kwamba Hakimi, 27, alishindwa na rufaa ya hivi majuzi ya kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali.

    Hakimi, ambaye anatazamiwa kukiongoza kikosi chake kwenye mechi ya pili ya Kombe la Dunia dhidi ya Scotland siku ya Ijumaa (saa 23:00 BST), amekuwa akikanusha shutuma hizo.

    "Mfumo wa haki ulinitazama machoni na kusema, 'Kama haungekuwa maarufu, haingewahi kuwa na kesi," Hakimi aliandika kwenye mtandao wa kijamii Ijumaa. "Nilichagua kukaa kimya kwa miaka mingi.

    Niliamini kwamba kudumisha heshima yangu, kuwa mvumilivu, na kuamini mfumo wa haki kungeruhusu maamuzi sahihi kufanywa.

    "Leo, hadithi ambayo si yangu inasimuliwa kwa gharama ya familia yangu, maisha yangu, na zaidi ya yote, ukweli. Wakati mwingine ninahisi kama nimekuwa shabaha rahisi. "Nimekuwa nikingojea kesi hii tangu siku ya kwanza. Na sasa ninaisubiri kwa hamu. Hatimaye, nitaweza kuzungumza."

    Rachel-Flore Pardo, wakili wa mlalamikaji alisema katika taarifa yake: “Baada ya zaidi ya miaka mitatu ya kesi za kisheria, na baada ya mteja wangu, kwa maoni yake, kukashifiwa na kuvurugwa kwenye tope na utetezi wa Achraf Hakimi, uamuzi huu unamletea ahueni na matumaini. "Afueni kwamba amesikilizwa na mfumo wa haki na atakuwa na haki ya kusikilizwa.

    "Tunatumai kuwa jaribio hili litawasaidia wanawake wengine na kudhoofisha zaidi ukuta wa kunyimwa haki na kutokujali kuhusiana na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na katika ulimwengu wa soka ya wanaume."

  3. Mtoto wa miaka 3 alishambuliwa na mamba katika bustani ya wanyama Uingereza

    Polisi wamethibitisha kuwa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aliyepata majeraha mabaya katika bustani ya wanyama alishambuliwa na mamba.

    Polisi wa Cambridgeshire walisema mwanaume mwenye umri wa miaka 30 aliyekamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuua kufuatia tukio hilo amepewa dhamana ya muda, lakini kwa sasa "hafai kuhojiwa" kutokana na hali yake.

    Kwa mujibu wa taarifa, mtoto huyo alishambuliwa na mamba mmoja baada ya kuingia katika eneo la mamba. Tukio hilo lilitokea katika Johnsons of Old Hurst karibu na mji wa Huntingdon, nchini Uingereza, siku ya Alhamisi.

    Mtoto huyo bado yuko katika hali mahututi lakini imara hospitalini. Polisi walisema alipata majeraha makubwa akiwa ndani ya eneo la mamba na baadaye aliokolewa na wafanyakazi wa bustani hiyo.

    Alipatiwa huduma ya kwanza katika eneo la tukio kabla ya kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.

    Maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ni kwa muda gani mtoto huyo alikuwa ndani ya eneo la mamba kabla ya kuokolewa.

    Polisi pia walisisitiza kuwa mamba waliohusika katika tukio hilo hawajakamatwa wala kuuawa wakati uchunguzi ukiendelea.

    Polisi walisema kuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 30 aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo anatoka eneo la Norfolk.

    Mamba waliletwa kwa mara ya kwanza katika shamba hilo linalomilikiwa na familia mwaka 2006.

    Wanyama hao wanahifadhiwa ndani ya jengo la zamani la kufugia ng'ombe ambalo limebadilishwa matumizi, likiwa na njia za kutembelea zilizoinuliwa na kuzungushiwa uzio wa chuma. Wageni wanaweza kutazama mabwawa makubwa ya maji yaliyozungukwa na mimea ya kitropiki kutoka juu.

    Kwa ajili ya kuadhimisha miaka 20 tangu kufunguliwa kwa eneo la kwanza la shambani, makumbusho mapya katika eneo hilo yalitarajiwa kufunguliwa kwa hafla maalumu ya mwishoni mwa wiki kuanzia Jumamosi. Hata hivyo, bado haijulikani ikiwa ufunguzi huo utaendelea kama ulivyopangwa baada ya tukio hilo.

    Polisi walisema wanaendelea kuzungumza na watu waliokuwepo katika bustani ya wanyama wakati tukio hilo lilipotokea.

    Unaweza kusoma;

  4. Watu 35 wauawa baada ya watu wenye silaha kushambulia uwanja mkubwa wa ndege nchini Niger

    Watu 35 wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia uwanja mkubwa zaidi wa ndege nchini Niger siku ya Alhamisi, kwa mujibu wa maafisa wa serikali.

    Hili ni shambulio la pili kulenga uwanja huo ndani ya kipindi cha chini ya miezi mitano.

    Wakazi wa nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Waislamu waliiambia BBC kuwa walikuwa wamemaliza sala za alfajiri wakati waliposikia milipuko na sauti za risasi kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani uliopo katika mji mkuu, Niamey.

    Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema waliofariki ni pamoja na washambuliaji 22, wanajeshi 11 na raia wawili.

    Jioni ya Alhamisi, kundi la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), ambalo lina uhusiano na mtandao wa al-Qaeda, lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo.

    Niger imekuwa ikikabiliana na uasi wa makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali kwa zaidi ya muongo mmoja.

    Mwezi Januari mwaka huu, kundi linalohusishwa na kile kinachoitwa Islamic State lilidai kuhusika na shambulio jingine dhidi ya uwanja huo huo wa ndege.

    Machafuko ya Alhamisi yalidhibitiwa kufikia katikati ya asubuhi, na vikosi vya usalama vimeanzisha msako wa kuwatafuta washambuliaji wowote waliobaki.

    Mmoja wa wakazi wa eneo la karibu na uwanja wa ndege huo, Lawalli Tsalha, aliiambia BBC:

    "Tulimaliza sala zetu saa 5:50 asubuhi (04:50 GMT) na muda mfupi baadaye tukasikia mlipuko mkubwa, kana kwamba kitu kililipuka, labda tairi."

    Aliongeza:

    "Ni baada ya muda kidogo ndipo tulitambua kilichokuwa kinaendelea."

    Uwanja huo wa ndege pia unatumika kama kituo cha kijeshi, jambo linaloufanya kuwa moja ya maeneo muhimu ya kimkakati nchini Niger.

  5. Wabunge wa Zimbabwe wapitisha muswada wa kuongeza muda wa rais madarakani

    Bunge la chini la Zimbabwe limepitisha muswada wa sheria unaolenga kuongeza muda wa muhula wa rais kutoka miaka mitano hadi saba, hatua ambayo inaweza kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa kubaki madarakani hadi mwaka 2030.

    Zaidi ya wabunge 200 walipiga kura kuunga mkono muswada huo siku ya Alhamisi, idadi iliyozidi kiwango kinachohitajika cha theluthi mbili ya kura ili kufanya marekebisho ya katiba.

    Muswada huo pia unapendekeza kufutwa kwa uchaguzi wa moja kwa moja wa rais, ambapo marais wa baadaye watachaguliwa na bunge badala ya wananchi kupiga kura moja kwa moja.

    Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, aliingia madarakani mwaka 2017 baada ya kumuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kwa msaada wa jeshi. Baadaye alishinda uchaguzi wa urais wa mwaka 2018 na 2023, ingawa uchaguzi huo ulikumbwa na malalamiko na mabishano kuhusu uhalali wake.

    Muswada huo sasa unapelekwa katika Seneti ya Zimbabwe, ambako unatarajiwa pia kupata idhini kabla ya kutiwa saini na rais na kuwa sheria rasmi. Ikiwa utapitishwa kikamilifu, mabadiliko hayo yatakuwa na athari kubwa katika mfumo wa kisiasa na kidemokrasia wa Zimbabwe.

    Vyama vya upinzani, makundi ya kiraia na wanasheria wa masuala ya katiba wamepinga mabadiliko hayo, wakisema kuwa marekebisho makubwa kama hayo yanapaswa kuamuliwa kupitia kura ya maoni ya wananchi (referendum) badala ya kuidhinishwa na Bunge pekee.

    Mwanzoni, Rais Emmerson Mnangagwa alisifiwa na wafuasi wake kama kiongozi wa mageuzi ambaye angerudisha ukuaji wa uchumi na kuimarisha utawala wa kidemokrasia. Hata hivyo, utawala wake umekumbwa na changamoto za kiuchumi, uchaguzi wenye utata na kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu kudhoofika kwa misingi ya demokrasia nchini humo.

    Marekebisho haya ya hivi karibuni ya katiba yamezidisha mjadala kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Zimbabwe. Wapinzani wanaonya kuwa yanaweza kudhoofisha uwajibikaji wa kidemokrasia, huku wafuasi wake wakidai kuwa ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha mwendelezo wa uongozi na utulivu wa nchi.

    Katiba mpya iliyopitishwa mwaka 2013 iliweka kikomo cha mihula miwili kwa rais. Pia ilieleza kuwa hatua yoyote ya kuongeza muda wa mihula ya urais lazima iidhinishwe na wananchi kupitia kura ya maoni. Zaidi ya hayo, rais aliyepo madarakani haruhusiwi kunufaika na ongezeko la muda wa mihula isipokuwa wananchi waidhinishe hatua hiyo kupitia kura nyingine ya maoni.

    Unaweza kusoma;

  6. Lebanon yasema mashambulizi ya Israel yameua 18, Israel ikisema wanajeshi wake wanne wameuawa na Hezbollah

    Watu wasiopungua 18 wameuawa kusini mwa Lebanon kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel yaliyofanyika usiku kucha, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon.

    Wakati huo huo, jeshi la Israel (IDF) limesema kuwa wanajeshi wake wanne pia wameuawa.

    Jeshi la Israel limesema lililenga wapiganaji na miundombinu inayohusishwa na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

    Tukio hili linakuja siku moja baada ya Marekani na Iran kusaini makubaliano yaliyolenga kumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati, ikiwemo kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu nchini Lebanon.

    Hata hivyo, Israel na Hezbollah zimeendelea kushambuliana tangu makubaliano hayo yalipotangazwa, jambo linalozua maswali kuhusu mustakabali wa usitishaji huo wa mapigano ulioratibiwa kati ya Marekani na Iran.

    Makubaliano ya Marekani na Iran yanataka kusitishwa kwa uhasama katika maeneo yote ya mzozo na kuheshimiwa kwa mamlaka na uhuru wa eneo la Lebanon.

    Lakini Israel imesema haina mpango wa kuondoa majeshi yake kutoka Lebanon na imesisitiza kuwa vita vyake dhidi ya Hezbollah ni tofauti na vita dhidi ya Iran.

    Shirika la habari la serikali ya Lebanon lilieleza mashambulizi ya usiku kucha katika wilaya ya Nabatieh kusini mwa Lebanon kuwa miongoni mwa mashambulizi makali zaidi tangu vita hivyo vianze.

    Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 18, kujeruhiwa kwa wengine 33, na uharibifu wa majengo kadhaa.

    Kwa upande wake, Hezbollah imesema ilivizia kikosi cha Israel kusini mwa Lebanon na kuharibu mizinga mitatu ya kivita kwa kutumia makombora ya kuongozwa. Kundi hilo pia lilidai kulenga wanajeshi wa Israel kwa mashambulizi ya roketi na mizinga.

    Unaweza kusoma;

  7. Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yaahirishwa huku Vance akijiondoa katika safari ya Uswizi

    Mazungumzo mapya ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran yameahirishwa baada ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, kuahirisha safari iliyokuwa imepangwa kwenda Uswisi.

    Ikulu ya White House ilitangaza usiku wa Alhamisi kwamba Vance hangesafiri kuhudhuria mazungumzo hayo na kusema kwamba maandalizi ya kiutendaji hayakuwa “rahisi wala ya kutabirika”.

    Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Marekani kuondoa mzingiro wake wa kijeshi wa majini dhidi ya Iran, kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano kati ya nchi hizo mbili yaliyolenga kumaliza mzozo huo.

    Ingawa makubaliano hayo pia yalisema mapigano yanapaswa kusitishwa nchini Lebanon, Wizara ya Afya ya Lebanon ilisema mashambulizi ya Israel yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 18 kusini mwa nchi hiyo usiku kucha.

    Jeshi la Israel lilisema limelenga kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, na kuongeza kuwa wanajeshi wake wanne waliuawa.

    Wapatanishi walikuwa wanatarajiwa kukutana kwa kile maafisa wa Marekani walichokiita “majadiliano ya kiufundi” kuhusu hatua zinazofuata za utekelezaji wa makubaliano yaliyotiwa saini mapema wiki hii.

    Hata hivyo, katika taarifa yake, Ikulu ya Marekani ilisema mipango ya mazungumzo hayo “haikuwa imekamilishwa”. Iliongeza kuwa Marekani inatazamia “kuanza mazungumzo ya kiufundi haraka iwezekanavyo”.

    Baadaye, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi ilithibitisha kwamba mazungumzo yaliyopangwa kufanyika katika mapumziko ya milimani ya Burgenstock yameahirishwa, ingawa ilisema maandalizi ya mazungumzo hayo yanaendelea.

    Soma zaidi:

  8. Ukatili unaweza kutokea hivi karibuni katika jiji la El Obeid, Sudan

    Muungano wa zaidi ya nchi 20 umeonya kuhusu hatari inayoweza kutokea ya ukatili mkubwa nchini Sudan, ukisema kuwa hadi raia 500,000 wanaweza kuwa katika hatari huku vurugu zikiongezeka karibu na mji wa El Obeid katika eneo la North Kordofan.

    Muungano wa Kuzuia Ukatili na Kuendeleza Haki nchini Sudan ulisema kuwa takriban raia 50 wameuawa katika kipindi cha siku kumi mfululizo za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika El Obeid na kaskazini mwa Kordofan.

    Pia ulitaja “taarifa za kuaminika za vurugu zinazolenga makundi ya kikabila ikiwemo unyanyasaji wa kingono na wa kijinsia,” na kuonya kuwa zaidi ya watu 100,000 waliokimbia makazi yao ndani ya nchi wanaweza kuwa hatarini ikiwa mapigano yataongezeka.

    "Tunatoa wito kwa Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) kusitisha mara moja mashambulizi yao dhidi ya El Obeid," muungano huo ulisema, huku ukiwataka wahusika wote kupunguza mivutano na kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu.

    Pia ulitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza shinikizo kwa pande zote zinazopigana ili kuzuia ukatili zaidi.

    Onyo hilo linakuja wakati Umoja wa Mataifa pia umeonyesha wasiwasi kuhusu taarifa za uwezekano wa mashambulizi ya ardhini dhidi ya mji huo, ambao ni mojawapo ya vituo muhimu zaidi vya misaada ya kibinadamu na biashara nchini Sudan.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, wote wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali inayoendelea kuzorota.

    "Katibu Mkuu ameshtushwa na taarifa za uwezekano wa mashambulizi ya ardhini yanayoweza kutokea muda wowote huko El Obeid," msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, alisema katika taarifa.

    El Obeid ipo kwenye njia muhimu inayounganisha maeneo yanayodhibitiwa na RSF huko Darfur na maeneo yanayodhibitiwa na jeshi mashariki mwa Sudan. Mji huo pia ni kitovu muhimu cha usafirishaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo lote la Kordofan. Aidha, inahifadhi idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano katika maeneo mengine ya Sudan.

    Soma zaidi:

  9. Khamenei: Nilikubali makubaliano baada ya kupewa uhakikisho kuhusu maslahi ya Iran

    Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ametoa ujumbe mpya kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na Marekani, akisema alikubali mpango huo licha ya kuwa na msimamo tofauti hapo awali.

    “Nilikuwa na mtazamo tofauti kimsingi. Hata hivyo, kwa kuwa Rais wa Iran, kama mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, aliniahidi kwa niaba yake na wanachama wengine wa baraza hilo kwamba haki za wananchi wa Iran na Muungano wa Upinzani zitalindwa, na akakubali wazi kuwajibika kwa hilo, nilitoa idhini yangu,” alisema Khamenei.

    Wakati huo huo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imethibitisha kuondolewa kwa mzingiro wa majini uliokuwa umewekwa dhidi ya meli zote zinazoingia au kutoka katika bandari za Iran.

    Katika taarifa yake, CENTCOM ilisema operesheni zote za kijeshi za kutekeleza mzingiro huo zimesitishwa na kwamba vikosi vya Marekani havitazuia wala kuingilia harakati za meli zinazoelekea au kutoka katika bandari za Iran kwenye Ghuba.

    Hata hivyo, meli zitakazopita katika Mlango wa Hormuz zitalazimika kufuata mfumo wa uratibu wa Iran, kwa mujibu wa Baraza la Usalama la Taifa la Iran.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kuwa ushuru na ada zilizokuwa zikitozwa meli zimesitishwa, huku Iran ikikubali kugharamia ada hizo ndani ya siku 60 kama sehemu ya waraka wa makubaliano uliotiwa saini kati yake na Marekani.

    Licha ya hatua hiyo, meli bado zitalazimika kuwasilisha maombi kwa mamlaka mpya ya mamlaka ya ghuba ya uajemi , chombo kilichoanzishwa na Iran wakati wa vita ili kuimarisha udhibiti wa njia hiyo muhimu ya majini.

    Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatarajia usitishaji wa mapigano kutekelezwa katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon na mapigano kati ya Israel na Hezbollah.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema anatumaini mataifa ya Mashariki ya Kati “yatatekeleza ahadi zao ili kuwezesha mazungumzo yetu kuendelea.”

    Pia unaweza kusoma:

  10. Kombe la Dunia 2026: Canada waidhalilisha Qatar iliyoishia kuwa na wachezaji tisa

    Wenyeji Canada wamewadhalilisha wenyeji wa fainali zilizopita za 2022 Qatar kwa kuwachabanga 6-0.

    Kila kipindi kilizaa magoli matatu huku Qatar wakimaliza na wachezaji tisa dimbani kutokana na wachezaji wake wawili kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

    Mchezaji Jonathan David wa Canada anayecheza katika klabu ya Juventutus Tulin ya Italia alipachika magoli matatu na kuwa wa pili katika fainali za mwaka huu baada ya Lonel Messi kufanya vivyo hivyo dhidi ya Algeria.

    Kabla ya hapo, Uswiss iliionesha Bosnia Herzegovina kile kilichomnyoa kanga manyoya kwa kuwashushia kichapo cha mogili 4-1 huku kiungo Jonathan Manzambi anayesakata soka katika klabu ya Freiburg ya Ujerumani akiziona nyavu mara mbili.

    Soma zaidi:

  11. Kombe la Dunia 2026: Mexico yafuzu kutoka hatua ya makundi baada ya kuifunga Korea Kusini

    Timu ya taifa ya Mexico imekuwa ya kwanza kufuzu hatua inayofuata ya mashindano baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1 kwa 0 dhidi ya Korea Kusini.

    Mexico, ambayo ilishinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Afrika Kusini kwa mabao 2 kwa 0 baada ya sherehe za ufunguzi jijini Mexico City, ilipata ushindi wake wa pili Alhamisi usiku baada ya Romo kufunga bao pekee la mchezo katika dakika ya 50.

    Kwa ushindi huo, Mexico imefikisha pointi sita na kufuzu rasmi hatua inayofuata huku ikiwa bado haijaruhusu kufungwa bao lolote katika mashindano hayo.

    Korea Kusini, ambayo ilifanya mgeuko wa kuvutia na kuifunga Czechia katika mchezo wake wa kwanza, ilikuwa ikitarajia kufuzu kwa kuishinda Mexico. Hata hivyo, baada ya kipigo hicho, italazimika kuepuka angalau kushindwa katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Afrika Kusini ili kuendelea na mashindano.

    Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, Afrika Kusini na Czechia zilitoka sare na kila timu kujikusanyia pointi yake ya kwanza. Matokeo hayo yanamaanisha kuwa timu zote mbili zinapaswa kushinda mechi zao za mwisho ili kudumisha matumaini ya kufuzu.

    Kwa upande wa bara la Asia, Alhamisi haikuwa siku nzuri. Mbali na Korea Kusini kupoteza dhidi ya wenyeji Mexico, Qatar ilikumbana na kipigo kizito cha mabao 6 kwa 0 dhidi ya Canada, hali iliyozifanya timu za Asia kushindwa kuhimili ushindani wa wenyeji na wapinzani wao.

    Soma zaidi:

  12. Iran yatafuta maridhiano na majirani zake wa Ghuba baada ya makubaliano na Marekani

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Kuwait, Abdullah Ali Al Yahya, akisisitiza umuhimu wa mazungumzo kati ya Iran na mataifa ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi ili kupunguza kile alichokiita “kutokuelewana” na kuimarisha uhusiano wa kikanda.

    Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Alhamisi, Araghchi pia alieleza matumaini yake kwamba makubaliano ya amani kati ya Iran na Marekani yatachangia kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.

    Soma zaidi:

  13. Trump: Natarajia makubaliano ya kusitisha mapigano yaheshimiwe katika pande zote, ikiwemo Lebanon

    Siku moja baada ya kutiwa saini kwa makubaliano kati ya Iran na Marekani, Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatarajia usitishaji mapigano kuheshimiwa katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon.

    Wakati nchini Marekani mjadala mkubwa umejikita katika masharti ya kiuchumi na vipengele vinavyohusu mpango wa nyuklia wa Iran, mjini Tehran mjadala umeelekezwa zaidi kwenye hatma ya Mlango Bahari wa Hormuz na kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Israel nchini Lebanon. Masuala hayo yamevutia kwa kiasi kikubwa viongozi wa Iran, hususan wahafidhina wenye msimamo mkali.

    Alhamisi, katika ujumbe uliohusishwa na Mojtaba Khamenei, anayeelezwa kama kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu makubaliano hayo, lakini alikubali yaendelee na sasa anasubiri kuona jinsi yatakavyotekelezwa.

    Wakati huo huo nchini Uswisi, ambako mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufanyika, usalama umeimarishwa katika eneo litakalowakutanisha Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance na Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf siku ya Ijumaa.

    Soma zaidi:

  14. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 19 Juni 2026.