Mwanamume mmoja amekiri mashtaka 14 ya kusaidia wengine kujiua
nchini Canada baada ya kuuza sumu mtandaoni.
Kenneth Law, mwenye umri wa miaka 60, alikiri kosa hilo
katika mahakama ya Ontario siku ya Ijumaa, kama sehemu ya makubaliano na
waendesha mashtaka, ambao waliondoa mashtaka makubwa zaidi ya mauaji.
Mamlaka zilisema mpishi huyo wa zamani aliuza takriban
vifurushi 1,200 vya sumu kwa wateja - ambao alikutana nao katika mijadala ya
kujiua mtandaoni - katika nchi 40, takriban robo ya vifurushi hivyo vikitumwa Uingereza.
Mashtaka yote yanahusiana na waathiriwa wa Canada - lakini
familia za waathiriwa wa Uingereza zimesema zimekasirika kwamba waendesha
mashtaka wa Uingereza hawangemshtaki Law kuhusiana na vifo vya Waingereza 79,
ambavyo mamlaka inasema vinahusiana na bidhaa alizouza eneo hilo.
Barua kutoka Huduma ya Mashtaka ya Kifalme, iliyoonekana na
BBC, ilisema Law hatakabiliwa na mashtaka nchini Uingereza kwa sababu anaweza
kupinga kupelekwa kwake baada ya kupatikana na hatia ya makosa kama hayo nchini
Canada.
Law alikamatwa mnamo mwezi Mei 2023, kufuatia uchunguzi tata
uliofanywa na takriban mashirika 11 ya kutekeleza sheria na kuwahusisha
wachunguzi kutoka takriban nchi kumi na mbili, ikiwa ni pamoja na Uingereza,
Italia na Marekani.
Kukamatwa kwake kulikuja wiki moja baada ya uchunguzi wa
Times kudai alikuwa akiwauzia vijana sumu, baada ya mwandishi wa habari
kujifanya mteja na kuzungumza na Law moja kwa moja.
Inasemekana Law alimshauri mwandishi wa habari jinsi ya
kutumia bidhaa zake ili "kuhakikisha anakufa".
Makachero wa Canada waliiambia BBC mnamo 2023 kwamba Law aliendesha
tovuti nyingi zinazotoa vifaa na sumu ili kuwasaidia watu kujiua.