Marekani haijasema lolote baada ya mkutano wa kuamua 'hatma' ya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa na mkutano na wasaidizi wake wakuu ili kufanya "maamuzi ya mwisho" kuhusu mfumo wa kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran, lakini ulihitimishwa bila ufafanuzi kuhusu hatua zinazofuata.
Trump alisema Iran lazima ikubali kwamba haitawahi kuwa na silaha ya nyuklia au bomu, ili Mlango-Bahari wa Hormuz ufunguliwe tena kwa ajili ya "usafiri wa meli bila vikwazo kwa pande zote mbili", na mabomu yoyote katika njia ya maji "yaharibiwe".
Mkutano wa Ijumaa ulifanyika katika Ikulu ya White House, katika sehemu inayotumika kushughulikia migogoro mikubwa. Iran awali ilisema haikuwa ikijadili kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Siku ya Alhamisi, nchi hizo mbili zilikubaliana kuhusu mfumo wa makubaliano - unaojulikana kama mkataba wa makubaliano - ukisubiri idhini ya Trump na uongozi wa Iran, kulingana na maafisa wa Marekani.
Inaripotiwa kwamba makubaliano hayo yangeongeza muda wa kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuanzisha mazungumzo kuhusu mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran.
"Rais Trump atafanya tu makubaliano ambayo ni mazuri kwa Marekani na yanayoangazia masuala yenye kuleta utata. Iran haiwezi kamwe kumiliki silaha ya nyuklia," afisa mmoja wa Ikulu ya White House aliambia CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani.
Tangu kuanzishwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano tarehe 8 Aprili, Trump amependekeza mara kwa mara kwamba Marekani na Iran ziko karibu kufikia makubaliano na mazungumzo yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna matokeo yoyote ya msingi yaliyopatikana.
Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii mapema Ijumaa, Trump alisema alikuwa tayari kuondoa kizuizi cha Marekani kwenye utumiaji wa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kuruhusu meli zilizokamatwa kwenye njia ya maji "kuanza mchakato wa 'kuelekea nyumbani!'"
Soma zaidi:
