Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hegseth aonya Marekani itarejesha kizuizi cha majini makubaliano ya Iran yasipozingatiwa
Makubaliano hayo yenye vipengele 14, yanabainisha kuwa Iran haitamiliki silaha za nyuklia. Pia yanaanzisha mfuko wa dola bilioni 300 kwa ajili ya "ujenzi upya na maendeleo ya kiuchumi" ya Iran.
Muhtasari
- Hafla ya kutia saini makubaliano ya Iran nchini Uswizi yaahirishwa
- Ukraine yashambulia Moscow
- Vikosi vya usalama vyafanya msako mkali baada ya uwanja wa ndege wa Niger kushambuliwa
- Marekani itarejesha kizuizi cha majini makubaliano ya Iran yasipozingatiwa - Hegseth
- Uganda: Wakili wa Besigye ashtakiwa kwa kosa linalohusiana na uhaini
- Uswizi: Wajumbe wa Iran, Marekani kukutana kesho kwa mazungumzo na wapatanishi
- Iran kuzitoza ada meli zinazopita kwenye Mlango wa bahari wa Hormuz
- Milio ya risasi yasikika katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Niger
- Mama yake Vozinha awasili Praia kabla ya safari ya Marekani
- Utafiti waonesha mafanikio makubwa ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi
- Ruto awaalika Arsenal Kenya baada ya sherehe za kukata na shoka
- Kombe la Dunia 2026: Vozinha kujumuika na mama yake
- Urusi na Ukraine zashambuliana huku Zelensky akizungumza na Trump, Ulaya
- Kombe la Dunia 2026: Ghana yafunga bao la ushindi dakika ya 95
- Kombe la Dunia 2026: Díaz aisaidia Colombia kupata ushindi dhidi ya Uzbekistan
- Trump na rais wa Iran watia saini mkataba wa awali unaolenga kumaliza vita
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Ambia Hirsi
Hafla ya kutia saini makubaliano ya Iran nchini Uswizi yaahirishwa
Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan, Ishaq Dar, ameiambia BBC Idha ya Urdu kwamba hafla ya kutia saini makubaliano ya Iran hapo kesho mjini Geneva imeahirshwa kwa kwa sababu mkataba wa makubaliano tayari umetiwa saini.
Afisa mkuu wa Pakistan hapo awali aliiambia BBC kwamba Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alikuwa amehirisha ziara yake huko Geneva, akisema: "Awamu inayofuata itaendelea kupitia viwango tofauti vya kiufundi ili kushughulikia maswala kadhaa chini ya mfumo huu wa kina."
Maswali yaliibuka mara ya kwanza kuhusu kufanyika kwa tukio hilo baada ya Sharif kubadilisha chapisho lake wake mapema leo asubuhi kwenye mtandao wa X, akiondoa aya iliyosema "Pakistan kwa msaada wa mpatanishi mwenza Qatar itaandaa hafla rasmi kama ilivyopangwa mnamo 19 Juni 2026 nchini Uswizi, kuadhimisha tukio hili muhimu na kuanza mazungumzo ya kiwango cha kiufundi".
Nyuma ya pazia asubuhi ya leo nchini Pakistan, vyanzo viliihakikishia BBC kuwa hafla hiyo itafanyika kama ilivyopangwa.
Lakini kufikia jioni ya leo mpango huo ukabadiliswa.
Sharif alikuwa mmoja wa watia saini wa MoU kama mpatanishi.
Soma zaidi:
Ukraine yashambulia Moscow
Jiji kuu la Urusi Moscow, limekumbwa na shambulio kubwa zaidi tangu kuanza kwa vita vya Ukraine.
Hii ni baada ya takriban ndege 200 zisizo na rubani za Ukraine kushambulia maeneo ya jiji hilo na kuacha moshi mzito ukitanda angani.
Watu 17 walijeruhiwa katika mkoa wa Moscow, kulingana na gavana wa eneo hilo Andrei Vorobyov.
Takriban ndege 1,000 zisizo na rubani na makombora manne ya Ukraine yalinaswa na kuharibiwa kote nchini katika muda wa saa 24, wizara ya ulinzi ya Urusi ilinukuliwa ikisema.
Hifadhi ya mafuta ilishambuliwa katika eneo la la Rostov kusini mwa nchi hiyo, ambapo mtu mmoja aliuawa.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Kyiv ilipiga tena eneo la Moscow kwa "silaha za masafa marefu" - neno la kusisitiza shambulio la Ukraine la masafa marefu dhidi ya Urusi.
"Wakati wa kumaliza vita hivi umewadia, na Urusi lazima ichukue hatua zinazohitajika kiplomasia," aliongeza.
Alisema shambulio hilo kubwa la ndege zisizo na rubani ni hatua ya kujibu shambulio la wiki iliyopita la Urusi dhidi ya Kyiv.
Soma pia:
Vikosi vya usalama vyafanya msako mkali baada ya uwanja wa ndege wa Niger kushambuliwa
Ripoti kutoka kwa serikali ya Niger zinasema kuwa vikosi vya usalama vimeongeza operesheni kubwa katika maeneo ya mji mkuu kufuatia shambulio la asubuhi kwenye eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani.
Milipuko na masaa ya milio ya risasi vilikodi hewa mapema Alhamisi.
Vyanzo vya usalama na wakaazi wanasema shambulio hilo lililenga uwanja wa ndege muhimu wa kimkakati na kituo cha kijeshi kilicho karibu.
Wanajeshi limedhibit hali ya usalama huku mamlaka ikianzisha shughuli za kuwatafuta watu wanaoshukiwa kuhusika na shambulio hilo.
Operesheni za usalama zilizidi kupamba moto, huku ripoti zikionyesha kuwa mtu anayeshukiwa kuwa mwanamgambo alikamatwa karibu na Msikiti Mkuu wa Niamey huku mamlaka ikipanua msako wa kuwatafuta wanamgambo wanaoaminika kuhusika na shambulizi hilo.
Kanda za video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ambazo hazijathibitishwa kikamilifu na BBC, zilionekana kuonyesha takriban miili sita iliyotambuliwa kuwa ya washukiwa wa uvamizi huo waliouawa wakati wa operesheni za usalama.
Wenyeji wanasema wawili kati ya waliofariki walikuwa wamevalia kiraia huku wanne wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi.
Mashahidi katika wilaya ya uwanja wa ndege walisema wanajeshi waliingilia kati kuwazuia wakaazi kuwashambulia washukiwa wengine wanaodaiwa kukamatwa katika kitongoji hicho.
Vikosi vya usalama vilidumisha vimeshika doria katika eneo la uwanja wa ndege, ambapo upekuzi wa kina na shughuli za uchunguzi ziliendelea hadi alasiri.
Mamlaka haijatangaza mwisho wa msako huo.
Maeneo ya uwanja wa ndege yamefungwa, vizuizi vya barabarani kuwekwa huku vikosi vya ulinzi na usalama vikifanya upekuzi na ukaguzi wa magari yanayoingia na kutoka eneo hilo.
Hakuna mtui aliyejeruhiwa na hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.
Hata hivyo, tukio hilo linakuja takriban miezi sita baada ya shambulio kubwa katika uwanja huo wa ndege ambalo lilidaiwa kufanywa na wanamgambo wa Islamic State.
Shambulizi hilo la Januari lililenga uwanja wa ndege wa kiraia na kambi inayopakana nayo ya Air Base 101.
Ripoti zinasema mashambulizi hayo ya kijeshi yalisababisha vifo vya washambuliaji wengi na kuimarisha ulinzi katika kambi hiyo.
Uwanja wa ndege wa Niamey ni sehemu ambayo ina vifaa vya ulinzi huhifadhiwa,hutumika kama kitovu cha usafiri wa anga na kambi ya kijeshi.
Pia ni mwenyeji wa vifaa vinavyohusishwa na Muungano wa Nchi za Sahel (AES), unaojumuisha Niger, Mali na Burkina Faso.
Soma pia:
Marekani itarejesha kizuizi cha majini makubaliano ya Iran yasipozingatiwa - Hegseth
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth anasema Iran isipozingatia masharti yaliyopo kwenye mkataba wa kumaliza vita, basi Marekani itakuwa "haina budi kuweka tena kizuizi cha majini," dhidi yake.
Marekani imekubali kuondoa kizuizi chake cha majini ambacho kilizuia meli kuingia au kutoka kwenye pwani ya Iran tangu Aprili kama sehemu ya makubaliano yaliyotiwa saini wiki hii.
"Ikiwa Iran haitatimiza ahadi," ya kukomesha kuunda silaha za nyuklia, basi Hegseth anasema "idara ya ulinzi iko tayari kuanza tena mashambulizi ikilazimika kufanya hivyo tutahitaji".
Anasema hatua zozote za kijeshi za Marekani na mazungumzo "yatazingatia" silaha za nyuklia za Iran.
Hegseth pia anasema kuna nchi za Ulaya ambazo "ziko tayari" kusaidia kusafisha Mlango-Bahari wa Hormuz.
Lakini anatoa wito moja kwa moja kwa Uingereza "kuongeza kasi, kufanya hata zaidi, kutumia hata zaidi" - haswa, anasema nchi hiyo inapaswa kusaidia Marekani kufikia kambi za kijeshi ndani ya Uingereza na Diego Garcia.
Diego Garcia ni sehemu ya Visiwa vya Chagos katika Bahari ya Hindi, makao ya kambi ya siri ya jeshi la Marekani na Uingereza.
Waziri Mkuu Keir Starmer aliahirisha mpango wake wa kukabidhi umiliki wa visiwa hivyo kwa Mauritius licha ya Trump kupinga hatua hiyo.
Soma zaidi:
Uganda: Wakili wa Besigye ashtakiwa kwa kosa linalohusiana na uhaini
Meya wa zamani wa Uganda na wakili wa kiongozi wa upinzani anayezuiliwa nchini Kizza Besigye kwa tuhuma za uhaini pia ameshtakiwa kwa kosa linalohusiana na uhaini.
Erias Lukwago alifikishwa mbele ya mahakama ya hakimu mkazi mji katika mkuu Kampala akionekana kuwa dhaifu, vyombo vya habari vya ndani viliripoti, siku chache baada ya kukamatwa nyumbani kwake.
Amekanusha mashtaka dhidi yake na kurudishwa gerezani hadi wiki ijayo kesi yake itakaposikizwa.
Kukamatwa kwake siku ya Jumatatu kulizua shutuma baada ya mkuu wa jeshi la nchi hiyo na mwana wa rais Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kujigamba kwenye mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo.
Mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, ambaye alitoroka nchini Uganda kwa kuhofia maisha yake baada ya kugombea urais wa Januari, alidai kuwa Lukwago alikamatwa kwa amri ya Kainerugaba alipokuwa akijiandaa kuwasilisha wito wa mahakama kwa mkuu wa jeshi.
"Ninatoa wito kwa pamoja kupinga hali hii ya kutokujali sheria," alichapisha kwenye mtandao wa X.
Familia ya Lukwago ilienda mahakamani kudai amri ya kuwalazimisha maafisa wa usalama wanaowatuhumu kumteka kufichua aliko na kumwachilia ikiwa "amekufa au yuko hai".
Familia inasisitiza kuwa Kainerugaba alihusika na kukamatwa kwa Lukwago kwa sababu alijigamba kumdhulumu kwenye mitandao ya kijamii.
Maelezo zaidi:
Uswizi: Wajumbe wa Iran, Marekani kukutana kesho kwa mazungumzo na wapatanishi
Uswizi ambayo ni mwenyeji rasmi wa mazungumzo ya makubaliano ya kumaliza vita kati ya Iran na Marekani imesema kuwa imejiandaa kwa mkutano kati ya wajumbe hao.
"Mpango uliofikiwa ni ni kwamba wajumbe wa Marekani na Iran, pamoja na wawakilishi wa Pakistan na Qatar kama wapatanishi na nchi nyingine zenye nia, watakutana kesho mjini Bergen kwa majadiliano ya awali juu ya utekelezaji wa makubaliano," ilisema nchi hiyo katika taarifa.
Taarifa hiyo pia imearifu kwamba, "Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu muda na maelezo ya mkutano huo."
Soma zaidi:
Iran kuzitoza ada meli zinazopita kwenye Mlango wa bahari wa Hormuz
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema katika mahojiano yaliyopeperushwa kwenye televisheni ya taifa ya nchi hiyo kwamba Mlango wa bahari wa Hormuz "hautarejea katika hali ya kabla ya vita."
Ameongeza kuwa: "Iran ina haki ya kusimamia Mlango-Bahari wa Hormuz na, bila shaka, tutatoza ada kwa huduma hizo."
Nchi hiyo sasa itatoza meli zinazopitia njia hii muhimu ya baharini baada ya siku 60.
Maelewano ambayo Trump alitia saini yalisema kwamba katika muda mrefu, Iran itashirikiana na Oman na mataifa mengine ya Ghuba kuunda makubaliano "ya kina" juu ya jinsi ya kusimamia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Marekani inaamini kuwa Iran itadai haki zake "kichokozi", lakini mataifa ya Ghuba "hayatakubali" siku zijazo ambapo kuna mfumo wa kodi, afisa mmoja alisema.
Maelezo zaidi:
Milio ya risasi yasikika katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Niger
Milipuko na milio ya risasi imesikika ikitokea uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Niger, Niamey, wakazi wameiambia BBC.
"Nilisikia milio ya kwanza ya risasi saa 06:00 (05:00 kwa saa za hapa) nilipokuwa msikitini. Lakini hali sasa imedhibitiwa," mtu mmoja alisema.
Milio ya risasi iliodumu kwa saa mbili, ilitoka kwenye mlango wa kuingia uwanja wa ndege, aliyeshuhudia aliambia shirika la habari la AFP.
Niger imekuwa ikipambana na uasi wa wanamgambo wa Kiislamu kwa muongo mmoja na mwezi Januari washukiwa wa jihadi walianzisha shambulio kwenye uwanja huo wa ndege.
Kama majirani zake, Burkina Faso na Mali, Niger inaongozwa na kikosi cha kijeshi ambacho kiliingia madarakani kwa sababu ya serikali kushindwa kushughulikia vurugu.
Wakazi wameiambia BBC kwamba shambulio la Alhamisi lilizuiwa na jeshi, ambalo sasa linawasaka washambuliaji waliokimbia ambao inasemekana waliacha silaha zao.
Mamlaka bado haijatoa maoni na hakuna kundi lililokiri kuhusika na shambulizi hilo. Lakini mshirika mmoja wa kundi la Islamic State alisema ndilo lililofanya shambulio la Januari.
Pia unaweza kusoma:
Mama yake Vozinha awasili Praia kabla ya safari ya Marekani
Mama yake kipa mkongwe wa Cape Verde Vozinha amewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Praia kujiandaa kwa safari yake ya kuelekea Marekani.
Ana Cândida Évora aliondoka katika mji wake wa São Vicente Jumatano usiku, akiandamana na mbunge anayewakilisha wilaya yake.
BBC inafahamu kuwa Bi Évora anaweza kuwasili Marekani kati ya Ijumaa na Jumamosi, kabla ya mchuano wa Jumapili kati ya Cape Verde na Uruguay huko Miami.
"Nina furaha," aliiambia BBC, akionyesha matumaini kwamba kila kitu kitaenda sawa.
"Ninabeba ujasiri wa kipekee kwa raia wa Cape Verde walioko huko. Tutapambana na kung'ara kwenye uwanja huo," aliongeza.
Kwenye uwanja wa ndege wa São Vicente, aliwakumbatia wanafamilia na wapendwa wake kabla ya kuelekea Praia.
Soma zaidi:
Utafiti waonesha mafanikio makubwa ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi
Takriban maisha ya watu 200 yameokolewa nchini Uingereza kufikia sasa kutokana na chanjo inayokinga saratani ya shingo ya kizazi, hii ikiwa ni kulingana na uchambuzi uliochapishwa katika jarida la la Lancet.
Utafiti huo wa kwanza wa aina yake umeonyesha kwamba vifo vimepungua sana tangu wasichana wenye umri wa kwenda shule walipopewa chanjo ya human papillomavirus (HPV) mwaka 2008.
Ripoti ya utafiti huo inaonesha kuwa kati ya 2020 na 2024, hakuna vifo vya saratani ya shingo ya kizazi vilirekodiwa kwa wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 - mara ya kwanza kutokea kwa kipindi cha miaka mitano.
Bila chanjo, takribani vifo ishirini na vitatu vingetarajiwa.
Prof Peter Sasieni, mtafiti mkuu katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London amesema:
"Inashangaza kufikiria kwamba chanjo inaweza kukaribia kumaliza aina fulani ya saratani,"
Utafiti huo pia uligundua kuwa watoto hao waliochanjwa wakiwa na umri wa miaka 12 au 13 sasa hawakabiliwi kabisa na hatari ya kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo kabla ya umri wa miaka 30.
Kabla ya kampeni ya chanjo ya HPV, takribani vifo 20 kila mwaka vilikuwa vikirekodiwa katika kundi hilo la umri.
Kwa ujumla, saratani ya shingo ya kizazi bado ni saratani ya 14 kati ya wanawake nchini Uingereza, na watu 3,300 hugunduliwa kila mwaka.
Inafikiriwa kuwa HPV, virusi ambavyo huenezwa kwa mgusano wa karibu wa ngozi kwa ngozi, husababisha asilimia 99 ya maaambukizi yote ya saratani hiyo.
Maambukizi mengi ya HPV hupita bila matatizo yoyote, lakini mengine husababisha mabadiliko yasiyo ya kawaida ya seli na yanaweza kusababisha saratani miaka mingi baadaye.
Soma zaidi:
Ruto awaalika Arsenal Kenya baada ya sherehe za kukata na shoka
Rais William Ruto amewaalika mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza Arsenal kutembelea Kenya kufuatia sherehe zilizojumuisha shangwe, nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki wao baada ya klabu hiyo kumaliza kiu ya muda mrefu kwa kupata ushindi wa taji la ligi.
Rais alisema alishangazwa na ukubwa wa sherehe zilizoshuhudiwa jijini Nairobi baada ya Arsenal kutwaa ubingwa.
Akizungumza na Reuters wakati wa Mkutano wa G7 nchini Ufaransa, Rais alibainisha kuwa msisimko miongoni mwa mashabiki wa Kenya ulimfanya afuatilie uwezekano wa kuileta klabu hiyo ya Kaskazini mwa London nchini humo mwaka ujao.
abu hiyo.
"Arsenal hatimaye ilipata ubingwa, na kuwa sherehe kubwa. Nilishangaa sana kilichotokea jijini Nairobi," Ruto alisema.
"Ilikuwa sherehe kubwa, najaribu kufuatilia kama Arsenali wanaweza kuja nchini mwaka ujao. Nimetuma mwaliko kwa sababu nafikiria itakuwa wakati mzuri kwa Arsenal kuja Kenya. Wana mashabiki wa kipekee."
Kenya ni mojawapo ya nchini zenye mashabiki wengi wa Arsenal barani Afrika na mashabiki hukusanyika mara kwa mara katika miji mikubwa mbalimbali kutazama mechi za kl
Ushindi wa taji la Gunners ulisababisha sherehe kote nchini Kenya, huku mashabiki wakijitokeza mitaani, katika mitandao ya kijamii na sehemu za burudani kuadhimisha ushindi wa kihistoria wa klabu hiyo.
Urusi na Ukraine zashambuliana huku Zelensky akizungumza na Trump, Ulaya
Urusi imeshambulia Kyiv kwa makombora na ndege zisizo na rubani za Ukraine katika kiwanda cha kusafishia mafuta cha Moscow huku nchi zote mbili zikishambuliana saa chache baada ya Rais Volodymyr Zelensky kuzungumza na Rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wa Ulaya.
Kwa mujibu wa Reuters alisikia milipuko huko Kyiv na mamlaka katika mji wa Sumy kaskazini mashariki mwa Ukraine zilisema mtu mmoja aliuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani.
Tahadhari za mashambulizi ya anga zilitolewa kwa eneo kubwa la Ukraine.
"Adui anashambulia mji mkuu kwa makombora ya balestiki. Kaeni katika maeneo salama hadi tahadhari ya uvamizi wa anga itakapoondolewa!" Tymur Tkachenko, mkuu wa utawala wa kijeshi wa Kyiv, alisema katika chapisho la Telegram mapema Alhamisi.
Shambulio dhidi ya Kyiv ni la pili wiki hii na limetokea huku Zelensky akijaribu kuongeza shinikizo kwa Urusi ili kujadili kukomesha vita vyake vya miaka minne.
Katika mji mkuu wa Urusi, ndege zisizo na rubani zilishambulia kiwanda cha kusafishia mafuta cha Moscow, Meya Sergei Sobyanin alisema kwenye Telegram, akiashiria shambulio la pili kwenye kituo hicho ndani ya wiki moja.
Soma zaidi:
Kombe la Dunia 2026: Vozinha kujumuika na mama yake
Mama wa kipa wa Cape Verde, Vozinha, amepewa viza ya kusafiri kwenda Marekani ili kumtazama mwanawe katika michuano ya Kombe la Dunia.
Tangazo hilo lilitolewa na Kiongozi wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi, Hakeem Jeffries, ambaye alisema amezungumzia suala hilo binafsi na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio.
Vozinha alijipatia umaarufu mapema katika michuano hiyo baada ya kuokoa timu yake isifungwe mara saba katika mchezo ambao Cape Verde na kutoka sare tasa ya kushtusha dhidi ya Uhispania.
Baada ya mchezo huo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alisema mama yake alishindwa kuhudhuria michuano hiyo kwa sababu ya gharama kubwa ya kupata viza ya Marekani.
Bw. Jeffries amesema ada zimefutwa na mipango ya safari sasa inaandaliwa ili mama huyo aweze kumtazama mwanawe akicheza dhidi ya Uruguay mjini Miami siku ya Jumapili.
Mama yake pia aliithibitishia BBC akiwa nyumbani kwake huko Sao Vicente kwamba mipango ilikuwa imefanywa ili asafiri hadi Miami.
"Nina furaha sana," alisema Ana Candida Evora.
"Hili linatokea haraka sana, lakini nina furaha mno. Nitamuona mwanangu akicheza Kombe la Dunia, Mungu akipenda."
"Ninaenda huko kumsaidia, kumpa nguvu na ujasiri. Nitamkumbatia baada ya mchezo."
Soma zaidi:
Kombe la Dunia 2026: Ghana yafunga bao la ushindi dakika ya 95
Fainali za Kombe la Dunia huko Marekani, Mexico na Canada zinazidi kupamba moto.
Umekuwa usiku wenye ahueni kubwa kwa bara la Afrika, ambalo wawakilishi wake wawili walikuwa dimbani: Ghana imefanikiwa kupata alama 3 baada ya kuichapa Panama 1-0.
Goli hilo la pekee katika mchezo uliopigwa usiku wa manane limepachkwa naCaleb Yirenky katikadakika ya tisini ya mchezo huko Toronto Canada.
Ghana ni timu ya pili kupata ushindi miongoni mwa wawakilishi 10 wa Afrika, nyingine ni Ivory Coast.
Timu nyingine 4 zimepata sare huku 4 zikichezea vichapo.
Awali, Jamhuri ya Kidemokras ya Congo ilionesha mbinu za hali ya juu za ulinzi na nidhamu kubwa ya mchezo na kufanikiwa kupata alama 1 mbele ya moja ya vigogo vya soka duniani Ureno, kwa sare ya goli 1-1.
Hiyo ni alama na goli la kwanza katika fainali za Kombe la Dunia kwa DRC iliyorejea baada ya miaka 52, kwani waliposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1974 huko Ujerumani, walipoteza michezo yote mitatu ya hatua ya makundi bila kufunga bao.
Kwa upande mwingine, mabingwa wa dunia wa mwaka 1966, England wamejipatia ushindi wa 4-2 dhidi ya washindi wa pili wa fainali za 2018, Croatia.
Magoli ya Harry Kane aliyepachika mawili na Jude Bellingham na Marcus Rashford yalitosha kuipa ushindi England huku mawili ya Croatia yakitiwa kimiani na Martin Baturina na Petar Mussa.
Soma zaidi:
Kombe la Dunia 2026: Díaz aisaidia Colombia kupata ushindi dhidi ya Uzbekistan
Pambano lililomalizika saa moja asubuhi hii kati ya Uzbekistan wanaoshiriki kwa mara ya kwanza na Colombia wanaorejea baada ya kushindwa kufuzu huko Qatar 2022.
Luis Díaz alifunga bao na kutoa pasi ya bao katika mechi yake ya kwanza kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka, na kuiwezesha Colombia kushinda 3-1 dhidi ya Uzbekistan katika mchezo wake wa ufunguzi wa Kombe la Dunia.
Daniel Muñoz, ambaye pia alicheza katika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 40 baada ya pasi kutoka kwa Díaz, ambaye alifunga bao la kusawazisha dakika ya 65.
Fayzullaev Abbosbek amefunga bao dakika ya 60 kwa Uzbekistan katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia.
Jaminton Campaz aliongeza bao katika kipindi cha pili kwa Wakolombia, ambao wako katika nafasi ya 13 duniani na walikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kuliko Uzbekistan iliyo katika nafasi ya 50.
Colombia ilipanda kileleni mwa Kundi K, mbele ya Ureno na Congo, ambazo zilitoka sare ya kushangaza ya 1-1 mapema Jumatano.
Soma zaidi:
Trump na rais wa Iran watia saini mkataba wa awali unaolenga kumaliza vita
Viongozi wa Marekani na Iran wamesaini makubaliano ya awali ya amani yanayolenga kukomesha vita hivyo, na kuanza kutekelezwa mara moja.
Mkataba huo unajumuisha kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, mpango wa dola bilioni 300 (£224bn) kwa ajili ya "ujenzi mpya" wa Iran, na Marekani kukomesha "aina zote za vikwazo" dhidi ya Iran.
Lakini suala la mpango wa nyuklia wa Iran, sababu kuu iliyotajwa na Marekani kwa mzozo huo, bado halijajadiliwa kwa muda wa siku 60 za kusitisha mapigano ulioongezwa.
Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alisaini makubaliano hayo nchini Ufaransa wakati wa mkutano wa kilele wa G7, alitetea pendekezo hilo, akisema litaepusha "janga la kiuchumi". Hata hivyo, alionya kwamba Marekani "itaishambulia" Iran ikiwa hakuna makubaliano ya mwisho yatakayofikiwa.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian pia alisaini hati hiyo Jumatano, Tehran ilithibitisha.
Spika wa bunge la Iran na mjumbe mkuu wa mazungumzo Mohammad Bagher Ghalibaf aliviambia vyombo vya habari vya serikali kwamba imani yake kwa Marekani bado ipo, na Iran "iko katika hali ya tahadhari".
"Ikiwa adui haelewi lugha ya mantiki, tutaingia tena na lugha ya nguvu," aliambia chombo cha habaro cha serikali cha Fars.
Marekani na Israel zilianzisha vita dhidi ya Iran mnamo tarehe 28 Februari, na kumuua Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei na maafisa wakuu wa kijeshi siku ya kwanza.
Trump aliwaambia waandishi wa habari nchini Ufaransa katika eneo la mapumziko la Evian-les-Bains kando ya ziwa, ambapo mkutano wa kilele wa G7 uliandaliwa, kwamba mpango huo utaepusha " dhiki kwa dunia nzima".
"Sikutaka kuona janga la kiuchumi," Trump aliwaambia waandishi wa habari. "Kama ungeendelea hivi, hilo lingetokea."
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 18/06/2026.