Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mfamasia wa Uingereza alivyovumbua jinsi moto unavyowashwa
Mnamo 1826, tukio lililotokea kwa bahati nzuri liliibua uvumbuzi ambao ungebadilisha ulimwengu wa mwanadamu na uhusiano wake na mwanga na joto.
Mfamasia wa Muingereza John Walker alikuwa akichanganya kemikali katika jaribio la kutengeza vilipuzi wakati kijiti kilichokuwa kimefunikwa kwenye mchangayiko huo kilipogusa jiwe mbele ya jiko lake na kuwaka ghafla.
Walker alizaliwa 1781 katika mji wa bandari wa Stockton-on-Tees, katika Kaunti ya Durham, wakati wa mabadiliko makubwa ya Mapinduzi ya Viwanda. Injini ya mvuke ya James Watt ilikuwa imeanza kutumika kibiashara mwaka wa 1776, kabla ya njia ya kwanza ya reli ya umma ya Stockton, inayoendeshwa kwa injini za mvuke, kuanza kutumika mwaka wa 1825.
Miaka minne baadaye, Locomotive Rocket ya George Stephenson ilithibitisha kuwa injini za mvuke zinaweza kuvuta treni za abiria kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa. Safari ambazo hapo awali zilichukua siku 12 kwa farasi sasa zilikamilika kwa saa nane tu.
Lakini kuwasha moto unaozalisha nishati hiyo ilisalia kuwa kitandawili kigumu. Watu waliendelea kutegemea jiwe na chuma, au walijitahidi kuweka makaa ya moto kila wakati. Hii iliendelea hadi uvumbuzi wa bahati mbaya wa Walker ulipobadilisha uzalishaji, matumizi, na usafirishaji wa moto.
Walker alikuwa amehitimi kuwa daktari-mpasuaji, lakini matukio ya vya karne ya 18 katika vyumba vya upasuaji, yakiandamana na umwagaji mkubwa wa damu, yalimfanya aachene na upasuaji na kugeukia ufamasia.
Kufikia 1826, alikuwa akitumia muda wake mwingi kuandaa dawa, sio kwa ajili ya wanadamu tu, bali pia wanyama kama vile farasi, ng'ombe, na hata kuku, kulingana na Alan Middleton, mwandishi wa "Tale of Hope and Despair: The North of England Match Company of West Hartlepool 1932-1954."
Lakini cha muhimu zaidi, Walker aliendelea na majaribio yake ya kemikali.
Middleton anasema: "Walker alikuwa mtu mwerevu sana na mkarimu, na wengine wangesema labda alikuwa mgeni."
Anaongeza: "Kemia ilikuwa shauku yake, na alikuwa akichanganya kemikali ili kutengeneza pellets za kuwasha (vifaa vinavyowezesha bunduki kupiga risasi) kwa marafiki zake wakulima."
Siku moja, alichanganya fomula fulani na kuiacha ikauke. Ilipokauka, akapiga kipande cha kuni kwenye jiko, na kikawaka. Huo ulikuwa ugunduzi wa kipekee ambao hakuna mtu yeyote ulimwenguni aliyewahi kubaini hapo awali."
Anaendelea: "Walker alitambua uwezo wa kibiashara wa ugunduzi huu. Hili lilitokea mnamo mwaka wa 1826. Hatujui tarehe kamili, lakini uuzaji wa kwanza ulifanyika Aprili 1827. Aliziita Vibiriti vya msuguano, na awali ziliuzwa kzikiwa ndani ya mkebe."
"Vibiriti" vya Walker vilikuwa nyembamba sana, vijiti vya mbao hafifu, ambavyo ncha yake moja ilikuwa imetumbukizwa kwenye klorati ya potasiamu, salfidi ya antimoni, gum arabic, na maji. Kijiti kilipokandamizwa kwenye kipande cha sandpaper kilichokunjwa, kiliwaka mara moja.
Walker hakufichua siri ya uvumbuzi wake, lakini hakuiwekea haki miliki. Bidhaa yake ilikuwa bei nafuu, na aliweza kukidhi mahitaji yake ndani ya Stockton.
Hata hivyo, kulingana na "Jarida la Madawa,"vibiriti vya Walker havikuwa vyema. Sehemu iliyokuwa na sulfer inayowaka wakati mwingine huanguka kutoka kwa kijiti, na kuharibu sakafu au mavazi ya mtumiaji.
Kufikia 1829, Samuel Jones, huko London, alikuwa ametengeza vibiriti vyake vilivyojulikana kama "Lucifers," nakala sawa za "taa za msuguano" za Walker. Hizi zikawa vibiriti vya kwanza kutengenezwa kwa wingi.
Watu wengine walianza shughuli za kuboresha fomula hiyo, Derek Judd, mwenyekiti wa Chama cha Waweka alama za Matchbook cha Uingereza, aliiambia BBC News.
Ukubwa na sura ya sanduku la chuma pia ilibadilika. Lakini sanduku la kibiriti ya kisasa ilienea kwa kasi na kuanzishwa kwa toleo la Kiswidi mnamo 1844.
Jad anasema, "Hilo lilikuwa kisanduku cha kwanza cha mechi ambacho kilikuwa na hati miliki."
Katika maeneo mengi, utengenezaji wa vibiriti uligeuka kuwa ufundi wa nyumbani. Utengenezaji wa vibiriti ulifanyika majumbani, kupatia familia mapato ya ziada, licha ya hatari yake.
Jad anasema, "Wanawake na watoto wanaoishi karibu na kiwanda walikuwa wakitengeneza makopo hayo kwa kiwango kidogo, kumaanisha kuwa walilipwa kwa idadi waliyozalisha, kwa malipo yasio rasmi." Kisha mashine zikaja, na hapo ndipo tasnia ikabadilika kuwa biashara ya mamilioni ya dola.
Jad anasema, "Shughuli halisi ya sekta hii imepungua kwa miaka mingi. Makampuni mengi yametoweka."
Lakini, vibiriti bado viko kila mahali. Ingawa zinasalia kuwa zana muhimu, pia, kulingana na Middleton, zimebadilika kuwa kauli ya mtindo, na masanduku maalum yaliyoundwa ambayo yanaweza kugharimu hadi $250.
Mvumbuzi wake, hata hivyo, amesalia nje ya macho ya umma. Middleton na Judd wanaafiki kwamba Walker, takribani miaka 200 baadaye, anastahili kutambuliwa zaidi leo.
Judd anasema, "Walker alikuwa mtu maarufu katika historia ambaye hakutaka kuendeleza uvumbuzi wake. Kama angefanya hivyo, jina lake leo hii lingekuwa maarufu."
Wakaazi wa Stockton wanaonekana kuunga mkono maoni hayo. Wengi wao wanatumai kwamba sherehe za miaka mia mbili, zinazoanza Mei 29, siku ya kuzaliwa ya Walker, hatimaye zitampa mvumbuzi huyu wa ajabu wa ndani utambuzi anaostahili.
Mwenyekiti wa Baraza Lisa Evans anasema: "Tunatumai kwamba matukio yanayotokea mwaka huu na ujao yatatoa fursa kwa watu zaidi kujifunza kuhusu jukumu lake katika kuendeleza kiberiti ambayo sote tunaijua."
Anaongeza: "Uvumbuzi wa kibiriti ya msuguano ulimaanisha kuwa motocungeweza kupatikana mara moja na kwa juhudi kidogo. Ujio wa kibiriti ulifanya kazi za kila siku, viwandani na majumbani, kuwa rahisi na haraka zaidi." Anasema: "Cheche ya moto aliyowasha hadi wa leo inaendelea kuwatia moyo watu."