Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mythos ni nini na kwa nini inaonekana kuwa tishio kubwa kuliko Mlango bahari wa Hormuz?
"Wanaogopa nini?"
Hili ndilo swali aliloulizwa mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva.
Katika mikutano ya majira ya kuchipua ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki kuu ya dunia (World Bank) mjini Washington, mawaziri wa fedha, magavana wa benki kuu na baadhi ya wataalamu mashuhuri wa uchumi duniani walikutana kujadili changamoto zinazoikabili dunia.
Ingawa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran pamoja na athari za kiuchumi za kufungwa kwa mlango bahari wa Hormuz vilikuwa miongoni mwa masuala makuu yaliyojadiliwa, Faisal Islam mhariri wa masuala ya uchumi BBC anasema kulikuwa na jambo jingine ambalo kwa baadhi ya washiriki lilionekana kuwa tishio kubwa zaidi.
Wasiwasi wao ulielekezwa kwa mfumo mpya wa akili unde unaoitwa Mythos, ambao una uwezo wa kutikisa mfumo wa kifedha wa dunia.
Hofu hii imezua maswali kuhusu iwapo teknolojia hiyo ikiangukia mikononi mwa wahalifu wa mtandao, athari zake zitabaki kwenye sekta ya benki pekee au zitaathiri pia akaunti za watu binafsi, simu za mkononi, kompyuta na vifaa vingine vya kidijitali.
Swali hilo ndilo pia lililoelekezwa kwa Georgieva, huku maafisa wakuu wa fedha wa Marekani wakionesha wasiwasi kama huo.
Katibu wa Hazina wa Marekani na mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani walikutana na viongozi wa sekta ya fedha ya Wall Street mjini New York City kujadili vitisho vya usalama wa mtandao vinavyoweza kusababishwa na teknolojia hiyo mpya.
Jina la teknolojia hii ni Mythos, iliyoundwa na kampuni ya Marekani ya Entropic.
"Ndiyo, tuna wasiwasi"
Katika mahojiano na mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, mtangazaji wa CBS News alirejelea wasiwasi uliotolewa kuhusu teknolojia hiyo na kuuliza, "Wanaogopa nini?" Pia alimuuliza Kristalina Georgieva, "Je, wewe pia una wasiwasi?"
Alijibu, mkuu wa IMF alisema kuwa vitisho vya usalama wa mtandao vinaongezeka kwa kasi: "Ndiyo, tuna wasiwasi kuhusu hilo."
Kwa baadhi ya viongozi wa sekta ya fedha, tishio la akili unde lilionekana kuwa kubwa kuliko hata mzozo wa Mashariki ya Kati.
Mkuu wa benki ya Barclays, C.S. Venkatakrishnan, alisema hofu yake kubwa ni iwapo akili unde na teknolojia zimeanza kuenea kwa kiwango kisichoweza kudhibitiwa.
Kufuatia vita hivi, Iran ilifunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao ulitatiza usambazaji wa mafuta na nishati katika masoko ya kimataifa, na athari zake zinaonekana kote ulimwenguni.
Waziri wa Fedha wa Canada, François Philippe Champagne, pia alieleza wasiwasi wake kuhusu Mythos.
Alisema:
"Tunajua Mlango Bahari wa Hormuz ulipo na ukubwa wa tishio lake, lakini bado hatuelewi kikamilifu hatari tunayokabiliwa nayo kutoka Mythos."
Mythos ni nini?
Mythos Cloud ni mfumo wa akili bandia uliotengenezwa na Anthropic, kampuni ya teknolojia ya Marekani.
Mfumo huo ni sehemu ya familia ya mifumo ya akili unde ya kampuni hiyo inayoshindana na OpenAI ChatGPT na Google Gemini.
Watafiti wa usalama wa mtandao walioufanyia majaribio mfumo huo walibaini kuwa una uwezo wa hali ya juu wa kutambua mapungufu ya siri katika programu za kompyuta na kuyatumia kuvamia mifumo hiyo.
Kwa maneno rahisi, unaweza kugundua dosari ambazo hata watengenezaji wa programu hizo hawajawahi kuzitambua.
Watafiti hufanya kazi katika vikundi vya tathmini ya usalama vinavyojulikana kama "timu nyekundu."
Katika majaribio, mfumo huo uliripotiwa kugundua kasoro za usalama zilizokuwa zimejificha katika programu kwa zaidi ya miaka 20.
Kutokana na uwezo huo, Anthropic haikuruhusu mfumo huo kupatikana kwa umma mara moja. Badala yake, iliwapa ufikiaji mdogo washirika wachache wa teknolojia kupitia mradi unaoitwa Glasswing.
Miongoni mwa kampuni zilizoshirikishwa ni Amazon Web Services, Apple, Microsoft, Google, NVIDIA na Broadcom.
Lengo ni kuimarisha mifumo yao kabla teknolojia kama hiyo haijafika mikononi mwa wahalifu wa mtandao.
CrowdStrike, kampuni iliyosababisha usumbufu mkubwa duniani kutokana na sasisho lenye hitilafu la programu yake mnamo Julai 2024, ni miongoni mwa washirika wa mradi huo. Anthropic imesema pia imewapa zaidi ya mashirika 40 mengine yanayosimamia programu muhimu fursa ya kutumia Mythos.
Kwa mujibu wa Anthropic, Mythos imeonesha uwezo ambao haukutarajiwa wakati wa hatua za mafunzo ya mfumo huo. Kampuni hiyo inaamini uwezo huo unaweza kusaidia kugundua na kurekebisha udhaifu wa programu kwa ufanisi zaidi.
Hata hivyo, uwezo huo huo umeibua wasiwasi mkubwa. Ikiwa Mythos itaangukia mikononi mwa watu wenye nia mbaya, inaweza kutumiwa kuvamia au kuhatarisha karibu mfumo wowote wa kompyuta.
Kwa nini ni hatari?
Mfumo wa uendeshaji wa OpenBSD, unaojulikana kwa viwango vyake vya juu vya usalama, nao haukusalimika.
Mythos ilifanikiwa kugundua dosari ya kiusalama iliyokuwa imejificha katika mfumo huo kwa muda wa miaka 27.
Akimnukuu mwanzilishi wa kampuni moja ya usalama wa mtandao, mtaalamu wa teknolojia na usalama wa kimataifa Gordon M. Goldstein aliandika katika makala yake kwa baraza la masuala ya mambo ya kigeni na kusema:
"Mfumo huu kwanza hubaini udhaifu wa aina ya zero day, kisha huunganisha udhaifu huo na mapungufu mengine na unaweza kubaki ndani ya mfumo kwa muda usiojulikana bila kugunduliwa."
Kwa maneno mengine, Mythos inaweza kugundua dosari ambazo hazijawahi kufahamika hapo awali, kuzitumia pamoja na mapungufu mengine ya kiusalama, na kujipenyeza kwenye mfumo wa kompyuta kwa njia ambayo ni vigumu sana kutambuliwa.
"Kwa kutumia mbinu hiyo, Mythos inaweza kutwaa udhibiti kamili wa mfumo husika," alisema.
Je, inaweza kutishia miundombinu muhimu?
Entropic imeonya kuwa kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ya akili bandia, huenda isiwe muda mrefu kabla uwezo kama huo haujapatikana kwa watu wengi zaidi na hatimaye kuangukia mikononi mwa watu wasioweza kuutumia kwa usalama na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, hali kama hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi, usalama wa umma na usalama wa taifa.
Naye mtaalamu wa teknolojia na usalama wa kimataifa, Gordon M. Goldstein, ameonya kuwa miundombinu muhimu duniani inakabiliwa na vitisho vinavyoongezeka.
Miundombinu hiyo ni pamoja na mifumo na mitandao ya kimwili au ya kidijitali ambayo ikiharibiwa au kuvurugwa inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa usalama wa taifa, uthabiti wa uchumi na afya ya umma.
Kwa mujibu wake, sekta kama mabwawa ya maji, vinu vya nyuklia, mifumo ya usambazaji wa chakula na gridi za umeme bado zinategemea programu za zamani ambazo zimepitwa na wakati.
Akinukuu mtaalamu wa akili unde Dan Hendrycks, Goldstein aliandika kuwa:
"Mifumo kama Mythos inaongeza hatari hizi na kuifanya miundombinu hiyo kuwa rahisi zaidi kushambuliwa."
Aliongeza kuwa wasiwasi mkubwa wa usalama wa mtandao kuhusu mifumo hiyo ni kwamba inarahisisha kwa makundi yasiyo ya kiserikali au wahalifu wa mtandao kulenga na kushambulia miundombinu muhimu
Kinachozua hofu zaidi
Sehemu hii ya taarifa ya Anthropic ndiyo inayochukuliwa kuwa muhimu zaidi na inayozua hofu kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mythos ilifanikiwa kugundua mapungufu manne ya kiusalama katika kivinjari cha mtandao na kuvuka moja kwa moja ngome za ulinzi za mifumo ya uendeshaji.
Aidha, ilifanikiwa kupenya mifumo ya usalama katika mifumo mingine ya uendeshaji pamoja na mazingira ya Linux, na hata kubuni yenyewe mbinu ya kushambulia seva iliyokuwa ikifikika kupitia mtandao.
Mfumo wa uendeshaji wa Android unaotumika katika simu za mkononi duniani kote pia umejengwa kwa msingi wa Linux, jambo linaloonesha ukubwa wa wasiwasi unaotokana na uwezo wa mfumo huo wa akili unde.
Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi?
Bado ni mapema kutoa hitimisho la mwisho.
Wataalamu wengi huru wa usalama wa mtandao hawajapata fursa ya kuifanyia majaribio Mythos kwa kina, na baadhi yao wana mashaka kuhusu kiwango halisi cha uwezo wake.
Aidha, taasisi ya usalama wa akili unde ya Uingereza imehitimisha kwamba tishio kubwa zaidi la mifumo kama hii litaelekezwa kwenye mifumo yenye ulinzi dhaifu au iliyopitwa na wakati.
Hata hivyo, mjadala unaoendelea miongoni mwa viongozi wa uchumi na usalama duniani unaonesha kwamba baadhi yao wanaanza kuiona akili bandia kama tishio linaloweza kuwa kubwa zaidi kuliko migogoro ya kijeshi au usumbufu wa biashara katika Mlango Bahari wa Hormuz.